Kutoka Makavani. Kwa Nini Muundo wa Shirikisho Utaua Muungano

Mchakato wa Kutunga Katiba unaendelea, na sasa uko katika hatua ya Bunge Maalumu la Katiba. Takribani wiki tatu Bunge Maalumu lilikuwa likijadili kanuni za kuendesha Bunge hilo. Pamoja na kuwepo mambo mengi yaliyojadiliwa hoja mbili kuu zilizua mjadala mkubwa. Hoja ya kwanza ni juu ya mamlaka na mipaka ya Bunge la Katiba, hoja ambayo ilizua mijadili mingi kabla na wakati bunge linaendelea. Hoja ya pili ilikuwa ni juu ya namna ya upigaji wa kura, kwenye Bunge Maalumu, wakati wa kufanya maamuzi ya kupitisha ama kutopitisha vifungu mbalimbali vya Rasimu ya Katiba na hatimaye Rasimu ya Katiba yenyewe kwa ujumla wake.

Lakini ni wazi hoja kuu iliyopo mbele ya Bunge hili maalumu, ni juu ya Muundo wa Muungano. Toka Tume ya Katiba itoe Rasimu yake ya kwanza na kupendekeza kuwepo kwa Muundo wa Shirikisho, na hivyo kuwepo kwa Serikali Tatu, ya Shirikisho (Muungano), ya Tanganyika, na ya Zanzibar mjadala na mabishano mengi yamezuka juu ya maana, mantiki, na matokeo ya kuundwa kwa Serikali Tatu katika Jamhuri ya Muungano.

Kama tutakavyosoma katika baadhi ya aya kutoka katika kijitabu cha Jaji Joseph Warioba, pendekezo la Serikali tatu katika Muungano wa Tanzania halikuanza leo. Na upinzani dhidi ya Muundo wa Serikali Tatu pia haukuanza leo. Kipya, na ambacho pengine kitawastua baadhi ya wasomaji ni kuwa, ni kuwa waliokuwa watetezi wa Serikali mbili huko nyuma sasa wamebadilika na kuwa watetezi wa Serikali Tatu. Mmoja katika hao ni Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba. Hivi sasa Jaji Warioba ni mtetezi wa Muundo wa Serikali Tatu (Kwa niaba ya Tume!), na pengine kwa niaba ya Wananchi kama ambavyo amekuwa akisema mara kwa mara! Kama mawili haya ni sawa, na Jaji Warioba hajaacha msimamo wake wa 1994, basi ni wazi anachokitetea sicho anachokiamini! Na kwa mujibu wa maandishi yake mwenyewe, anachokitetea sasa haiyumkini anayajua madhara yake, mbali na kusema hadharani kuwa muundo unaopendekezwa na Tume ndio dawa ya kudumisha muungano!

Kutoka Makavani inapitia baadhi ya aya za chapisho la Jaji Joseph Sinde Warioba, lenye kichwa cha Habari Tanzania: Hatima ya Muungano, lililochapishwa July 1994. Kutoka Makavani inaamini hoja hizo za mwaka 1994 ni nzito, hata kama Jaji Warioba mwenyewe  haziamini tena (hatujui hatujamuuliza). Ni wazi hoja zake zinaweza kupanua fikra na mjadala unaoendelea hivi sasa juu ya Muundo unaofaa kwa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania.

Asili ya Hoja ya Muungano (Kijitabu), dhidi ya Muundo wa Jumuiya, ya Jaji Warioba ni “Mkusanyiko wa makala ambazo zilitolewa na gazeti la RAI kati ya Mei 23 na Juni 1994.”

Michango hiyo ya Jaji Warioba katika gazeti la RAI ilisukumwa na Taarifa ya Serikali ya Muungano Bungeni Mwezi Mei 1994 na  ‘Taarifa ya Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano wa Tanzania ya 1992.’ Ni baada ya kuzisoma taarifa zote mbili ndipo Jaji Warioba aliamua kuandika maoni yake kuhusu taarifa hizo, maoni ambayo yalichapishwa katika gazeti la RAI.

Warioba anaandika hivi:

Taarifa ya Shellukindo, Taarifa ya Amina, na Taarifa ya Awali ya Serikali ya Muungano zikisomwa kwa pamoja itaonekana wazi kwamba dhamira ya Serikali zote mbili haikuwa kuondoa vikwazo au kero kwa wananchi kwa jinsi tulivyoelewa bali dhamira ilikuwa kubadili aina ya Muungano wa Tanzania (Uk 1).

Warioba anaendelea kubainisha kuwa taarifa zote zinaonesha wazi wazi kuwa:

  … nia ya Serikali zetu mbili ni kuondoa Muungano wa sasa ambao ni mzito wa aina ya “union” na badala yake kuleta Muungano mwepesi wa aina ya jumuiya … Ingawa Serikali zote mbili zimeeleza mara kwa mara kwamba dhamira ni kulinda na kuimarisha Muungano kama ulivyo, mantiki ya maelezo yaliyo katika taarifa zote … ni tofauti kabisa. … Sura inayojitokeza ni Muungano wa Serikali tatu ambamo Serikali za nchi zote mbili zitakua na madaraka makubwa kila moja, na Serikali ya Muungano itakuwa na madaraka madogo  (Uk 1).

Kwa kifupi, Jaji Warioba anazishangaa Serikali zote mbili ya Muungano ikiongozwa na Ally Hassan Mwinyi, na ya Zanzibar ikiongozwa na Dk. Salmin Amour, kwa kuficha dhamira yao kutaka kubadili Muundo wa Serikali ya Muungano uliopo, na hata kuvunja Muungano.

Jai Warioba anaendelea kusisitiza kuwa:

Hoja ya Serikali ya Mapinduzi kama inavyojitokeza katika taarifa ya Amina ni kupunguza sana madaraka ya Muungano na taarifa ya awali ya Serikali ya Muungano inakubali hoja hiyo. Kwa hiyo Serikali ya Muungano imekubaliana na Serikali ya Mapinduzi kupunguza sana madaraka ya Muungano na imekubaliana pia na hoja ya Wabunge ya kuunda Serikali ya Tanganyika (UK. 2).

Kwa nini Taarifa zote anazosisoma Jaji Warioba zikakubaliana juu ya Suala la kubadili Muundo wa Muungano? Katika ukurasa wa 2 wa Kijitabu chake Jaji Warioba anatoa jumuisho la sababu zilizotolewa ambazo ni:

…Kuna matatizo katika utekelezaji wa mambo ya Muungano kwa sababu ama kuna matatizo ya tafsiri ya Katiba au kuna mchanganyiko wa mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Sababu zinazotolewa ni kwamba ama mambo yaliingizwa katika Muungano kwa papara papara bila uchambuzi au yalifumbiwa macho bila kuzungumzwa kwa undani kwa sababu viongozi na wananchi walikuwa wanazuiwa (Uk.2).

Jaji Warioba anasema madai “yote haya mawili sio kweli.” Kwa sababu:

Kwanza siyo kweli kwamba mambo yaliyoongezwa baada ya 1964 ndiyo yanakabiliwa na matatizo makubwa zaidi.

Kwa maoni yake mambo ya Muungano ambayo yameleta matatizo ni i) Mambo ya Nchi za Nje, ii) Ulinzi na Usalama, iii) Mamlaka ya Hali ya Hatari, iv) Uraia, v) Uhamiaji, vi) Mikopo na Biashara, vii) Kodi ya mapato na ushuru wa forodha, na viii) Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu (Uk 4-5).

Kuhusu hoja ya orodha ya mambo ya Muungano kuongezeka kutoka 11 hadi kufikia 22. Mambo ambayo Taarifa ya Amina inadai ndio yaliingizwa kwa papara papara, Jaji warioba anasema kuwa mambo hayo yote, ukiacha suala la 22 (juu ya uandikishaji wa vyama vya siasa lililoongezwa mwaka 1992), mengine yote yaliongezwa baada ya 1964 yalikuwa ni masuala yanayoshughulikiwa na illiyokua Jumuiya ya Afrika Mashariki. Na baada ya kuvunjika kwa Jumuiya mwaka 1977, “tulikubaliana yaongezwe kwenye orodha ya Muungano”. Na kwa maoni yake “Uamuzi huo haukuwa wa Ajabu kwani kama tulikubaliana mambo hayo yawe chini ya Jumuiya kulikuwa na matatizo gani kuwa chini ya Muungano?”

