Dhana na Maana ya Bunge Maalum la Katiba

Na Issa Shivji

Bunge Maalum la Katiba (constituent assembly) ni chombo mahsusi cha wananchi kutunga katiba yao. Katika falsafa ya kisasa ya kikatiba, wananchi ndiyo wenye mamlaka (sovereign power) na kwa kutumia mamlaka haya wananchi ndiyo huunda chombo chao cha kujadili na kupitisha katiba. Ndiyo maana, nchi nyingi duniani, hutumia Bunge Maalum na Kura ya Maoni kujiwekea katiba za nchi zao. Bunge Maalum la Katiba ni kielelezo cha mamlaka ya wananchi. Kwa hivyo, katika halisia, wajumbe wa Bunge Maalum wanatakiwa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika uchaguzi mkuu. Kazi ya Bunge Maalum ni moja tu: kutunga katiba na baada ya hapo uhai wake unamalizika.

Kwa kuwa wananchi hawawezi kukutana wote kujadili kwa pamoja katiba yao, wananchi kwa hiari yao wanawachagua wajumbe wao kukaa, kujadili na kuwatungia katiba na hatimaye wananchi wanakubali au kukataa katiba iliyopitishwa na Bunge lao katika kura ya maoni. Kwa hivyo, Bunge la Katiba linakuwa na madaraka makubwa kuliko hata Bunge la kawaida kwa sababu mamlaka na madaraka ya Bunge la Katiba yanatokana na wananchi moja kwa moja. Hii ni dhana ya Bunge Maalum. Katika hali halisi, mambo yanakuwa tofauti.

Mchakato wa kutunga katiba unaweza kuwa tofauti kutokana na hali halisi na mazingira ya kisiasa ya nchi inayohusika. Na wajumbe wa Bunge Maalum pia wanaweza wakachaguliwa moja kwa moja au kuchaguliwa kupitia vyombo vingine. Katika historia ya nchi yetu, hatujawahi kuwa na Bunge Maalum lililochaguliwa na wananchi moja kwa moja. Bunge Maalum la kwanza katika Tanganyika lilikuwa mnamo mwaka 1962 kupitisha katiba ya Jamhuri ya Tanganyika. Bunge la kawaida (National Assembly) lilipitisha sheria kujigeuza kuwa Bunge Maalum. Hata hivyo, kudhibitisha kazi na mamlaka yake, Katiba na sheria zingine zilizopitishwa na Bunge Maalum halikuenda kwa Gavana kwa ajili ya idhini yake kama ilikuwa taratibu za kupitisha sheria wakati ule.

Bunge Maalum la Katiba la pili lilikuwa 1977. Kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Rais, Mwalimu Nyerere, na Mkataba wa Muungano (Articles of Union), Mwalimu, kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar, aliunda Bunge Maalum la Katiba lililopitisha Katiba ya 1977, ambayo ni katiba tuliyonayo. Ni kweli kwamba wajumbe walioteuliwa na rais kuingia katika Bunge Maalum wote walikuwa wabunge, theluthi moja wakiwa kutoka Zanzibar na theluthi mbili kutoka Bara. Lakini hawakuingia katika Bunge Maalum kwa nyadhifa zao za kibunge bali kwa kuteuliwa na rais chini ya mamlaka aliyopewa na Mkataba wa Muungano.

Pia kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano kulikuwa na Tume ya Katiba. Watu ishirini, 10 kutoka Bara na kumi kutoka Zanzibar, walioshughulikia kuandaa katiba ya CCM ndio ikageuzwa kuwa Tume ya Katiba ya Muungano. CCM kupitia Tume hii ilitoa maelekezo kwa Wizara ya Sheria kuandika Rasimu ya Katiba. Waziri wa Sheria alikuwa Mama Julie Maaning na Mheshemiwa Joseph Sinde Warioba alikuwa Mwanasheria Mkuu. Niongeze pia kwamba katibu wa Tume alikuwa Mhe. Pius Msekwa na mwenyekiti Mzee Thabit Kombo.

* * *

Pamoja na kwamba mchakato unaweza kutofautiana na hata upatikanaji wa wajumbe wa Bunge Maalum, bado kidhana hadhi na mamlaka ya Bunge Maalum yanabaki palepale, kama kielelezo cha mamlaka ya wananchi. Dhana hii ya Bunge maalum ilieleweka kwa ufasaha mkubwa nyakati zile. Marehemu Sokoine, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, alielezea vizuri akiwasilisha rasimu/pendekezo mbele ya Bunge Maalum. Namnukuu:

Katiba ya nchi ndiyo sheria ya msingi kabisa kwa Taifa lolote, na chombo kinachotunga Sheria hiyo ni lazima kiwe ni chombo chenye madaraka makubwa kabisa. Kwa hiyo Bunge hili maalum lina madaraka kuliko Bunge la kawaida. Bunge hili linaweza kukataa au kukubali mapendekezo haya.

Lakini Nd. Spika, katika kutumia madaraka yetu ni lazima tujue mipaka ya madaraka hayo. Mapendekezo tutakayofikiria hivi sasa yametokana na maagizo ya Chama. Kwa busara yetu Watanzania tumeamua, na bila kusita, kwamba Chama kitashika hatamu za uongozi nchini. Kwa hiyo Bunge hili linaweza kabisa kuyakataa ama kuyabadilisha mapendekezo ya Serikali iwapo litaona kuwa yanapinga maagizo ya Chama. Na iwapo mapendekezo yote yanayopendekezwa yanatekeleza maagizo ya Chama naomba Bunge lisione uzito wa kuyapokea na kuyapitisha bila kusita. (Makofi.) [1]

Pamoja na ukweli kwamba enzi zile zilikuwa enzi za chama kimoja, na chama kushika hatamu, Sokoine hakutafuna maneneo yake, au kupinda dhana ya Bunge maalum. Alichokuwa anakumbushia wajumbe ni kwamba wao wote walikuwa wananchama wa CCM na walikuwa wanabanwa na maaumuzi ya chama chao. Kwa mantiki hiyo, mipaka ya madaraka ya Bunge maalum hayakutokana na nyadhifa zao kama wajumbe bali ilitokana na uanachama wao.

Kwa sababu zisizoeleweka, katika mchakato wetu wa sasa, dhana na maana ya Bunge Maalum imepotoshwa sana na baadhi ya wasomi na wasemaji. Mheshimiwa Warioba katika hotuba yake aliyotoa katika mkutano wa Tanzania Centre for Democracy amejenga hoja kama ifutavyo:

Madaraka ya Bunge Maalum yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Maadiliko (sic!) ya Katiba au Chombo cha aina hiyo. Bunge Maalum linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalum kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa Wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalum yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Watalaam wa masuala ya Katiba, wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge Maalum katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba.

Kanuni za Bunge Maalum la Katiba sharti zizingatie kwamba Bunge Maalum, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa chini ya kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83, ni chombo cha kuboresha masharti ya Rasimu ya Katiba.

Katika kutekeleza madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya kikatiba, Bunge Maalum litazingatia msingi kwamba masharti ya kikatiba ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto za wananchi ambazo zimeelezwa kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi ya wananchi kupitia asasi, taasisi, jumuiya na makundi ya Watu wenye malengo Yanayofanana.

