GORAN HYDEN, NADHARIA YA USASA NA MUSTAKABALI WA WAKULIMA WAVUJA JASHO

Makala haya ni kumbukumbu ya Kongamano lililoandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kutabaruku kazi za mwanazuoni Prof. Goran Hyden. Kongamano hilo lilifanyika Jumamosi, 9 Juni 2012 katika Hoteli ya Serena iliyokuwa ikijulikana zamani kama Moven Pick.

Kama kawaida, sehemu kubwa ya walioalikwa ni wale ‘waliozaliwa mara ya pili’ kitaaluma, wakala kiapo cha kuutumikia ubepari kwa mioyo na akili zao zote. Hao ni wahadhiri, wanafunzi wa uzamili na baadhi ya watumishi wenye nyadhifa za juu serikalini kama Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu, Katibu Mkuu mstatafu wa EAC, Balozi Juma V. Mwapachu na wengineo. Prof. Hyden mwenyewe pia alikuwepo.

 Nadharia ya usasa
Goran Hyden mwenyewe ni kati ya wana-nadharia wa usasa (modernisation theory). Wanausasa waitazamapo Afrika, hudai kuwa inajididimiza yenyewe kiuchumi kwa kuendelea kukumbatia mifumo ya kijadi ya maisha na uzalishaji. Waafrika husemekana kutokuwa na uwezo wa kiteknolojia na kiakili wa kujiletea maendeleo. Hivyo ili Waafrika waweze kuendelea sharti waachane na ujadi, wapambane kuvutia mitaji na teknolojia toka ughaibuni ili wajenge ubepari. “Beparika utajirike”, wanausasa huimba.

Mjadala ukaanza
Hivyo mjadala ulipoanza, vitabu vya Goran Hyden vikachambuliwa. Kilichoibua mjadala hasa ni kitabu chake kiitwacho “Beyond Ujamaa in Tanzania: Underdevelopment and an Uncaptured Peasantry”. Kwa bahati mbaya washiriki wengi hawakuwa na hamasa ya mjadala wa tafakuri tunduizi. Wengi waliishia kukubaliana na Goran badala ya kuhoji nadharia yake.

Goran anadai kuwa mkulima mdogo (peasant) hajatekwa (uncaptured). Mkulima mateka (captured peasant) ni yule azalishae kwa ajili ya soko, mwenye kutumia mbinu na dhana za kisasa, na mwenye kiu ya kulimbikiza faida. Kwa ufupi, ni mkulima bepari.

Walipozungumzia hali ya sasa, washiriki walikiri hata kuwa bado mkulima mdogo (peasant) haja-sasaishwa [najaribu kuunda kitenzi cha usasa, yaani modernization]. Wakamuuliza Goran: “Sasa tutafanyaje ili kumbadili peasant awe farmer?”

Majibu ya Goran yalikuwa bado ni mwendelezo wa fikra zake za usasa. Goran aliingia katika historia na kudai kuwa makosa ya awali kabisa yalifanywa na serikali ya awamu ya kwanza. Si ajabu kuwa jitihada za kumsasaisha mkulima zilishindwa. Kwa nini zilishindwa?

Mosi, Goran alidai, mkulima mwenyewe aliendelea kugoma. Hii ni kwa sababu aliendelea kukumbatia tabia za kijadi na hivyo kumfanya kuishi katika uduni wa maendeleo uliojikita katika uchumi wa kufadhiliana (economy of affection).

Pili, serikali ya Mwl. Nyerere iliendelea kutumia mbinu za ushawishi ikiwemo kuwapatia zawadi wakulima. Zawadi hizo ni kama huduma za bure za elimu, afya, maji n.k. Hii iliendelea kuwafanya wabweteke na hivyo kutokuwa na ari ya kuongeza uzalishaji.

Walipopewa dhana pamoja na pembejeo za kisasa, wakulima hao waliziuza kwa wakulima mabepari au walanguzi na kutumia fedha hizo kununua pombe, kuoa, kufanya sherehe na matambiko ya kijadi. Kwa maneno mengine ni kuwa watu hawa wanaoishi katika ukale hawaelewi thamani ya maendeleo ya kisasa.

Goran aliendelea kusema kuwa Mwongozo TANU wa 1971 uliwapa nguvu kubwa wafanyakazi, hasa wale wa viwandani. Kutokana na Mwongozo yakaundwa mabaraza ya wafanyakazi yaliyowapa nguvu za kuwagomea mabosi warasimu.

Pia wafanyakazi waliongezewa stahiki zao na kupewa likizo n.k. Mafao hayo yalitumwa kwa ndugu zao huko mashambani na muda wa likizo pia ulitumika kutembelea ndugu, kuhudumia wagonjwa, n.k. Haya yote yaliendeleza uchumi wa kufadhiliana na kudidimiza uzalishaji  viwandani na mashambani.

