Changamoto ya mfumo wa serikali tatu: Kugharamia serikali ya muungano

Mada hii ni mawazo binafsi. Imeandaliwa kusaidia Mjadala wa Rasimu ya Katiba katika Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Imewasilishwa katika Mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania uliojadili kuhusu ‘Tafakuri na Maridhiano kuelekea Katiba Mpya’ na kufanyika Whitesands Hotel,. Dar es Salaam, kuanzia tarehe 12 hadi 13 Februari, 2014.

Na Prof. Ibrahim Haruna Lipumba

I. Utangulizi

Rasimu ya katiba Mpya imependekeza mfumo wa Muungano wa Shirikisho wenye serikali tatu; serikali ya Muungano, serikali ya Tanzania Bara na serikali ya Zanzibar. Katiba inaonesha kuwa mambo ya Muungano ni saba: Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Uraia na Uhamiaji; Sarafu na Benki Kuu; Mambo ya Nje; Usajili wa Vyama vya Siasa; na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
 
Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na Rasimu, Serikali ya Muungano haishughulikii sekta za uzalishaji na kwa hiyo haina vyanzo vya mapato ya kodi vya uhakika. Jaji Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, anaamini kuwa kwa kuorodhesha ushuru wa bidhaa kuwa jambo la Muungano, Tume imetatua tatizo la kugharamia serikali ya Muungano. Amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema kuwa “kama mfumo wa Serikali tatu utakubalika, Serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha.” Kwa heshima zote Tume imeshindwa kuelewa ugumu wa vyanzo vya mapato ikiwa tutakuwa na serikali ya Tanganyika na serikali ya Muungano.

II. Vyanzo vya Mapato ya Serikali ya Tanganyika Wakati Tunaungana 1964

Vyanzo vikuu vya mapato ya serikali ya Tanganyika wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana mwaka 1964 vilikuwa kodi ya mapato ya watu binafsi na kampuni (Income Tax), ushuru wa forodha (Custom Duty) na ushuru wa bidhaa (excise duty). Vyanzo hivyo vya mapato vilichangia wastani wa robo tatu ya mapato yote ya serikali ya Tanganyika. Robo iliyobakia ilichangiwa na kodi ya mali isiyohamishika (property tax), kodi nyingine na mapato mengine ya serikali.
 
Kodi ya mapato, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zilikusanywa Umoja wa Huduma za Pamoja wa Afrika Mashariki East African Common Service Organization asasi iliyochukua nafasi ya Tume Kuu ya Afrika Mashariki (East African High Commission) baada ya Tanganyika kupata uhuru.
 
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulianzishwa na wakoloni wa Kiingereza. Kenya na Uganda walikuwa na soko la pamoja na sarafu moja. Baada ya vita ya kwanza, washindi wa Ulaya wa vita hivyo waligawana makoloni ya Mjerumani. Ruanda-Urundi ikamegwa na kupewa Ubelgiji na Tanganyika ikachukuliwa na Uingereza na kuingizwa katika soko la pamoja na Bodi ya sarafu iliyojumuisha Kenya na Uganda.

Utaratibu rasmi wa huduma za pamoja wa Kenya, Tanganyika na Uganda ulianzishwa mwaka 1948 na kupewa jina la Tume Kuu ya Afrika Mashariki (East African High Commission (EAHC)). Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) ilitokana na mikutano ya Magavana wa Kiingereza wa Kenya, Tanganyika na Uganda waliokuwa wanakutana kuratibu masuala ya utawala na huduma za pamoja za Afrika Mashariki. Zanzibar ambayo ilikuwa ikishiriki katika baadhi ya huduma haikuwa mwanachama rasmi wa Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) kwa kuwa ilikuwa siyo “koloni” bali hifadhi (protectorate) ya Uingereza na haikuwa na Gavana bali alikuwepo Afisa Mkazi (Resident.) Haidhuru mamlaka ya Afisa Mkazi (Resident) hayakuwa tofauti sana na ya Gavana. Serikali ya Sultan iliachiwa mamlaka zaidi ya kuendesha mambo ya utawala ya Zanzibar. Afisa Mkazi (Resident) wa Zanzibar alikuwa akifanya kazi chini ya uongozi wa Gavana wa Kenya.
 
Chombo cha juu cha maamuzi cha Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) kilikuwa mkutano wa Magavana wa Kenya, Tanganyika na Uganda chini ya uenyekiti wa Gavana wa Kenya ambaye alikuwa Gavana Mwandamizi wa Afrika Mashariki.
 
Huduma za Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) zilikuwa katika maeneo matano;
a) Usafiri na mawasiliano
b) Ukusanyaji wa kodi za serikali
c) Uchumi na takwimu
d) Utafiti
e) Huduma nyingine maalum

Usafiri na mawasiliano

Huduma za usafiri zilitolewa na Shirika la Reli na Bandari la Afrika Mashariki (East African Railways and Harbours) lililosimamia huduma za reli na bandari. Huduma za posta na simu zilisimamiwa na Shirika la Posta na Simu (East African Post and Telecommunication). Huduma za usafiri wa anga zilitolewa na Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (East African Airways). Mashirika haya yalijiendesha yenyewe kwa kutegemea mapato ya tozo za huduma zao. Msaada wa Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) ulihitajika pale mashirika hayo yalipokuwa yanatekeleza miradi ya maendeleo iliyohitaji mikopo ili kuitekeleza. Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) ilichukua dhamana kwa mashirika haya ili kupata mikopo katika soko la fedha la Uingereza.
 
Huduma nyingine za usafiri na mawasiliano  ambazo hazikuweza kujigharamia kwa mapato ya tozo za huduma zao zilibidi zipewe fedha na Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC). Huduma hizo ni pamoja na mambo ya anga (civil aviation) na huduma za utabiri wa hali ya hewa (metereological services) ambazo ni za lazima kwa safari za ndege. Sehemu ya kodi iliyokusanywa toka makoloni matatu ilitengwa kuhudumia shughuli za Tume ya Afrika Mashariki (EAHC).

Huduma za kukusanya mapato

Huduma za kukusanya mapato zilikuwa chini ya idara mbili. Idara ya forodha na ushuru (Customs and Excise Department) na idara ya kodi ya mapato (Income Tax Department). Kila koloni lilitunga sheria za kodi zake za mapato na Idara ya kodi ya Mapato ilikusanya kodi na kukabidhi kwa serikali husika. Kiutendaji sera za kodi za mapato za makoloni yote matatu zilifanana.

Na Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
 
Ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa ulifanana kwa sababu makoloni yote matatu yalikuwa chini ya soko la pamoja na bidhaa nyingi zilizokuwa zinatozwa ushuru (excise duty) kama vile bia na sigara zilikuwa zinatengenezwa Kenya au kuagizwa toka nje.  Takwimu ya kiasi na thamani ya bidhaa zilizotumiwa katika kila nchi zilikusanywa ili kuelewa mgao wa mapato ya kodi kwa kila koloni.
 
Zanzibar ilikuwa na utaratibu wake wa kupata mapato ya serikali na yalitegemea zaidi kodi ya bidhaa (exercise duty) zinazouzwa nchi za nje na hasa karafuu.
 
Gharama za huduma nyingine zikiwemo za uchumi na takwimu, Utafiti wa kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, afya na viwanda ziligharamiwa na Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC).
 
