Bunge la Katiba: ‘Wasaka Fursa’ na Madai ya Posho na Hadhi

Na Ng’wanza Kamata

Siku moja tu baada ya kuzinduliwa kwa Bunge la Katiba, hoja kuu iliyotawala ikawa posho na hadhi za wajumbe wa Bunge. Mijadala ndani na nje ya ukumbi wa Bunge, kwenye mitandao ya jamii, magazetini, vijiweni na mabarazani ikatawaliwa na hoja hii ya madai ya posho. Februari 20, 2014 Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo akateua kamati ya Posho.

Japokuwa suala hili limeshajadiliwa sana, na uamuzi wa posho umekwisha tolewa, nilidhani ni muhimu kuendeleza mjadala kidogo, kwa sababu madai na msingi wenyewe wa madai unadai fikra zaidi haswa juu ya aina ya wajumbe waliomo katika bunge hili. Hii ni muhimu kwa sababu katika hatua hii ambapo mchakato upo mustakabali wan chi umo mikononi mwa ‘mkusanyiko’ wa wajumbe hawa.

Kinachotusukuma kudadisi aina ya wajumbe wa bunge hili sio msingi wa madai ya posho tu bali pia namna walivyopatikana na msukumo wa wao kutaka kuwa sehemu ya Bunge hili maalumu.

Kuhusu posho, siku chache tu baada ya wajumbe 201 kuwa wameteuliwa na majina yao kutangazwa magazeti yalianza kudokeza, kwa kubashiri au kwa tetesi, kuwa wajumbe wa Bunge la katiba watalipwa kiasi cha Shs 700,000 kwa siku. Jambo hili lilipofahamika, lilizua maswali, na wanachi sio tu walihoji bali walipinga kiasi hicho kulipwa. Na baadae ilipotangazwa kuwa kiasi watakacholipwa ni shs 300,000 hakukuwa na maswali mengi sana kwa wananchi, waliridhika, japo wapo waliohoji na kudai bado hata hizo shs. 300,000 zilikuwa nyingi.

Lakini haikuwa hivyo kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hili maalumu. Kwa sababu siku ya pili tu baada ya kukutana na kupata nafasi ya kwanza kuzungumza hawakuchelea kutoa duku duku zao, ‘mheshimiwa mwenyekiti posho haitoshi’. Japo hatujui ni wengi kiasi gani [kwa sababu kuna baadhi walipinga wazi wazi], lakini ni wazi hoja hii ilifurahiwa na wengi wa wateule hawa, hata ambao hawakusemi, lakini moyoni wakitamani iwe inavyodaiwa, posho iongezwe.

Kwa nini hoja hii ya posho ikapewa nafasi ya mwanzo kabisa katika jambo muhimu kama hili? Sababu zaweza kuwa nyingi, katika hizo moja iliyo kubwa ni aina ya watu waliomo katika bunge lenyewe. Hawa tutawaita wasaka fursa (opportunists). Na kwa bahati nzuri Bunge la Katiba linazo fusra nyingi zikiwemo za kipato, za madaraka makubwa, za nafasi kubwa na zenye mamlaka ya kisiasa, na fursa nyinginezo.

Usaka fursa kwa upande mmoja imekuwa ndio kauli mbiu ya nchi – ‘changamkieni fursa’ utasikia viongozi wetu wakihimiza. Wafanyabiashara wakubwa, wajasiriamali, kina mama lishe na machinga, wote huhimizwa kuchangamkia fursa. Na inaanza kujengeka imani kuwa ukichangamkia fursa mambo yako yatakuwa mazuri na ukizubaa fursa zitakupita na ‘itakula kwako’. Lakini ni wazi yote haya ni kiini macho tu, cha kuhalalisha unyonyaji, dhuluma na unyang’anyi kwa upande mmoja, na kuwafanya masikini wajilaumu wao wenyewe kwa umasikini wao – kwa hoja kuwa hawakuchangamkia fursa.

Katika mtazamo huu wa kuchangamkia fursa, ni wazi wajumbe wa bunge maalumu la Katiba katika madai yao ya nyongeza ya posho walisukumwa na fikra hii ya kuchangamkia fursa. Waliposikia kuwa itakuwa shs 700,000 walifurahia, na walipoambiwa ni shs. 300,000 walifadhaika. Kwa hivyo wakadai iongezwe na pia wapewe Ipad.

