Buriani Mwalimu Yohana J. Muganyizi: Bingwa wa Hisabati na Fizikia Aliyewajali Watoto Wa Wanyonge

“Bwana rubani wa ndege ya Rais, umesikia kauli ya Waziri Mramba? Kwamba ndege ya Rais lazima inunuliwe hata kama itawalazimu Watanzania kula nyasi! Aliniuliza mwalimu YohanaMuganyizi, ambaye alikuwa akinifundisha fizikia na hisabati nilipokuwa kidato cha tatu na cha nne, katika shule ya sekondari Kahororo iliyopo mjini Bukoba. Siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa ndoto yangu ya utotoni ya kuwa rubani. “Siutaki tena urubani,” nilimjibu, moyoni nikiwa nimejaa hasira. “Utasoma nini sasa?” aliniuliza. “Nitasoma siasa. Na nataka kuwa mwalimu kama wewe!” Wengi tuliokuwa katika darasa lile la sayansi hatukuendelea tena na sayansi licha ya kufaulu masomo ya sayansi kwa alama A katika mtihani wa kidato cha nne. Wengi wetu sasa ni walimu, tangu sekondari mpaka vyuo vikuu.

Mwalimu Yohana J. Muganyizi alihamia shuleni Kahororo mwaka 2003, akitokea shule ya wavulana ya Bwiru iliyopo jijini Mwanza. Alikuwa mwalimu bora wa sayansi, na hasa katika masomo ya hesabu na fizikia. Sayansi kwake haikuwa nadharia tu, bali pia vitendo. Aghalabu ungemkuta akitembea na bisibisi akijaribu kurekebisha taa na mifumo ya umeme shuleni hapo. Kubwa kuliko yote ni kwamba hakuwa mwalimu wa sayansi wa kawaida: alichanganya sayansi na siasa.

Wengi wetu tulivutiwa na hadithi zake kuhusu siasa, na jinsi alivyoichambua historia ya nchi hii. Si ajabu kwamba ujio wake shuleni Kahororo uliamsha vuguvugu la kupigania haki na usawa miongoni mwa wanafunzi, na baina ya wanafunzi na walimu.

Binafsi nilikuwa karibu naye, huku akinishauri namna ya kuendesha vuguvugu la kupigania haki na usawa. Nilikuwa kiongozi wa taaluma, na baadaye kiranja mkuu, huku yeye akiwa mwalimu wa taaluma, hivyo tulikuwa karibu sana.

Mapambano ya dhidi ya uonevu
Kufikia mwaka 2004, viongozi wa wanafunzi shuleni Kahororo tulikuwa tumegawanyika katika makundi matatu. Kundi la kwanza, ni lile miungu watu. Hawa walijiona wako juu ya sheria. Waliwapiga wanafunzi, walipora chakula, na hasa wali na sukari, na walifurahia zaidi kuwa karibu na walimu madikteta, na hasa aliyekuwa mwalimu mkuu msaidizi. Kundi hili lilitengenezwa na mwalimu mkuu msaidizi, na wengi wao wakiwa ni watu wa dini yake na kabila lake.

Kundi la pili ni lile lililojibainisha kama kundi la wanamapinduzi. Tulikuwa wachache katika kundi hili. Tuligoma kuweka sahani zetu katika meza ya viongozi na tukajichanganya na wanafuzi wenzetu. Ilipofika zamu yetu, na hasa siku ya wali, tulihakikisha kuwa wanafunzi wenzetu wanapata chakula cha kutosha. Tuliongoza kwa upendo, na hatukuwahi kumpiga mwanafunzi.

Kundi la tatu ni lile la mrengo wa kati ambalo halikutaka kuchukua upande. Hivyo basi mgongano mkubwa ulikuwa kati ya wanamapinduzi na madikteta. Walimu pia waligawanyika katika makundi hayo matatu. Mwalimu Muganyizi alikuwa katika kundi la walimu wanamapinduzi.