Mambo yaliyoongezwa kwenye orodha ya Muungano na ambayo Jaji Warioba anasema yalikuwa yakiendeshwa kwa pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa niaba ya nchi zote tatu ni pamoja na 1) Mambo yanayuhusu sarafu, mabenki, fedha za kigeni, na usimamizi wa masuala ya fedha za kigeni, 2) Leseni za viwanda na takwimu, 3) Elimu ya Juu, 4) Maliasili ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa, 5) Baraza la Mitihani, 6) Usafiri na Usafirishaji wa Anga, 7) Utafiti, Utabiri wa hali ya hewa, 8) Takwimu, 9), na  Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano (Uk. 3-4).

Katika ukurasa wa 8  wa Kijitabu chake Jaji Warioba anazungumzia Haja na Umuhimu wa Muungano. Hapa anapitia hoja mbalimbali za Taarifa ya Amina juu ya uhalali wa Muungano, na madhara ya miuondo ya miungano mbalimbali.

Cha kwanza anachokibainisha Jaji Warioba ni uchambuzi mzuri wa Taarifa hiyo juu ya chimbuko na historia ya Muungano na uhalali wake. Hapa Jaji Warioba anasema “Kwa uchambuzi huo kamati ya Amina imefikia maoni kwamba Muungano wa Tanzania ni halali kisheria” (Uk 8).

Katika kusoma kwake uchambuzi wa Taarifa ya Amina Jaji Warioba anabainisha kuwa:

Baadaya ya uchambuzi mzuri wa aina ya miungano kamati ya Amina inafikia maoni kwamba Muungano wa Tanzania uko kati ya Union na shirikisho. Muungano wetu una sura ya Union kwa sababu Tanganyika iliachia madaraka yake yote na Zanzibar iliachia madaraka yake kwa baadhi ya mambo. Baada ya uchambuzi pia kamati ya Amina inafikia maoni kwamba aina hii ya muungano inafaa na inashauri tubaki hivyo, ikiwa ni pamoja na kuendelea na muundo wa serikali mbili, yaani Tanganyika iendelee kuachia mambo yake kuendeshwa na muungano” (Uk. 11).

Kinachomstajaabisha Jaji Warioba ni kwa Kamati ya Amina kutoa “maoni ambayo yanaharibu kabisa mantiki ya uchambuzi wake wa aina ya miungano”. Kamati ya Amina inapendekea mambo yale yote yaliyoingizwa kwa papara na ujanja yatolewe kwenye orodha ya Muungano (Uk 11) (Mambo haya yameshatajwa awali, hapo Juu).

Kwa nini mapendekezo haya yana matatizo. Kwa maoni ya Jaji Warioba ni kuwa:

Mambo haya ni mazito sana na ndiyo baadhi ya yale ambayo Zanzibar iliachia madaraka yake. Kwa uzito wa mambo haya kama yakiondolewa kutoka orodha ya mambo ya Muungano, Zanzibar itakuwa ni nchi huru katika kuendesha mambo yake ya ndani na nje. Kwa kuwa Tanganyika iliachia madaraka yake yote na kamati inapendekeza hali ibaki ilivyo, basi Tanganyika ndiyo itabaki Muungano. Kwa maana nyingine Zanzibar itakuwa huru lakini itakuwa na ubia wa kutawala Tanganyika (Uk. 12).

“Katika mambo ambayo kamati ya Amina inapendekeza yaongezwe kwenye orodha ya Muungano ni pamoja na Bodi ya Sarafu ya Tanzania. Hii inafanana na Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Hilo linaonyesha kamati ya Amina inataka muundo wa Jumuia ambapo nchi wanachama ni huru.

Jaji Warioba pia anaendelea kubainisha kama Taarifa ya Awali ya Serikali (Taarifa ya Awali ya Maafikiano) nayo ina mapendekezo yake. Mapendekezo hayo hayana tofauti sana na yale ya Kamati ya Amina. “Kati ya mambo ishirini na mbili ambayo yako kwenye ordodha ya Muungano, kumi na matano ama yameondolewa au yamepunguzwa kabisa uzito. Mambo hayo ni:- i) Ulinzi, ii) Mambo ya Nje, iii) Hali ya Hatari, iv) Uraia, v) Uhamiaji, vi) Biashara na mikopo ya nje, vii) Kodi ya mapato, viii) Bandari, ix) Leseni za Viwanda, x) Usafiri na usafirishaji wa anga, xi) Utabiri wa hali ya hewa, xii) Takwimu, xiv) Utafiti, xiv) Posta na Simu, xv) Mahakama ya Rufaa” (Uk 12-13).

Kutokana na Mapendekezo ya Taarifa zote Jaji Warioba ana hoji nini hatima ya Muungano?

“Kwa mantiki ya mapendekezo ya kamati ya Amina na Taarifa ya Awali ya Serikali”, anaeleza jaji Warioba, “hakuna uwezekano wa kuendelea na Muungano wa sasa (yaani muungano wa aina ya union) na hakuna uwezekano wa kuendelea na muundo wa serikali mbili. Kwa mujibu wa uchambuzi wa kamati ya Amina ‘Union’ ni Muungano ambapo Serikali za nchi zinazoungana huachia Madaraka karibu yote kwa serikali ya Muungano” kama serikali zetu mbili zilikuwa zinataka tuendelee kuwa na ‘union’ zingependekeza kuongeza mambo ya Muungano badala ya kuyapunguza.” (Uk 15).

“Kwa upande mwingine”, Jaji Warioba anaeleza,

… haiwezekani tukabaki na muundo wa Serikali mbili kama mambo muhimu na mazito yakiondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Tanganyika ilikubali kuachia madaraka yake juu ya mambo muhimu kisiasa na kiuchumi. Kama Zanzibar inataka madaraka yake yarudi hakuna sababu ya kung’ang’ania kwamba Tanganyika haina haki ya kuondoa baadhi ya mambo yake kutoka kwenye shughuli za Muungano. (Uk. 15).

Kisha katika uchambuzi wa taarifa zote mbili, Jaji Warioba anabainisha hatari ya Muungano kuvunjika.  Katika hili anasema:

“Lakini kama mapendekezo yaliyotolewa katika taarifa ya awali yatakubaliwa Muungano utakuwa dhaifu sana na unaweza kuvunjia kwa urahisi …” (Uk 16). Jaji Warioba anaendelea kueleza zaidi athari za mapendekezo haya kwa Muungano:

Lakini kama mapendekezo yaliyo katika Taarifa ya Awali yakikubaliwa Muungano utakuwa dhaifu sana. Kama Zanzibar ikikubaliwa kuwa na madaraka zaidi katika mambo kama uraia, ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa mataifa, viwanda, biashara, hali ya hatari, posta na simu, kodi na mabenki, Tanganyika nayo itapewa madaraka hayo hayo … Matokeo yake Serikali za Tanganyika na Zanzibar zitakuwa na nguvu sana na Serikali ya Muungano itakuwa dhaifu kabisa. Mambo yanayobaki yatafanya Muungano uwe dhaifu kuliko Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ilivyokuwa. (Uk. 17).

Aidha Jaji Warioba anasema, “… kukubali mapendekezo ya taarifa ya Awali ni kuwagawanya wananchi wa Bara na Visiwani badala ya kuwaunganisha. Muungano ni wa Wananchi, siyo wa Serikali.” (uk. 17).