Goran akatoa mfano wa serikali iliyowahi kuitawala Afrika na kufanikiwa, kwa kiasi fulani, kumbadili mkulima. Ni serikali ya kikoloni. Mbinu zilizotumika ni pamoja na kuwanyang’anya ardhi wakulima kisha kuwageuza manamba katika mashamba ya wakoloni, na huko wakajifunza kilimo cha kisasa. Halikadhalika Waafrika wakalazimishwa kulipa kodi hali iliyowalazimu kuzalisha mazao ya biashara kwa ajili ya viwanda vya Ulaya.

Goran Hyden akaenda mbali na kusema kuwa tunaweza kujifunza toka kwa wakoloni. Akasisitiza kuwa kamwe hakutakuwa na maendeleo iwapo mkulima huyu hatabadilishwa! Sharti abadilishwe ndipo nchi itaweza kupiga hatua. Akaongeza kuwa ujio wa wakulima wakubwa (wawekezaji katika kilimo) usipingwe. Ni mbinu njema ya kisasa ya kuongeza tija katika uzalishaji na kutoa mfano kwa wakulima wadogo kujifunza.

Tuukosoe usasa
Ebo!? Wachache wetu tulishangaa na kujiuliza, “iweje mwanausasa huyu atoe mawazo ya aina hiyo nasi tukayakumbatia pasi na kuyahoji?” Hivyo, tukapiga moyo konde na kuomba kuchangia.

Kwanza, tulihoji uhalali wa nadharia ya usasa na wanausasa wenyewe katika kuleta maendeleo. Hii ni nadharia ya kibwenyenye inayowagawa watu katika makundi mawili. Kundi la “sisi” wana-usasa, tuliostaarabika na kuendelea; na “wao” wana-ukale wasiostaarabika na wanaojididimiza kimaendeleo. Hivyo, kundi la wanausasa hujiona lina haki ya kuwabadili wanaukale.

Hivyo ndivyo nchi za kibeberu zilivyoitazama, na zinavyoitazama, Afrika! Waliowapeleka Waafrika utumwani ama wakoloni walihalalisha biashara hiyo haramu kama mbinu ya kumstaarabisha na kumuendeleza Mwafrika. Mwafrika alionwa kama nusu-mtu, nusu-mnyama, asiye na akili za uvumbuzi na asiyejua thamani ya maendeleo.

Nitatoa mfano. Mwaka 1899 Winston Churchill, ambaye baadae alikuja kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza (1940–1945, na 1951–1955), aliandika ripoti kuhusu Sudani.

Katika ripoti hiyo Churchill aliwabainisha Waafrika wenye ngozi nyeusi kama “washenzi wenye akili fupi, walioishi kama tunavyoweza kuwafikiria watu wa zama za giza – kuwinda, kupigana, kuoana na kufa. Kikomo cha fikra zao ni kutimiza hamu zao za kimwili, na hawana hofu isipokuwa zisababishwazo na mapepo, uchawi, ibada za mizimu, na kila aina ya ushirikina ufanywao na watu wasio na maendeleo. Udogo wa akili yao ni udhuru tosha wa matendo yao yasiyo na hata chembe ya ustaarabu”.

Churchill, kama ilivyokuwa kwa wasomi wengine wa kikoloni, alisema kuwa nchi zilizostaarabika zina wajibu za kuwastaarabisha (au kuwasasaisha) washirikina wa Kiafrika. Naam, Bara letu likaletewa ustaarabu. Kwanza, babu na bibi zetu wakapelekwa katika utumwa ili kustaarabishwa. Baada ya utumwa tukaletewa ustaarabu wa kikoloni. Baada ya ukoloni ukaja ukoloni mambo-leo, ambao sasa unaitwa ubinafsishaji, uwekezaji na soro huria.

Mtazamo wa Churchill ni mtazamo wa nadharia ya usasa, inayoshabikiwa na akina Hyden. Mwafrika analaumiwa kwa kujididimiza mwenyewe. Katu wanausasa hawasemi jinsi ubeberu katika sura zake za utumwa, ukoloni na sasa uliberali mamboleo ulivyoidumaza, na unavyoendelea kuididimiza Afrika!

Naam, wachache tukaendelea kuhoji: kama ilivyokuwa kwa wakoloni, na sisi “wasomi tuliostaarabika na kuishi maisha ya kisasa”, tunakaa katika Hoteli ya nyota tano (baada ya mfadhili kutoa pesa) na kujadili jinsi ya kumbadili peasant awe farmer? Tena tunasema eti wakoloni walifanikiwa kidogo? Tuna tofauti gani na mabeberu? Je, tuna uhalali gani wa kufanya hivyo?