Bunge Maalum litafanya kazi ya kuboresha masharti ya Kikatiba yailyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba. (uk. 10-11) [2]

Tunaweza tuka jumlisha hoja kuu za Mhe. Warioba kama ifuatavyo:

 1. Madaraka ya Bunge maalum kubadilisha misingi mikuu ya rasimu au la inategemea nani aliandika rasimu. Kama Bunge lenyewe limeandika rasimu, Bunge lina madaraka hayo, lakini kama rasimu imeandaliwa na ‘Tume ya Mabadiliko ya Katiba au Chombo cha aina hiyo’, Bunge Maalum linaweza kuirekebisha na kuiboresha lakini sio kuibadilishi misingi yake.
 2. Hoja hii inatokana na ukweli kwamba wananchi wameshiriki kutoa maoni yao yaliyowekwa katika rasimu. Bunge likibadilisha misingi itakuwa sawa na kunyang’anya ‘madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Hii maana yake halisi ni kwamba utolewaji wa maoni mbele ya rasimu ilikuwa “act of popular sovereignty” ya wananchi; maoni yao ni kielelezo cha mamlaka yao.
 3. Hoja hizi kuu ni kwa mujibu wa (a) ‘Wataalam wa masuala ya Katiba’; na (b) kifungu cha 25(1) cha sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.

Kutokana na hoja hizi za Mhe. Warioba, anatoa maelekezo kwamba Kanuni za Bunge Maalum zitakazotungwa na Bunge Maalum lenyewe ‘sharti zizingatie kwamba Bunge maalum … ni chombo cha kuboresha masarti ya Rasimu ya Katiba.’

Hatuna budi tuchambue hoja hizi moja baada ya nyingine.

1. Kuhusu madaraka ya Bunge kutegemea mchakato:

Kama nilivyoeleza hapo juu, historia ya dhana ya Bunge maalum (constituent assembly) inasisitiza kwamba Bunge Maalum ni mwakilishi wa mamalaka (sovereignty) ya watu. Kujitungia katiba yao ni kwa mujibu wa mamlaka (sovereignty) ya watu. [3]

Kwa kuwa mamilioni ya wananchi hawawezi kukaa chini ya mti na kujadili na kuandika katiba yao, wao wanachagua wajumbe wao na wanawatuma kufanya kazi moja hii ya kuwatungia katiba.

Rasimu yenyewe ya Katiba inaweza kuandikwa na kamati iliyoteuliwa na Bunge lenyewe (kama ilivyokuwa India kuandika katiba yao ya 1950) au rasimu inaweza kuandaliwa na kuandikwa na Tume (kama ilivyokuwa Uganda kuandika katiba yao ya 1995). Lakini hii haibadilishi dhana na maana ya Bunge Maalum au kuweka mipaka ya madaraka ya Bunge Maalum.

Katika mifano hii yote miwili, Bunge Maalum lilibadilisha mambo makubwa katika rasimu. Uweli ni kwamba, mchakato wa Uganda haukuwa tofauti kubwa sana na mchakato wetu.

Tume ya Katiba ya Uganda chini ya Jaji Mkuu ilikusanya maoni na kuandaa rasimu pamoja na Taarifa ya uchambuzi wa kina (majuzuu matatu zaidi ya ukurasa 1000). Lakini mikono ya Bunge maalum haikufungwa na rasimu bali lilijadili mambo mengi sana ya msingi kinyume kabisa na misingi ya rasimu. Kwa mfano, kulikuwa na sauti nzito kutoka kwa wawakilishi wa Buganda ambao walitaka muundo wa shirikisho (federal structure) badala ya muundo wa serikali moja (unitary state). Hata hivyo, hakuna yeyote katika Bunge hili – na lilikuwa na wanasheria waliobobea pamoja na marehemu Profesa Nabudere – waliopinga kwa msingi kwamba mjadala ule ulikuwa ni batili kwa sababu ulikuwa unapinga misingi ya rasimu. Kulikuwa pia mjadala mkali kuhusu mfumo wa vyama vingi badala ya mfumo wa ‘movement system’ uliopendekezwa na Tume. Vilevile hakuna aliyepinga kwa msingi kwamba mjadala ulikuwa kinyume cha sheria au taratibu kwa sababu rasimu iliandaliwa na Tume kutokana na maoni ya wananchi. Isitoshe, pendekezo la Tume lililotokana na maoni ya wananchi kuwa na ‘National State Council’ kusulihisha migogoro kati ya mihimili ya dola lilitupiliwa mbali na Bunge maalum, tena kwa sauti moja. [4]

Kwa kujumuisha, ni wazi kwamba mchakato wenyewe wa kuandika rasimu ya katiba unaweza kutofautiana kutokana na hali halisi. Lakini mchakato haubadilishi mamlaka ya Bunge Maalum au haiathiri dhana yake kama chombo mahasusi cha wananchi.

Ingawa, kisiasa Bunge Maalum lililochaguliwa moja kwa moja na wananchi linakuwa na uhalali zaidi na hadhi ya juu kabisa, katika hali halisi, kutokana na uwiano wa nguvu za kitabaka na makundi katika jamii, wanaoingia katika Bunge Maalum wanaweza wakapatikana kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuteuliwa, kama tutakavyona hivi punde. Hata hivyo, bila kujali nani ni wajumbe wa Bunge la Katiba, kisheria dhana na hadhi ya Bunge Maalum haibadiliki.

2. Kuhusu ushirkishaji wa watu kutoa maoni:

Hoja hii ya Mhe. Warioba kwa kweli ni kuhalalisha pendekezo la Tume la serikali tatu, ambayo ni msingi mkuu wa rasimu. Hoja ni kwamba pendekezo hili limetokana na wananchi wenyewe. Niseme tu, kwanza, pamoja na kazi zito inayofanya na Tume, pamoja na kukusanya maoni ya wananci, hii haitoshi kunyang’anya wananchi mamlaka yao ambayo wanaidhihirisha kupitia Bunge Maalum. Tume kamwe haiwezi kuwa na hadhi sawa au zaidi ya Bunge Maalum. Tume sio mwakilishi wa wananchi, wala haikuchaguliwa na wananchi, wala sio chombo cha kufanya maamuzi. Tume inatoa mapendekezo. Mapendekezo yanaweza kukubaliwa au kutupiliwa mbali.

Kama kweli, jukumu la Bunge Maalum ni kuboresha tu au kurekebisha tu mapendekezo bila kubadili misingi yake, basi hatukuwa na haja ya kuwa na Bunge lenyewe. Mapendekezo ya Tume yangeenda moja kwa moja kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.

Pili, ukiangalia kwa makini takwimu zilizotolewa na Tume yenyewe, wala sio sahihi kusema kwamba wananchi waliowengi walitaka serikali tatu. Kwa jumla, waliotoa maoni mbele ya Tume ni watu 351,664 (ang. Jedwali 3, uk. 9 [5]). Kati ya hao, 47,820 tu (asimilia 14) waligusia muundo wa muungano. Asilimia 86 wala hawakuzungumzia muundo wa muungano kwa maana ya serikali moja, mbili au tatu au muungano wa mkataba. Wao walikuwa na mambo tofauti kabisa kuhusu maisha yao. Kati ya waliyogusia muundo asilimia 30 walitaka serikali mbili, asilimia 37 walipendekeza serikali tatu, na asilimia 25 walitaka muungano wa mkataba; asilimia nane walitaka serikali moja.

Kwa hivyo, waliopendekeza serikali tatu ni theluthi moja tu waliogusia muundo wa muungano, na ni asilimia 5 tu waliotoa maoni. Waliotaka serikali mbili na muungano wa mkataba ni asilimia 55, yaani zaidi ya nusu ya waliotoa maoni juu ya muundo wa muungano. Hata ukichanganya waliotaka serikali moja na serikali mbili ni asilimia 38, inazidi kidogo wale waliotaka serikali tatu. Kwa takwimu hizi za Tume yenyewe, utasema je kwamba serikali tatu ni chaguo la wananchi na ni ‘taswira, dira na ndoto za wananchi’?

