FIKRA ZA MWALIMU NYERERE JUU YA AMANI

Utangulizi
Ni rahisi siku hizi kuhubiri kwa jazba kabisa kwamba Mwalimu alipenda amani; alitetea amani; alieneza amani na kadhalika. Lakini sio kawaida kufanya uchambuzi wa kina wa mtazamo wa Mwalimu wa kifalsafa na kwa hivyo kuainisha misingi mikuu ya amani ambayo yeye aliona ni muhimu. Mwalimu alijitahidi kujenga misingi ya amani na aliamini katika misingi hiyo.

Kwa maoni yangu amani haihubiriwi wala haiombwi. Amani inajengwa kwa kufuata misingi yake mikuu. Siku hizi ni kawaida kuhubiri amani wakati unatenda au unatetea mfumo ambao haufungamani hata chembe na misingi ya amani.

Kwa hivyo, katika mada yangu ya leo ningependa, kwanza, kuainisha na kuchambua misingi ya kifalsafa ya amani ambayo Mwalimu alikuwa anaisisitiza kila mara. Pili, ninaainisha mfumo wa maendeleo ambao mtu yeyote anayeamini kwa dhati katika amani hana budi kuutetea na kuusimamia. Na mwisho katika kuhitimisha nitauliza maswali kuhusu mitazamo na mifumo tunayoisimamia siku hizi na kudadisi uwezo au udhaifu wake wa kujenga amani.

Misingi miwili ya amani
Mwalimu alijikita kwenye misingi miwili muhimu ya amani: moja, ni dhana ya usawa wa binadamu, na pili, ni dhana ya haki-jamii (social justice). Nianze na usawa.

Nini maana ya usawa?
Ukweli ni kwamba kwa kuangalia juu juu tu binadamu wote sio sawa. Wana maumbile tofauti; wana rangi tofauti – wengine ni warefu na wengine ni wafupi kama mimi. Na wana jinsia tofauti. Na pia wana vipaji tofauti. Sasa katika hali hii nini maana ya kusema kwamba binadamu wote ni sawa!?. Binadamu wote ni sawa katika UTU wao, katika UBINADAMU wao. Sifa ya mtu kuwa na utu ni ya kipekee; ni ya binadamu tu; mnyama hana utu. Katika UTU binadamu mmoja hatofautiani na binadamu mwingine.

Usawa wa binadamu unasemwa kama vile ni dhana rahisi sana na kwa kweli dhana hii haipingwi popote pale. Hata mpinga-maendeleo au mbaguzi, kinadharia, hawezi kuupinga usawa wa binadamu. Lakini dhana yenyewe ina uzito wa kipekee katika mapambano ya maendeleo ya binadamu. Mapambano ya kujenga usawa ni mapambano ya muda mrefu, ya zaidi ya karne kumi na bado hatuna usawa. Pamoja na mapambano hayo ya muda mrefu bado kuna aina nyingi za ukosefu wa usawa. Kwa hiyo, katika hali mbalimbali, mazingira mbalimbali, kwa sura na njia mbalimbali, mapambano ya kuleta usawa yanaendelea. Ingawa mapambano haya yanaendelea, mapambano hayo ya kudai usawa yanapingwa kote kwa ukali, tena kwa ukali wa kikatili .

Ni vema tukatambua kwamba, tendo lolote lile linalodhalalisha utu ni kinyume cha usawa. Hivyo basi
Ujinga unadhalilisha utu;
Maradhi yanadhalilisha utu;
Umaskini unadhalilisha utu;
Unyonyaji unadhalilisha utu;
Ukandamizaji unadhalilisha utu; na
Unyanyasaji unadhalilisha utu.
Na kwa kuwa ubepari ni haya yote, Basi ;
Ubepari unadhalilisha utu;
Kwa hivyo, ubepari ni ushezi;
Ubepari ni unyama; sio ubinadamu.
NDIVYO ALIVYOAMINI MWALIMU.