Mgomo mkubwa wa Wanafunzi
Migongano kati ya makundi hayo mawili ya wanafunzi yalipelekea mgomo mkubwa wa wanafunzi mwaka 2004. Viogozi madikteta walikuwa wamempiga mwanafunzi mmoja na kumjeruhu vibaya sana, huku waking’oa ngozi ya kiganja cha mkono wa kulia. Kilichoumiza zaidi ni kuwa mwanafunzi yule alitakiwa kufanya mtihani wa majaribio (MOCK) wa kidato cha pili siku inayofuata. Wanafunzi waliingia katika mgomo na kuanza kurusha mawe katika ofisi kuu ya viongozi, huku madikteta wakiwemo ndani. Ni Mwalimu Muganyizi aliyeshirikiana na wanamapinduzi kutuliza urushaji wa mawe. Tulimwambia Muganyizi kuwa auambie uongozi wa shule, unaowalinda madikteta kuwa hatutaingia darasani, mpaka viongozi wale wafukuzwe shule.

Hivyo jioni ya siku ile kikaitishwa kikao cha viongozi, pamoja na Mwalimu mkuu msaidizi na Mwalimu Muganyizi. Cha kushangaza ni kuwa mkuu msaidizi alitugeuzia kibao wanamapinduzi na kusema kuwa tunataka kuchoma shule na ni sisi ndio tunaosababisha mgomo. Tulimwambia wazi kuwa mgomo anausababisha yeye na kundi lile la madikteta. Sisi jukumu letu ni kuhakikisha haki inatendeka. Alipojaribu kupindisha haki, na hata kumnyima mwanafunzi aliyejeruhiwa ruhusa ya kwenda hospitali, wanafunzi walikasirika na kuanza kurusha mawe. Kwa mara ya kwanza katika historia ya shule ile ulitokea mgomo mkubwa uliosababisha uharibifu mkubwa wa majengo na mali za shule, na hata kusababisha polisi kuingilia kati ili kutuliza vurugu.

Mapambano yanaendelea
Gharama za mgomo ule walizilipa wanafunzi wasio na hatia, ambao walifukuzwa shule. Wengine walisimamishwa masomo na kulipishwa faini ili kufidia uharibifu. Madikteta ambao ndio waliosababisha wanafunzi kufanya vurugu hawakuguswa.

Wanamapinduzi tulisakamwa, na hasa mimi niliyekuwa kiongozi wa kundi hilo, ambaye pia nilisingiziwa kuchochea wanafunzi kufanya uharibifu. Kama isingekuwa ujasiri wa walimu wanamapinduzi wakiongozwa na Mwalimu Muganyizi, ilikuwa tufukuzwe shule.

Japo ulisababisha uharibifu, mgomo ule ulikuwa mwanzo wa kipindi kipya. Madikteta walipunguza uonevu dhidi ya wanafunzi. Lakini baadhi yetu tuliendelea kusakamwa, huku mkuu msaidizi akitutamkia kuwa hatukupaswa kuwepo shuleni pale. Kwa kuongozwa na Mwalimu Muganyizi, tulipeleka malalamiko yetu kwa mkuu wa shule, marehemu Mwalimu Lutanjuka. Baadhi ya walimu waliokuwa wakitunyanyasa na kututisha walionywa na kutakiwa kuja kutuomba msamaha. Yupo mwalimu mmoja ambaye tulihakikisha kuwa anavuliwa nyadhifa zake za uongozi wa bweni na nidhamu.

Walimu madikteta wakiongozwa na mkuu msaidizi walikuwa wamemdanganya mkuu wa shule kuhusu chama cha wanafunzi wavukao ziwa, kilichoitwa Kahororo Overlakers’ Association (KOA) ambacho kilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kusaidia wanafunzi waliotoka mikoa ya mbali pale wanapopata shida, hasa katika gharama za matibabu, nauli na hata ada. Mimi nilikuwa mwenyekiti wa chama hicho, na Mwalimu Muganyizi ndiye aliyekuwa mlezi wetu. Walimu madikteta walimlisha sumu mkuu wa shule na kumfanya akifute. Kwa kushirikiana na Mwalimu Muganyizi tulikwenda mbele ya mkuu wa shule na kuhakikisha kuwa anabadili uamuzi wake. Aliubadili. Tukashinda. Walimu madikteta wakabaki wamepigwa butwaa.