Na katika kuipa uzito hoja hii Jaji Warioba katika Uk. wa 23 anasema anachoamini:

Wakati wote mimi naamini Muungano ni kwa ajili ya Wananchi, hasa wa kawaida. Wananchi hao wanasafiri kwa madhumuni ya kutembelea ndugu zao, kufanya kazi, kufanya biashara na kadhalika. … Wapo wananchi wa Bara na Visiwani ambao Muungano umewaletea manufaa na wanafanya kazi na biashara pande zote. Tukiwagawa katika haki zao za uraia na kutaka watumie pasipoti au vitambulisho, muungano, hasa wa aina ya Shirikisho, hautakuwa na maana na utavunjika kwa urahisi. (Uk. 23).

Kuhusu hoja hiyo hiyo ya Wananchi Jaji Warioba anabainisha kuwa:

Muungano umekuwa na maana zaidi kwa wananchi kwa sababu ya kuunganisha uchumi. Mahali popote nchini wananchi wanaendesha shughuli zao za uchumi bila ubaguzi wa Bara wala Visiwani. Katika soko la Zanzibar utawakuta wananchi wa Bara wananunua vitu na kuja kuuza Bara. Mtu akizunguka Dar es Salaam, Tanga n.k. atawakuta wananchi wa Zanzibar wanafanya biashara ya kila aina, kununua na kuuza mali ya aina mbalimbali, kuendesha taxi, kujenga majumba mengi tu na kilimo. … Kuna wananchi wengi wa Visiwani walio na ardhi na mali nyingine Bara …. Hivi uzalendo unaoenezwa na viongozi unamsaidiaje mwananchi wa kawaida? Utawaongezea nini zaidi ya kile ambacho wanakipata sasa? (uk. 25).

Uchambuzi wa Jaji Warioba juu ya mapendekezo ya taraifa ya Tume ya Amina na Taarifa ya Awali ya Serikali yanamsukuma kuamini mambo matatu yafuatayo.

Kwanza, Mapendekezo hayo yatadhoofisha muungano na hatimae kuuvunja kabisa. Na anabainisha kuwa Mfumo wa shirikisho ndio hatari kwa kuwepo kwa Muungano.

Kwa kifupi matokeo ya mapendekezo ya Serikali zote mbili ni kuvunja Muungano tulionao, yaani Union. Mapendekezo hayo pia yatafanya iwe vigumu kuunda Muungano wa aina ya shirikisho wala jumuiya ya kiuchumi. Ni Mapendekezo ambayo yatafanya Muungano uvunjike. (p. 28).

Pili, Kuwa Mapendekezo yote haya yakitekelezwa hayamwongezei shibe wala siha mtu wa kawaida.

Tatu, msukumo wa mapendekezo haya na hisia za kutaka kudhoofisha Muungano ni viongozi na mahitaji yao binafsi ya hadhi, vyeo na madaraka.

Nukuu kwa hoja ya kwanza na pili zilizotajwa punde zimeshatolewa awali, sasa tumalizie na nukuu kutoka katika Kijitabu cha Jaji warioba kuhusu hili la Tatu, Viongozi na tamaa zao za madaraka na hadhi. Kuhusu hili Jaji Warioba anaeleza kiini cha tatizo kwa maneno haya:

Sisis tunapenda hadhi, siyo Muungano. Tunapenda Muungano wa Serikali siyo Muungano wa wananchi. Tofauti yetu na waasisi ni kwamba kwa wao Muungano ulikuwa umeandikwa katika mioyo yao na matatizo yalishindwa kuyaondoa maandiko hayo. Sisi Muungano tunauandika kwenye makaratasi na kuuimba kwenye midomo yetu na tunatumia matatizo kuuhujumu. Waasisi walizingatia maslahi ya wananchi na hawakujali hadhi yao, sisi tunajali madaraka na hadhi na tunakwepa majukumu ya uongozi. (Uk. 20).

Kusistiza hili Jaji Warioba anasema:

Katika taarifa ya Amina hakuna mahali ambapo masilahi ya wananchi wa kawaida yanazungumziwa. Hakuna mahali ambapo shughuli za kiuchumi za wananchi wa kawaida yanazungumziwa. Hakuna mahali ambapo shughuli za kawaida za wananchi zinaonyeshwa kama zimeathirika na Muungano. Kinachozungumziwa zaidi ni madaraka ya wakubwa na vyeo vya wakubwa. (Uk.26).

16 thoughts on “Kutoka Makavani. Kwa Nini Muundo wa Shirikisho Utaua Muungano

 1. Nakushukuru sana Kamata kwa kumkumbusha jaji Warioba. Kwa hakika dhambi ya kuudhoofisha Muungano haiwezi kumwacha jaji na tume yake. Dhambi hiyo inaongezeka zaidi pale ambapo wabunge tunalazimishwa kutobadili maudhui ya rasimu ya katiba na bila kujali kwamba hata sheria ya mabadikiko ya katiba imekiukwa waziwazi. Inasikitisha zaidi kuona kwamba matokeo ya kazi ya tume (research) ambayo hata hayawakilishi maono ya watanzania 45 milioni ndiyo tunanazimishwa kuyaamini kama ni matakwa ya watanzania wengi. Watanzania wanapaswa kujua kwamba kwa hali inayoendelea sasa inayosukumwa na dhamira ya waroho wachache haivutii na wala haina mashiko katika kuilinda amani tulio nayo. Katika hili hatuhitaji ushabiki bali ni utashi na uzalendo na uchungu wa kulinda udugu wetu.

 2. Hoja ya jaji Warioba ya 1994 (tuiite Warioba 1994) in kwamba Zanzibar ikiwa na mamlak makubwa Kama ripoti ya Amina inapendekeza na kukubalika an viongozi wa muungano wa wakati ule, “Tanganyika” pia itakuwa an mamlaka makubwa na serikali ya shirikisho itakuwa dhaifu kuliko hata jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatima yake ni kuvunjika kwa muungano.

  Ukisoma kwa makini rasimu (Warioba 2014), hoja hi inaapply moja kwa moja na vile vile serikali ya muungano ni dhaifu kiasi kwamba hatutakuwa na hata customs union wala common market Kati ya Zanzibar na TAnganyika kwa sababu mambo yote yahusuyo ushuru wa forodha na soko ya nje sio ya muungano. Je Zanzibar ikiamua Kuwa na soko ya pamoja na Malawi itakuwa je? Na kwa mantiki hiyo Tanzania Kama nchi moja haiwezi ikiwa mshirika katika jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Muungano utavunjika!