Kwa maana na mantiki hiyo, huwezi ukawa na amani kama huna usawa wa binadamu. Msingi mkuu wa amani ni usawa.

Msingi wa usawa una ngazi mbili. Ngazi ya kwanza ni haki ya mtu mmoja mmoja, at the individual level. Ngazi ya pili ni haki-jamii, hii ni ngazi ya watu kwa ujumla wao, yaani, ujamaa at the collective level.

Nini maana ya haki-jamii?
Labda ningeweza kufafanua maana ya haki-jamii, nikitofautisha haki-jamii (social justice) na haki-sheria (legal justice). Haki-sheria maana yake ni kila mtu ana haki sawa mbele ya sheria. Huu ni msingi wa mfumo wa kibwanyenye. Sheria haijali wewe ni nani – maskini au tajiri – wote mna haki sawa. Na wote, maskini na tajiri, wana haki, kwa mfano, haki ya kuishi. Kisheria, maskini na tajiri wana haki ya kuishi. Lakini katika hali halisi usawa huo ni wa kinadharia tu, hauna maana kwa sababu maskini na tajiri, kwa vyovyote vile sio sawa. Haki-sheria haiangalii hali halisi; haijali tofauti za kijamii na za kiuchumi kati ya mtu na mtu. Kwa sababu kinacholinganishwa katika dhana hii sio ubinadamu bali ni haki. Sheria haijali kama mie ni maskini au tajiri; wala haijali uwezo wangu kiuchumi au kitaaluma. Inanipa haki, kama sina uwezo wa kufurahia haki yangu ni shauri yangu, sio hoja kisheria. Ndiyo maana ya haki-sheria, yaani, haki inayotokana na sheria.

Haki-jamii ni tofauti. Haki-jamii hutokana na hali halisi ya jamii. Haki-jamii inatambua kwamba mfumo wa jamii ndio huzaa tofauti za kitabaka. Na kama katika jamii kuna tofauti kati ya maskini na tajiri, kati ya mjinga na mwerevu, kati ya mwenye shibe na mwenye njaa, basi kamwe huwezi ukawa na haki katika jamii kama hiyo. Kwa ufupi, haki-sheria ni kiini macho.

Katika falsafa na mtazamo wa Mwalimu, usawa wa binadamu na haki-jamii vinafungamana, ni mapacha. Huwezi ukawa na usawa wa binadamu bila haki-jamii. Ndiyo maana Mwalimu alisisitiza kwamba Amani hujengwa juu ya msingi wa usawa na haki-jamii. Bila usawa, hukuna haki, na bila haki hakuna amani.

Mtazamo wa maendeleo
Mwalimu alitumia misingi hii miwili ya kifalsafa, yaani haki-jamii na usawa wa binadamu, kujenga hoja zake katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Kila mara alipigania uwepo wa usawa kati ya nchi tajiri za Kaskazini na nchi maskini za Kusini. Alisisitiza kwamba tofauti kubwa za utajiri na umaskini kati ya nchi hizo ndio zinahatarisha amani. Mapema mnamo mwaka wa 1963, akipotubia mkutano wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) huko Roma, Italia Mwalimu alisema, ninanukuu:

There is no doubt, therefore, that for reasons of human dignity, and for the sake of peace and justice, these economic inequalities in the world must be reduced and the mass of the people must be able to relieve them from the burden of poverty. … …
And for good or evil, mankind has been so created that many will refuse to acquiesce in their own degradation; they will destroy peace rather than suffer under it.

Anachosisitiza Mwalimu ni kwamba bila kupunguza pengo kati ya utajiri na umaskini katika dunia, hutaweza kupunguza, na hatimaye kufuta umaskini; na bila kufanya hivyo hutakuwa na amani. Kimaumbile, binadamu hawezi kustahamili kudhalilishwa; ataangamiza amani badala ya kuteseka chini yake.