Ualimu bila viboko
Yapo megi ya kusimulia juu ya mapambano tuliyofanya na Mwalimu Muganyizi. Yalikuwa ni mapambano ya kupinga uonevu, uporaji na dhuluma. Nje ya mapambano ya kimapinduzi, yeye alikuwa ni mfano mzuri wa kuigwa katika uongozi. Licha ya  mwili wake ulioshiba katika ujazo na urefu, pamoja na mazoezi ya viuongo aliyofanya, alikuwa mvivu wa kushika kiboko. Katika miaka mitatu tuliyokuwa pamoja sikuwahi kumwona ameshika fimbo, au kumchapa mwanafunzi. Kinywa chake chenye simulizi nyingi hakikuwa kikitoa amri za kiimla au makaripio ya ukali. Kwa ufupo, alikuwa ni mwalimu mwenye utu na aliyejiheshimu. Hii ilimjengea heshima kubwa miongoni mwa wanafunzi, ambao walimpenda na kumthamini.

Utumishi uliotukuka
Mwalimu Muganyizi alijitolea kuwatumikia wanyonge kwa moyo wake wote. Yeye, kama ilivyo kwa walimu wengine, alikuwa na familia kubwa (mke mmoja, watoto saba na wajukuu wanne) na ndugu wanaomtegemea. Malipo aliyopata mwisho wa mwezi, kama ilivyokuwa kwa walimu wengine, yalikuwaya kijungu jiko, na kwa kweli hayakutosha hata kuihudumia familia yake. Lakini uhafifu wa malipo hayo haukumfanya awachukie na kuwaadhibu watoto wa wakulima wasio na hatia. Hivyo, alitumia muda mwingi kutafuta maarifa katika vitabu, na kisha kuyahamishia maarifa hayo katika vichwa vya wanafunzi. Alitumia muda mwingi wa ziada kutufundisha na kutupatia mazoezi.

Katika fikra za Mwalimu Muganyizi, ukombozi wa pekee kwa wanyonge wa nchi hii utapatikana kwa kuwapa elimu bora watoto wao. Elimu bora ni zaidi ya kufundisha kanuni za hesabu na fizikia, bali kuwafungua macho wauone uonevu na unyonyaji unaofanywa na watawala, pamoja na kuwaongezea hasira ili wakapambane na unyonyaji huo. Mapambano dhidi ya udhalimu yanaanza katika jamii na taasisi uliyomo.

Pumzika kwa amani
Mwalimu Muganyizi hatunaye tena. Alikoma kufundisha fizikia na hesabu Jumatano 5 Machi 2014. Alianguka akiwa anatoka darasani kusimamia mtihani, na kukimbizwa hospitali ambako alikata roho baada ya muda mfupi. Amefariki tarehe ambayo wanyonge duniani kote walikuwa wakiadhimisha mwaka mmoja tangu kuondokewa na shujaa wa mapambano ya wanyonge, El Commandante Hugo Chavez, aliyekuwa rais wa Venezuela. Chavez alihakikisha kuwa utajiri wa nchi hiyo unawanufaisha watu wa tabaka la chini, ambao ndio wengi. Naam, Mwalimu Yohana J. Muganyizi naye alihakikisha kuwa maarifa yaliyomo kichwani mwake yanawanufaisha watoto wa wanyonge.

Twakuhakikishia Muganyizi,

Ulotufunda tutakuenzi,

Si kwa kununua mabenzi,

Au maghorofa ya Mbezi.

Tutawajali wanyonge,

Ambao ndio wengi.

Historia itakukumbuka,

Kwa utumishi uliotukuka.

Kwa amani, pumzika.

One thought on “Buriani Mwalimu Yohana J. Muganyizi: Bingwa wa Hisabati na Fizikia Aliyewajali Watoto Wa Wanyonge

 1. Kaka inauma sana,
  ni kama ninayaona,
  yote uloyasema,
  Nimekumbuka ya nyuma,
  Enzi tupo tunasoma
  Muganyizi ni mlima,
  Utakaokuwepo daima,
  mchana na siku nzima,
  Buriani wetu Mwalimu,
  Uliyetupa Timamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box