Lakini kuna dalili kuwa wajumbe wa Bunge hili walianza kuchangamkia fursa hii hata kabla. Ukiacha wabunge na wawakilishi ambao walichangamkia fursa na mapema kwa kuhakikisha kuwa wamo – na wasingetaka kusikia kabisa Bunge maalumu la watu tofauti bila wao kuwemo, hawa 201 habari zao kidogo kidogo zimeanza kutoka. Walichangamkia fursa – ama kwa kujipendekeza wenyewe au wao na wenzi wao, kwa kuitisha mikutano ya ‘usiku’ bila kuwahusisha wenzao, na kila hila na ghiliba waliyoweza kuitumia – ili wawemo. Hata hivyo itakuwa ni makosa kumdhania kila mjumbe wa Bunge hili kuwa ni msaka fursa, lakini kama wapo wasio wa aina tunayoieleza basi tunashawishika kusema watakuwa si wengi.

Na kwa kuwa dalili za mwanzo zimeanza kuonesha namna wasaka fursa hawa wanavyopenda posho, ni wazi watakuwa na bei! Kwa kila jambo muhimu litakalohitaji uungwaji mkono, jambo la ushindani baina ya makundi yenye mikakati na maslahi kinzani ya kisiasa, wataamua kwa msukumo wa ‘posho’. Na posho zipo, na watoa posho si haba, na zitakuwepo za aina na sura mbalimbali.

Katika hali hii ni nini mustakabali wan chi?

Kuna mambo mawili. La kwanza, kuna mambo mengi yanafanywa kwa jina la wananchi, hata kama wao hawataki na wala hawaungi mkono. Lakini bahati mbaya sana wananchi wenyewe hawana nguvu ya maamuzi na hivyo hutegemea fadhila za wafanya maamuzi – wafanye yale yanayowaridhisha. Hili la posho ni wazi halikuwafurahisha wananchi lakini hawakuwa na uwezo wa kulizuia, zaidi ya kulalamika. Kulikuwa na matarajio, mwanzoni mwa mchakato huu kuwa utamaduni mpya wa kisiasa ungezuka wa wananchi kuwa na uwezo wa kujenga nguvu na mfumo wa uhamasishaji na ujenzi wa umoja na mshikamano wa kupinga na kuzuia wasiyoyataka, na kushinikiza wale wayatakayo. Hili halijawa kwa kiwango cha kubadilisha mwelekeo wa siasa zetu. Wananchi bado ni ‘mateka’ wa siasa za vyama.

La pili ni kuwa dai la nyongeza ya posho lilikuwa na dalili za kuchochea hasira za makundi mbali mbali ya wananchi. Hii ingekuwa ni kuchochea hali ambayo imeshaanza kujitokeza toka rasimu ya kwanza ya katiba ilipotoka na kupendekeza serikali tatu. Hisia za U-Tanganyika na U-Zanzibari (U-Pemba na U-Unguja) zimeanza kujengeka. Hofu yangu ni kuwa kama mchakato katika hatua ulipofikia uko mikononi mwa wasaka fursa – na hawa wamo kwenye vyama vyote vya siasa, NGOs na Asasi zingine, tutapona? Kwa sababu kwa wasaka fursa, maslahi binafsi au ya kundi (kwa kivuli cha wananchi au taifa) ndio hutangulia fikra na huongoza na kuelekeza maamuzi.

Kwa msukumo wa wasaka fursa ni wazi hata pale nyumba itakapokuwa inaungua moto – kitu cha kwanza kwao sio kuwahi kusaidia kuzima moto na kuokoa nyumba. Kwanza watajiuliza, tukizima au tukiacha iungue tutapata faida gani? Endapo maslahi makubwa yako katika kuacha nyumba iteketee kwa moto wataiacha iungue na pengine kuuchochea moto ili numba iteketee haraka.

Kwa jinsi mambo yalivyo wenye maslahi ya kudumu na nyumba ndio wanaoweza kuiokoa, na hao ni wanyonge, wavuja jasho wa Tanzania – Bara na Visiwani. Ili matakwa yao yaweze kupata sauti na nguvu hawana budi kukataa kutenganishwa. Kwani katika mgawanyiko na mfarakano baina yao ndio wasaka fursa huneemeka.

