HATMA YA MIGOGORO BAINA YA WAFUGAJI NA WAKULIMA IMO MIKONONI MWAO

Jioni ya Jumatatu tarehe 14 Disemba 2015 vyombo vya habari, hususan televisheni, vilibeba habari iliyoonyesha kiasi cha ng’ombe zaidi ya 70 waliouwawa. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa ng’ombe wengine kiasi cha 80 walikuwa wamejeruhiwa. Aidha ilitaarifiwa kuwa mtu mmoja alikuwa ameuwawa. Yote haya yametokana na kile kinachosadikiwa kuwa ‘mapigano’ baina ya wafugaji na wakulima yaliyotokea katika kijiji cha Dihinda wilaya ya Mvomero. Katika taarifa hizo za habari alionekana Waziri mpya wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na mkuu wa wilaya ya Mvomero wakiwa kwenye eneo la tukio wakitoa maelekezo mbalimbali.

Siku iliyofuata, Jumanne, tarehe 15 Disemba 2015 na magazeti ya Jumatano tarehe 16 Disemba 2015 kulikuwa na taarifa nyingine inayohusu ugomvi baina ya wafugaji na wakulima. Katika taarifa hiyo ilielezewa kuwa watu 16 walikuwa wamejeruhiwa vibaya baada ya kuvamiwa na wafugaji katika kijiji cha Tindiga B wilayani Kilosa. Watu hao wanadai kuvamiwa na wafugaji wakati wakielekea kwenye uhakiki wa mashamba yao.

Kwa wanavijiji wa wilaya za Kilosa na Mvomero na kwa watu wanaofuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi hapa nchini matukio haya mawili sio mapya. Yamekuwa yakitokea nyakati mbalimbali katika Mkoa wa Morogoro. Wilaya ya Kilosa ndio hasa imekuwa na matukio mengi ambayo, kadri ya taarifa za vyombo vya habari na baadhi ya tafiti, yamewahusisha wakulima na wafugaji wa maeneo hayo. Aidha kwa muda wa miaka mingi sasa kumekuwa na jitihada mbalimbali za kujaribu kutatua kinachoonekana, kwa juu juu, kama mgogoro baina ya wafugaji na wakulima. Tafiti na taarifa mbalimbali juu ya matukio hayo zimejaribu kubainisha asili na vichocheo vya migogoro hiyo na kutoa mapendekezo mbalimbali ya namna ya kuitatua.

Kwa kadri ya hali ilivyo na kwa ushahidi wa matukio tuliyoyanukuu hapo awali ni wazi kwamba ugomvi na migogoro baina ya wazalishaji wadogo wadogo katika maeneo haya bado haujakoma. Na ukizungumza na wakulima na wafugaji watakwambia wakati wote wanaishi kwa hofu na wasiwasi wasijue lini kutatokea mapigano au ugomvi wenye sura ya kutishia maisha yao na usalama wa mali zao. Hali hii ilijidhihirisha wazi siku chache kabla ya vyombo vya habari kutaarifu juu ya ugomvi baina ya wafugaji na wakulima.

Tarehe 9 Disemba 2015 siku ambayo watanzania walikuwa wakiazimisha siku ya uhuru wa Tanzania Bara kwa kufanya usafi wanachama wa HAKIARDHI walijumuika katika mazungumzo ya pamoja na wanakijiji wa Parakuyo na wananchi kutoka vijiji vingine vya jirani kama vile Mbwade, Ngaiti, Tindiga, Mkata, Kambala, Mabwegere, Kibamba, Madoto, Mfikisi, Kiduikilanga, na Magona. Pia walikuwepo wananchi kutoka vijiji vya Msomelo wilayani Handeni na Kambara wilaya ya Mvomero. Mjadala ulikuwa wa wazi na ukijadili suala la hatma ya mahusiano baina ya wazalishaji wadogo wadogo katika vijiji hivyo vyenye mchanganyiko wa wafugaji na wakulima. Katika mjadala huo mambo mengi na muhimu yalijitokeza yakiainisha chanzo na vichocheo vya ugomvi usiokwisha baina ya wafugaji na wakulima, na mapendekezo ya namna ya kuepukana na ama kuondokana kabisa na ugomvi na migogoro hiyo.