 3. Nimemsikiliza Mheshimiwa Jaji Warioba kwa makini sana alipokuwa anawasilisha Rasimu ya Katiba mpya Bungeni leo na kuridhika alivyofahamisha kwamba pendekezo la muungano wa serikali tatu badala ya uliopo wa serikali mbili limelenga kuudumisha kwa kuutoa kwenye mwelekeo wa kufa na kuuweka kwenye ulio endelevu.
  Kuridhika kwangu kumetokana na kukubali kwamba kuendelea kupungua kwa yaliyokuwa ya Muungano wakati wa kuanzishwa kwake na Zanzibar kujitangaza kuwa nchi kinyume na ilivyokubaliwa kwenye hati za Muungano ni dalili tosha kwamba Muungano tayari uko kwenye mwelekeo wa kuvunjika kwani kilichotarajiwa kadri ya muda ulivyokuwa unakwenda ni ongezeko la yaliyokuwa ya Muungano na punguko la yaliyokuwa ya nchi washirika na madaraka ya serikali zake kama kiashirio muhimu cha mwelekeo sahihi kuelekea kwenye ule Muungano wa serikali moja uliolengwa na waasisi wake.
  Naipongeza Tume ya Mh. Jaji Warioba kwa kuweza kutambua kwamba Muungano uliopo wa serikali mbili upo kwenye mwelekeo wa kufa kwa sababu kinachodhaminiwa zaidi na nchi washirika, na hasa Zanzibar ni ‘’sovereignity’ zao badala ya muungano na kuzirudishia sovereignity zao kupitia muundo wa serikali tatu badala ya wa serikali mbili uliopo na kupunguza ya muungano kwa kuundolea yale yasiyokuwa muhimu kuwa ya muungano chini ya muundo wa serikali tatu ndiyo iliyo njia pekee ya kuudumisha.
  Ukweli ni kwamba ya muhimu kuwa ya Muungano Tanzania ni mambo ya Ulinzi na Mambo ya nchi za nje lengo likiwa ni kuwezesha washirika kuwa na jeshi moja kabambe la ulinzi na balozi nyingi na imara nchi za nje zinazofadhiliwa na kutumiwa kwa pamoja kwa gharama ndogo badada ya kila nchi mshirika kuwa na jeshi lake kabambe la ulinzi na balozi zake binafsi nchi za nje kwa gharama kubwa karibu mara mbili zaidi. Kwa mfano jengo la ubalozi nchi za nje linaweza kuwa na Balozi wa Muungano na madeski mawili (la Zanzibar na Tanganyika).
  Muundo unaopendekezwa wa serikali tatu ndio pia unaofaa kuufanya muungano uwe kivutio kwa nchi nyingine kujiunga na kuuwezesha wenyewe na/au washirika wake kujiunga kirahisi na jumuia ya Afrika ya Mashariki tarajiwa na unaowezesha kila mshirika kujiunga na jumuia nyinginezo nyingi za kimataifa zilizotofautiana kwenye maswala ya kiuchumi, kibiashara, kitamaduni na zenye manufaa zaidi kwake.
  Tanganyika na Zanzibar zinaweza kuungana kwenye mambo ya ulinzi na nchi za nje kwa sababu kwa pamoja itakuwa gharama ndogo sana kufanikisha hayo lakini kwa mambo mengine Tanganyika na Zanzibar zikashiriki kwenye mashirikisho mengine duniani yenye manufaa zaidi kwenye hayo mambo mengine.
  Sidhani ni lazima serikali ya muungano iwepo ili kuwezesha watu wa Zanzibar na Tanganyika kuendelea kushirikiana kwenye mambo ya ulinzi na nchi za nje na kwenye mengineyo mengi wanayoshirikiana kwa sasa chini ya muundo wa serikali mbili. Zanzibar na Tanganyika hawana la kugombania, ni ndugu na majirani wenye utegemeano wa asili kwenye mengi.
  Naamini pasipokuwepo muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali mbili Zanzibar haingekuwa imeweka pingamizi kwa watanganyika kumiliki ardhi Zanzibar kama pingamizi hilo haliko kwa wengine wote duniani. Zanzibar imeweka pingamizi hilo ili kujikinga na uwezakano wa Muungano kuwezesha watanganyika kununua ardhi na kuhamia kwa kasi Zanzibar kutakakoharibu utamaduni wao na hata kupelekea watanganyika kuwa wengi zaidi kuliko wazanzibari wa asili huko Zanzibar na tishio kwa sovereignty yake. Imenikumbusha kinachoendelea huko Crimea na kinachoweza kutokea kwingineko mashariki ya Ukraine kwenye uhamiaji mwingi kutoka nchi jirani uliowezeshwa na muungano wa kisoviet. Hapana, Muungano uwe wa serikali tatu kama Tume ilivyopendekeza badala ya wa serikali mbili uliopo, na kama ni wazanzibari kumiliki ardhi na/au kuhamia Tanganyika na watanganyika kumiliki na/au kuhamia Zanzibar taratibu zilizopo kwa wengine wote duniani ziwe ndizo hizo hizo za kuzingatiwa. Mheshimiwa Jaji Warioba na Tume yake ya marekibisho ya katiba ni wakupongeza kwa kuweza kugundua kinachosabisha kero za muungano na kubuni njia sahihi ya kuuboresha ili kuudumisha. Nimatumaini kwamba Baraza la katiba litamwelewa Mh. Jaji Warioba na Tume yake vizuri na kukwepa vishawishi vya wachache ndani ya makundi yanayopigania Katiba mpya iwe ni ile inayoendeleza maslahi yake binafsi waliokuwa wanafaidi kirahisi dhidi ya maslahi ya wengi ndani ya nchi washirika nchini ya muungano wa serikali tatu uliokuwepo.

  • Tarehe 18/3/2014 Jaji Warioba alitoa hotuba ya kihistoria ndani ya Bunge Maalum la Katiba kwa muda wa saa 4 (kuanzia saa 3.30 asubuhi- hadi 7.00 adhuhuri). Ni hotuba ndefu iliyochambua historia ya miaka 50 ya Muungano (1964-2014) kwa lengo mahsusi la kutetea Rasimu ya Katiba ya Serikali tatu. Jaji Warioba ameigawa historia ya Muungano katika awamu mbili. Awamu ya kwanza (1964-1984) ni ya muungano madhubuti wa Nchi moja na serikali mbili. Amesema kuwa katika awamu hii ya miaka 20 ya Muungano kiwango cha utashi wa kisiasa kilikuwa cha hali ya juu sana na viongozi wa kisiasa walikuwa na dhamira ya kweli ya kudumisha Muungano kwa mujibu wa masharti ya Hati za Muungano na Katiba za serikali mbili. Ndicho kipindi ambacho vyama vya ASP na TANU viliungana na kuunda CCM. Awamu ya pili (1984-2014) ni ya Muungano legelege. Awamu hii ilianza mara baada ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa mwaka 1984. Amesema kuwa katika awamu hii ya miaka 30 serikali zote mbili za CCM zimeshindwa kabisa kutatua kero za Muungano na maamuzi yake mengi yamekuwa yakikiuka Katiba na sera ya CCM ya serikali mbili. Kwa hiyo, CCM imekuwa ikinadi serikali mbili majukwaani lakini kichini chini imekuwa ikivunja misingi ya Katiba na sera yake. Anadai kwamba kasi ya kuunda nchi ya Zanzibar ilianza mwaka 1994 ambapo mambo mengi ya Muungano yalipunguzwa bila hata kubadili katiba. Ingawa hakusema kuwa mwaka 1994 yeye aliandika makala kadhaa magazetini kupinga MRADI huo wa kuvunja nchi kimyakimya, lakini hoja zake, ambazo baadhi yake zimo katika makala ya Kamata tunayoijadili, zinathibitisha kwamba hali ya mambo ndani ya CCM na serikali zake mbili haikuwa shwari. Kwamb hali ya kisiasa iliyochafuka tangu 1984 ilikuwa haijatengemaa. Amedai kuwa hata maoni ya taasisi nyeti za serikali (kama ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Baraza la Wawakilishi) yaliyowasilishwa katika tume yake yanamwelekeo wa Muungano wa serikali tatu.
   Ingawa Jaji Warioba alivunja ukimwa mwaka 1994, miaka kumi baada ya kuchafuka kwa hali ya hewa, amethubutu kukaa kimya hadi 2014. Jaji Warioba wa mwaka 2014 ameibuka akiwa na msimamo mpya, msimamo wa Tume ya Marekebisho ya Katiba. Anatetea Mundo wa serikali tatu kwa madai kwamba hayo ni maoni ya wananchi wengi ambayo yanashabihiana na uchambuzi na matokeo ya tafiti za Tume yake. Ukimya wa Jaji Warioba kwa miaka 20 (1994-2014) unatatiza sana. Kama aliweza kuwa jasiri mwaka 1994 na kuandika anayoyaamini kuhusu umuhimu wa Muungano wa serikali 2 kwa nini amekaa kimya kwa miaka 20 huku akishuhudia chama chake kinavunja Katiba ya Muungano na Katiba yake chenyewe? Kwa nafasi ya Jaji Warioba kama mwanasiasa mzoefu ndani ya CCM na kiongozi wa kitaifa wa muda mrefu aliwezaje kukaa kimya kwa miaka 20 huku katiba za nchi na chama chake zikivunjwa?
   Kwa mtazamo wangu, hotuba ya Jaji Warioba imeandikwa mahsusi kujibu hoja na sauti kinzani kuhusu muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume yake. Yeye hakubaliana na wale wote wanaodai kwamba muundo wa serikali tatu utavunja nchi. Ujumbe wa Jaji Warioba katika hotuba yake ni kwamba serikali tatu haziepukiki na wala hazizuiliki. Kwamba makosa yaliyofanywa na chama chake cha CCM kwa miaka 30 (1984-2014) (yeye akiwa kiongozi wa chama na serikali) hayasahihishiki ndani ya Muundo wa serikali mbili; kwamba Muungano wa serikali mbili haupo tena kwa sababu Zanzibar tayari ni nchi na mambo mengi ya Muungano hayatekelezwi ipasavyo. Na kwamba Wazanzibari wote hawatofautiani juu ya haki yao ya kujitawala. Kwamba misingi ya Muungano ni hiari, ushirikiano, mshikamano na kutegemeana. Kwa namna alivyochambua nguvu za makundi ya kisiasa na kijamii yanayopendelea serikali tatu, tena kutoka pande zote mbili za Muungano, Jaji Warioba nadhani alijiandaa kuwaeleza wazi wazi wapinzani wa serikali tatu kwamba wasijisumbue kwani wazanzibari wengi wanataka serikali tatu.
   Kwa maoni yangu, hotuba ya Jaji Warioba itachochea zaidi hisia za Utanganyika na Uzanzibar ndani na nje ya Bunge Maalum. Hata hivyo, hotuba hiyo, na hata ripoti za tume, havijatoa majawabu ya maswali mengi magumu. Kwa mfano, hotuba ya Jaji Warioba na ripoti za Tume yake havichambui mwelekeo wa mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi katika kipindi hicho cha miaka 30 ya ulegevu wa Muungano na athari zake kwa hatima ya Muungano.
   Maswali yafuatayo yanatakiwa kujibiwa kabla ya kukubaliana na hoja za Jaji Warioba wa 2014: Je, uchu wa wanasiasa wa kutafuta vyeo na kulimbikiza mali vina mchango kiasi gani katika kuchochea au kupunguza kinachoitwa ‘kero’ za Muungano? Je, wenye mtaji, yaani mabeberu wanapendelea muundo wa aina gani kati ya Muungano legelege wa serikali tatu na Muungano madhubuti wa serikali mbili? Je, nchi washirika zinaweza kukabiliana barabara na misukosuko ya kimataifa inayoghubika shughuli za uvunaji wa ziada katika sekta za bandari, ardhi, biashara, fedha, kodi, viwanda, gesi na mafuta bila kutikisa Muungano wenyewe? Je, wananchi watapata faida au hasara kiasi gani iwapo utaifa wa kitanganyika na Kizanzibari utapamba moto katika nchi zao mpya? Kwa kuwa Tume ya Jaji Warioba haijayajibu maswali haya kwa ufasaha, ni muhimu tuendelee kuyajadili ili Wajumbe wa Bunge Maalum waweze kufanya uamuzi ambao hautaivunja nchi.