3 thoughts on “Bunge la Katiba: ‘Wasaka Fursa’ na Madai ya Posho na Hadhi

 1. Asante ndugu Ng’wanza. Umefanya fizuri kwa kutambua umuhimu wa kuendelea kulitafakari hili la posho kwa wajumbe wa Bunge la Katiba.
  Hili la nipe zaidi bila kikomo ni matokea ya tamaa binafsi iliporuhusika iote mizizi na kuendelea kukua kwa kasi kubwa miongoni mwa jamii yetu, hasa serikalini na kwenye taasisi za umma na kusababisha uwepo kwenye taasisi hizo uzidi kuwa ni uliolenga kufankisha maslahi binafsi dhidi ya yale ya taifa kupitia taasisisi hizo.
  Kuwepo kwa wingi wa magari ya anasa serikalini na kwenye taasisi za umma; wingi wa majumba ya kifahari yamilikiwayo na watumishi kwenye taasisi hizo; wingi wa safari na vikao vya hapa na pale uliolenga kujilimbikizia mali binafsi dhidi ya maslahi ya umma kupitia taasisisi hizo ukilinganishwa na hali kwenye taasisi binafsi ambazo ndio vyanzo vya mapato serikalini kunadhihirisha kwa kiwango kikubwa kwamba tamaa binafsi za anasa zinazidi kuota mizizi na kuongezeka hapa nchini dhidi ya maendeleo ya jumla kwa taifa letu.
  Mataifa kama China ambayo mpaka sasa ni miongoni mwa mengi yanayochangia misaada mingi iliyolenga kuboresha uzalishaji na pato la taifa letu ni yale yaliyofanikisha kujijengea maendeleo makubwa ya kiuchumi na uwezo wa kusaidia mataifa mengine yaliyobaki nyuma kiuchumi kutokana na uzalendo wa hali ya juu na tabia iliyojengeka miongoni mwa wote ndani ya mataifa hayo ya kukwepa anasa ili kutoa fursa kwa pato la taifa litumike zaidi kwenye kuboresha miundo mbinu itakayowezesha ongezeko endelevu la kasi ya ukuaji wa chumi za mataifa yao kwa manufaa ya vizazi.
  Itakuwa sahihi zaidi kuita hizi tamaa binafsi za anasa dhidi ya maendeleo ya uchumi wa taifa letu kama tendo la kuhujumu ukuaji wa uchumi wa taifa letu kulikolenga kufanikisha anasa binafsi badala ya kuziita matendo la kuchangamkia fursa ambayo ni matendo mema.
  Nimependezwa na hoja kwa ujumla ila sikubaliana na fikra kwamba ni tamaa binafsi zinawafanya wengi kutaka mabadiliko kwenye muundo wa serikali ya Muungano yaliyolenga kuondoa kero na kuboresha uhuru wa washirika wa kutumia fursa zilizoko kwenye utandawazi kiasi iwezekanavyo ili kujiletea maendeleo makubwa zaidi kiuchumi kuendana na hali inayobadilika badilika ulimwenguni, Pia, bila ya nguvu ya hoja itaniwia vigumu sana kukubaliani na fikra kwamba mabadiliko kwenye Muundo wa serikali ya Muungano Tanzania yatasababisha Utengano kati ya Zanzibar na Tanganyika.
  Hii ni karne ya utandawazi na hakuna kurudi nyuma. Sio tena ndoa za kisiasa za kudumu milele bali ni ushirikiano na mataifa karibu yote duniana uliojengeka kwa misingi ya hiari kwenye kuingia na kujitoa kwenye mikataba ya ushirikiano wa kitamaduni, kiuchumi, kibiashara, kiusalama, kiulinzi,n.k. na na taifa lolote duniani ili kufaidi zaidi utandawazi kuendana na mazingara yabadilikayo mara kwa mara kuendana na wakati.
  Zanzibar imekaa vizuri sana ndani ya Bahari ya Hindi na kuwezeshwa kuwa na mahusiano mazuri sana ya kiuchumi, kibiashara, kitamaduni, kiulinzi, kiusalama, n.k. na Tanganyika bila ya kuwepo ndoa ya Kisiasa. Labda ni mataifa kama Rwanda, Burundi, ‘DRC’, Zambia na Malawi yanaonekana kuhitaji sana kuwa na ndoa ya kisiasa na Tanganyika ili kujihakikishia shea ya Bandari sehemu za Bahari ya Hindi kupitia Tanzania na soko kubwa ndani ya ndoa hiyo ya kisiasa.
  Njia nzuri za kutambua kero za ndoa za kisiasa chini ya miundo ya ya serikali moja au mbili kwenye harakati za nchi washirika kujitafutia maendeleo kupitia fursa zilizopo ndani ya utandawazi ni kufananisha kero husika kwenye ngombe wawili walioko malishoni huku wakiwa wameunganishwa pamoja kwa kamba miguuni na wengine wawilli walioko kwenye malisho hayo hayo pasipo kuunganishwa pamoja kwa kamba miguuni.
  Muundo wa serikali ya Muungano Tanzania unatakiwa uwe ni ule usiokuwa kero kwa kwa Zanzibar au Tanganyika kwenye harakati zao za kujiletea maendeleo yao zenyewe kupitia fursa zilizoko kwenye utandawazi ulimwenguni na kuendana na mazingara yanayobadilika badilika kuendana na wakati. Fursa za utandawazi kwa Zanzibar sio hizo hizo kwa Tanganyika. Sijui kamba itafungwaje ili kuwaondolea kero ngombe wawili walionganishwa pamoja kwa kamba miguuni ili waweze kuwa na uhuru wanaofaidi wawili wanaotembea malishoni pasipo kuunganishwa kwa kamba miguuni!?
  La muhimu ni kuzingatia kwamba ni nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu itakayotupatia muundo bora zaidi wa muundo wa serikali ya Muungano Tanzania na tusione vigumu kuvunja ndoa ya kisiasa Tanzania pale enzi ya utandawazi ulimwenguni inapotutaka tufanye hivyo. Lolote aliloumba mwanadamu linaweza kuvunjwa pale Muumba atakapotaka iwe hivyo kuendana na wakati.
  Wengine mnasemaje?