Sizani kuna haja ya kusema zaidi juu ya hoja hii: haina mshiko wala ushahidi wa maana.

3. Kuhusu maoni ya wataalam wa kikatiba:

Mhe. Warioba anadai kwamba watalaam wa masuala ya kikatiba wanaunga mkono kwamba Bunge Maalum lina mipaka ikiwa mchakato umefuata kuwa na Tume kuandaa rasimu. Bahati mbaya Mheshimiwa hakutaja majina yao wala kunukuu maandishi yao. Kwa hivyo ni vigumu kujua hao watalaam ni nani na walisema nini na katika muktadha gani.

4. Kuhusu kifungu cha 25(1) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba:

Inadaiwa na Mhe. Warioba na wengine kwamba kifungu cha 25(1) cha sheria ya mabadiliko ya katiba imeweka mipaka ya madaraka ya Bunge Maalum. Kifungu hiki kwa lugha ya Kiswahili kinasema:

25(1) Bunge Maalum litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba inayopendekezwa…

Kwa mujibu wa kifungu hiki Bunge Maalum lina uwezo wa (1) kujadili; na (2) kupitisha. Kifungu hiki hakisemi kwamba baada ya kujadili masharti ya rasimu, Bunge halina mamlaka ya kuyabadili. Yaani maana sahihi ni kwamba baada ya kujadili Bunge (a) linaweza kupitisha masharti haya kama yalivyo; au (b) kubadili, na kuyapitisha mabadiliko. Hakuna popote pale neno ‘kuboresha’ limetumika. Kama kweli, nia ilikuwa ni kulipa Bunge mamlaka ya kuboresha au kurekebisha tu sheria ingesema hivyo. Kuna mantiki gani ya kujadili kama huna uwezo wa kuibadili au hata kuitupilia mbali?

Kifungu 25(1) cha Kiingereza kimeweka jambo wazi zaidi:

The Constituent Assembly shall have and exercise powers to make provisions for the New Constitution of the United Republic of Tanzania…

Maana ya ibara hii ni wazi kabisa. Bunge Maalum ndiyo chombo kinacho weka masharti ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano. Inaelekea tafsiri ya Kiswahili ni mbaya lakini mantiki yake ni ileile ya yale inayoelezwa katika kifungu cha Kiingereza.

Kwa kuhitimisha, ni wazi kabisa kwamba sheria ya mabadiliko ya katiba haikuweka mipaka ya mamlaka ya Bunge Maalum kama invyodaiwa. Na isingeweza kufanya hivyo kwa sababu sheria yenyewe ilipitishwa na Bunge la Kawaida, tena sio kwa theluthi mbili, ambayo ingempa sheria ya mabadiliko hadhi ya sheria ya kikatiba (constitutional act). Na hatimaye pendekezo (proposed constitution) la Bunge Maalum halirudi kwa Bunge la Kawaida bali linapelekwa moja kwa moja kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni. Kwa hivyo, wananchi watapigia kura zao kwa pendekezo la Bunge Maalum na sio rasimu ya Tume. Rasimu ya Tume itakuwa na nafasi ya kihsitoria tu, sio ya nguvu za kisheria.

Nafasi ya Bunge Maalum ni la kipekee kabisa katika mchakato wa kutunga katiba mpya. Nafasi yake ni nzito kuliko ile ya Tume na muhimu kuliko kura ya maoni. Hii ni kwa sababu Bunge Maalum ndiyo chombo cha kufanya maamuzi mazito, sio Tume. Bunge ndiyo litapitia rasimu ibara kwa ibara, kufanya uchambuzi, kutathmini athari zake kwa Taifa, kuhakikisha kwamba hakuna migongano katika ibara, kuangalia kwa undani mfumo na muundo unaopendkezwa unatekelezeka au hapana na, muhimu kuliko yote, mfumo unaopendekezwa utaimarisha utulivu na amani na umoja wa nchi (national and territorial integrity) au utazaa vurugu, migogoro na hatimaye uvunjaji wa nchi.

Ndiyo maana, wachache wetu tulipendekeza tuwe na Bunge Maalum la kuchagliwa na wananchi moja kwa moja. Lakini watawala wetu, pamoja na watawala watarajiwa na wengi wa wanaharakati, katika busara zao na kwa maslahi yao, hawakutilia maanani pendekezo letu. Tumepoteza nafasi ya kipekee ya kihistoria ya kuwa na Bunge Maalum la kuchaguliwa, jambo ambalo limetufikisha hapa tuliko.

Tufanye lololote linalowezekana pamoja na kuibua mijadala na uelewa miongoni mwa wananchi bila jazba za kichama. Hili ni jukumu letu kama wasomi. Tusije tukavunja nchi yetu na kuisambaratisha taifa. Historia na vizazi vijavyo havitatusamehe.

* * *

[1] Imenukuliwa kutoka Majadiliano ya Bunge (HANSARD), Taarifa Rasmi, Mkutano wa Sita, 25 Aprili-28 Aprili, 1977, UK. 11.

[2] Maelezo ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba katika Mkutano wa Tanzania Center for Democracy, kuhusu Tafakuri na Maradhiano kuelekea Katiba Mpya: Whitesands Hotel, Dar es Salaam, 12 Februari, 2014.

[3] Angalia Ben Nwabueza, Constitutional Democracy in Africa, vol. 1, Ibadan: Spectrum Books, uk. 195-198. Angalia pia Mahendra P. Singh, V. N. Shukla’s Constitution of India, 9th edn. Lucknow: Eastern Book, uk. A-24- A-25.

[4] Angalia David Mukholi (1995) Uganda’s Fourth Constitution: History, Politics and Law, Kampala: Fountaion Publishers, uk. 49)

[5] Takwimu na jedwali zote zinatokana na Takwimu za Ukusanyaji wa maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Disemba, 2013.

4 thoughts on “Dhana na Maana ya Bunge Maalum la Katiba

 1. Mkanganyiko wa tafsiri ya sheria ya marekebisho ya Katiba Sura ya 83 haujaisha. Ufafanuzi wa Jaji Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, kuhusu vifungu vya 25 (1) na 9 (2) siyo tu kwamba unabishaniwa na wanasheria wenzake bali pia unatatanisha. Katika gazeti la Mwananchi la leo kuna makala yenye kichwa cha habari ‘Warioba ampa somo Werema’ yanayomkariri Jaji Warioba asisitiza kwamba Rasimu ya Katiba itakayowasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba wiki ijayo ni mali ya wananchi na mawazo na mapendekezo yaliyomo yanapaswa kuheshimiwa kwani yametoka kwa wananchi. Jaji Warioba anawashauri wanasheria wenzake kwa kusema: ‘someni sheria vizuri mtajua’. Makala ya Profesa Shivji imefafanua vizuri dhana ya Bunge la Katiba lakini bado naona wanasheria wenzake waliopewa dhamana za kisiasa hawakubaliani na uchambuzi wake. Sisi tusiyojua sheria inabidi tufuatilie kwa makini malumbano haya ya kisheria ambayo kimsingi yanawachanganya Wajumbe wa Bunge Maalum. Jaji Warioba amekaririwa na Gazeti la Mwanchi la leo akisema kuwa ‘mimi ndiye msemaji wa mwisho katika hili’. Je, tafsiri ya kisheria ya Jaji Warioba kuhusu vifungu vya sheria ya mchakato vinavyobishaniwa ndiyo sahihi zaidi kuliko tafsiri za wanasheria wenzake? Au tafsiri ya Jaji Werema ndiyo tafsiri rasmi? Je, ni nini nafasi ya Wanasheria wakuu wa serikali zote mbili katika Bunge hili maalum la Katiba?