   • Katika makala hii nimekuwa wa kwanza kuchangia tena kwa hisia kali sana! lakini kwa ujumla nimesema nilichokiamini na ninapenda ieleweke wazi kwamba bado ninadiriki kuamini kwamba Jaji Warioba na wenzake kwa hakika wamedhamiria kuudhoofisha zaidi kuliko kuuimarisha Muungano wetu. Ninasema asante jaji Warioba na Tume yako maana mmeandika historia ya kuujaribu Muungano wetu kwa mara nyingine tena! Mbali na kukubaliana na uchambuzi wa ndugu Bashiru, ninadiriki kusema kwamba Warioba na wenzake wametuuzia mbuzi kwenye gunia! Ati wanasema katika mfumo wa muungano wa NCHI TATU patakuwa na uraia wa nchi moja tu, nayo ni Tanzania! (nadhani hili ndugu Bashiru umesahau kulitaja kama moja ya maswali magumu yaliyotanda vichwani mwetu). Kimsingi Warioba na wenzake hawakupaswa kulazimika kutuambia suala la uraia kwani ni dhahiri kwamba ni nchi ndiyo inayotoa uraia. Kwa msingi huo tukiwa na nchi tatu, maana yake ni kwamba kila mshirika wa Muungano atakuwa na uraia wa nchi mbili, Mzanzibar atakuwa raia wa nchi Zanzibar na nchi ya Tanzania, wakati Mtanganyika (ninalichukia hili neno!) atakuwa raia wa nchi ya Tanganyika na nchi ya Tanzania. Kwa maana hiyo basi, raia wa nchi ya Tanganyika hawezi kuwa raia wa nchi ya Zanzibar, kadhalika raia wa nchi ya Zanzibar hawezi kuwa raia wa nchi ya Tanganyika. Nimejaribu kutafuta nchi ambayo imewahi kuwa na Muungano wa namna hii mpaka sasa sijaona. Niombe sana wataalamu wa utafiti wanisaidie kwa hilo. Nia yangu ni kutaka kujua kama kuna Muungano wa aina unaopendekezwa na Tume ya Warioba umedumu kwa muda gani na kama umefanikiwa au la. Nachelea kusema kwamba aina ya Muungano inayopendekezwa na Jaji Warioba na wenzake utekelezaji wake ni wa majaribio tu, na wala hatujui ni kwa kiasi gani tunaweza kufanikiwa kutuvusha kwa zaidi ya miaka hamsini tukiwa salama bin salimini.

    • Nakubaliana na Zainabu Kawawa kwa hili la uraia mmoja ndani ya shirikisho linalohusisha uwepo wa serikali za washirika na ya muungano, yaani nchi washirika na muungano.
     Sahihi ni raia watanzania kuwa na uraia wan nchi zao washirika (Zanzabar, Tanganyika) lakini wenye haki sawa mbele ya yale ya muungano.
     Vinginevyo, kama uraia wa watanzania ni mmoja, basi ni lazima, basi ni lazima uendane muungano Tanzania ulioondokana na uwepo wa nchi washirika na serikali zake (Zanzibar, Tanganyika).
     Hili la uraia ni mojawapo ya mengi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba mpya yanayosubiria kufanyiwa maboresho na Bunge letu tukufu la utunzi wa Katiba mpya inayokidhi matarajio ya wengi ndani ya muungano.
     Hata hivyo siwezi kukubaliana hata kidogo na hoja kwamba muundo wa serikali tatu uliopendekezwa utapelekea muungano kudhoofika na hata kuvunjika.
     Pamoja na kwamba Muungano Tanzania ni wa pekee uliobakia duniani, ni vizuri tukakubaliana pia kwamba na wenyewe ulikuwa uko mbioni kuvunjika kama mingine yote duniani ilivyovunjika kutokana na kutokuzingatia umuhimu wa kushirikisha wananchi walio wengi na matakwa yao kinzani kwenye maamuzi yote husika kwenye kuundwa kwake na kudumisha ‘sovereignties’ za nchi washirika wakati wa kubuni maswala ya muungano na muundo wa serikali yake.
     Tume ya Katiba ilipendekeza serikali tatu baada ya kutambua kwamba wananchi walio wengi ndani ya nchi washirika (Zanzibar,Tanganyika) wangeendelea kuupenda zaidi na kuudumisha muungano wao Tanzania kama muundo wake ungekuwa ni ule unaodumisha na usiodhoofisha ‘sovereignties’ za nchi zao washirika na usioinyima au kuipunguzia nchi yeyote mshirika uhuru wake wa kushikiana na/au kuungana na nchi nyingine zozote duniani zenye manufaa makubwa zaidi kwake kuliko manufaa yatakapotikana kutongana na kushirikiana kwake na Tanganyika au Zanzibar kwenye baadhi ya maswala.
     Ilipopendekeza muundo wa serikali tatu, Tume ilizingatia umuhimu wa kudumisha ‘sovereignities’ za nchi washirika na kuhusisha kwenye muungano Tanzania yale tu yenye manufaa makubwa zaidi kwa nchi nchi zote washirika ikilinganishwa na yale manufaa tarajiwa kutokana na maswala hayo hayo kuhusishwa kwenye muungano wa nchi yeyote mshirika na nchi nyingine zozote duniani.
     Marajio yangu makubwa kwenye hili ni kwamba michango kinzani kutoka kwa makundi yote shiriki kwenye Bunge la Katiba yatapelekea kuboresha pendekezo zuri la muundo wa serikali tatu, hasa kwa njia ya kuzidi kupunguza ya muungano hadi machache tu muhimu sana kwenye muungano Tanzania, kama vile Mambo ya ulinzi na nchi za nje peke yake na kukubaliana wazanzibari wawe raia wa Zanzibar na watanganyika wawe raia wa Tanganyika badala ya watanganyika na wazanzibari kuwa raia wa Tanzani. Ni kisichoeleweka hadi sasa wazanzibari na watanganyika kuendelea kuitwa raia wa Tanzania wakati watanganyika hawana haki sawa na wazanzibari ndani ya Zanzibari.
     Bunge la Katiba limeundwa kutokana na makundi yenye mitazamo kinzani kuhusu yanayopashwa kuwemo ndani ya katiba ya Muungano ili kuwezesha ufanisi kwenye maboresho ya yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba mpya na upatikani wa hybrid inayozingatia matarajio ya Muungano badala ya nchi washirika, baadhi ya makundi au wachache dhidi ya matarajio ya wote ndani ya muungano Tanzania.
     Bunge la Katiba halitarajiwi lifanye kazi kwa kuzingatia hoja ya kundi fulani inayopendwa zaidi kwa wingi wa kura zitokanazo na kundi hilo kuwa na wajumbe wengi zaidi na/au wenye hila na washirika wao wanafiki ndani ya Bunge la Katiba, yaani hoja ya nguvu.
     Linatarajiwa lifanye kazi kwa kuzingatia hoja zote kinzani zenye manufaa katika ngazi ya Muungano na kuhakikisha andiko la hoja kwenye Rasimu ya Katiba linaboreshwa kwa zingatia zote hizo muhimu hadi kuwa hybrid inayokidhi matakwa ya wengi zaidi katika ngazi ya muungano Tanzania.
     Ni muhimu pia Bunge likazingatia kwamba baadhi ya hoja za minorities zinaweza kuwa na usahihi na umuhimu mkubwa zaidi kuliko hoja za baadhi ya walio wengi ndani ya Bunge la Katiba na kwamba baadhi ya waliochangia hoja zilizozaa Rasimu ya Katiba ni wenye ujuzi bora zaidi husika kwenye utunzi wa Katiba mpya kuliko ya walionao wengi ndani ya Bunge la Katiba na hivyo kuhakikisha yanayopendekezwa na minorities na yaliyomo kwenye Rasimu) hayadharauliki kwenye Bunge la Katiba.
     Tukubaliane kwamba Katiba nzuri kwenye ngazi ya Muungano haitapatikana na uwepo wa wenye hila na wahirika wao ndani ya Bunge la Katiba uliolenga kufanikisha upatikanaji wa Katiba mpya inayodumisha na kuendeleza maslahi yao binafsi dhidi ya maslahi ya walio wengi katika ngazi ya muungano Tanzania.