Tanganyika ilipopata uhuru Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC) ambayo ilikuwa ikiongozwa na Magavana wa makoloni matatu ilibidi ibadilishwe jina na kuitwa Umoja wa Huduma za Pamoja wa Afrika Mashariki (East African Common Services Organization (EACSO)). Majukumu yake yalibakia yale yale ya Tume Kuu ya Afrika Mashariki (EAHC). Chombo cha juu cha maamuzi kilimuhusisha Waziri Mkuu wa Tanganyika na Mawaziri wa Kiafrika waliokuwa katika Baraza la mawaziri la Kenya na Uganda.
 
Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964, jambo la 10 katika orodha ya mambo ya Muungano likawa ni “Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini na kusimamiwa na Idara ya Forodha”  (Income Tax, Corporation Tax, Customs and Excise). Ukusanyaji wa kodi zote hizi ulikuwa chini ya Umoja wa Huduma za Pamoja wa Afrika Mashariki (EACSO) na ulichangia robo tatu ya mapato ya serikali kuu ya Tanganyika. Sababu muhimu ya Mwalimu Nyerere kuingiza robo tatu ya mapato ya Tanganyika kuwa jambo la Muungano ni kuwa mfumo wa muungano ulikuwa hauna serikali ya Tanganyika. Ilieleweka wazi vianzio vya mapato ya Tanganyika ndiyo kwa sehemu kubwa vitakagharamia mambo ya Muungano.

Mapato ya Serikali ya Tanganyika 1960-61

III. Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ibara ya 133 ya katiba ya sasa inaeleza kuwa “Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza akaunti maalum itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” na ambayo itakuwa ni sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.” Ibara hii haitekelezwi na kimsingi hakuna Akaunti ya Fedha za Pamoja inayogharamia mambo ya Muungano.
 
Katika kipindi chote cha Muungano, Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitenganishi vyanzo vya mapato na matumizi kwa utaratibu wa mambo ya Muungano na mambo ya Tanganyika. Ukweli ni kuwa katika mambo ya bajeti, tuna bajeti ya serikali moja inayoshughulikia mambo ya muungano na mambo ya Tanganyika kwa pamoja.
 
Bajeti ni nyenzo muhimu ya sera ya Serikali yeyote. Bajeti ni kielelezo au kioo cha mapato na matumizi kinachoonesha maeneo ambayo Serikali inayapa kipaumbele. Misingi mizuri ya bajeti ni pamoja na Serikali kukusanya mapato toka kwa walipa kodi kwa uadiifu na kupanga na kutumia mapato hayo kwa uangalifu katika maeneo yatakayotoa huduma bora kwa wananchi na kuchochea maendeleo.
 
Malengo ya uchumi mpana ni kukuza uchumi, matunda ya kukua kwa uchumi yawafikie wananchi wote, na uchumi usiyumbishwe kwa mfumko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni na thamani ya sarafu kuporomoka au kupanda sana. Uchumi unapoyumbishwa na mfumko mkubwa wa bei au thamani ya sarafu kubadilika badilika kwa kiasi kikubwa unapunguza motisha kwa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na biashara ndogo na za kati kuwekeza na kwa hiyo kukuza uchumi wa kuongeza ajira.
 
Ili uchumi usiyumbe ni muhimu kuwa na nidhamu katika sera za mapato na matumizi ya sekta ya fedha za umma.
 
Madhumuni ya sera bora ya matumizi ya fedha za umma ni kuwa na nidhamu katika matumizi (fiscal discipline), kupanga na kutumia fedha kufuatana na vipaumbele vya sera na kuwa na usimamizi mzuri wa matumizi haya siku hadi siku.
 
Usimamizi mzuri wa siku hadi siku unasisitiza kuwepo kwa tija katika matumizi ya Serikali. Gharama za kununua bidhaa na huduma ziwe za chini huku ukizingatia ubora wa bidhaa na huduma zenyewe. Matumizi ya Serikali yafanikishe malengo ya sera kwa mfano fedha zilizotengwa katika sekta ya elimu zifanikishe watoto wapate elimu iliyo bora.
 
Kuwepo kwa nidhamu katika mapato na matumizi kunategemea makadirio mazuri ya mapato na matumizi.
 
Bajeti isiyotabirika inahujumu vipaumbele vya sera na matokeo ya matumizi ya Serikali.
Bajeti ya Serikali ijumlishe mapato na matumizi yote ya Serikali bila kujali taratibu maalum za kuendesha baadhi ya miradi na programmu. Kwa ujumla mapato yote yakusanywe na matumizi yapangwa bila kujali chanzo cha mapato. Ikiwa kuna mahusiano ya karibu kati ya mapato na wanaonufaika na matumizi ya mapato hayo, hoja ya mapato husika  kulipia matumizi ya huduma inakubalika.
 
Maamuzi ya Serikali na viongozi ambayo yanahitaji matumizi ya fedha za Serikali katika mwaka wa bajeti au miaka ijayo yawekwe wazi na kuchambuliwa.
 
Utayarishaji wa bajeti uzingatie:-
i) Kufikia malengo ya uchumi mpana. Ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, akiba ya fedha za kigeni, thamani ya sarafu.
ii) Matumizi yagawiwe kulingana na malengo ya sera ya taifa.
iii) Kujenga mazingira ya utekelezaji mzuri wa bajeti.
iv) Uchambuzi wa kina wa mahitaji ya fedha na rasilimali nyingine ya mapendekezo ya bajeti na kuhakikisha kuwa bajeti ndiyo inayoshika hatamu katika mapato na matumizi ya Serikali.
 
Jambo linaloathiri sera, utayarishaji na utekelezaji wa bajeti bora ni uanzishaji wa sera na utamkaji wa ahadi katika majukwaa ya siasa ambao hauendani na vipaumbele vilivyotumiwa kuandaa bajeti.
 
Kwa kuwa chanzo cha mapato ya serikali ya Muungano na serikali ya Tanganyika ni kimoja kuna mantiki na tija ya kupanga vipaumbele vya matumizi ya serikali kwa pamoja. Kuongeza bajeti ya matumizi ya ulinzi ambalo ni jambo la Muungano kutamaanisha kupunguza matumizi ya elimu au afya ambalo siyo jambo la Muungano.
 
Mapendekezo ya mfumo wa serikali tatu katika muungano wa nchi mbili ambapo moja ni kubwa sana kuliko nyingine na ambayo ndiyo itakayogharamia serikali ya Muungano itaathiri utaratibu mzuri wa bajeti wa kukusanya mapato toka vianzio vyote na kuyagawa kwa matumizi kufuatana na vipaumbele. Vipaumbele vya serikali ya muungano vitakuwa mambo ya Muungano bila kujali sana vipaumbele vya mambo ya Tanganyika.
 
Mwalimu Nyerere alieleza mantiki ya kuamua kuwa na Muungano wa  serikali mbili kama ifuatavyo:

Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la serikali Tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye Serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya Shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika nchi zilizoungana basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.

Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zilikuwa ni Nchi Tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi Tatu zilizoungana kuwa Nchi Moja yenye muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni Nchi Moja yenye Serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali mbili za nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.

Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zan­zibar na ukubwa wa Tanganyika. Zan­zibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja Ungefanya ionekane kama Tangan­yika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe hata kwa makosa, kwanba tunaanzisha ubeberu mpya!

Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzi­bar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tan­ganyika ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tan­ganyika ingeendesha Serikali yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.

Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tan­ganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tan­ganyika.

Kwa hivyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na SerikaIi yake, itaoekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana. Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi.

Labda ni vizuri kukumbusha kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe nchi moja. Na wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katikati ya mazungumzo ya kutafuta uwezekano, wa kuungana. Kama jambo hilo, lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungelikuwa ni Shirikisho; au la Shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne, na Shirikisho la Nchi Nne zenye Serikali Tano.

Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika ya Mashariki zikiamua kuungana, na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili – ya Zanzibar na ya Tanganyika – kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar. Wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa Nchi Moja. kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.

Sensa ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Zanzibar ina watu 1,303,569 na Tanzania Bara ina watu 43,625,354. Huu ni uwiano wa watu wawili Zanzibar kwa kila watu 67 Tanzania Bara. Pato la taifa la Tanzania Bara mwaka 2011 linakadiriwa kuwa shilingi trilioni 37.5 na Pato la taifa la Zanzibar ni shilingi trilioni 1.2. Mapato yote ya serikali ya Zanzibar mwaka wa fedha wa 2011/12 yalikuwa shilingi bilioni 220 wakati mapato ya serikali ya Jamhuri ya Muungano yalikuwa shilingi trilioni 7.2 sawa na mara 33 ya mapato ya Zanzibar.

Hoja ya Mwalimu kuwa gharama za serikali ya tatu itabebwa na serikali ya Tanzania Bara bado ina uzito. Kuna tatizo la msingi la Muungano wa nchi mbili, moja ikiwa ndogo sana ukilinganisha na ya pili. Sehemu kubwa ya gharama ya Muungano inabidi ibebwe na nchi kubwa.

IV. Mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba

Tume ya jaji Warioba haikufanya uchambuzi wa kina wa mantiki ya kuingiza sehemu kubwa ya vyanzo vya mapato ya serikali ya Tanganyika kuwa jambo la muungano. Badala yake wametazama gharama za wizara zinazoshughulikia mambo ya Muungano na kutazama chanzo gani cha mapato kitakidhi gharama hizo na kukiainisha kuwa ni jambo la Muungano.
 
Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano haina vyanzo vya mapato ya kodi. Ibara ya 231 ya Rasimu ya Katiba imeeleza Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa: “(a) ushuru wa bidhaa; (b) mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na taasisi za Muungano; (c) mchango kutoka kwa Nchi Washirika; (d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano na e) mapato mengineyo”. Rasimu ya Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya kukusanya kodi. Jambo la saba la Muungano ni Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya Muungano hayalipi ushuru wa bidhaa. Biashara siyo jambo la Muungano kwa hiyo serikali za washirika zinaweza kujenga hoja kuwa ushuru wa forodha (Custom duty), kodi za ongezeko la thamani (Value Added Tax, (VAT)), ushuru wa bidhaa (excise duty), kodi ya mauzo (sales tax) haziwezi kuwa suala la Muungano. Katiba yenyewe inakinzana. Inawezekana suala la mamlaka ya kutoza kodi likawa mgogoro wa kwanza wa kikatiba ambao itabidi uamuliwe na mahakama.

Kodi ni chanzo cha mapato ya serikali lakini pia ni sera ya uchumi. Kwa mfano kulinda viwanda vya ndani serikali inaweza kuongeza ushuru wa forodha. Kupunguza gharama za kilimo, serikali inaweza kuondoa ushuru wa mbolea na pembejeo. Serikali za Washirika wa Muungano hawatakubali Serikali ya Muungano kutoza kodi katika maeneo ambayo siyo ya Muungano.
 
Rasimu ya Katiba haiko wazi kuhusu maana ya ushuru wa bidhaa. Kwa kiingereza ushuru wa bidhaa ni taxes on goods. Kwa tafsiri hii ushuru wa bidhaa (excise duty) unajumuisha ushuru wa forodha, kodi ya mauzo ya bidhaa, kodi ya ongezeko la thamani ya bidhaa, kodi ya mazao na kodi ya mauzo ya nje ya bidhaa. Nadhani Tume ya Jaji Warioba imetumia dhana ya ushuru wa bidhaa kuwa ni excise duty inayotozwa kwenye bidhaa kama vile sigara, bia, soda, pombe kali, bidhaa za petroli na bidhaa nyingine. Ushuru wa bidhaa (Excise duty) pia inaweza kutozwa kwenye huduma za simu, huduma za kuhamisha fedha, huduma za hoteli na migahawa na kadhalika. Hata hivyo Rasimu ya Katiba inazungumzia ushuru wa bidhaa na kwa hiyo ushuru wa huduma siyo jambo la Muungano.

Katika mahojiano na gazeti la Mwananchi la tarehe 8 Juni 2013, Jaji Warioba amenukuliwa akieleza
“Katika Katiba ya sasa mapato ya Muungano yanatokana na vyanzo vitatu, Kodi ya Mapato (income tax), Ushuru wa Forodha (custom duty) pamoja na ushuru wa bidhaa (excise duty).

Kodi ya mapato ndiyo inatoa fedha nyingi sana na inafuatiwa na kodi ya ushuru wa bidhaa na ushuru wa forodha. Kutokana na hesabu tulizopiga, tumeona matumizi katika Serikali ya Muungano yapo katika sehemu mbili, moja ni yale ya Muungano na ya pili ni yale ya Tanganyika ambayo yanachukua fedha nyingi.

Mwaka 2010/2011 mapato ya kodi ya mapato yalikuwa Sh2 trilioni na mapato ya ushuru wa bidhaa yalikuwa Sh1trilioni na mapato ya ushuru wa forodha yalikuwa Sh600 bilioni.

Ni kwamba matumizi ya mambo ya Muungano yalikuwa chini ya Sh1trilioni, ndiyo maana tumechagua ushuru wa bidhaa, kwani tukipata fedha zile zitaweza kumaliza matumizi yote ya Serikali ya Muungano.

Hivyo basi kama tukiendelea na utaratibu huu wa Serikali tatu, ni wazi kwamba Serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha kwa kuwa itakuwa nazo za kutosha, Serikali zitakazokopa ni hizo mbili.

Tulikuwa tukijua wazi kuwa Serikali ya Muungano lazima iwe na chanzo cha uhakika cha fedha, na kwa utaratibu huu Serikali hizo tatu ndizo zitakazokubaliana jinsi ya kukusanya fedha hizo.”

Jedwali na. 2 linaonesha ukusanyaji wa mapato ya Mamlaka ya Kodi (TRA) ya mwaka 2010/11. Jumla ya makusanyo yote ya TRA yalikuwa shilingi bilioni 5366.7. Mapato ya TRA yaliyokusanywa Zanzibar yalikuwa shilingi bilioni 76.4 sawa na asilimia 1.4 ya mapato yote. Mapato ya exercises duty (ushuru wa bidhaa na huduma) ni shilingi bilioni 974.1. Exercises duty iliyokusanywa Zanzibar ambayo yote ilitokana na bidhaa kutoka nje ilikuwa shilingi bilioni 6.1 sawa na asilimi 0.6 ya ukusanyaji wa excise duty.

Tume haikuzingatia kuwa matumizi ya mambo ya Muungano hivi sasa yanaandaliwa kwa kuzingatia matumizi yanayohitajika katika mambo yasiyokuwa ya Muungano kama vile elimu, afya na miundombinu. Katika mfumo wa serikali tatu, serikali ya Muungano itapanga bajeti yake kwa kuzingatia mambo ya Muungano. Mathalani serikali ya Muungano ikihitaji kuimarisha ulinzi wa anga na bahari kwa kununua ndege za kivita na manoari shilingi trilioni 1 (dola milioni 625) ni fedha kidogo sana.