  Kwa mujibu wa Prof. Shivji, Bunge Maalum la Katiba hufanya kazi moja tu ya kutunga Katiba na hupata mamlaka yake kutoka kwa wananchi. Je, kwa kuwa Bunge hili halikuchaguliwa na wanachi haliwezi kuwa na uhalali wa kisiasa wa kutunga katiba kwa niaba ya wananchi? Je, tume iliyoteuliwa na Rais kwa mujibu wa sheria ina hadhi kubwa na uhalali zaidi wa kisiasa kuliko Bunge Maalum la katiba ambalo halikuchaguliwa na wananchi?Haya ni maswali ambayo yananitatanishwa na ningefurahi kupata ufafanuzi kutoka kwa yeyote mwenye utaalamu wa sheria na masuala ya katiba.

  • Ng’wanza ametusaidia kwa kutofautisha uzalendo (patriotism) na utaifa (nationalism). Uzalendo unakita kwenye ngazi ya dola/serikali; utaifa unakita kwenye ngazi ya nchi/taifa. Uzalendo unakupeleka kwenye kutii serkali/dola iliyoko madarakani; utaifa unakupeleka kwenye kudadisi walioko madarakani. Uzalendo unafundishwa madarasani kama somo la uraia mwema (good citizenship) – kutii serikali na”viongozi” yaani watawala; kulipa kodi kwa wakati; kuimba wimbo la taifa kama kasuku; n.k. Kwa jumla, uzalendo unakufanya uwe mtiifu; utaifa unakufanya uwe mpambanaji. Uzalendo ni itikadi ya kukubali hali ilivyo (status quo); utaifa unakufanya uhoji hali ilivyo. Utaifa unakufanya uwe mlinzi na mkombozi wa nchi/taifa.

   Kuna utaifa wa aina mbili – utaifa wa mrengo wa kushoto (radical nationalism) na utaifa wa mrengo wa kulia (narrow nationalism/chauvinism). Utaifa wa mrengo wa kushoto unakita kwenye ukombozi, mabadiliko makubwa. Utaifa wa mrengo wa kulia unakuzamisha kwenye ukabila, urangi, udini, uzawa, na hatimaye ufasishti.

   Katika hali halisi yetu ya bara la Afrika, kwa vyovyote vile, utaifa ni utaifa wa Kiafrika, sio wa kinchi. Kwa sababu hizi nchi zetu (au kama alivyokuwa anasema Mwalimu, vinchi) ni muumbo wa ukoloni. Ukweli ni kwamba umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) ndiyo uliozaa utaifa na sio utaifa uliozaa umajumui. Hata hivyo, baada ya kizazi cha kwamza cha manationalists waliposhindwa kuunganisha nchi zao na kuingia madarakani, basi, wakajaribu kujenga utaifa wa kinchi – Utanzania, Ughana n.k. Kama alvyosema Mwalimu, dola huru la Afrika lilikuwa na majukumu mawili makubwa – ujenzi wa Taifa na kuletea wananchi maendeleo. Licha ya kuwa na nia na dhamira ya dhati, hata viongozi kama Mwalimu na Nkrumah hawakufanikiwa. Na miongo miwili ya uliberali-mambo leo umedhihirisha wazi wazi kwamba katika enzi za ubeberu/utandawazi vinchi vya kiafarika hawawezi kujenga mataifa; bali wanatakiwa kujenga Taifa moja la Kiafrika (the African nation). Na ubeberu, ukisaidiwa na vibaraka vyake, unaendelea kuvunja hata hivi vinchi vipande, vipande kama tumeshuhudia – mfano, Somalia, Libya, Sudan. Sasa imetufikia sisi: tunaleweshwa na Utanganyika na Uzanzibari, na huo, Uzanzibari unaweza kumegeka kuwa uunguja na upemba.

   Siku nyingine tutazungumzia zaidi ujamaa. Labda, kwa kujumisha, niseme hivyo: kama uzalendo unakita kwenye ngazi ya dola na utaifa kwenye ngazi ya kitaifa, basi ujamaa unakita kwenye ngazi ya kijamii, yaani ya kitabaka. Na kama tabaka-tawala ndiyo msukumo wa uzalendo na umma ndiyo msukumo wa uataifa, basi, wavujajasho ndiyo msukumo wa ujamaa.

 2. UFAFANUZI (COMMENTARY) JUU YA KIFUNGU CHA 25 CHA SHERIA NAMBA 83 YA MABADILIKO YA KATIBA KWA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA: MADARAKA NA MIPAKA YA BUNGE LA KATIBA LA TANZANIA
  “Madaraka yake Yamebinywa na Mchakato, Sheria Na Muundo Wake”

  Mchakato wa Katiba
  Mchakato wa kupata katiba ya Jamhuri ya Muungano ulianza kwa kutungwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye kupitia sheria hiyo Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ikaundwa kwa ajili ya kukusanya maoni na kuandaa rasimu ya katiba. Kwa mujibu wa sheria hiyo ya mabadiliko ya katiba kwa sasa tumebakiza hatua mbili ili kukamilisha mchakato wa katiba. Hatua hizo ni Bunge la Katiba na kura za maoni (Referendum). Hatua zote za mchakato wa kupata katiba zinatofautiana na zina mamlaka tofouti na zinapaswa kuwa shirikishi.

  Katika taifa lolote lile msingi wa uendeshaji wa Taifa hutegemea sana sheria kuu (Grund Norm). Katiba huainisha tunu na misingi ya nchi yoyote, pia hutoa migawanyo na ukomo wa madaraka na majukumu mbalimbali ya mihimili mikuu ya dola. Kutokana na umuhimu huu mchakato wa katiba ni lazima uwe shirikishi katika ngazi zote likiwemo hili la Bunge la Katiba. Katiba inapaswa kuakisi mambo ya wananchi ili kuifanya waimiliki na kuiheshimu katiba hiyo. Ukiwa na Katiba ambayo wananchi hawakushiriki vizuri, lazima Katiba hiyo itakuwa vigumu kupata utekelezaji na umiliki wa wananchi.

  Historia inatushitaki kuwa michakato mingi ya kikatiba baada ya kupata uhuru haikuwashirikishi bali ilihusisha tu viongozi. Katiba ya kwanza ya Tanganyika ya 1961 ilipatikana kupitia Bunge la Kikoloni, katiba ya 1962 ilipatikana kupitia white paper na sheria ya Bunge la Katiba ikatumika kugeuza bunge la kawaida kuwa Bunge la Katiba, hali kadhalika katiba ya Muungano ya 1964 na ile ya Muda ya 1695 zote hazikupata Baraka za wananchi. Mwaka 1977 Katiba yetu inayotumika hadi leo iliundwa na kamati ya chama iliyogeuzwa kuwa tume ya katiba na baadae tume hiyo kupeleka maoni yake kwa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kamati hii ya Chama ndiyo ilipeleka rasimu kwenye Bunge ili kujadiliwa na kupitishwa. Michakato yote hiyo haikushirikisha wananchi tofouti na huu wa sasa.