 4. Oktoba 10, 2011 Jaji Joseph Alifanya Mahojiano na Mwandishi wa Raia Mwema, mahojiano yaliyochapishwa katika Gazeti la Raia Mwema, Toleo la 209, Tarehe 26 Octoba 2011. Mahojiano hayo katika gazeti yalibeba kichwa cha Habari “Jaji Warioba: Tusidanganyane, kutaka Serikali tatu ni kuvunja Muungano.

  Kutokana na umuhimu wa maoni yake, na msimao wa Jaji Warioba wa 1994 kufanana na huu wa mwaka 2011, tunaweka hapa sehemu ya mahojiano hayo kuhusu muungano kuwa sehemu ya mjadala unaoendelea hivi sasa kuhusu katiba na hususan muundo wa Muungano (Moderator).

  Suala la Muungano pia liwe katika Katiba. Tusipokuwa makini kwa maneno yanayozungumswa sasa tutavunja Muungano.

  Muungano huu una misingi yake na upo kwa manufaa ya wananchi. Tufafanue manufaa hayo ni nini kwa mwananchi wa kawaida.

  Wakati wote kwa mwananchi wa kawaida, kumekuwa hakuna matatizo ya Muungano. Matatizo yanatoka kwenye midomo ya viongozi.

  Shughuli za wananchi wa kawaida haziangalii orodha ya mambo ya Muungano, bali haki yao kama raia. Wanajiona ni raia katika shughuli zao za kibiashara au nyingine. Mwananchi wa kawaida anaona anayo haki ya kufanya biashara mahali popote. Wananchi wamezoa hivyo. Msiwafikishe mahali wakajiona kuwa kwenda Zanzibar au kuja Bara inabidi wafuate taratibu za kwenda Kenya au Uganda.

  Tunayo matatizo ya madaraka, kwamba unazo Serikali mbili kwa hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha Serikali hii ina madaraka gani. Wanagombania madaraka.

  Kama suala ni mafuta au mengine tuzungumze. Inategemea mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo yatakuja kuwatenganisha wananchi. Kama kwa mfano, kuna watu wanafikiri kuimarisha Muungano ni kuwa na serikali tatu, unaimarishaje?

  Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote.

  Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa.

  Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa pande zote mbili. Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake unavunja Muungano.

  Endelea kusoma zaidi hapa: http://www.raiamwema.co.tz/jaji-warioba-tusidanganyane-kutaka-serikali-tatu-ni-kuvunja-muungano

  • Hotuba ya Rais wa Tanzania (Mh. Jakaya Mrisho Kikwete) alipokuwa akifungua rasmi Bunge maaluma la utunzi wa Katiba mpya ya Tanzania, ilikuwa nzuri mno kwa sababu kwa kuonyesha bayana kwamba muungano wa serikali tatu ulipondekezwa kwenye rasimu ya katiba mpya unahitaji kazi kubwa ya kubuni majibu ya changamoto zake nyingi, mpya na ngumu ikilinganishwa na kazi ndogo ya kubuni majibu ya changamoto chache, zilizozoeleka na rahisi kwenye muungano tulio nao wa serikali mbili, hotuba hiyo imepelekea kwenye chaguo la muungano wa serikali tatu kwani mafanikio makubwa hayapatikani kwa njia za mkato zinazopelekea upatikanaji wa majibu rahisi rahisi.Tuchague ile njia refu na yenye vikwazo vingi na vigumu, yaani muungano wa serikali tatu na Bunge letu tukufu liwekeze akili na bidii zote kwenye kubuni majibu sahihi kwa changamoto zake ili kuwezesha upatikanaji wa katiba mpya na nzuri iliyojengeka kwenye msingi madhubuti wa muungano wa serikali tatu ulioboreshwa kikamilifu. Kama ni muda na nguvu za ziada Bunge hilo liongezewe kwani gharama inapolinganishwa na faida ni sawasawa na kulinganisha tone la maji na rundo la maji baharini. Jamii iliyosheheni wavivu wa kufikiri na wapendeleo njia za mkato na majibu rahisi rahisi kwenye maswala magumu na yenye uzito mkubwa kwenye uhai na maendeleo ya jamii yao kama hili la muundo wa serikali ya muungano Tanzania mara nyingi hubakia kuwa miongoni mwa zilizobakia nyuma sana kimaendeleo hapa duniani. Ushabiki wa kisiasa ulioonekana waziwazi kutawala Bunge letu la Katiba wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa akiwasilisha hotuba ya ufunguzi ukiendekezwa Bunge hilo halitafanikiwa hata kidogo kutupatia hotuba nzuri. Muungano wetu ukitumia akili nyingi na maarifa hautashindwa kubuni Katiba mpya iliyojengeka kwenye msingi madhubuti wa muungano wa serikali tatu itayodumisha na kuendeleza muungano wetu na kuleta manufaa makubwa zaidi kwa taifa letu la Tanzania.

 5. Michango yenu mingi imelenge kumshutumu warioba badala ya kazi ya tume.
  Kwa maoni yangu Zanzibar ina sehemu kubwa ya kufanya kuhusu katiba yao ili maridhiano yapatikane juu ya serikali 2 au tatu.
  Wanzibari wakiendeleza utaifa wao hakika hakuna mfumo wowote wa muungano ambao utafaa na kutusukuma kwa miaka 50-100 ijayo.