Ukusanyaji wa Mapato wa Mamlaka ya Kodi TRA 2010-11

Kwa muda mrefu bajeti ya serikali ya Muungano imeendelea kutegemea wafadhili wa nje bila ya kuweka mkakati wa kujikwamua toka kuwa nchi tegemezi. Theluthi moja ya matumizi ya serikali yanategemea mikopo na misaada kutoka nje. Katika miaka yote mikopo na misaada ya nje ni zaidi ya matumizi ya maendeleo. Kimsingi Serikali haitoi fedha yeyote kugharamia matumizi ya maendeleo na inategemea wafadhili kulipia sehemu ya matumizi ya kawaida. Jedwali namba 3 linaonesha mapato ya ndani yamegharamia asilimia 57-70 ya matumizi ya serikali kati ya 2006/07 na 2011/12.

Toka mwaka wa fedha wa 1996/97 utaratibu wa utekelezaji wa bajeti umekuwa wa fedha taslim (cash budget). Bunge linapitisha bajeti lakini utekelezaji wake unategemea fedha zinazokusanywa na mamlaka ya kodi na fedha za misaada zilizowasilishwa serikalini. Wizara, Idara na taasisi nyingi za serikali hazipati fedha zilizotengwa katika bajeti zao kwa sababu mapato yaliyokusanywa ni madogo kuliko matumizi yaliyopangwa kwenye bajeti. Bajeti ya maendeleo ndiyo inayoathirika zaidi. Asasi za serikali zisizokuwa na nguvu za kisiasa pia zinapata matatizo makubwa ya kutekeleza majukumu yake. Kwa mfano Mamlaka ya Vitambulisho vya Tafia (NIDA) iko nyuma sana katika kukamilisha kazi yake kwa sababu haikutengewa fedha za kutosha na hata walichotengewa wamepewa kiasi kidogo sana. Serikali inapaswa kuwa na nidhamu na kuandaa bajeti inayotekelezeka na kuachana na Cash Budget.

Athari za Cash Budget kwa Serikali ya Shirikisho zitakuwa kubwa zaidi ikiwa serikali hiyo haitasimamia ukusanyaji wa mapato yake.

Mapato ya Serikali ya Muungano

Mapato na Matumizi (shilingi milioni)

Rasimu ya Katiba haielezi utaratibu utakaotumiwa na Serikali ya Muungano kukusanya mapato yake. Mamlaka ya mapato haijatajwa ndani ya katiba. Serikali itakayopanga viwango vya ushuru wa bidhaa haijatajwa. Kwa kuwa suala la kodi ni la mapato na la sera, Serikali za Nchi Washirika zinaweza kudai kuwa uzalishaji wa bidhaa siyo jambo la Muungano na kwa hiyo Serikali za Nchi Washirika ndizo zinazostahiki kupanga ushuru wa bidhaa. Sera za kodi zinahitaji uratibu wa karibu. Kuwa na mamlaka mbili zinazopanga kodi mbalimbali za bidhaa kunaweza kuathiri maendeleo ya sekta za uchumi. Bidhaa zinatozwa kodi (excise duty) na Kodi ya Thamani (VAT). Serikali ya Muungano inaweza kuamua kuongeza kodi ya bidhaa (excise duty) na Serikali za Nchi Washirika zikaongeza Kodi ya Thamani (VAT) na kuwabebesha wananchi mzigo mkubwa wa kodi.
 
Suala la fedha za serikali ni zito na linahitaji lieleweke vizuri. Kwa tafsiri ya Excise Duty iliyomo katika Hati ya Muungano, Chanzo cha Mapato kilichoainishwa katika Rasimu ya Katiba hakiwezi kukidhi matumizi ya sasa ya Wizara, Idara, Tume na Taasisi nyingine za Muungano zinazotajwa katika Rasimu hiyo.
 
Jedwali Na. 5 linaainisha matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya baadhi ya kasma (vote) ambazo zitakuwa za serikali ya Muungano kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba. Kasma za Mahakama za Muungano, Bunge la Muungano na Tume nyingi ambazo zimependekezwa ndani ya Katiba hazijaainishwa katika jedwali hili. Makadirio haya ni madogo kuliko hali halisi itakavyokuwa kwenye bajeti ya Shirikisho kama itakavyoandaliwa na serikali ya Shirikisho.

Matumizi ya Kasma (Vote) za Muungano 2011-12 (shilingi milioni)

Kasma za matumizi zilizoainishwa katika Jedwali namba 5 zimo katika mambo ya Muungano yaliyopendekezwa ndani ya Rasimu ya Katiba Mpya. Katika mwaka 2011/12 matumizi ya ‘vote’ hizo yalikuwa shilingi trilioni 1.56 wakati mapato ya ushuru wa bidhaa (excise duty) yalikuwa shilingi bilioni 721.3 sawa na asilimia 46. 3 ya matumizi ya kasma za Muungano. Ikiwa serikali ya Muungano itaamua kujenga jeshi imara la anga (Air Force) na jeshi la Majini (Navy), ndege za kivita na manoari zina gharama kubwa. Ushuru wa bidhaa katika mfumo wa sasa hauwezi kutosha kulipia gharama hizo.

Ukijumuisha masuala ya nchi za nje, polisi, uhamiaji na mambo mengine ya Muungano, serikali ya Muungano itakuwa na matatizo makubwa ya fedha ikiwa itategemea ushuru wa bidhaa kama chanzo kikuu cha mapato ya serikali kinyume na Jaji Warioba anavyoeleza.

IV. Kugharamia Serikali ya Muungano

Ikiwa serikali ya Muungano haitashughulikia masuala ya maendeleo ya uchumi isipokuwa masuala ya benki ni vigumu kukubali mantiki ya serikali hiyo kutoza kodi. Katiba haina mwongozo wowote wa michango ya Nchi Washirika.
 
Marekani ni Shirikisho la majimbo (states) 50. Kila jimbo lina serikali yake na kuna serikali ya Shirikisho ambayo ndiyo yenye nguvu za Kiuchumi. Serikali ya Shirikisho la Marekani inategemea vyanzo vitano vya mapato: 1) kodi ya mapato ya kila mtu (individual income tax), 2) kodi ya ajira (payroll tax) kuchangia gharama ya hifadhi ya jamii, 3) kodi ya mapato ya kampuni, 4) ushuru wa bidhaa (excise duty)  kwenye bidhaa kama vile sigara, pombe, petroli na huduma za usafiri wa ndege, 5) ushuru wa forodha (Custom duty).
 
Serikali za majimbo zinategemea zaidi kodi ya mauzo (sales tax) na kodi ya nyumba (property tax)
 
Kodi ya mapato ya kila mtu ndiyo chanzo kikubwa cha mapato ya serikali ya Shirikisho la Marekani na inachangia karibu nusu ya mapato yote ya serikali. Serikali ya Marekani ina majukumu ya ulinzi, mambo ya nje, ujenzi na ukarabati wa baadhi ya miundombinu hasa barabara zinazounganisha majimbo, hifadhi ya jamii na utengamavu wa uchumi mpana.
 
Ni vigumu kwa mfumo wa shirikisho wa Tanzania kujifunza lolote kutoka vyanzo vya mapato vya serikali ya Shirikisho ya Marekani au shirikisho lingine kwa sababu Shirikisho letu ni la nchi mbili, moja kubwa na nyingine ndogo. Rasimu ya Katiba haijaipa serikali ya Muungano jukumu la kusimamia na kukuza uchumi.
 