 2. Nashanga kwamba Ng’wanza anashanga waheshemiwa Wajumbe wa Bunge Maalum wakasaka fursa ya kujipatia posho nono pindi tu walipopata fursa. Ndivyo tulivyolelewa kisiasa na kiuchumi katika kipindi hiki cha ‘mageuzi’ ya uliberali mamboleo (neo-liberalism), au kwa maneno mengine, utandawazi. Tukahubiriwa na tukafurahia propaganda kwamba utandawazi una changamoto zake na fursa zake. Sasa sisi watanzania tusake fursa za utandawazi (ndio mantiki, na hoja, kwa ufupi, ya Dr. Massawe pia katika mchango wake). Popote pale ulipo – Bungeni, serikalini, migodini, mashambani, viwandani (kama bado vipo!), ofisini, ‘saka fursa, ruksa’.

  Mpiga kura akipewa doti la khanga au kibaba cha unga kwa kumpigia kura mhe. fulani, anapokea: anasaka fursa. Mhe. akiingia bungeni, anasaka fursa kuingia katika kamati za kudumu, anasaka fursa. Anafanya juu chini ili hatimaye ateuliliwe kuwa waziri. Akipata uwaziri, alhamdullahi, akapata fursa ya kusaka fursa. Anfunga safari kwenda Loondon, kuweka saini katika mkataba “mbovu”; ndiyo mbovu kwako, lakini ni fursa kwake – kasaka fursa. Ukiambiwa kuhusu rushwa, corruption na blabla zingine, unatikia, ‘naam tumepoteza maadili’, uzalendo, n.k. – angalia hata wapiga kura wetu wanapokea hongo!! Wanaharakati wanapata fursa kuandika proposal ya kupata funding kwenda kuelimisha wapigakura. Wanakuwabizi kuwafundisha, kuwaelimisha wapiga kura kuacha kusaka fursa – angalao kwao inatokea mara moja katika miaka mitano. Wanapata funding kutoka wafadhili – wao pia wanasaka fursa!

