Kwa Wajumbe wa Bunge Maalum: Wasuteni Mabeberu na Vibaraka Wao

Makala hii kwanza ilitoka katika Gazeti la Raia Mwema la 19th Februari 2014

Na Bashiru Ali

Kwa yakini, upo ushahidi wa kihistoria unaobainisha kwamba mapambano ya ukombozi barani Afrika yanaendelea. Kwa ujumla, bado nchi zote za Afrika zinaendelea kudidimizwa na kukandamizwa na Mabeberu kwa kushirikiana na vibaraka wao. Mabeberu ni watu au asasi ambazo asili ya mitaji yao na uendelevu wa utajiri wao ni matokeo ya vitendo vya Uporaji, Ujangili, Uonevu, Dharau , Unyonyaji, Unyanyasaji, Ufisadi na Dhuluma . Vitendo hivyo vimetendwa, kuenezwa na kuendelezwa kwa mbinu mbalimabali duniani kote tangu enzi za Ukoloni hadi zama hizi za Utandawazi. Mabeberu wana vibaraka wao katika kila nchi ya Kiafrika. Afrika ndilo bara pekee linaloendelea kudidimizwa na kukandamizwa zaidi na vitendo hivyo viovu vya mabeberu kuliko bara lingine lolote duniani. Tanzania ni mojawapo ya nchi chache duniani zenye historia ya kuongoza mapambano dhidi ya ubeberu duniani.Historia hii inapaswa kuendelezwa na kudumishwa kwa mustakabali wa uhai wa kizazi hiki na vizazi vingi vijavyo.

Ikiwa wajumbe wa Bunge Maalum watakuwa waangalifu, wazalendo na wabunifu, mchakato huu wa Katiba unaweza kuchochea zaidi mapambano dhidi ya mabeberu na vibaraka wao. Bila shaka mapambano yenyewe yataendelea hata baada ya Katiba Mpya kupatikana. Ni ukweli wa kihistoria pia kwamba ipo siku, mabeberu kama wakoloni, nao watasalimu amri.Natambua kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum wamepata nasaha za makundi na watu mbalimbali hasa kuhusu namna bora ya kulitumikia Taifa. Hili ndilo lengo la makala haya pia.

Kwa kuzingatia muktadha wa sasa, ninawanasihi Wajumbe wa Bunge Maalum wajihadhari na vishawishi na hila za Mabeberu na Vibaraka wao. Utangulizi wa makala haya ni sehemu ya ufafanuzi wa nasaha zangu. Hata hivyo, itabidi Wajumbe wa Bunge Maalum wapime uzito wa hoja na mantiki ya nasaha wanazopewa. Hii siyo kazi rahisi kwa sababu kila mtoa nasaha ana shabaha yake na mtazamo wake . Bila shaka Wajumbe wanatambua kwamba sheria inayoongoza mchakato wa Katiba haijawabana kwa namna yeyote ile bali imewapa mwongozo wa namna bora ya kutekeleza wajibu wao. Wanatakiwa watimize wajibu wao huo bila woga, ghilba, inda, jazba, ubinafsi au ushabiki.

Ninawasihi pia wausome kwa makini Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 (Toleo la 2010) kisha wautafakari na wayatumie maudhui yake wakati wa kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba. Kwa maoni yangu, Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar una ujumbe mzito unaobainisha kwa ufasaha jukumu la Waafrika la kuendeleza na kudumisha mapambano dhidi ya ubeberu.

Katika Utangulizi huo, Watanzania tunakiri na ‘kukubali kwamba jukumu letu…katika historia ya kuimarisha umoja ni kuendeleza Mapinduzi ya Kijamaa na kusukuma Mapambano ya Ukombozi nchini, katika Afrika na duniani kote’.

Kuhusu asili ya umoja wetu, Watanzania tunakiri na ‘kutambua kwamba Umoja wa nchi unatokana na ushirikiano wa miaka mingi… wakati wa mapambano ya kupigania uhuru… na siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea’.