Kwa sababu ya uzoefu wa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” na Tume ya pamoja ya Fedha, Rasimu ya Katiba haina pendekezo la kuwepo kwa chombo kinachoshirikisha serikali tatu kujadili na kukubaliana mgao wa mapato ya serikali za washirika kugharamia serikali ya Muungano. Hata hivyo ni vyema mapato ya kugharamia serikali ya Muungano yakachangiwa na mapato ya serikali mbili. Katiba itamke wazi serikali za washirika zitachangia sehemu ya mapato yao yote kwenye serikali ya Muungano. Ili kuzuia migongano ni vyema tukafikia mwafaka wa asilimia ngapi ya  mapato ya serikali yaende kwenye shughuli za Muungano. Kwa mfano Katiba inaweza kutamka kuwa kiasi kisichopungua asilimia 20 ya mapato yote ya serikali za Washirika yatawasilishwa katika mfuko wa serikali ya Muungano kwa kadri mapato hayo yanavyokusanywa. Izingatiwe kuwa kwa utaratibu huu bado mshirika mwenye uchumi mkubwa ndiye atakayechangia sehemu kubwa ya gharama za Muungano. Uamuzi wa kufikia kiwango hicho ulipaswa utokane na utafiti wa gharama za mambo ya Muungano ukilinganisha mambo yasiyo ya Muungano.
 
Kutaja asilimia ndani ya Katiba inaweza kuonekana kuwa ni utaratibu usionyumbulika lakini, ndiyo pekee utakaolinda serikali ya Muungano iwe na mapato ya uhakika. Isitoshe hali ya uchumi inaweza kubadilika. Ikiwa Serikali za Nchi Washirika zitapata mapato makubwa kutoka sekta ya maliasili kama vile gesi, petroli au madini ambayo siyo mambo ya Muungano, mapato ya serikali ya Muungano nayo yataongezeka.

Taasisi ya kukusanya kodi muhimu ikiwa ni pamoja na kodi ya mapato, kodi ya forodha, ushuru wa bidhaa na huduma na kodi ya ongezeko la thamani inaweza kuwa ya Muungano lakini sera za kodi zikaamuliwa na kila serikali baada ya kushauriana. Wakati wa ukoloni na miaka ya awali ya uhuru kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Idara ya forodha na ushuru (Customs and Exercise Department) na idara ya kodi ya mapato (Income Tax Department) ilikusanya kodi katika nchi zote za Afrika Mashariki na kuwasilisha mapato husika kwa kila nchi haidhuru kila nchi iliweza kupanga kodi zake.

Fedha fedheha. Serikali za Nchi Washirika zinaweza kudanganya mapato wanayokusanya. Katiba itamke kuwa Bunge la Muungano litatunga sheria ya kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa sehemu yake ya mapato yanayokusanywa na serikali za Nchi Washirika yanawakilishwa kwenye mfuko wa Serikali ya Muungano.

Katiba inaweza kutaja kuwepo kwa Tume ya Pamoja ya Fedha itakayokuwa na jukumu la kupitia mahitaji ya fedha kwa shughuli za Muungano ukilinganisha na mapato ya washirika wa Muungano na kutoa mapendekezo kama kuna sababu za kuongeza asilimia ya mapato yanayopelekwa kwenye serikali ya Muungano. Hata hivyo kwa uzoefu tulionao haitakuwa rahisi kwa Tume ya Pamoja ya Fedha kuweza kuifanya kazi hii na kuafikiana na ndiyo maana naona bora mchango wa asilimia ya mapato utajwe ndani ya Katiba. Asilimia ngapi itakidhi mahitaji ya Muungano ni suala linalohitaji utafiti na uchambuzi wa kina.

V. Hitimisho
 
Tanganyika na Zanzibar zilipoungana, jambo la 10 katika orodha ya Muungano lilikuwa ni “Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini na kusimamiwa na Idara ya Forodha”. Vyanzo hivi vilichangia robo tatu ya mapato ya serikali kuu ya Tanganyika. Sababu muhimu ya Mwalimu Nyerere kuingiza robo tatu ya mapato ya Tanganyika kuwa jambo la Muungano ni kuwa mfumo wa Muungano ulikuwa hauna serikali ya Tanganyika. Ilieleweka wazi vianzio vya mapato ya Tanganyika ndiyo kwa sehemu kubwa vitakagharamia mambo ya Muungano.
 
Katiba ya sasa imeeleza kuwepo kwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.” Ibara hii haitekelezwi na kimsingi hakuna Akaunti ya Fedha za Pamoja inayogharamia mambo ya Muungano.
 
Katika kipindi chote cha Muungano, Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitenganishi vyanzo vya mapato na matumizi kwa utaratibu wa mambo ya Muungano na mambo ya Tanganyika. Ukweli ni kuwa katika mambo ya bajeti, tuna bajeti ya serikali moja inayoshughulikia mambo ya muungano na mambo ya Tanganyika kwa pamoja.
 
Bajeti ya Serikali ijumlishe mapato na matumizi yote ya Serikali bila kujali taratibu maalum za kuendesha baadhi ya miradi na programmu. Kwa ujumla mapato yote yakusanywe na matumizi kupangwa bila kujali chanzo cha mapato.
 
Mapendekezo ya mfumo wa serikali tatu katika muungano wa nchi mbili ambapo moja ni kubwa sana kuliko nyingine na ambayo ndiyo itakayogharamia serikali ya Muungano itaathiri utaratibu mzuri wa bajeti wa kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote na kuyagawa kwa matumizi kufuatana na vipaumbele. Vipaumbele vya Serikali ya Muungano vitakuwa mambo ya Muungano bila kujali sana vipaumbele vya mambo ya Tanganyika.
 
Kuna tatizo la msingi la Muungano wa nchi mbili, moja ikiwa ndogo sana ukilinganisha na ya pili. Sehemu kubwa ya gharama ya Muungano inabidi ibebwe na vyanzo vya mapato ya nchi kubwa.

Tume ya Jaji Warioba haikufanya uchambuzi wa kina na kubaini kuwa mfumo wa serikali ndiyo msingi wa mantiki ya kuingiza sehemu kubwa ya vyanzo vya mapato ya serikali ya Tanganyika kuwa jambo la Muungano. Msingi huu ukiondolewa, utaratibu wa kugharamia serikali ya Muungano unahitaji kufikiriwa kwa makini la sivyo serikali ya Muungano itakuwa haina vyanzo vya mapato vya uhakika.

Ukizingatia mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano haina vyanzo vya mapato ya kodi kwa sababu haitasimamia sekta za uzalishaji. Rasimu ya Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya kukusanya kodi.

Kodi ni chanzo cha mapato ya serikali lakini pia ni sera ya uchumi yenye athari katika sekta za uzalishaji. Kwa kuwa serikali ya Muungano haisimamii sekta za uzalishaji hakuna mantiki na tija ya serikali hiyo kusimamia sera za kodi.

Rasimu ya Katiba haiko wazi kuhusu maana ya ushuru wa bidhaa lakini inaelekea wanamaanisha excise duty na siyo kodi ya bidhaa (taxes on goods). Inaelekea Tume imekadiria gharama za mambo ya Muungano kwa hivi sasa siyo zaidi ya shilingi trilioni 1.

Tukitazama bajeti ya 2011/12 kasma za baadhi ya mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Rasimu ya Katiba yalitumia shilingi trilioni 1.56 wakati mapato ya excise duty ni shilingi bilioni 413.2 sawa na asilimia 26.5 ya matumizi. Ni wazi ushuru wa bidhaa kwa tafsiri ya excise duty hauwezi kugharamia serikali ya Muungano.