  • ‘Wanzibari wakiendeleza utaifa wao hakika hakuna mfumo wowote wa muungano ambao utafaa na kutusukuma kwa miaka 50-100 ijayo’.

   Hakuna uhakika wa muungano chini ya muundo wa serikali 2 kuweza kutusukuma kwa miaka mingine 50-100 ijayo hata kama Zanzibar itaamua leo hii kuachana na utaifa wake kupitia marekibisho ya Katiba yake, kwani baada ya marekebisho hayo bado inaweza tena kujirudishia utaifa huo siku za karibuni kupitia marekebisho mengine ya Katiba yake.
   Uhakika wa muungano kutusukuma kwa miaka mingine 50-100 ijayo haupo hata kama utakuwa chini ya muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Warioba kwani nchi ya Zanzibar au Tanganyika bado inaweza kuamua kujiondoa kwenye muungano huo wakati wowote kupitia mabadiliko ya Katiba yake au kura ya maoni.
   Uhakika wa muungano kutusukuma miaka mingine 50-500 na zaidi ijayo utakuwepo tu Zanzibar itakapoamua kuachana na utaifa wake na serikali yake na kujiunga na Tanganyika ili kuifanya Tanzania iwe chini ya mwongozo wa Katiba moja na utawala wa serikali moja isiyotoa fursa kwa mshirika yeyote kujitoa.
   Inaonekana muundo wa serikali mbili za washirika na muungano wa mkataba uliopendekezwa kwa wingi wa kura na chama cha wananchi CUF huko Zanzibar ndio ungefaa kwenye mazingara haya ya kutokuwepo uhakika wa muungano Tanzania chini ya muundo wa serikali 2 au 3 kutusukuma miaka mingine 50-100 au zaidi ijayo.
   Kwa hiyo changamoto kubwa zaidi Bunge maalumu la utunzi wa Katiba mpya ya Tanzania litakalokumbana nayo ni ile ya kuwapatia watanzania muundo wa serikali ya muungano na Katiba mpya inayowapa uhakika wa muungano kutusukuma mbele miaka mingine 50-100 na zaidi ijayo.
   .

  • Kinachodajiliwa hapa barazani siyo watu au vikundi vya watu bali ni fikra zao, mitazamo yao na hoja zao. Shabaha kuu ya milubi inayojitokeza hapa barazani ni kuchambua namna fikra, mitazamo na hoja hizo vinavyoathiri mustakabali wa wavujajasho wa bara zima la Afrika, Tanzania ikiwemo. Kujadili fikra, mitazamo na hoja za mtu au kikundi cha watu.

   Tatizo la kuendekeza Utanganyika na Uzanzibari liko katika sehemu zote mbili za Muungano na wala siyo kweli kwamba tatizo hili linaendekezwa upande wa Zanzibar. Vile vile hoja zinazopinga Utanaganyika na Uzanzibari zinatolewa na watu kutoka pande zote za Tanzania

   • Ingekuwa ni kweli kwamba uwepo wa muungano Tanzania ni matokeo ya moyo wa dhati walio nao wengi ndani ya Tanganyika na Zanzibar kupendelea zaidi kuungana na kuwa taifa moja lenye fursa na haki sawa na nyingi zaidi kwa wote badala ya kuendelea kuwa mataifa mawili tofauti yenye fursa na haki tofauti na chache zaidi, basi muungano huo ungekuwa ni hiyo nchi moja ya muungano Tanzania inayotawaliwa na serikali moja ya muungano au ni ule unaohusisha nchi mbili (ya Tanganyika na serikali yake na ya Zanzibar na serikali yake) na unaotawaliwa na serikali moja ya muungano.
    Kero zote za muungano zimesababishwa na muundo wake usiotoa fursa na haki sawa na nyingi zaidi kwa wote (ndani ya Tanganyika na Zanzibar) kutokana na kuhusisha nchi ya muungano Tanzania (inayotawaliwa na serikali ya muungano) na nchi ya Zanzibar (inayotawaliwa na serikali ya Zanzibar) huku Tanganyika ikiwa imepoteza utaifa wake na serikali yake.
    Kuwepo kwa hisia za utanganyika ndani ya muungano ni kiashirio cha watanganyika kuwapo kwenye harakati za kupigania fursa na haki sawa na wenzao wazanzibari ndani ya muungano Tanzania. Wakati huo huo, kuwepo kwa hisia za uzanzibari ndani muungano ni kiashirio cha uwepo wa wazanzibari usiokuwa wa hiari na unaoendeleza kupigania fursa na haki nyingi zaidi dhidi ya wenzao watanganyika ndani ya muungano Tanzania.
    Njia pekee ya kumaliza kero za muungano Tanzania na hisia za utanganyika na uzanzibari ndani yake ni kuupatia muundo wa serikali na Katiba mpya inayotoa fursa na haki sawa na nyingi zaidi kwa watanzania wa pande zote mbili kwenye muungano. Hili ndilo linalotarajiwa na watanzania wengi kwenye Katiba mpya iliyoko kwenye utunzi unaofanywa na Bunge maalumu huko Dodoma.

 6. Tumeanza kuijadili Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya kwanza (1) ya Rasimu ya Katiba inaitafsiri Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba ni NCHI na SHIRIKISHO lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru. Kwanza kabisa, neno NCHI na SHIRIKISHO yananipa taabu kuya changanya pamoja. Lakini neno Shirikisho linanipa taabu zaidi hasa ukizingatia kwamba tafsiri ya Shirikisho au \”federation\” linataka nchi mbili ambazo kila moja inayo mamlaka kamili, ziungane. Kwa tafsiri hiyo ili tuweze kuwa na Shirikisho kwanza, itatulazimu kuuvunja Muungano, pili, tuanzishe nchi inayoitwa Tanganyika (iwe ni nchi kamili yenye katiba yake) na hatmaye nchi hizo mbili yaani jamhuri ya Tanganyika pamoja na Jamhuri ya watu wa Zanzibar kwa ridhaa zao wenyewe ziunde Shirikisho linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanziania! Je, kuna haraka gani ya tume ya Jaji Warioba kutuletea katiba ambayo inataka kuwepo kwa shirikisho kabla ya kuwa na nchi mbili tofauti na zenye mamlaka kamili? na je, kuna uhalali gani wa kuendelea kuijadili katiba hii ilihali hatuna nchi inayoitwa Tanganyika? JE, AINA YA MUUNGANO ULIOPENDEKEZWA NA KATIBA INAENDELEZA DHAMIRA YA DHATI YA KULINDA, KUIMARISHA NA KUUDUMISHA MUUNGANO ULIPO??? JE, MUUNGANO ULIOPENDEKEZWA NA TUME YA JAJI WARIOBA NI DHAIFU???