Katika ngazi ya taifa, Mwalimu alitoa hotuba yake ya kipekee mnamo mwaka wa 1989, wakati kulikuwa na uvumi wa kuzika Azimio la Arusha. Namnukuu:

Lakini Waswahili wanasema ukiona vyaelea vimeundwa. Vimeundwa. Sio tu utulivu umekuja wenyewe tu. Utulivu wa Tanzania sio kwamba Azimio la Arusha limeondoa umaskini hata kidogo. Umaskini si huu bado tunaendelea nao? Si huu mpaka leo? Uchumi si huu huu bado tunasumbuka nao? Si kwamba Azimio la Arusha limeondoa umaskini hata kidogo, wala halikutoa ahadi hiyo. Azimio la Arusha limetoa ahadi ya matumaini. Ya haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio watu wengi wa Tanzania wanaendelea kuwa na matumaini hayo. Madhali yapo matumaini hayo, mtaendelea kuwa na amani. Hapa tuna umaskini Tanzania, lakini hakuna ‘social cancer’. Inawezekana, sijui kama kameanza anza kidogo, sijui; lakini hatuna ‘social cancer’. hakuna ‘volcano’ inayojengeka kwamba ukiweka sikio chini hivi, unasikia hiyo ‘volcano’ inajengeka na kwamba siku moja italipuka tu. Hatujafika hapo bado kwa sababu watu bado wana matumaini yanayotokana na msimamo wa Azimio la Arusha. Halikuondoa umaskini lakini limewapeni wote nyinyi wa chumba hiki, mabepari na wajamaa, limewapeni nafasi hiyo – kwamba mjenge nchi ina matumaini kwa wengi. Bila hivyo hamna, watakataa; na mtawafanyaje? Hivi kweli mtawafanyaje? Hivi kweli Waswahili wachache nyinyi mtawale Watanzania kwa nguvu bila matumaini, halafu watakaa tu kwa amani – amani ya matumaini – matumaini yakiisha kutakuwa na ghasia za kijamii na nitawashangaa Watanzania hawa wakatae kufanya ghasia. Kwa nini?

Hivi sasa katika kofia yangu ile nawaambia Wazungu wa Kaskazini. Nasema hivi, msingi wa amani duniani ni haki. Kwa hiyo, kama mnataka amani ya kweli sio kwamba mashariki na magharibi mzungumze yaishe, hata kidogo. Kwa hiyo, mtakuwa mnaondoa migogoro yenu mtaona mmetengeneza namna moja ya haki, lakini bila kuondoa migogoro ya Kaskazini na Kusini, amani tutaikataa sisi. Haitakuwa dunia ya amani kwa sababu ni watu sisi, na ndani ya kila nchi ni hivyo hivyo. Uingereza ni hivyo hivyo, Marekani ni hivyo hivyo, Ujerumani ni hivyo hivyo na Tanzania ni hivyo hivyo.

Kama wengi hawana matumaini, tunajenga ‘volcano’. Siku moja italipuka na lazima ilipuke. Isipokuwa watu hao wawe wajinga. Wengi kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa hivi hivi na wingi wanao, wajinga hao. Kwa hiyo, Watanzania hawa watakuwa wajinga, wapumbavu, kama wataendelea kukubali kuonewa na watu wachache katika nchi yao. Kwa nini? Kwa hiyo hatuwezi tukasema sasa eti umefikia wakati tukasema Azimio la Arusha tulisahau. Msijidanganye hivyo. Hiyo ni sawa na mjinga ametumia ngazi amepanda amefika juu, halafu anaipiga teke ile ngazi. Unaipiga teke ile ngazi, haya kaa huko maana tutakata jiti sasa. Sisi tuko chini, wewe uko juu; ngazi umekwishaipiga teke, tutaliangusha sasa jiti – nalo ni refu hili. Kishindo chako cha kuanguka bwana kitakuwa kikubwa kweli ; tusiseme hivyo.