Kuhusu mapambano dhidi ya mabeberu na vibaraka wao, Watanzania tunaahidi kuendeleza mapambano dhidi ya ‘Ukoloni, Ubepari, Unyonge, Uonevu na Dharau’.

Mtu yeyote atakayesoma Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar atabaini haraka kwamba hii ni Katiba ya nchi huru ya Kiafrika yenye historia ya kuongoza mapambano dhidi ya ubeberu na iliyoungana na nchi nyingine huru ya Kiafrika na kuunda Jamhuri moja ili kudumisha umoja na kuendeleza mapambano dhidi ya ubeberu. Kwa maoni yangu, Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar una maudhui yanayofaa kujumuishwa kwenye Utangulizi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wajumbe wote wakiyazingatia maudhui hayo, watakuwa wamewasuta mabeberu na vibaraka wao.

Kwa bahati mbaya, Utangulizi uliopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba hauitambulishi vema historia ya mapambano ya ukombozi wa nchi yetu na hauenzi ushiriki wetu katika mapamabano dhidi ya ubeberu duniani. Ni utangulizi mrefu ambao hauwasuti mabeberu na haubainishi kwa uwazi mwelekeo wa mapambano dhidi ya Ubeberu katika siku za usoni . Haya ni makosa yakusahihishwa na Bunge Maalum. Bila shaka yako makosa mengi zaidi ya haya.

Vile vile ni muhimu watanzania tutamke waziwazi ndani ya Utangulizi wa Katiba Mpya kwamba mapambano dhidi ya Ubeberu yataendelezwa na vizazi vijavyo. Napendekeza hivyo kwa sabau bado mirija ya mfumo wa kinyonyaji haijakatwa, mbegu zake zinaendelea kuota, maua yake yanaendelea kuchanua, matunda yake yanaendelea kukomaa na hila za mabeberu dhidi ya uhuru wa nchi za Afrika hazijakoma.

Mabeberu na vibaraka wao wanaendelea kuwekeza mitaji yao barani Afrika na wanaendelea kufadhili miradi mbalimbali kwa visingizio vya kukuza ubia wa maendeleo na demokrasia. Pamoja na kiwango cha uwekezaji na ufadhili kukua, ufukara barani Afrika unaongezeka kwa kasi, ufisadi unatamalaki, machafuko ya kisiasa yanasambaa na uporaji wa raslimali za Afrika unashamiri. Kwa hiyo, lengo halisi la mabeberu siyo maendeleo wala demokrasia bali ni kulinda maslahi yao ya zamani, ya sasa na yajayo. Mabeberu wanatumia mbinu za biashara, uwekezaji, misaada na ufadhili kulinda maslahi yao. Hata nguvu za kijeshi na hila za kisiasa zinatumiwa pale inapobidi. Mabeberu wamefanya hivyo huko nyuma na wanaendelea kufanya hivyo leo. Ningependa kuthibitisha hoja yangu kwa mifano ifuatayo.

Katika miaka ya sitini, mabeberu walimuua kikatili Waziri Mkuu wa Kongo, Patrick Lumumba, na walimpindua Kwame Nkrumah, Kiongozi Mkuu wa Ghana. Hawa walikuwa wapinzani wakuu wa Ubeberu. Utawala wa Rais Mobutu wa Zaire nao ulifadhiliwa na kulindwa na mabeberu pamoja na kwamba alikuwa mtawala katili na fisadi. Rais Mstaafu Nelson Mandela wa Afrika Kusini na mamia ya wapigania uhuru wenzake walifungwa na kuteswa na utawala wa kikaburu. Ukaburu uliungwa mkono kwa hali na mali na mabeberu. Nchi ya Libya imetumbukizwa kwenye machafuko ya kisiasa tangu 2011 kutokana na uvamizi wa kijeshi wa mabeberu. Libya imesambaratika na raslimali zake za mafuta zinaporwa na mabeberu. Maslahi ya kisiasa na kiuchumi ndiyo yaliyowasukuma mabeberu kufanya vitendo hivyo vya kikatili na kinyama. Maovu haya hayasahauliki.