Ni vyema mapato ya kugharamia serikali ya Muungano yakachangiwa na mapato ya serikali mbili. Katiba itamke wazi serikali za washirika zitachangia sehemu ya mapato yao yote kwenye serikali ya Muungano. Kuzuia migongano ni vyema tukafikia mwafaka wa asilimia ngapi ya  mapato ya serikali yaende kwenye shughuli za Muungano. Kwa mfano, Katiba inaweza kutamka kuwa kiasi kisichopungua asilimia 20 ya mapato yote ya Serikali za Nchi Washirika yatawasilishwa katika mfuko wa Serikali ya Muungano kwa kadri mapato hayo yanavyokusanywa. Mamlaka ya kukusanya mapato inaweza kuwa ya Muungano na ikakusanya mapato na kuyawasilisha kwa Serikali za Nchi Washirika na Serikali ya Muungano kwa uwiano uliokubaliwa.

Katiba itamke kuwa Bunge la Muungano litatunga sheria ya kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa sehemu yake ya mapato yanayokusanywa na Serikali za Nchi Washirika yanawasilishwa kwenye mfuko wa Serikali ya Muungano. Asilimia ngapi itakidhi mahitaji ya Muungano ni suala linalohitaji utafiti na uchambuzi wa kina.

9 thoughts on “Changamoto ya mfumo wa serikali tatu: Kugharamia serikali ya muungano

 1. Namshukuru na kumpongeza sana Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa mchango wenye manufaa makubwa aliotoa kuhusu ugumu kwenye kufanikisha makusanyo kwa ajili ya kugharamia bajeti za serikali ya Muungano Tanzania chini ya mfumo wa serikali tatu.
  Hata hivyo ushauri kwamba itabidi kila nchi mshirika ichangie kiasi sawa cha mapato yake yote kwa ajili ya kugharamia serikali ya Muungano huenda ukawa vigumu kukubalika kutokana na kwamba Serikali ya Muungano siyo chimbuko kuu la mapato yote kwenye nchi washirika na bajeti ya Muungano haigharamii nchi washirika nusu kwa nusu au kuendana na viwango vya uchangiaji kutoka kwa nchi washirika.
  Ushauri hautoi haki pale unapomtaka mshirika mwenye juhudi zaidi kwenye kukuza mapato yake achangie zaidi ya yule mshirika mwenye juhudi ndogo kwenye kukuza yake.
  Ningeshauri nchi washirika zichangie bajeti ya Muungano kuendana na idadi zake za watu na ukubwa wa maeneo yake. Nchi mshirika kubwa na/au yenye watu wengi zaidi ichangie zaidi kuliko ile ndogo na/au yenye watu wachache zaidi.
  Uko uwezekano mkubwa wa Zanzibar kuweza kupata mapato makubwa zaidi ya Tanganyika kutokana na juhudi kubwa ya kukuza mapato yake chini ya uongozi mzuri na hata kufanana kimapato na nchi kama Singapore. Kwanini itakapokuwa hivyo Zanzibar itakiwe ichangie kiasi kikubwa zaidi cha bajeti ya Muungano kuliko Tanganyika itakachochangia!?

 2. Profesa Lipumba katika makala haya amechambua kwa undani na kwa ustadi mkubwa tatizo sugu la mapato, matumizi na gharama za serikali ya muungano katika Rasimu ya Tume inayopendekeza serikali tatu. Sitarudia, isipokuwa ningependa nisisitize yafuatayo:1. Chanzo kikubwa cha mapato ya serikali kupita vyote vingine ni kodi ya mapato (income tax) wanayotozwa watu binafsi na mashirika makubwa. Na katika muundo wa muungano wa serikali mbili uliyopo, chanzo hiki kilikua jambo la muungano. Kwa hivyo, anavyoeleza Lipumba, kodi hii ilikuwa inakusanywa na serikali ya muungano, amabyo pia ilikuwa inapanga bajeti yake na kufanya matumizi bila kujali kwamba matumizi haya ni kwa ajili ya jambo la muungano au kwa jambo la Tanzania Bara. Hii pia iliwezesha serikali ya muungano kumudu hali ya dharura, k.m. vita au tishio kutoka nje, kwa kurekebisha kasma na kuhakikisha kwamba fedha za kumudu hali ya hatari zinapatika kwa haraka na kwa wakati. 2. Chini ya Rasimu ya Tume, chanzo hiki sio jambo la muungano. Vyanzo vikuu vya mapato vya serikali ya muungano ni viwili: 1) ushuru wa bidhaa; na 2) mchango wa washirika. Ukweli huu unaibua masuali matatu muhimu yasiyoepukika:a) Kiasi cha mchango kutoka washirika hakiko wazi katika Rasimu. Kwa vyovyote vile, Bara ndio itakuwa mchangiaji mkubwa. Na kwa kuwa, taasisi na vyombo vya kukusanya kodi sio jambo la muungano, watakavyo kusanya kodi ni vyombo vya washirika na baadai kuwasilisha kwa serikali ya muungano. Hii ina maana kwamba serikali ya muungano itakuwa tegemezi, na kama, washirika, hususun, Bara, haikuwasilisha mchango wake kikamilifu na kwa wakati, uendeshaji wa serikali ya muungano wenyewe unakwama. Mbaya zaidi, ikitokea hali ya hatari na serikali ya muungano inahitaji kuandaa mara moja, kupeleka jeshi mipakani (kwa mfano kusini, ziwa la Nyasa), haina uwezo kufanya marekebisho ya kasma harakaharaka na kuhakikisha kwamba jeshi linapata fedha za kutosha kumudu usafiri, ununuaji wa zana ya vita n.k. Ulinzi wa nchi wenyewe unawekwa njia mpanda, rehani! b) Prof. Lipumba anaonyesha kwa takwimu na hoja kwamba ushuru wa bidhaa hautoshelezi kabisa kwa matumizi muhimu ya serikali ya muungano. Na haina uwezo wa kuchukuwa mikopo kwa sababu njia kuu za uzalishaji (ambayo pia ni vyanzo vikuu vya kodi/mapato ya serikali) haziko chini ya serikali ya muungano. Tukipenda, tusipenda, maana yake halisi ni kwamba serikali ya muungano haikopesheki!c) Prof. Lipumba, kwa hoja zisizopingika, anaonyesha kwamba huwezi kamwe kutenganisha suala la kodi/mapato na matumizi ya serikali kutoka sera za uzalishaji, uchumi, fedha na maendeleo. Lakini, chini ya Rasimu ya Tume, mambo haya sio mambo ya muungano; kwa hivyo, serikali ya muungano haihusiki kabisa na sera hizi wala mwelekeo wa maendeleo. Upangaji wa kodi, kwa mfano ushuru wa bidhaa, bila kujali sera za uchumi, fedha (fiscal policies), na mwelekeo wa maendeleo, una madhara mengi, pamoja na athari za kisiasa. Mfano mmoja tu mepesi. Serikali ya muungano, kwa lengo la kupata mapato, inaweka ushuru mkubwa tu kwenye mafuta. Bei za mafuta zinapanda, gharama za usafiri wa watu na bidhaa na uzalishaji unapanda. Wananchi wanalalamika, wanafurika mitaani na maandamono, wenye daladala wanagoma – haya, nani atakayeadhirika kisiasa, sio serikali ya muungano, bali ni serikali ya Tanganyika. Waandamaji hawatamgomea rais wa muungano; watamlalamikia rais wa Tanganyika. Kutokana na shinikizo na ili kuwatuliza wananchi wake, rais wa Tanganyika anafuta hizi kodi. Serikali ya muungano inakosa mapato; it comes to a standstill! Kuna constitutional crisis, katiba imevunjwa, haitekelezeki; itakuwaje, kama sio hatua ya kwanza ya kuvunja muungano?Kwa kuhitimisha, Prof. Lipumba anasema kwamba Tume ya Jaji Warioba hayakufikiria kwa maakini masuala haya; majawabu ya juujuu hayafai. Anapendekeza, kwa uelewa wangu wa hitimisho yake, kwamba sera za uchumi, uzalishaji, fedha, na maendeleo na vyombo vya ukusanyaji kodi, viwekwe mikononi mwa serikali ya muungano, yawe mambo ya muungano; kwa hivyo, orodha ya muungano iongezeke. Tunajuwa sote, pamoja na Lipumba, kwamba hili haliwezi kukubalika na washirika, pamoja na Tanzania Bara. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba rasimu ya Tume ILIVYO haitekelezeki.HITIMISHO yangu, kutokana na hoja za Profesa Lipumba, ni:1) Ama mambo mengi muhimu – sera za uchumi, fedha, maendeleo, uzalishaji, na vyombo vya ukusanyaji wa kodi – yawekwe katika orodha ya muungano, ambayo haitakubalika; au2) Turudi kwenye mfumo wa serikali mbili lakini uliyobuniwa upya kutokana na hali halisi na historia yetu; au3) Tupitishe Rasimu kama ilivyo tukijua kwamba mwisho wa siku haitadumu na kuna uwezekano mkubwa wa muungano kuvunjika, tena, labda, sio kwa amani.Kwa hivyo, kwa maana na mantiki hayo, hakuna tofauti kati ya wale wanaotaka muungano wa mkataba na wale wanaoshabikia muungano wa serikali tatu ilivyopendekzwa na Tume; zote mbili ni njia kuelekea kwenye kuvunja muungano. Siamini kwamba, msomi maakini kama Prof. Lipumba, hatambuwi uwezekano huu, au kama, huu. Lakini, kama tunavyofahamu, KISIASA, Lipumba ni mshabiki wa rasimu ya Tume ya serikali tatu. Swali langu linalonikera: inawezekanaje, kuwa na misimamo hii miwili, ya KISOMI na ya KISIASA, ambayo yanapingana moja kwa moja, katika mtu mmoja huyohuyo?! Bila shaka, Lipumba amevaa kofia mbili, ya msomi na mwenyekiti wa CUF. Lakini, kichwa ni kilekile … …. I