Anachosema Mwalimu ni wazi kabisa. Bila matumaini ya kujenga jamii yenye usawa na haki-jamii, mtapoteza amani kwa sababu Watanzania sio wapumbavu. Hawawezi wakala amani. Wataipinga, wataiangamiza amani ya wachache badala ya kuendelea kuvumilia unyonge, dhuluma na umaskini.

Hitimisho
Katika kuhitimisha mada yangu niulize swali moja tu: Je, baada ya takriban miongo miwili tangu Mwalimu atoe hotuba niliyoinukuu, bado hakuna ‘social cancer’? Au watawala na matajiri wetu siku hizi hawaweki masikio yao chini ya ardhi – wanaruka hewani kwa hivyo hawasikii kuna ‘volcano’ inanguruma. Leo jamii yetu imepasuka, hakuna usawa wala haki-jamii wala hakuna matumaini kwamba sote kwa pamoja tunajenga jamii yenye usawa na haki-jamii. Na kutokana na ukweli huu, tumerudi nyuma, tena sana. Leo jamii yetu ina ubaguzi wa kila aina – udini umeingia, ushirikina umezagaa, ukanda, ukabila, ubaguzi wa rangi, ukanda usiseme. Tena mbaya kuliko yote, tunachanganya bila aibu dini na siasa. Hiyo ni sawa na kuchanganya petroli na majani makavu. Itawaka. Ikiwaka itaangamiza hii amani na utulivu tunaojivunia.

Huwezi ukapiga teke ngazi ya kwenda juu, halafu ukafikiri kuwa utaweza kurejea chini ukiwa salama. Ni ndoto ya mchana. Huwezi ukatupilia mbali misingi ya kujenga usawa wa binadamu na haki-jamii, halafu ukajidai kuwa unajenga amani kwa kuhubiri au kuomba.

Kama nilivyoeleza katika utangulizi wangu: Amani haihubiriwi wala haiombwi. Amani inajengwa na ina misingi yake. Misingi hii nimeitaja. Kwa upande wangu, unapofuata misingi hii, unadhamiria kujenga jamii inayoitwa Ujamaa. Ukijigamba kwamba Ujamaa umepitwa na wakati, basi ukubali kwamba amani pia imepitwa na wakati.
Kila la heri!

***

Kabla sijakaa, nichukue nafasi hii ya kuwatangazia rasmi habari njema. Takriban miaka mitatu iliyopita, pamoja na wanazuoni wenzangu wawili, Profesa Saida Yahya-Othman na Dkt. Ng’wanza Kamata, tulianza kufanya utafiti ili kuandika biografia ya Mwalimu tukiwezeshwa na Tume ya Sayansi na Teknologia, COSTECH. Tumekusanya taarifa nyingi tu na sasa tuko katika hatua ya kuandika. COSTECH wamekubali kuanzisha Nyerere Resource Centre (au Kituo cha Mwalimu Nyerere cha Kufikirisha) ambacho kitahifadhi nyaraka zote tulizokusanya ili watafiti wetu waweze kufaidika. Kuna mengi ya kuandika kutokana na fikra za Mwalimu. Pamoja na kuwa mahali pa kufanyia utafiti. Kituo hiki pia kitakuwa na programu za kuandaa shughuli mbalimbali zote zikiwa na lengo la kupanua uelewa wetu wa fikra za Mwalimu.

Tunatarajia kuzindua Kituo hiki mapema mwaka ujao. Tutahitaji ushirikiano wenu.
Ahsanteni.

 

[Mada hii iliwasilishwa kwenye Kongamano la Kuadhimisha Miaka Kumi na Mitano ya Kumbukumbu za Mwalimu tarehe 17 Oktoba 2014, Makumbusho ya Taifa. Kongamano liliandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF)]

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box