Mnamo tarehe 27, November 2013 gazeti la ‘the Guardian’ la Uingereza lilichapisha malumbano baina ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Tony Blair, na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, kuhusu namna serikali ya Uingereza ilivyojaribu kuishinikiza serikali ya Afrika Kusini ili ishiriki katika mpango wa kuipindua kijeshi serikali ya Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe. Huo ulikuwa wakati wa machafuko ya kugombea ardhi mwanzoni mwa miaka ya 2000. Pamoja na Bwana Tony Blair kukanusha tuhuma hizo, Komredi Thabo Mbeki ameshikilia msimamo wake kwamba mpango huo haramu ulikuwepo na kwamba yeye aliupinga kwa sababu aliamini kwamba jukumu la kujenga demokrasia nchini Zimbabwe ni la Wazimbabwe wenyewe na sio la Wakoloni wao wa zamani.

Hivi sasa Bwana Tony Blair anafadhili ‘mradi wa utawala bora’ barani Afrika na ofisi za taasisi inayoratibu na kuendesha mradi huo ziko katika nchi za Liberia, Rwanda, Siera-Leone, Malawi na Sudani Kusini. Tusisahau kwamba nchi za Sudani Kusini, Liberia, Rwanda na Siera-Leone zimekumbwa na machafuko makubwa ya kisiasa amabayo chimbuko lake hasa ni migongano ya kimaslahi baina ya mabeberu na vibaraka wao. Machafuko kama hayo yamezikumba nchi za Afrika ya Kati, Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Somalia. Machafuko hayo hayawazuii mabeberu kuendeleza uporaji.

Hivi sasa serikali ya Kenya inalumbana na serikali ya Marekani. Serikali ya Kenya inalituhumu Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) kwa kuwafadhili kwa kificho wanaharakati wanaoendesha kampeni dhidi ya utendaji wa serikali ya Rais Uhuru Kenyata. Balozi anayeiwakilisha Marekani nchini Kenya amekanusha tuhuma hizo. Malumbano haya yameripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa hasa BBC. Lisemwalo lipo na kama halipo laja.

Kwa mifano hiyo michache, ninajenga hoja kwamba mabeberu wana historia na hulka ya kuingilia na kuvuruga mifumo ya kisiasa na kiuchumi katika nchi za Kiafrika kwa nia ya kuendeleza, kukuza na kulinda maslahi yao ya zamani, ya sasa na yajayo. Kwa mantiki hiyo hiyo na kwa kutumia ushahidi wa kihistoria, sina shaka kwamba mabeberu wanafuatilia kwa ukaribu mchakato wa kutunga katiba mpya hapa nchini. Huu ndiyo ukweli wa kihistoria unaotakiwa kukaririwa na kila mwanachi na hasa kila mzalendo. Ni wale tu wasioielewa vema historia ya ubeberu barani Afrika au wale wanaoishi kwa makombo ya mabeberu ndiyo wanaoweza kupingana na hoja hii. Huu ndiyo msingi wa nasaha zangu kwa Wajumbe wa Bunge Maalum.

Kwa hiyo, Wajumbe wa Bunge Maalum wanatakiwa kuwa makini na hila za mabeberu wakati wote watakapokuwa Dodoma. Waepuke kuwa vibaraka wa mabeberu na wakatae vishawishi na hoja za kilaghai zinazoenezwa na mawakala wao amabao nao bila shaka watapiga kambi Dodoma. Wakifanya hivyo watakuwa wamewasuta mabeberu na vibaraka wao. Kitendo hicho kitakuwa kitendo cha kihistoria na cha kishujaa.

Hata hivyo, kazi ya kuwasuta mabeberu na vibaraka wao ni ngumu zaidi hivi sasa kuliko enzi za TANU na ASP. Enzi za TANU na ASP, ‘[M]wamko wa kitaifa na wa kizalendo ulikuwa rahisi kumpata Mwafrika wa Tanzania… maana adui, ambaye ni mtawala wa kigeni, alikuwa anaonekana wazi wazi na hivyo suala la fedheha ya kutawaliwa ilikuwa rahisi kulieleza na rahisi pia kueleweka na kumkera mtu. Uadui wa mfumo wa kibepari ni mgumu zaidi kuuelezea mpaka ueleweke na kumtia mtu mori ya kuuchukia na kuukataa. Ubepari au unyonyaji si suala la rangi ya mtu na hivi sasa baadhi ya wanyonyaji ni Waafrika wenzetu’[soma ibara ya 41 ya Mwongozo wa CCM wa 1981).