  Mwisho wa siku utandawazi/uliberali mamboleo ni awamu mojawapo ya mufumo wa kibepari. Itikadi ya kibepari/kibwenyenye inakita kwenye kila mtu kusaka fursa – ‘equality of opportunity’ – ingawa hakuna EQUALITY of opportunity: fursa ya kupata doti la khanga kwa mama mkulima sio sawa na fursa ya kupata mamalioni ya dola kwa kuweka saini katika mkataba mbovu! Anayesaka fursa (opportunity) kwa kuona mwanya, wewe unamwiita opportunist, lakini utambulisho wake rasmi ni mjasiriamali. Usimuonee……! Tafakari, ndiyo mfumo tuliyokumbatia na hii rasimu ya katiba haizungumzii kabisa mfumo wenyewe ambao umekita kwenye kusaka fursa. Ina maneno mengi juu ya maadili n.k. haya yatabaki kuwa maneno yasiyona maana kama mfumo wenyewe hauzungumziwi/haujadiliwa.

  Nielimishe ndugu yangu Ng’wanza: kati ya hao walioingia katika Bunge Maalum – kundi la wanasiasa watawala, kundi la wanasiasa watawala-watarajiwa, kundi la wanasiasa chipukizi (wanaharakati), nani atahoji MFUMO WA KUSAKA FURSA.

 3. Kwenye mchango wake, Issa bin Mariam kaelezea vizuri sana umuhimu wa watanzania kuchangamkia fursa za utandawazi mahali popote walipo na zilipo kwenye harakati zao za kujitafutia maendeleo, huku akitutajia mojawapo ya zile fursa haribifu zilizopo kwenye jamii na utandawazi ambazo huwezesha wanajamii wachache watoe au kupokea rushwa ili kufanikisha matarajio yao binafsi kwa gharama ya maendeleo kwa jamii wanamoishi kwa ujumla.
  Fursa ya kutoa au kupokea rushwa huisababishia jamii madhara makubwa na kurudi nyuma kimaendeleo pale inapotumika ili kufanikisha dhaifu wachaguliwe kuwa viongozi badala ya wale bora waliopo; kodi stahili zisilipwe; biashara haramu (kwa mfano za viungo vya wanyama pori na madawa ya kulevya); haki isitendeke mahakamani na kwingineko ; n.k.
  Njia kudhibiti uwepo wa fursa haribifu na matumizi yake ni kuhakikisha sheria na taratibu madhubuti zipo ili kuzuia wasaka fursa wasizichangamkie zile haribifu na wote wanaozikiuka wanakamatwa na kuadhibiwa kuendana sheria zilizopo, na vyombo vya dola vya kotosha na madhubuti vipo ili kusimamia utekelezaji wa sheria dhidi ya uwepo wa fursa haribifu na matumizi yake.
  Jukumu la wote ndani ya Bunge la Katiba ni kuhakikisha kwamba Katiba mpya inayosukwa inavyovipengele toshelezi kufanikisha sheria madhubuti ziweze kutengenezwa dhidi ya uwepo wa fursa haribifu na matumizi yake kwenye jamii na utandawazi. Hii ni kuzingatia kwamba uwepo na uchangamkiaji wa fursa haribifu kwenye jamii na utandawazi ni kuu miongoni mwa zile zinazosababisha visababishi nchi nyingi zinazoendelea kuzidi kudidimia kwenye dimbwi la umaskini pale mtaji wao mkubwa kwenye raslimali za asili (kama madini) zinapozidi kupungua pale zinapovunwa na wageni wasiolipa kodi stahili kutokana na matumizi ya uwepo kwenye jamii na utandawazi fursa haribifu ya kuweza kutoa au kupokea rushwa ili kuwezesha wageni wasilipe kodi stahili kutokana na utajiri mkubwa wavunao kwenye hizo nchi.
  Jukumu la wote ndani ya Bunge la Katiba ni kuhakikisha Katiba inayotengezwa ni toshelezi kwenye jukumu lake la kuwezesha vita ya jamii dhidi ya uwepo fursa harifu na matumizi yake, na siyo kukemea tu uwepo wa fursa hizo haribifu na matumizi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box