Kilosa 3

Mjadala haukuwa rahisi na kuna wakati ulitawaliwa na hisia kali kutoka kwa wazungumzaji mbalimbali. Kuna wale waliovutia upande wao kama wafugaji au wakulima na kuwalaumu wenzao kwa kuwa chanzo cha mgogoro au uchokozi unaozua migogoro na ugomvi. Na kwa hili pande zote zililaumiana. Kuna wale walioutazama ugomvi wa mara kwa mara baina ya wafugaji na wakulima kwa kina na mapana na kubainisha kuwa asili ya mgogoro sio wao bali sababu zingine zilizo ama ndani au nje ya uwezo wao.

Wale walioongea kwa mtazamo ulioegemea upande wa wafugaji walionyesha hisia za kupuuzwa na kubaguliwa kwa wafugaji. Mmoja wa wazungumzaji alihoji ‘Iweje katika vijiji 164 vilivyopo wilayani Kilosa wafugaji wawe na vijiji 6 tu! Kosa letu nini, kufuga?’ Mwingine alilaumu mtazamo wa viongozi wa wilaya ambao unawabagua wafugaji, hususan wa kimasai, dhidi ya makundi ya wazalishaji na wafugaji wa makabila mengine wasio Wamaasai. ‘Mmasai hatakiwi. Wilaya ya Kilosa wanachukia Wamasai. Mbona wasukuma na Wamang’ati hawachukiwi na wao ni wafugaji kama sisi?’ Ubaguzi huu wa kikabila, alibainisha msemaji mwingine, unaingia hadi katika masuala ya kisiasa kwamba mgombea wa kimaasai hawezi kuchaguliwa kwenye nafasi ya kisiasa hata kama anafaa kwa sababu atabaguliwa kwa sababu ya kabila lake.

Waliozungumza kwa kuvutia upande wa wakulima waliwalaumu wafugaji kwa mambo mbalimbali. Waliwalaumu wafugaji kwa kutumia uwezo wao wa kifedha kupindisha maamuzi na maelekezo yatolewayo na viongozi wa wilaya. Mathalani, kwa mujibu wa mzungumzaji mmoja, uongozi wa wilaya hutoa maagizo na matangazo ya kuwataka wafugaji walioingia kwenye maeneo ya vijiji bila kufuata taratibu kuondoka baada ya muda fulani. Lakini hata baada ya muda huo kufika na kupita wafugaji huendelea kuwepo na hakuna hatua zozote zichukuliwazo na uongozi wa wilaya. Hisia za wakulima ni kuwa wafugaji, mara baada ya matangazo kama hayo kutolewa, huchangishana fedha kwa ajili ya kuwapoza viongozi na kuachana na utekelezaji wa matangazo yao. Wazungumzaji mbalimbali walibainisha kuwa viongozi wa wilaya wamegeuza jambo hilo kama mradi wa kujipatia fedha toka kwa wafugaji. Mmoja wa wazungumzaji akadokeza kuwa ‘ukija Kilosa kama DC baada ya muda unatajirika.’ Kwa sababu ya uwezo wao wa kifedha wafugaji huwalipa viongozi na watendaji wilayani na hivyo kupindisha sheria na taratibu. Na matokeo yake, alidai mmoja wa wachangiaji, baadhi ya vijiji huanzishwa bila kufuata sheria na taratibu.

Wapo baadhi ya wachangiaji ambao walichukua msimamo wa kati wakiwa na mtazamo kuwa ardhi ni haki ya wazalishaji wote bila kujali kabila la mtu. Mathalani mzungumzaji mmoja alisema:

Nchi ya Parakuyo ni ya wote bila kujali kabila … Ni kosa kwa mawazo yetu (wengine) kujengeka kuwa fulani ndio anastahili kuwa eneo fulani. Tuepuke kuchochewa.

Pamoja na mikinzano katika mitazamo wazungumzaji mbalimbali waliungana katika baadhi ya hoja hususan zilizojaribu kubainisha vyanzo na vichocheo vya msingi vya ugomvi baina yao.