  Mamlaka na Mipaka ya Bunge la Katiba
  Hivi karibuni, siku chache kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba kumetokea mikinzano tofouti kuhusu madaraka na mipaka ya Bunge la Katiba. Utata huu umeanza pale Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM aliposema katika maadhimisho ya miaka 37 ya CCM huko Mbeya tarehe 3, February 2014. Rais Kiwete alinukuliwa na gazeti la umma la Daily News akisema;

  “The assembly will be free to discuss and shape the final draft of the Constitution in the way they deem fit, adding that the assembly may even produce a “totally different document” if it can reach a common understanding and manage to compose it” Bunge litakuwa huru kujadili rasimu ya katiba kwa wanavyoona ni sawa, na ikiwezekana Bunge linaweza kuja na rasimu tofouti kabisa kama watahafikiana na kuweza kuandaa rasimu hiyo” President Kikwete.

  Maneno na mawazo kama haya yalirudiwa tena na Prof Issa Shivji alipokuwa akitoa mada katika kongamano la wajumbe wapya wa Bunge la Katiba hivi karibuni Jijini Dar es Salaam. Prof Shivji alidai kuwa;
  “Rasimu ya Katiba sio Msahafu, Bunge la Katiba linaweza kubadili rasimu na kuja na rasimu mpya kabisa. Bunge ndio chombo cha maamuzi na wanauwezo wa kuibadili rasimu” Prof Shivji

  Katika mafunzo hayo kwa wabunge wa Bunge la Katiba, Prof Shivji alitoa msimamo wake na mimi kutoa msimamo wangu na kuwafanya wajumbe hao waende Bungeni na maswali juu ya mamlaka halisi ya Bunge la Katiba. Maneno hayo ya Prof Issa Shivji na Rais Jakaya Kiwete yanapingana na msimamo wa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Sinde Warioba. Jaji Warioba katika mkutano wa serikali na wanasiasa uliondaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania alilisitiza kuwa Bunge la Katiba halina mamlaka ya kubadili masharti na mambo ya msingi wa katiba bali wanauwezo wa kujadili na kuboresha mambo ya kawaida.

  Kwa mujibu wa Jaji Warioba Bunge la Katiba la Tanzania halina mamlaka ya kubadili masharti ya katiba kwa kuwa mchakato huu wa Tanzania ni tofouti na nchi zingine kama Africa Kusini, Namibia na Cambodia ambapo Bunge maalumu ndio lililopewa jukumu la kuandika Rasimu. Katika mazingira haya Bunge Maalum linauwezo kabisa wa kuandika Rasimu mbadala.

  Mimi binafsi kama mwanasheria naungana moja kwa moja na Jaji Warioba na kusisitiza kuwa Bunge Maalum la Katiba la Tanzania halina madaraka ya kubadili Rasimu hii zaidi ya kuijadili, kuiboresha na kuileta kwa wanachi kwa ajili ya kupitishwa.Mzozo huu pia umeendelea hadi katika mikutano ya awali ya Bunge la Katiba. Mwanasheria Mkuu wakati anajibu hoja za wajumbe naye ameendelea kushikilia kuwa Bunge la Katiba linaweza kuja na katiba mpya kabisa. Nasema Bunge letu hili halina mamlaka yoyote kubadili rasimu hii kwa sababu kuu zifuatazo:

  Kwanza, Bunge hili halina mamlaka ya kubadili rasimu hii zaidi ya kujadili, kuboresha na kuongeza masharti ya mpito.Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Bunge lina madaraka tu ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba, kutunga sheria ya masharti ya mpito, Kanuni za kuendeshea Bunge hilo na masharti yatokanayo. Hivyo kwa mujibu wa sheria hii tayari madaraka ya Bunge hili yamewekewa mipaka na wakitaka kuja na rasimu mbadala watakuwa wamevunja sheria hii.

  Kutokana na tafsiri yangu kama mwanasheria, Bunge Maalum linapaswa kuzingatia masharti ya kifungu hiki cha 25 wanapotunga Kanuni za Bunge Maalumu na wanapokuwa wanaendesha mjadala. Wanapaswa kuhakikisha hawatungi kanuni zitakazopingana na kifungu hiki. Kuna uwezekano mkubwa sana katika kuandaa kanuni hizi Bunge Maalum likajikuta linajipa madaraka ya kutunga “Rasimu ya Tatu” na kutupilia Rasimu hii ya wananchi.
  Inawezekana kabisa watu wakatumia wakati mwingine udhaifu wa sheria zetu kutafsiri vifungu kwa maslahi yao binafsi. Kuna baadhi ya watu wataweza kutafsiri kifungu hiki cha 25 kwa malengo ya kutaka kuonyesha kuwa Bunge la Katiba lina mamlaka ya kuja na rasimu mpya kabisa kitu ambacho si cha kweli. Kifungu cha 25(1) Kinasema;

  “Bunge litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha maharti ya katiba inayopendekezwa, kutunga masharti ya mpito na kutunga masharti yatokanayo kama Bunge Maalum litakavyoona inafaa”

  Kifungu hicho 25(1) kina sentensi tatu. Kwa mujubu wa sheria namba moja ya tafsiri ya vifungu vya sheria, neno kama “litakavyoona inafaa” liililotumika katika kifungu cha 25 linamaanisha sentensi ya pili na siyo sentensi inayozungumzia kujadili na kuboresha. Kwa maana hiyo Bunge linaweza ongeza masharti ya yatokanayo na ya mpito kadiri watakavyoona inafaa na si vinginevyo. Uhuru wa kama watakavyoona inafaa haitumiki katika mambo ya msingi ya katiba.

  Katika Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum la katiba, angalau kifungu cha 5 kimejaribu kutenganisha huo utata uliokuwa unatumika vibaya. Tofouti na sheria yenyewe rasimu ya kanuni imeweka kifungu hicho katika makundi mawili 3:

  5. (1) Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria, Bunge Maalum litakuwa na mamlaka ya- (a) kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba; na
  (b) Kutunga masharti ya mpito na masharti yatokanayo na Rasimu ya Katiba kadri litakavyoona inafaa.

  Kanuni hizi zimeweka bayana kuwa uhuru wa kadiri litakavyoona inafaa lipo kwenye masharti yatokanayo na na masharti ya mpito kama inavyojieleza kwenye kifungu (b).Tunaposema tunaposema masharti ya mpito na yatokanayo tunaaminisha yale masharti sawa nay ale ya mpito yaliwekwa katika sura ya 17 ya Rasimu ya Katiba.
  Sheria yenyewe imeacha mianya mingi ambayo kimsingi inaweza tumika vibaya, ilipaswa kuweka mipaka ya Bunge moja kwa moja (express provisions) kama ilivyokuwa kuwa kwa tume na hatua zingine zilizoainishwa katika mchakato wa katiba. Kwa mfano Tume ilipewa mipaka na mambo ya kuzingatia katika kifungu cha 9 cha sheria ya mabadiliko ya katiba, hali kadhalika tasisi ya kupiga kura za maoni ambayo ni mchakato wa mwisho nayo inamipaka yake ambayo ni kupiga kura ya ndiyo au hapana na si vinginevyo.

  Mwanasheria Mkuu, Jaji Werema alifanya kosa la kisheria kuwaambia wabunge kuwa makatazo na misingi ya utendaji yanatoka katika kifungu cha 9. Kifungu hiki hakina uhusiano kabisa na mamlaka ya Bunge. Mbaya zaidi katika Rasimu ya Kanuni za Bunge pia kosa hili limejirudia. Kosa la kisheria lipo zaidi katika kifungu cha 79(2) (a) ambacho kimewataka wabunge kufanya maboresho ambayo hayatakuwa kinyume na kifungu cha 9 cha seria ya mabadiliko ya Katiba. Kifungu hicho hakina uhusiano wowote na Bunge Maalum, ila ni kifungu ambacho kinatoa mipaka ya Tume tu.