  • mi cdhan mtu akitoa mafanikio kisha akatoa changamoto za kitu husika ati ni mfuasi wa vitu viwili tofauti! isipokuwa hizo ni changamoto zinazotakiwa kuangaliwa ili kufikia serikal tatu ambazo matatizo yake si mengi kama mfumo wa serikal mbili

 3. Nimepitia kwa haraka haraka Makala ya Prof. Lipumba na Maoni ya Prof. Shivji. Ninashawishika kukubaliana na Prof. Shivji kuwa hitimisho la uchambuzi wa Prof. Lipumba lingekuwa, kwa muundo wa muungano unaopendekezwa na Rasimu muungano hautasimama. Ni jambo lisilowezekana. aelezo niliyoyasoma katika gazeti la Tanzania Leo, ambamo Prof . Humphrey Mosha anadokeza kuwa muungano wa Serikali tatu hauwezekani, na hoja yake ni kwamba Zanzibar haiwezi kubeba gharama za Muungano. Prof. Humphrey Mosha, ambaye pamoja na mambo mengine, anabainisha kuwa kama toka kuundwa kwa Muungano Zanzibar imewahi kuchangia mara tatu tu gharama hizo. Kwa habari zaidi soma Tanzania Leo hapa:
  http://habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/22623-kwa-nini-serikali-2-haziepukiki-uchumi-zanzibar-unategemea-bara

 4. Nadhani haitakuwa sahihi hata kidogo kusema eti Zanzibar haiwezi kubeba gharama za Muungano kwa vile tu tokea Muungano uundwe Zanzibar imewahi kuchangia gharama za kuwepo kwake kwenye Muungano mara tatu tu. Sahihi ni kusema kwamba kasoro kwenye Muungano na Katiba yake chini ya mfumo wa serikali mbili ndizo zilizotoa fursa kwa Zanzibar kuweza kuendelea kuwepo kwenye Muungano pasipo kulipia gharama za uwepo wake, huku Tanganyika ikilazimika kubeba gharama zote za Muungano. Kusema Zanzibar haiwezi kulipia gharama za uwepo wake kwenye Muungano ni sawa na kusema kwamba Zanzibar haina uwezo wa kujiendesha kama nchi kwa sababu kama imeshindwa kabisa kuchangia kiasi chake kidogo cha gharama kwenye miundo mbinu na huduma za Muungano kama kwenye mambo ya Ulinzi na nchi za nje, basi haitaweza kabisa kugharamia kujijengea na kujiendeshea miundo mbinu yake binafsi kwa gharama kubwa zaidi kama kwenye Mambo ya Ulinzi na nchi za nje. Muungano umeipunguzia sana Zanzibar gharama za kujijengea na kujiendeshea kwa gharama kubwa zaidi taasisi zake yenyewe kama kwenye Mambo ya Ulinzi na nchi za nje.
  Faida kubwa zaidi kuliko nyingine zote za kuwepo Muungano ni ile itokanayo na kuwapunguzia washirika (hasa Zanzibar) mzigo mkubwa wa gharama za kujijengea na kujiendeshea taasisi zake binafsi, muhimu na za gharama kubwa kama kwenye mambo ya ulinzi na nchi za nje.
  Naamini kabisa kwamba muundo wa serikali tatu uliopendekezwa chini ya Katiba ya Muungano madhubuti ndiyo haswa utakaoweza kuwajibisha nchi zote washirika zichangie kiasi chao stahili cha gharama za Muungano na kwa wakati unaotakiwa. Itakuwa haki kabisa ikipangwa washirika wachangie kuendana na idadi zao za watu. Kwa mfano, kwa idadi ya watanzania iliyojumuisha watanganyika 43,625,354 (2012) na wazanzibari 1,303,569 (2012) ilibidi Tanganyika ichangie 97 % na Zanzibar ichangie 3 % ya bajeti ya Muungano kwa mwaka 2012. Mgawanyo wa fursa kama ajira kwenye taasisi za Muungano ulibidi pia uzingatie idadi za watu: 97 % kwa watanganyika na 3 % kwa wazanzibari.

  • Tatizo la mapato na matumizi ya serikali ya Muungano haliwezi kutatuliwa tu kwa kuweka kiwango cha mchango wa kila serikali au vifungu vya katiba vya kuwabana wachangiaji. Na hata kama kiwango cha michango kitabainishwa kikatiba, lazima mambo mengi zaidi yazingatiwe na siyo tu kutumia kigezo cha Idadi ya Watu. Profesa Lipumba amebainisha kwa usahihi kwamba eneo hili la gharama za Muungano ni mtambuka na linagusa masuala nyeti ya kisiasa na kiuchumi (Ulinzi, Usalama, maendeleo ya kijamii, ukusanyaji wa mapato, mipango na bajeti n.k). Amebainisha pia kwamba ili kuweza kupata ufumbuzi madhubuti wa tatizo hili, lazima utafiti ufanyike na uchambuzi wake ujadiliwe. Hili halijafanyika kwa uwazi na kwa kina Ndiyo, zipo tafiti kadhaa kuhusu jambo hili lakini matokeo ya tafiti hizo hayajadiliwa kwa kina. Tayari tuna rasimu ambayo iko kimya katika masuala na maswali mengi yaliyoibuliwa na wachumi wa mrengo wa kulia na kushoto. Tunaendelea kuyajadili masuala hayo lakini tuelewe kwamba muda ndio huo unatutupa mkono na wanasisasa wetu wana haraka ya kupata katiba kabla ya uchaguzi ujao. Kama suala la gharama, kwa mujibu wa nukuu ya Mwalimu iliyomo kwenye mada ya Prof. Lipumba, ndilo lililowaongoza waasisi wa Muungano kuchagua mmundo wa Muungano wa serikali mbili je sababu hizo hazipo tena? Je hali ya sasa ya kisiasa, kitaifa na kimataifa, inatupa uhakika kiasi gani kwamba Tanganyika itakuwa tayari kubeba gharama zake na za Muungano kwa sababu tu ya vifungu vya Katiba? Je? vifungu vya Katiba vinaweza kuzuia kutokea dharura na mitikisiko ya kiuchumi na kiusalama ? Kwa nini tukimbilie kutaja vyanzo vya mapato na vipaumbele vya matumizi pasipo kuudadisi mfumo wa ubeberu unaotawala dunia hivi sasa tena kinyama? Na uwezo wa vinchi vya Afrika katika kuhimili vitendo vya kijama vya mabeberu ni kiasi gani? Hivi tunaweza kujadili muundo wa Muungano bila kujadili muundo wa uchumi na aina ya siasa uchumi inayoongoza uchumi huo. Mjadala kuhusu gharama za muungano hauna budi kujielekeza katika kujibu maswali haya magumu