Suala moja lililojitokeza ni kuwa kuna sehemu kubwa ya ardhi wilayani Kilosa inayofaa kwa kilimo na ufugaji lakini imehodhiwa na watu wachache matajiri na wenye ushawishi kisiasa. Baadhi ya wanaohodhi ardhi hiyo waliipata baada ya Ranchi za Taifa kubinafsishwa kwa watu au kampuni binafsi. Katika baadhi ya mifano iliyotolewa ni pamoja na huu:

Kuna mtu ana ardhi kubwa lakini kazi yake ni kusubiri ng’ombe waingie kwenye eneo lake na kuwazuia, na kisha kutoza faini. Bila 100,000 ng’ombe hatoki. Huyu alipewa Ranchi lakini haitumii. Mbona wasipewe wengi wenye matumizi nayo!

Kutokana na malalamiko haya ya wananchi masuala mawili yanajitokeza. Moja ni kuzuka kwa aina mpya ya ukabaila na pili ni haja ya kutazama upya suala la ubinafsishwaji wa ardhi kwa kuzingatia mahitaji na maslahi ya wazalishaji wadogo wadogo vijijini – wafugaji na wakulima, na wazalishaji wengine.

Kuzuka kwa ukabaila mamboleo kwenye baadhi ya vijiji nchini, kwani si Kilosa tu kwenye ranchi, ni suala ambalo halina budi kukomeshwa. Ukabaila wa aina mbalimbali ukiwemo Unyalubanja ulikomeshwa miaka ya 1960s. Iweje leo unyonyaji wa aina hii urejee nchini chini ya kivuli cha ubinafsishaji! Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995 inatamka kuzuia hodhi ya ardhi kwa kuweka ukomo wa kiasi ambacho kinaweza kumilikishwa kwa mtu mmoja. Lakini katika sheria za ardhi bado hakuna ukomo wa kiasi cha ardhi ambacho mtu mmoja anaweza kumiliki katika eneo moja au maeneo tofauti ya nchi. Mwanya huu umewawezesha wapiga ramli ya bei ya ardhi na makabaila wapya kujilimbikizia ardhi ambayo hawaitumii kuzalisha na kuwabana wazalishaji. Utekelezaji wa Sera ya Ardhi kwa sasa hauna budi kufasiri tamko hili la kisera na kuweka ukomo wa ardhi. Na kisha baada ya sheria hiyo kupita yafanyike mapitio ya ukubwa wa maeneo yanayomilikiwa na mtu mmoja na kama yamezidi ukomo uliowekwa kisheria ile ardhi iliyozidi irejeshwe kwa mamlaka husika na igawiwe kwa wanaoihitaji.

Juu ya hoja ya ardhi kubinafsishwa kwa watu wasioiendeleza, wachangiaji wengi waliilaumu Serikali kwa kuwapa ‘Watu Wakubwa’ Ranchi hizo ambao si wawekezaji. Walizitaja Block mbalimbali za Ranchi wilayani Kilosa ikiwemo MKATA RANCHI kama baadhi ya Ranchi zilizobinafsishwa kwa watu ambao hawajaziendeleza. Pamoja wananchi kuwa wameomba baadhi ya ranchi hizo wapewe wao maombi yao hayakuzingatiwa. Wito wao ni kuwa Ranchi hizo, kama anavyobainisha mmoja wa wachangiaji kwenye mazungumzo hayo, wapewe wao:

Sisi hapa Kilosa hatujafikia hatua ya kugombania ardhi. Ardhi ipo ila imehodhiwa na watu wachache. Wao ndio chanzo cha sisi kugombana. Kama ardhi hiyo tutapewa sisi hatuna haja ya kugombana.