  Tulifanya kosa kubwa kutunga sheria bila kuweka mipaka ya Bunge la Katiba katika mfumo ambao mtu yeyote ambaye si mwanasheria angeweza kuelewa kama ilivyo katika kifungu cha 9 kwa Tume. Nashauri Kanuni ziweke mipaka ya Bunge hili vizuri kwa kuzingatia kifungu 25, kwani kifungu cha 9 hakina uhusiano na Bunge.

  Sheria ingepaswa kueleza wazi wazi kuwa misingi ya Kikatiba (Constitutionalism) katika rasimu hii haipaswi kubadilishwa na Bunge la Katiba. Misingi hiyo ni pamoja na mgawanyo wa madaraka, (Separation of Powers), Uhuru wa Mahakama, Tunu na misingi ya Taifa, haki za binadamu na mengineyo yanayoingia katika masharti ya kikatiba.

  Pamoja na hayo udhaifu huu wa kisheria bado Bunge la Katiba katika mchakato huu halina mamlaka ya kubadili mambo yote ya msingi katika rasimu ya katiba. Hivyo kwa mujibu wa sheria hii Bunge lina mamlaka kamili ya kujadili na kuboresha rasimu tu na si kutunga rasimu nyingine. Kazi yao ni kupendekeza katiba itakayotiwa mhuri na wananchi kwa kura ya ndiyo.
  Sheria hii ilipaswa kuweka majukumu na mipaka ya Bunge la Katiba kama ilivyokuwa kwa sheria iliyoanzisha Bunge la Katiba la Uganda. Lengo la kufanya hivi ilikuwa ni kuwabana wanasiasa wasihamishie migongano yao kwenye Bunge la katiba.

  Jambo la msingi katika mchakato wa Katiba ni kuangalai chombo hiki kama kinazingatia misingi ya uundwaji wa katiba. Hutegemea pia chombo hiki kinaaminiwa kwa kiasi gani na wananchi, pia utashi wa kufanya kazi yake kwa kuzingatia matakwa ya wananchi na si vikundi vya kijamii ni jambo la kuzingatiwa.

  Kutokana na mkanganyiko huu wa kisheria ni muhimu Bunge la Katiba likapewa elimu kuhusu majukumu yake na mipaka yake. Sheria ilikosea sana kuacha kufafanua zaidi kipengele cha kuonyesha majukumu na mipaka ya Bunge.

  Pili, Mchakato uliotumika hapa Tanzania tayari umeshaiwekea mipaka Bunge Maalumu kubadili Rasimu hii ya pili. Mchakato wa Katiba mpya Tanzania umepitia hatua za msingi zifuatazo:
  i. Kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Bunge la sasa,
  ii. Kuundwa kwa Tume ya Katiba,
  iii. Kukusanya maoni ya Wataalum,
  iv. Kukusanya maoni ya Watanzania,
  v. Kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine,
  vi. Kuchambua na kutathimini maoni ya Wananchi,
  vii. Kuandika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba
  viii. Wananchi kujadili Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba
  ix. Bunge Maalumu kujadili na kuboresha Rasimu ya Pili ya Katiba na hatimaye badaye
  x. Kura za Maoni za Wananchi katika kuridhia ama kukataa Katiba.

  Mchakato huu wa kupata katiba mpya umepata mamlaka katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura 83. Kila hatua kwa mujibu wa sheria hiyo uliwekewa mipaka na madaraka, mfano Tume ilikuwa na mipaka na madaraka yake. Mchakato huu tofouti na Nchi nyingine kama za Misri ndio hasa umeinyima Bunge Maalumu meno na mamlaka ya kuitupilia mbali Rasimu ya Katiba badala yake mchakato huu hutoa mamlaka ya kujadili na kuboresha tu Rasimu.

  Mchakato huu ulikuwa shirikishi na wananchi walishrikishwa toka kwenye utungaji wa sheria yenyewe na hata kwenye uteuzi wa wajumbe wa tume. Upatikanani wa wajumbe wa Tume ulihusisha watanzania kupitia makundi yao kama ya vyama vya sisa, ya kidini, Taasisi zisizo za kiserikali na mengineyo. Pia tume ilizunguka nchi nzima na kukusanya maoni ya wananchi na makundi mengine. Kwa utaratibu na mchakato huu Bunge Maalum kama anavyosema Warioba ni wazi halina mamlaka ya kubadili Rasimu.
  Jinsi ushirikiswaji wa wananchi unavyokuwa wazi ndivyo madaraka ya Bunge Maalum yanavyopungua…mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya madaraka ya wananchi “Pupular Soveregnity”. Jaji Warioba,

  Kwa mujibu wa mchakato wa katiba wa hapa Tanzania Bunge Maalum ni sehemu ya mchakato na kamwe hawawezi kuwa juu ya mchakatato wa katiba. Nasema hivyo kwa kuwa tayari michakato mingine imekwisha kamilika kwa mujibu wa sheria ya mabadilko ya katiba. Kulipa Bunge madaraka ya kubadili rasimu nzima ni sawa na kutaka Bunge lifanye kazi ya mabaraza ya Katiba na kazi ya Tume ya Katiba.

  Tume ya Katiba ilikuwa na majukumu ya kuandaa wananchi na kutoa elimu ya katiba, kukusanya maoni ya wananchi wa aina zote, kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine, kuchambua na kutathimini maoni ya wananchi, kuandika toleo la kwanza, kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu toleo la kwanza na kuandaa tole la pili kwa ajili ya Bunge la Katiba.
  Hivyo basi kusema kuwa Bunge lina mamlaka ya kubadili rasimu nzima ya katiba ni sawa na kusema Bunge lifanye kazi zote zilizokwisha fanywa na hatua za awali za mchakato. Bunge ni hatua ya pili kutoka mwisho wa mchakato wa katiba na halina budi kuheshimu nafasi ya michakato mingine.

  Kudai kuwa Bunge lije na katiba mpya ni sawa na kusema waanze upya kukusanya maoni, wapitie mabaraza ya katiba, wachambue maoni na kuandika rasimu mpya. Je nauliza kama watakuja na rasimu mpya kabisa , watakuwa wametengeneza kwa kutumia maoni ya watu wa nchi ipi au maoni yao wenyewe?. Na kama tulikuwa tunajua Bunge la watu 600 linaweza tengeneza katiba ya watu milioni 44, kwanini tuliruhusu michakato mingine kama ya Tume na ukusanyaji wa maoni ya wananchi?

  Bunge linapewa nafasi kubwa katika hatua ya kujadili (Debating) hasa baada ya wananchi kutoa maoni na Tume kuandaa rasimu. Hivyo Bunge linafanya mjadala wa kitaifa juu ya rasimu ya katiba na kuifanya katiba pendekezwa. Katika kujadili Bunge wanaiboresha rasimu kwa kuangalia vifungu, kuweka masharti na kuboresha mambo mengine kama muundo na lugha. Hapa ndipo eneo ambalo kuna uwezo wa kufikia muafaka mambo ya msingi.