  • Mheshimiwa Zainab, hapo umenena kama kiongozi huru na ambaye hakutawaliwaa na wengine kiakili. Naungana nawe mia kwa mia kwamba kilichotakiwa kwanza ni serikali na Katiba ya Tanganyika iwepo kwanza. Serikaliza za Tanganyika na Zanzibar zilibidi ziwepo ili kusimamia watanganyika na wazanzibari kwenye zoezi lao la kuchagua muundo wa serikali ya muungano waipendayo kupitia kura ya maoni na uchaguzi wa wakilishi wao kwenye Bunge maalumu la utunzi wa Katiba ya muungano ili kuhakikisha Katiba ya muungano itakayopatikana ni ile itakayoboresha zaidi matarijio kwenye Katiba zao kama nchi washirika.
   Bila serikali yao na Katiba yao ya Tanganyika, watanganyika wamenyimwa mwongozo wa Katiba na uongozi wa serikali yao kama wazanzibari wanavyofaidi mwongozo wa Katiba na uongozi wa serikali yao kwenye zoezi zima la utunzi wa Katiba ya muungano na hivyo kupelekea Katiba ya muungano itakayopatikana kuwa ni ile iliyosukwa kwa kuzingatia zaidi kero za muungano wa serikali 2 uliopo kwa wazanzibari na inayoboresha matarajio kwenye Katiba ya wazanzibari dhidi ya matarajio ya watanganyika.
   Mifumo ya shirikisho ndiyo iliyoonyesha mafanikio makubwa kwa nchi zote washirika kwenye ngazi za dola kwani inatoa fursa sawa kwa wote na ni boreshi badala ya kuwa kikwazo kwa nchi washirika kwenye harakati zao za kujitafutia maendeleo yao wenyewe kwa njia ya ushindani na nchi nyingine zote ndani ya utandawazi ulimwenguni. Shirikisho zuri ni lile linalohusisha nchi mbili zinazoungana ili kuzaa serikali moja ya muungano itakayoboresha majukumu ya serikali za nchi washirika na matarajio kwenye katiba zao kama nchi washirika na sio lile linalohusisha nchi mbili kuungana ili kuunda nchi ya tatu ya muungano. Muungano kama huo utakuwa na kero chungu mzima na sidhani mfano wake upo mahali popote duniani.
   Kwa hivyo nakubaliana na Mh. Zainab kwamba Katiba ya shirikisho ilipashwa itokane na nchi washirika zenye dola kamili na Katiba zao ili hiyo ya muungano iweze kuwa ni ile itakayoboresha utawala wa serikali zao na matarajio yao kama nchi washirika.
   Hapana, Tume ya Warioba haijafanya kosa kwa kutuletea Katiba ya muungano wakati nchi mshirika Tanganyika na hata serikali na Katiba yake haipo. Utunzi wa Katiba ya muungano unaohusisha chaguo la muundo wa serikali ya muungano linaweza sana kufanywa kwa pamoja kama Tume ya Warioba ilivyofanya na baadaye utunzi wa Katiba za nchi washirika na uundwaji wa serikali za washirika ukafuata baadaye kwa kuzingatia Katiba ya muungano. Nchi itakayoumia hapa ni Tanganyika ambayo haitakuwa na mwongozo wa Katiba yake na uongozi wa serikali yake kwenye kuhakikisha ushiriki wake kwenye utunzi wa katiba ya muungano ni uliolenga kuboresha ufanisi wa serikali yao ya Tanganyika na matarajio ya watanganyika kwenye Katibas yao ya Tanganyika.
   Cha muhimu hapa ni Bunge maalumu lijadili muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na kama wengi hawataridhika nalo, basi zoezi la utunzi wa katiba mpya lisitishwe ili kutoa fursa kwa watanzania waamue ni muundo gani wa serikali ya muungano wanaoutaka kama msingi muhimu kwenye utunzi wa katiba mpya ya muungano. Wengi wakilikubali pendekezo la serikali tatu, zoezi la utunzi wa Katiba ya muungano liendelee na zoezi la utunzi wa Katiba ya Tanganyika na uboreshaji wa ya Zanzibar lifuate kwa kuzingatia Katiba ya Muungano iliyopitishwa.
   Haraka haraka haina baraka, ikibidi kurudi nyuma ili tufanikishe upatikanaji wa Katiba iliyo bora zaidi kwa njia ya kuanza upya zoezi zima la utunzi wake kwa umakini na kupitia njia iliyo sahihi zaidi ni budi tukafanya hivyo.

  • Nimesoma kwenye gazeti la RAI toleo na. 1140 la tarehehe3-9 mada moja yenye mambo muhimu sana ya kuzingatia na Bunge maalumu la utunzi wa Katiba mpya ya Tanzania unaoendelea kwa sasa huko Dodoma.
   Mada hiyo ni sehemu ya kwanza ya inayoendelea chini ya kichwa cha habari ‘’Majibu kwa Malalamiko ya Warioba na hofu za Kikwete’ iliyoandaliwa na Mh. Zitto Kabwe (MP). Mheshimiwa amefanya utafiti mzuri sana uliomwezesha kupendekeza Muungano Tanzania uwe ni Muungano wa serikali 3 badala ya Shirikisho la serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba kwenye Rasimu ya katiba mpya.
   Nimefurahishwa sana Mheshimiwa alipotambua umuhimu wa kuongeza serikali ya 3 (ya Tanganyika) kwenye Muungano Tanzania uliopo chini ya muundo wa serikali 2 ili kuwatendea haki watanganyika kwa kuwapa haki ya kudumisha na kufaidi serikali yao ya Tanganyika kama wazanzibari wanavyofaidi yao iliyodumishwa ndani ya Muungano Tanzania.
   Hata hivyo sikubaliani na Mh. pale anapopendekeza kwamba badala ya Shirikisho Tanzania (linalotoa fursa kwa nchi yeyote mshirika kulivunja pale itakapoamua ni heri kujitoa kutokana na kero zitakazokuwa zikijitokeza kuendana na muda na ambazo hazina jibu jingine zaidi ya marekibisho ya muundo wa serikali ya Muungano au kuondokana nao) iwe Muungano Tanzania (usiotoa fursa kama ya kujitoa kwa nchi yeyote mshirika).
   Sikubaliani na Mh. kwa sababu vizazi vya leo havitakuwa vimevitendea haki vijavyo pale vya leo vinapovinyima vijavyo uhuru wa kurekebisha au kuondokanana na muundo wa serikali ya Muungano Tanzania uliopandikizwa kwa kuzingatia mazingara ya vizazi vilivyopo na ambayo yamebadilika na kuwa tofauti na mazingara ya vizazi vilivyo.
   Mazingara ya nyakati zijazo yanaweza kuwa tofauti sana na yaliyopo kwa sasa na hivyo kuhitaji mabadiliko ya muundo wa serikali Tanzania (hata kuuvunja) yafanywe ili kuwezesha mazingara ya nyakati zijazo yawe na tija zaidi kwa nchi mshirika au washirika ndani ya Tanzania.
   Hivyo, ni vizuri sana kama tungeanzia na Jumuia Tanzania itakayozaa Shirikisho Tanzania na hata kkwenye kilele cha Muungano wa serikali tatu na hata moja Tanzania kwa kuzingatia mazingara mapya yanavyozidi kujitokeza kuendana na muda na kukomaa kwa ushiriano baina ya watanganyika na wazanzibari.
   Tunaweza kuanzia na Shirikisho Tanzania moja kwa moja kwa sababu watanganyika na wazanzibari wameshazoeana kwa kiasi fulani ndani ya Muungano wa serikali 2 Tanzania na baadhi ya kero zikiwa zimekwisha kujulikana na kupatiwa ufumbuzi, hata kama nyingi bado hazijajitokeza na kupatiwa ufumbuzi kutokana na watanganyika kutokuwa na serikali yao kama wazanzibari walivyo na yao ndani ya Muungano Tanzania uliopo.
   Tuanzie na Shirikisho la serikali 3 Tanzania badala ya Muungano wa serilikali 3 Tanzania ili kutoa kwa vizazi vijavyo fursa ya kuboresha au kurekebisha kwa kuzingatia mazingara ya nyakati zao. Tanganyika au Zanzibar zitakuwa zimefanya makosa makubwa kuingia kwenye Muungano Tanzania wakati hazina uwezo wa kutabiri athari zake zote zitakazokuwa zikijitokeza na kuhitaji mabadiliko muundo wa serikali ya ushirikiano Tanzania au kuivunja kabisa kadri muda utakavyozidi kwenda.
   Zinazoitwa kero za Muungano wa serikali 2 Tanzania uliopo zimesababishwa zaidi na huo muundo wa serikali 2 usitoa fursa kwa watanganyika kuwasilisha (kupitia serikali yao ya Tanganyika) kero za Muungano wanazokumbana nazo kwa serikali ya Muungano ili zitatuliwe kwa mapema iwezekanavyo na kuinyima nchi yeyote mshirika uhuru wa kujitoa kwenye baadhi ya maswala ya Muungano au Muungano itakapoona ni muhimu kufanya hivyo ili iweze kufaidi zaidi mazingara mapya ya utandawazi ulimwenguni yatakayokuwa yakibadilika mara kwa mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box