Jambo moja lililokuwa dhahiri katika mazungumzo yale ni kuwa njia ya mazungumzo baina ya wakulima na wafugaji ndio njia pekee ya kubaini kwa pamoja asili na chanzo cha ugomvi wa mara kwa mara baina yao. aidha kwa njia hiyo wafugaji na wakulima wanaweza kujenga umoja na mshikamano wa kuitafuta suluhu ya matatizo na haki yao. Kwa kuwasikiliza wachangiaji wote toka makundi yote makubwa, yaani wakulima na wafugaji, ilikuwa dhahiri kuwa huwa hakuna mazungumzo bayana na ya moja kwa moja baina yao. Na kama hutokea, basi huhusisha wawakilishi wachache. Aidha, ilijitokeza wazi kwamba ili kuweza kupata suluhu ya kudumu na yenye maslahi kwa wazalishaji wadogo wadogo wote mazungumzo hayana budi kuwa ya kina, wazi, na ya muda wa kutosha. Hayawezi kuharakishwa wala kukatishwa kwa kuingiliwa na suluhu za haraka haraka za ‘kitaalamu’.

Kwa wanavijiji wengi waliokuwepo Parakuyo siku ya Uhuru pengine ile ndio ilikuwa mara na fursa yao ya kwanza kuzungumza kwa wazi mbele ya ‘wagomvi wao’.

Wanavijiji na Wanachama wa HAKIARDHI wakifuatlia mazungumzo kijijini Parakuyo

Wanavijiji na Wanachama wa HAKIARDHI wakifuatlia mazungumzo kijijini Parakuyo

Wapo waliokuwa na hofu juu ya nini wakiseme na wakiseme kwa namna gani. Kwa sababu, wakidhani, kama watasema kwa uwazi sana huenda wakaingia matatani. Hiki ni kiashiria tosha kuwa wanavijiji katika maeneo haya wanahofu juu ya mitazamo ya namna mamlaka za kiserikali zinavyotaka kuendesha na kutatua migogoro ya ardhi. Ndio maana wapo waliosema kwa uwazi kabisa kuwa tatizo si wafugaji wala wakulima, tatizo ni viongozi.

‘Tunazungumza kwa kuchagua chagua. Hatuna uhakika na usalama.Tusingeingiliwa tusingekuwa na migogoro.Viongozi ni wachonganishi wanaleta migogoro.’

Kwa nini wachangiaji wengi wanadhani viongozi ni wachonganishi? Baadhi ya majibu ya wachangiaji ni pamoja na madai kuwa: viongozi wana maslahi katika ugomvi baina ya wakulima na wafugaji. Wao hujipatia fedha kutokana na migogoro kuwepo. Hata hivyo katika kuchangia hoja hii mzungumzaji mwingine alitoa rai kuwa:

Jamii za wakulima na wafugaji ni jamii za wazalishaji. Wao ndio wanalisha Taifa. Hivyo wasikubali kugombanishwa, washikamane wao kama wazalishaji. Migogoro ni wazi ipo. Lakini migogoro hii chanzo chake ni madudu kuna hao wanaopora ardhi.

Na wachangiaji wengi walikuwa na maoni kuwa ikiwa watatafuta suluhu ya ugomvi baina yao bila kuwashirikisha viongozi basi suluhu itapatikana. Kutokana na mwelekeo wa mazungumzo na fikra hizi yalitolewa mapendekezo ya namna ya kutatua migogoro na ugomvi baina ya wakulima na wafugaji. Baadhi ya mapendekezo ya msingi yaliyotolewa ni pamoja na haya yafuatayo:

 • Mipango ya matumizi bora ya ardhi izingatie mahitaji ya wazalishaji wote. Mathalani huwezi kutenga eneo au kijiji cha wafugaji halafu ukakitenga na maeneo yaliko maji kwa ajili ya mifugo. Katika hali kama hiyo mifugo watafuata maji tu na hapo ugomvi utatokea.
 • Wapo waliopendekeza haja ya kukuza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kuwa na idadi ndogo ya mifugo lakini yenye ubora mkubwa; na haja ya kuwekeza katika miradi ya uboreshaji wa malisho ili kuhakikisha kuwa wakati wote kuna malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo.
 • Kuhusu ranchi na mashamba yote yaliyobinafsishwa katika wilaya ya Kilosa lakini wale waliopewa hawajayaendeleza kwa muda mrefu, ulitolewa wito kwa serikali kuzitwaa ranchi na mashamba hayo na kuyagawa kwa vijiji ambavyo tayari vimeonyesha kuwa vina mahitaji, uwezo na utayari wa kuyaendeleza. Hii pia itasaidia kutatua baadhi ya migogoro inayotokana na uhaba wa ardhi kutokana na kuhodhiwa na wachache.
 • Aidha, ilipendekezwa na kusisitizwa kuwa mazungumzo huru na ya wazi ni jambo muhimu sana. Na ndio baadhi ya misingi ambayo kwayo nchi yetu ilijengwa na waasisi wa Taifa letu. kutokana na umuhimu wa mazungumzo kama njia ya kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji wao kwa wao ilependekezwa kuanzishwe kwa kamati ya wilaya ya Usuluhishi na Maridhiano baina ya wakulima na wafugaji. Kamati hiyo itokane na iwe na uwakilishi toka pande zote za wazalishaji wadogo wadogo yaani wakulima na wafugaji.
 • Suala la kubaguana kikabila si jambo jema na lazima kwa pamoja lipingwe na kulaaniwa kwa nguvu zote. Aidha ikasisitizwa kuwa ni wajibu wa kila mshiriki katika mkusanyiko ule, na kila Mtanzania kupinga na kulaani hadharani pale anaposikia mtu au kiongozi yeyote analeta hoja za kuwabagua na kuwatenga watu kwa makabila au dini zao.

Katika kuhitimisha mazungumzo pale Parakuyo ilipendekezwa pia njia mbalimbali zitafutwe ili kusaidia kukuza imani na kuaminiana baina ya wafugaji na wakulima. Aidha ilisisitizwa kuwa wakulima na wafugaji wazingatie kanuni ya kwamba haki hupiganiwa hainunuliwi. Haki ya kununua haina heshima ila ya kupigania.

2 thoughts on “HATMA YA MIGOGORO BAINA YA WAFUGAJI NA WAKULIMA IMO MIKONONI MWAO

 1. Maonevu kwa wakulima wafanyayo wafugaji wanaohamia maeneo ya wenzao na mifugo mingi kulishia mashamba, kuwapiga-ndio yatakayoleta vita TZ. Land use planning and management na kuzingatia sheria na bylaws kwa wakulima na wafugaji zinahitajika na ziheshimiwe. Kila mtu akae kwake na mifugo yake kusiwe na kuhamahama.

 2. Nadhani migogoro kati ya wafugaji na wakulima hapa nchini inaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa au kutokomezwa kabisa hatua zifuatazo zikichukuliwa:

  1. Serikali za vijiji ziachiwe jukumu la kubaini maeneo ya vijiji yanayofaa kwa shughuli za ufugaji wa kwenye mbuga wazi, na mamlaka ya kutoa (kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mifugo)leseni za ufugaji kwenye maeneo hayo zinazoonyesha jina la mwenye leseni na taarifa zake nyingine muhimu; eneo la kijiji alimotengewa kufuga; na, aina za mifugo na idadi za juu kabisa za mifugo hiyo anazoweza kuwa nazo kwenye eneo la kijiji alimotengewa kufuga;

  2. Serikali za vijiji ziachiwe mamlaka ya kutoa (kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mifugo) vibali vya kuhamisha mifugo kutoka eneo hili kwenda lile la kijiji au kutoka kijiji hiki kwenda kijiji kile vinavyoambatanisha leseni za kufuga kwenye maeneo ya kijiji au kijiji anakohama na anakohamia;

  3. Na, Serikali za vijiji ziachiwe mamlaka ya kutoa (kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mifugo)vibali vya kupitisha mifugo kwenye maeneo ya vijiji au vijiji vyao kwa walio na leseni za kuhamisha mifugo kutoka maeneo haya ya vijiji au vijiji hivi kwenda maeneo yale ya vijiji au vijiji vile kwa kuhakikisha wanaohamisha mifugo hawatasumbua au kasababisha uharibifu kwa wafugaji na wakulima wa maeneo watakayoyapitia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box