  Nchi nyingine zimekuwa zikialika wataalam kufafanua baadhi ya hoja kwenye hatua ya mjadala. Nchi hizo ni Timor [2002], Afghanistan [2004], Nepal [2014], and Zimbabwe [2000].) Ila katika hatua hii kuna hatari kubwa pia ya kuibuka makundi na kutoelewa kabisa kama ilivyokuwa nchini Kenya 2010.

  Katika mchakato wa kutengeneza katiba, siku zote bunge la katiba haliwezi kuwa Tume ya kuandaa rasimu. Kazi ya kuanda (Drafting) ni ya kitaalum zaidi na ndio maana imeachiwa Tume. Tume inapendelewa kufanya kazi kwa kuwa kwanza nia wachache, wanauwezo wa kitaaluma, pia wanakuwa na nafasi kubwa ya kuaminika na jamii kwa kuwa hawa upande wowote. Pia ni rahisi kukubalika na makundi yote ya kijamii tofouti na Bunge ambalo tayari linamakundi mbalimbali na mengine yanahisi yameachwa nyuma.
  Ingawa katika michakato mingine kama uandaaji wa katiba ya umoja wa nchi za Ulaya, Somalia 2004 mjadala wa Bunge la katiba haukuwepo.Maanake ni kwamba rasimu ilitoka kwa waandaji (Drafters) na kwenda moja kwa moja kupigiwa kura. Mfumo wa maamuzi kuhusu katiba mara nyingi kunapaswa kuwe na chombo kimoja cha kupitisha katiba na wakati wote kura ya maoni imetumika.

  Tofauti na Kenya 2005, ilianza na vyombo vingi vya vya kuridhia katiba, walitumia bunge la kawaida, Tume ya Katiba na mwishoni kwa maamuzi ya mahakama ikaamuliwa kura ya maoni. Nasema kwa amri ya Mahakama kwa kuwa kuna shauri (Njoya v Attorney General [2004] L.L.R. 4788 HCK) lilifunguliwa na kuhoji mwenendo wa mchakato wa katiba Kenya 2002-2005, na baadaye Mahakama kuona walikosea kutokuweka na kipengele cha kura ya maoni.

  Mchakato wa Kenya ulizua migogoro kwa kuwa walikuwa mara nyingi wanakiuka misingi ya uandaji wa katiba. Mfano wao Kenya walitumia bunge la kawaida kama chombo cha kuridhia katiba ya nchi.Mchakato wa Kenya ulianza 1997 lakini katika makundi makundi, ndipo badaye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Prof Yash Pal Ghai akafanikiwa angalau kuunganisha kundi la wanasiasa na lile la makundi ya kijamii na kidini (Ufungamano).

  Baada ya Serikali ya Arab Moi kung’olewa madarakani na Muungano wa Upanga Mwekundu (NARC),Tume ya Katiba (KCRC) iliendelea na mchakato. Na baadaye Ghai draft ya katiba ikapatikana ali maarufu kama Bomas Draft. Baadaye serikali kupitia mwanasheria mkuu wa Kenya wakaanda rasimu yao iitwayo Wako’s Draft nayo ikapingwa vibaya kwenye kura za maoni 2005. Na kuazia hapo Kenya ikaingia kwenye mgogoro wa kikatiba na kuwa chanzo kikuu cha machafuko ya mwaka 2007-2008.

  Taswira ya Kenya toka 2000-2008 inatuonyesha ni jinsi gani tusipokuwa makini katika mchakato wa katiba tunaweza itumbukiza nchi katika mgogoro mkubwa. Ndipo baadaye Tume ya Maridhiano kupita sheria ya mabadiliko ya Kenya ya 2008 (Constitution of Kenya Review Act, 2008) ikaanzisha mchakato mpya hadi kupata katiba mpya 2010. Mchakato ulipitia muundo wa hatua 4; Kamati ya Wataalam, Bunge la Katiba, Kamati za Bunge la Katiba na Kura za Maoni.

  Lakini wakati mwingine matumizi ya kura za maoni yanaweza kuwa na faida na hasara na inategemea sana michakato mingine imekwendaji kuanzia kwenye kukusanya maoni na Bunge la katiba. Nchi nyingi zimeingia katika mgogoro sana katika mchakato wa kura za maoni mfano huo ni nchi jirani ya Kenya (2005 na 2010) na Iraq 2004. Lakini kuna nchi zingine ili kunusuru migogoro hupeleka hoja ambayo ina mvutano mkubwa kwenye kura za maoni na zingine kuishia Bungeni, Mfano 2008 Maldives walifanikiwa kufanya hivyo.

  Tanzania kama Bunge litashindwa kuridhia suala la Muundo wa Muungano wanaweza wakaacha ili badaye ipigiwe kura ya maoni na wananchi kama suala linalojitegemea. Lakini ukweli unabakia kuwa kura za maoni ni njia nzuri ya kujua kama maoni ya wananchi yamezingatiwa kwenye katiba inapendekezwa.

  Tatu, Muundo wa Bunge hili Maalum linajinyima nguvu ya kuwa na mamlaka ya kubadili Rasimu ambayo inanguvu ya wananchi. Bunge la Katiba halipaswi kuwa na sura ya Bunge la uwakilishi la kawaida. Bunge la Katiba linapaswa kuwa na mkusanyiko wa makundi karibu yote ya kijamii na siyo vinginevyo. Bunge hili limeundwa kwa aslimia 75 na Bunge la sasa na Baraza la Wawakilishi, kitaalum tayari Bunge hili Maalum linakosa uhalali wa kuitwa Bunge la Katiba kwa kuwa halina tofauti na Bunge la sasa na Baraza la Wawakilishi.

  Miaka ya nyuma kupitia sheria ya Bunge la Katiba miaka ya 1961, ilikuwa ni Bunge hilo hilo la kawaida linageuzwa kuwa Bunge la Katiba. Utaratibu huo ndio umefanya katiba ya sasa ikose uhalali wa kikatiba. Barani Africa nchi nyingi baada ya Ukombozi kuanzia miaka ya 1960-1980 zimekuwa zikutumia katiba ambazo hazikufuata utaratibu mzuri na shirikishi katika kuziandaa. Mchakato huu wa kugeuzwa mabunge ya kawaida kuwa Bunge la Katiba mara nyingi huondoa uhalisia wa kuwa na katiba ya wananchi. Kuanzia mwaka 1990 tumeshuhudia vuguvugu la kutaka kupata katiba za wananchi na si za watawala. Uganda mchakato ulianza 1988 -1995, Kenya ulianza 1997-2010 na Tanzania sasa ilianza 1998- 2014.

  Bunge letu hili pia nalo ni wazi kuwa ni lile lile bunge la kawaida limegeuzwa kuwa Bunge la Katiba na Rais kutumia nafasi yake ya viti maalum kuwateuwa wanasiasa 201 kujiunga na wanasiasa wenzao kujadili rasimu ya katiba ya Watanzania.Bunge Maalumu linapaswa kushirikiksha makundi yote ya wananchi. Kundi ambalo limechukua asilimia 75 ya Bunge la sasa ni wanasiasa na mmbaya zaidi wanasiasa wa upande mmoja.

  Tulipaswa kulitambua hili kabla ya kuamua idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba. Mbaya zaidi hata wale wajumbe 201 ambao wangepaswa kwa mujibu wa sheria kutoka katika makundi yasiyo ya kisiasa tumeona nao wanatoka kwa asilimia zile zile 75 toka kundi lile lile la wanasiasa. Kati ya wajumbe hao 201 kulikuwa na nafasi 40 tu za wanasiasa, lakini cha kushangaza tumeona wanasiasa na viongozi wa vyama vya siasa hasa CCM wakiteuliwa kupitia nafasi za makundi mengine. Mfano, Katika kundi la Asasi za Kiraia, katika nafasi ya watu 20 wajumbe takribani 10 ni makada na viongozi wa CCM, halikadhalika katika makundi mengine hali ni hiyo hiyo ya uwepo wa makada na viongozi wa vyama vya siasa.