 5. Nakubaliana na ndugu Bashiru kwamba yako mengi husika na muhimu kuzingatia wakati wa kupanga ni sehemu gani kila mshirika anapashwa achangie kwenye bajeti ya muungano chini ya muundo wa serikali tatu usiohusisha shughuli za kiuchumi na hivyo kila nchi mshirika kupashwa kukusanya mapato yake yenyewe kama chanzo cha mchango wake kwenye bajeti ya muungano.
  Kwa mfano ukubwa wa nchi mshirika ni muhimu ukazingatiwa kwa vile mara nyingi nchi kubwa (Tanganyika) itatumia sehemu kubwa zaidi ya bajeti ya muungano kuliko sehemu itakayotumiwa na nchi ndogo (Zanzibar). Kwa hiyo sehemu anayopashwa kila mshirika achangie kuendana na idadi yake ya watu kinapashwa pia kiongezeke au kipungue kuendana na ‘density yake ya watu’ kwani kwa idadi sawa za watu ni gharama zaidi kuhudumia ile iliyo ‘ high density” kuliko kuhudumia ile iliyo “low density’. Hata hivyo mengine yote ya kuzingatiwa hayatarajiwi yawe na uzito mkubwa ikilinganishwa na uzito wa idadi ya watu.
  Kilichozingatiwa na waasisi kwenye chaguo lao la muundo wa serikali mbili hakikuwa gharama kwani ingekuwa gharama chaguo lao lingekuwa muundo wa serikali moja ya muungano. Kuamini tatizo lilokuwepo la Zanzibar kushindwa kuwasilisha kikamilifu michango kake kwenye bajeti ya muungano chini ya muundo wa serikali mbili linatatulika kwa njia ya maboresho kwenye katiba mpya basi ni dhirisho kwamba tatizo kama hilo linatatulika kwa njia hiyo hiyo kwene muundo wa serikali tatu unaopendekezwa, tena rahisi zaidi iwapo kila nchi mshirika itakusanya mapato yake yenyewe kama chanzo kikuu cha mchango wake kwenye bajeti ya muungano.
  Hata hivyo njia nzuri zaidi ya kuondokana na tatizo la uchangiaji wa bajeti ya serikali ya muungano ni kupunguza gharama ya muungano kwa kupunguza mambo ya muungano na kuchagua muundo wa serikali mbili (ya Zanzibar, ya Tanganyika na muungano wa mkataba uliopendekezwa na wengi huko Zanzibar)
  Ya muungano tuanzie na mambo muhimu zaidi ya ulinzi na nchi za nje chini ya muundo wa serikali mbili (ya Zanzibar, ya Tanganyika na muungano wa mkataba). Tutakuwa tumeanzia na machache muhimu zaidi kwenye muungano kwa gharama ndogo na kuondokana na gharama ya serikali ya muungano isiyokuwa na tija kwetu. Hapo baadaye ya muungano yatakuwa yakiongezeka kidogo kidogo itakapokuwa muhimu.
  Ni kitu kisichoeleweka Tanganyika na Zanzibar kuendelea kuzungumzia muungano uliopo wa serikali mbili au wa tatu uliopendekezwa kwenye rasimu ya katiba mpya huku ikieleweka fika sera ya siasa na uchumi kitaifa tuliyoanzia nayo na iliyopitwa na wakati ya ujamaa na kujitegemea bado haijafanyiwa marekbisho na kukubalika na nchi zote washirika kama ndiyo hiyo kitaifa kwa nchi washirika na vyama vyote vya kisiasa ndani ya Tanzania huko tuendako. Ni muungano wa mkataba peke yake unaofaa pale ambapo hakuna sera moja ya siasa na uchumi kitaifa iliyokubalika na nchi zote washirika.

  • Kusema ukweli mimi binafsi siwezi kuendelea kujadili hoja zilizoibuliwa na Ndugu yetu Massawe kwa sababu hazijadiliki. Kama kweli ndugu Massawe anakubaliana na anayoyaita ‘mapendekezo ya wazanzibari wengi’ ya kuwa na Muundo wa Muungano wa mkataba utakaoundwa na Tanganyika, Zanzibar na Muungano wa Mkataba, basi tatizo la gharama halitakuwepo kwa sababu muungano wenyewe hautakuwepo.

   Naomba nimkumbushe ndugu Massawe kuwa mjadala wetu amabao tumekuwa tukiufanya kwa wiki kadhaa sana unahusu mada ya Prof. Lipumba ya changamoto za kugharamia Muungano wa serikali tatu-ya Tanganyika, ya Zanzibar na Shirikisho. Sasa ndugu Massawe ametutoa kwenye mstari wa mjadala husika na kutuletea mjadala mpya wa gharama za Muungano wa mkataba. Anazua mjadala mpya unaohitaji hoja mpya. Hajaleta hoja mpya ya gharama za muungano wa shirikisho.Mimi siwezi kukubali kutoka kwenye njia kuu ya mjadala uliotokana na mada ya Profesa Lipumba kwa sababu nilizozieleza hapo juu

 6. Tukiwa na mkataba wa ushirikiano badala ya Serikali ya Muungano bado gharama kidogo itasalia kwa sababu ni lazima kamati iwepo ya kusimamia utekelezaji wa Mkataba huo wa ushirikiano. Niaminivyo mimi ni kwamba kinachotakiwa ni ushirikiano wa kiuchumi na sio muungano wa kisisa nchi za Afrika, EAC na Tanzania zinapashwa kuwa zikizungumzia kufanikisha. Ushirikiano kama huo wa kiuchumi haupashwi kugusa hata kidogo sovereignity ya nchi yoyote mshirika kwa sababu matokeo yake yatakuwa ni hayo hayo tuyaonayo yakiendelea kwenye jumuia ya nchi za Kisoviet inayosambaratika kwa kasi kubwa. Muungano wa mkataba ni muhimu sana inapozingatiwa kwamba utamaduni wa Zanzibar na Tanganyika ni tofauti sana, Zanzibar na Tanganyika hazina sera ya maendeleo kitaifa iliyokubalika na wote iwe ya washirika na Muungano na EAC bado iko mbioni yaja na muundo wake bado haujakubalika kikamilifu ili kuwezesha ieleweke muungano Tanzania utajiunga vipi. Sijui ni kwa nini shirikisho la EAC na Muungano tanzania utakavyojiunga halikuzungumziwa popote kwenye Rasimu ya Katiba mpya?!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box