Ndivyo tufanyavyo wasomi, na ndivyo wafanyavyo watunga sera na watekelezaji wa sera. Na hivyo ndivyo mkakati wa “Kilimo Kwanza” ulivyoundwa. Matajiri kadhaa wakakaa na Mkuu wa Nchi hotelini, wakajadiliana huku wakinywa vinywaji laini na vyakula vinono. Halafu kesho yake tukasikia kaulimbiu: “Enyi wakulima msiostaarabika, sasa ni zama za Kilimo Kwanza. Achaneni na jembe la mkono, nunueni Power Tillers”. Ni mkulima gani mdogo aliyealikwa ili kuunda mkakati huo?

Swali likarushwa kwa Profesa mmoja mtaalamu wa sera za umma: Je, hukutufundisha darasani kwamba sera bora ni ile inayoanzia chini (bottom) na kwenda juu (up)? Kama hivyo ndivyo, kwa nini basi tusiende kwa huyo mkulima ili kujifunza badala kumuelimisha? Je, sisi tunajua mahitaji yake kuliko yeye mwenyewe? Profesa akabaki ameduwaa, maana naye ni shabiki wa usasa.

Na hapo ndipo nikakumbuka kisa cha yule msomi mwenye ma-digrii mengi ya kilimo/ufugaji aliyetumwa na serikali kwenda kuwastaarabisha Wamasaai. Kisa hiki kipo katika riwaya ya Profesa Chachage iitwayo Almasi za Bandia.

Basi mtaalam huyo na msaidizi wake walitembea umbali mrefu kwa siku kadhaa pasi na kuona makazi yoyote. Wakiwa wamekaribia kukata tamaa, kwa mbali wakaona manyatta. Wakakimbia kuifuata. Njiani kulikuwa na mto mkubwa, hivyo ikawalazimu kuogelea ili kuweza kuuvuka. Wakafanya hivyo. Hatimaye wakaifikia ile manyatta na kukuwakuta wenyeji. Mtaalamu hakutaka kupoteza muda. Akaanza kuwaelimisha Wamasaai. Akazungumzia juu ya ufugaji wao wa kuhamahama na jinsi unavyowadidimiza kiuchumi na kuharibu mazingira. Akawafundisha mbinu za kisasa na faida zake. Akawataka wabadilike!

Baada ya kumaliza, mzee mmoja akamuuliza swali: “Kijana kwa nini ulipovuka mto uliogelea badala ya kutumia daraja ambalo sisi wenyeji tunalitumia?” Msomi akapigwa na butwaa: “Ebo, kwani ninyi mna daraja? Mbona sikuliona wakati nakuja?” Mzee akamjibu, “Iwapo hujui kama tuna daraja ama la umewezaje kujua matatizo yetu hata kufikia hatua ya kuja kutubadilisha?”

5 thoughts on “GORAN HYDEN, NADHARIA YA USASA NA MUSTAKABALI WA WAKULIMA WAVUJA JASHO

  1. Kuna kitu kwa sasa ambacho nakiona kinalipekeka bara letu la Afrika katika machafuko makubwa sana, nacho ni uwekezaji (ukoloni mambo leo zamani). Hakika watu wanaonyang’anywa ardhi kwa kutumia maneno ya kilaghai kama maslahi ya umma hawatakaaa kimya siku zote. Na wengine wameshaanza kupinga kwa vitendo, ghasia zitazidi BARANI Afrika. Jeshi la Waafrika wanaoshirikiana na mabeberu kwa maslahi Yao binafsi itaongezeka, na wanyonge watazidi kupinga na watamwaga damu nyingi sana. Hakika WAZALENDO hawataisha watapambana mpaka tone la mwisho; Tuwazomee na tuwapinga hadharani hawa wabia wa Maendeleo maana ni hao hao wakoloni wamekuja na njia mpya tu.

  2. Ni wazo zuri sana. Je? Tumewahi kufikiria kwa nini miaka yote wakulima wanaoitwa Peasant hawana soko la uhakika?. Nasema hivyo kwa sababu hapa Tanzania ukiwa unasafiri barabarani kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, Mbeya, Kigoma, Mtwara, Tanga wakulima wadogo wanaoitwa Peasant utawaona wamepanga bidhaa zao barabarani wanatafuta soko la bidhaa zao. Hawa wasaliti wakubwa wanaokuja na maneno ya kilaghai ya Kilimo Kwanza lengo eti wawapatie matrekita najiuliza sana. Kama hii bidhaa ndogo tu wameshindwa kuipatia soko Je? Mkulima akitumia matrekita kama wanavyodanganya wataweza kuwatafutia soko la uhakika. Bila viwanda vyetu hatuwezi kwenda sehemu yoyote, lazima tuwekeze kwenye viwanda na tuna wazawa wengi tukiwawezesha wanao uwezo huo, siyo kuwakashifu kuwa hawana uwezo huo.