  Muundo huu wa Bunge la Katiba, tayari umeipokonya Bunge hili madaraka ya kubadili ama kutunga Rasimu mbadala kwa kuwa halina makundi yote ya kijamii. Na kama watabadilisha Rasimu hii, ni dhahiri kuwa Katiba hiyo itakuwa ni ya vyama vya siasa hasa chama chenye wajumbe wengi Bungeni (CCM). Na endapo watabadilisha mambo ya msingi ni wazi Katiba hiyo itapigiwa kura ya hapana na wananchi kwa kuwa wameondoa maoni ya wananchi na kuweka maoni ya vyama vyao (Hasa chama chenye makada wengi kwenye Bunge la Katiba). Bunge hili lingepaswa kuwa na moja ya tatu (1/3 ya wanasiasa tena wa vyama vyote) na mbili ya tatu (2/3) wa makundi ya kijamii ili angalau liweze kujiongozea uhalali wa kubadili mambo ya msingi.

  Muundo huu tayari wazi wazi umejionyesha unamakundi ya kisiasa yenye misimamo tofouti. Kwa kuwa hali hii ilishaonekana mapema, Rais Kikwete alipaswa kutumia busara ya hali ya juu kupunguza nguvu ya wanasiasa Bungeni kwa kuteuwa makundi yasiyo na uhusiano na vyama vya siasa, badala yake wote ni mashaidi wateule karibu wote ni wanasiasa.

  Mchakato wa katiba ya Uganda 1980-1995 ulikuwa na taswira nzuri kwa kuwa wajumbe 230 wa Bunge la Katiba walipigiwa kura na kuchaguliwa na si kuteuliwa. Wakati mwingine utaratibu huu unaweza rudisha imani ya wananchi. Na mchakato kama huu wakati mwingine hulipa bunge hilo sio mamlaka ya kujadili bali kuwa chombo cha mwisho kupitisha katiba. Tume ya Katiba chini ya Jaji Ben Odoki iliundwa kukusanya maoni na kuandaa rasimu na badaye kupelekwa katika bunge kuidhinishwa.

  Nne, Bunge la katiba ni taasisi ndani mchakato wa katiba. Tofouti na mabunge ya kawaida Bunge la Katiba sio chombo cha uwakilishi bali ni taasisi inayojitegemea katika mchakato wa katiba. Taasisi haihitaji uwakilishi na wala si chombo cha uwakilishi na ndio maana yoyote yule anaweza kuwa mjumbe wa chombo hiki bila kuzingatia kachaguliwa na wananchi ama lah.

  Tunasema si chombo cha uwakilishi kwa kuwa wao wamepatikana kwa mujibu wa sheria, lakini wabunge wa mabunge ya kawaida huchaguliwa na wananchi. Chombo hiki kimewekwa Kama taasisi muhimu ndani ya mchakato wa katiba kwa lengo la kujadili na kuboresha rasimu ya katiba itokanayo na wananchi wenyewe. Ila nchi nyingine taasisi hii hutumika moja kwa moja bila kuwa na Tume ya kukusanya maoni.

  Tufauti kubwa ya chombo hiki na Bunge la Kawaida, ni kwamba hujadili rasimu ya katiba, kuiboresha na kutengeneza katiba itakayopigiwa kura na wananchi kwa lengo la kuhakiki kama mawazo yao kupitia Tume yamezingatiwa na chombo hiki cha kikatiba ama siyo. Lakini Bunge la kawaida hutunga sheria na kupeleka kwa Rais kama sheria iliyopendekezwa ili kupitishwa na Raisi kama sheria kwa niaba ya wananchi. Katika mchakato huu Rais amepewa mamlaka kwa kuwa sheria nyingi hutungwa bila kuwahusisha wananchi. Lakini kwa sheria mama ya nchi, wananchi walitoa maoni na ndio maana wao ndio wenye kauli ya mwisho na si Bunge la Katiba.

  Uwepo wa kura za maoni, hueleza wazi wazi kuwa Bunge la Katiba si chombo cha uwakilishi na pia hakina maamuzi ya mwisho. Umuhimu wa kura za maoni ni kwa ajili ya kuhakiki kama mawazo ya wananchi kupitia chombo yamezingatiwa na Bunge la Katiba. Kwa utaratibu inakuwa ni vigumu kusema Bunge la Katiba lina madaraka kuja na katiba ambayo ni tofouti na rasimu ya wananchi. Kama Bunge la katiba lingekuwa chombo cha uwakilishi tusingekuwa na haja ya kupiga kura za maoni kwani wale ni wawakilishi wetu.

  Na kama watafanya hivyo watachukuwa mawazo ya nani kwa kuwa wao sio chombo cha uwakilishi bali ni chombo tu ndani ya mchakato wa katiba wenye mamlaka ya kupendekeza katiba kwa wananchi baada ya kujadili rasimu ya katiba.Itambulike kuwa chombo hiki hakitengenezi rasimu tena bali kinaanda katiba itakayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.

  Kama tungefuata utaratibu sahihi Bunge la katiba lisingekuwa na wabunge wala wawakilishi, bali lingekuwa na wajumbe si zaidi ya 300 wakiwemo baadhi ya wabunge na wawakilishi. Tena wangepigiwa kura kama ilivyokuwa Uganda.

  Namalizia kwa kuwashauri wabunge wa Bunge hili maalum wakizingatia mamlaka waliyopewa na wasiende zaidi ya mamlaka na madaraka yao kwani watakuwa wanaandaa katiba itakayokuja kupigiwa kura ya hapana.Na pia vigumu jopo la watu 600 tena wenye itikadi za kisiasa kukaa chini na kuanza kuandaa rasimu mpya. Kuandaa rasimu si jukumu la Bunge la Katiba bali wao wanajukumu la kuipa rasimu nguvu ya kuitwa katiba, pia kuandaa rasimu kuna hitaji utulivu na utaalamu na ndio lengo la kuwa na Tume ya watu wachache ambao pia pamoja na kupata maoni ya wananchi bado utaalamu wao utahitajika.

  Ni wazi kuwa michakato ya uandaaji wa katiba hutofoatiana toka nchi moja hadi nyingine. Nchi kama Misri waliunda Tume ambayo haikukusanya maoni ya wananchi bali waliandaa rasimu kama Tume ya Wataalum. Tunawasihi wasipeleke misimamo ya vyama kwenye Bunge la Katiba kwani kufanya hivyo ni sawa kuwadharau Watanzania na kuchezea rasimali za nchi.

  Bunge la Katiba lisipozingatia haya, watakuwa wanajiweka katika mazingira ya kufunguliwa kesi kwa kuvuruga mchakato wa katiba kama ilivyokuwa huko Kenya. Tunalitazama na endapo watakwenda kinyume tutaenda mahakamani.

  Na Onesmo Olengurumwa
  Mchambuzi na Mtafiti-Haki za Binadamu na Sheria
  opngurumwa@gmail.com

  [*Maoni haya yalichapishwa katika baadhi ya magazeti. na yanachapwa hapa kwa idhini ya mtoa maoni katika kupanua mjadala ulioanzishwa na Makala ya Prof. Issa Shivji – Moderator]

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box