Kwa maoni yangu, Ibara ya 41 ya Mwongozo wa CCM wa 1981 ina hoja nzito inayochochea tafakuri hasa katika kipindi hiki kigumu cha mpito kuelekea Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa 2015. Ikumbukwe kuwa, Mwongozo wa CCM wa 1981 ulipitishwa katika kipindi ambacho hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini ilikuwa ngumu sana kama ilivyo hivi sasa. Wakati huo, nchi ilikuwa imetoka vitani (Vita vya Kagera) na mpango haramu wa kulitungua Azimio la Arusha ulishaanza kutekelezwa na mabeberu na vibaraka wao.

Hata hivi sasa nchi yetu iko vitani, vita vya kupambana na ujangili, ufisadi, unyonyaji na uporaji wa raslimali za Taifa. Tena hakuna dalili hivi sasa kwamba mabeberu na vibaraka wao wataunga mkono mapendekezo ya mfumo mbadala wa ulimbikizaji mtaji na ugawaji ziada unaowanufaisha wavujajasho. Wangependa tuwe na Taifa legelege na linalonyonyeka kirahisi. Hata nchi ikivunjika wao hawatajali. Wamefanya hivyo Afghanistan, Libya, Sudan, Iraq na Syria na wanajaribu kufanya hivyo Ukrain na Venezuela.

Kwa hali ilivyo sasa, mabeberu na vibaraka wao wamo miongoni mwetu, wazalendo nao wamo miongoni mwetu na hata mafisadi pia wamo miongoni mwetu. Ndiyo maana mabeberu wameweza kutugawa watakavyo. Watanzania hatutambuani kiitikadi na kimsimamo na wala hatufanyi udadisi ili kutambuana. Hivi sasa vibaraka wa mabeberu wanapambana wao kwa wao ili watutawale kwa niaba ya mabwana zao. Wanatununua kama unga wa sembe tena kwa kutumia pesa chafu. Na kwa bahati mbaya tunashabikia siasa hizi za kutugawa bila hata kuzidadisi. Tunaendelea pia kukariri mawazo ya mabeberu kama Kasuku huku tukishangilia misaada yao. Umezuka pia mtindo katika baadhi ya maeneo nchini ambako wananchi hukosana, hupigana na hata kuumizana kwa sababu ya kutetea maslahi ya mabeberu na vibaraka wao.

Vijana wasio na ajira nao wanachonganishwa na vibaraka wa mabeberu pasipo kujua kwamba nishati na vipaji vyao vinaweza kutumiwa vibaya kulisambaratisha taifa lao. Katika baadhi ya maeneo, vijana wametoboana macho, wengine wameshambuliana kwa mapanga na wengine wamemwagiana tindikali kwa sababu za kipuuzi. Badala ya kushikamana na kupambana dhidi ya mabeberu na vibaraka wao, vijana wanatengana na kuhujumiana wao kwa wao. Hizi siasa uchwara sizipewe nafasi katika Bunge Maalum la Katiba. Hata hivyo, ni vigumu kutabiri kitakachotokea. Matarajio ya wengi ni kwamba mambo yatakuwa shwari.

Wajumbe wa Bunge la Katiba mna wajibu wa kukataa vishawishi na shinikizo za mabeberu na vibaraka wao. Mnao uchaguzi wa aina mbili: kuwatumikia mabeberu na vibaraka wao au kulitumikia Taifa na Bara la Afrika. Kama alivyotuasa Mwalimu Nyerere: “kupanga ni kuchagua”. Kumbukeni, historia ndiyo mahakama pekee duniani ambayo hutoa haki kwa wakati. Jiandaeni kuhukumiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box