  3. Ndugu Jilala,Umetoa mawazo la kufikirisha. Naam, usemavyo ni sahihi kuwa sera tulizozikumbatia za uwekezaji na ubinafsishaji ni sera za kiporaji. Makala yangu yatakayofuatia yatatoa mifano kuntu ya uporaji na dhahma zisababishwazo na sera hizo.Lakini pia kama ulivyouliza, je, tumewahi kufikiria kuhusu soko la bidhaa za huyo peasant? Naam. Kwanza, pengine tunapaswa kufahamu kwamba peasant ni mkulima huru. Ni mkulima ambaye hazalishi kwa ajili ya soko. Sababu kuu ya uzalishaji wake ni kuilisha familia yake. Sasa, kwa sababu anakuwa hajitoshelezi kimahitaji, huamua kuzalisha ziada ili abadilishane na wazalishaji wengine. Yaani, kama anazalisha mchele wa ziada, atauuza na kupata fedha. Lengo la fedha hizo si kulimbikiza mtaji, bali ni kununua mahitaji mengine, mathalani nguo.Kwa hiyo, uzalishaji wake wa ziada hufuata mkururo huu: B—P—B (Bidhaa—pesa—bidhaa). Huuza ili kununua. Wapo wengi pia ambao huzalisha pasi na kuingia sokoni.Kwa hiyo, anachohitaji peasant huyo pengine ni soko la kijamii (social market) ambalo litamwezesha kubadilishana mahitaji na wazalishaji wengine wadogo kama yeye.Lakini akidumbukuzwa katika soko la kibepari (capitalist market) ataingia katika mkondo ambao Goran Hyden anaushabikia. Lengo la uzalishaji wake utakuwa ni kupata faida na kulimbikiza mtaji. Akitanuka zaidi, ataanza kupora ardhi na kunyonya nguvu-kazi ya wanyonge wenzake. Kubwa kuliko yote ni kuwa hatma yake hutegemea uimara wa soko. Na kwa jinsi ambavyo soko lenyewe halitabiriki – leo bei juu, kesho bei chini – mkulima huyu ataishia kupoteza. Na zaidi, kwa kuwa lengo lake ni kulimbikiza, ataachana na mazao ya chakula na kuzalisha mazao ya biashara. Nani atawalisha wanyonge wenzake wa mjini: machinga, waokota makopo, mama ntiliye, wabeba zege, wasukuma mikokoteni na makondakta wa daladala? Hii ni kwa sababu mkulima bepari, hata kama akizalisha chakula hulenga penye rupia. Naam, atakiuza kwa kampuni za kimataifa ambazo hukitumia kutengeneza mafuta ya magari (ili wakubwa watembee wakiwa wamekaa), na vyakula vya wanyama kama kuku na nguruwe (ili wakubwa wale nyama iliyonona).Kwa hiyo changamoto iliyopo ni ile ya ujenzi wa mshikamano wa kitabaka, ambapo litaundwa soko la wanyonge, na watabadilishana bidhaa wao kwa wao. Mama ntiliye wa mijini wameonyesha njia kwa kuwapikia wanyonge wenzao na kuwafanya waendelee kuishi na kupambana. Huko Amerika ya Kusini mshikamano wa aina hiyo umeanzishwa baina ya nchi za Kijamaa kama Cuba, Venezuela, Bolivia na Nicaragua. Mbadala wa ubepari upo. Tutafakari. Tupambane.Asante kwa mawazo fikirishi.Sabatho Nyamsenda

  4. Nimekuelewa vizuri sana baada ya ufafanuazi murua ulionipatia hapa. Hakika nimejifunza kitu kizuri zaidi. Nasubiri hiyo makala ili niweze kujifunza zaidi na zaidi kaka.

  5. Mr.Nyamsenda pamoja na ufafanuzi murua ningependa kujua kutoka kwako ni jinsi gani hawa wakulima wadogo wanaweza kubadilika na kilimo chao kiwanufaishe vizuri. Nasema hivi kwa sababu wakianza kutumia matrekita watakuwa wanaelekea katika uzalishaji wa kupata faida na wakishaanza kupata faida watageuka na kuanza kuwanunulia ardhi wakulima wenzao ambao hawajafika huku. Pili, wako akin kama walivyo, wafanye nini sasa ili waweze kukabiliana na utandawazi uliotapakaa Kote duniani kwa sasa?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box