MADAI YA KATIBA MPYA: UNYONGE WA KATIBA AU KATIBA YA WANYONGE?

[Mhadhara huu uliwasilishwa katika Kongamano la Kwanza la Katiba lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA). Kongamano hilo lilifanyika Januari 15, 2011, katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza nia ya serikali yake ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya – moderator]

Tunaposoma magazeti, tunapowasikiliza wanasiasa na hata wanataaluma, tunaambiwa kwamba katiba ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Chimbuko la dhana hii ya katiba kuwa mkataba ni wanafalsafa kama Jean Jacques Rousseau na John Locke katika nadharia yao ya agano la kijamii (social contract). Na akina Locke na Rousseau walikuwa na nadharia hiyo katika kipindi cha mpito kati ya utawala wa kidikteta (absolute states) na kuelekea katika utawala wa kidemokrasia. Wengi wetu tunatumia nadharia hii kama maana ya katiba. Lakini nadharia hii ya agano la kijamii imepitwa na wakati. Maana na dhana ya katiba sasa ni mwafaka wa kitaifa. Kwa hiyo katiba ni kielelezo cha mwafaka wa kitaifa; yaani wananchi wa nchi husika wanakubaliana juu ya misingi mikuu ya jamii yao, utawala wao, mifumo yao ya kiuchumi na kisiasa. Hivyo, mwafaka huo huwekwa katika katiba. Chimbuko la dhana hii ya katiba ni mamlaka ya watu (people’s sovereignty), kwa maana ya kwamba mamlaka yote hutokana na watu wenyewe. Kwa mtazamo wangu, hii ndiyo dhana na maana halisi ya katiba. Kwa hiyo basi, katiba sio mkataba kati ya watawala na watawaliwa bali ni mwafaka wa kijamii – mwafaka wa kitaifa. Ndio maana tunasema kwamba katiba ni mali ya wananchi, kwa sababu ni yao.

Tukikubaliana na dhana hii ya katiba, moja kwa moja inakuja mantiki na sababu ya hoja kwamba utungaji wa katiba hauna budi kujikita katika ushirikishwaji wa wananchi. Kama katiba ni mali na mwafaka wa wananchi, je, wananchi wanawezaje kujenga misingi ya mwafaka huo ikiwa hawakushirikishwa kikamilifu? Suala la ushirikishwaji wa wananchi katika katiba lina umuhimu na mantiki ya kipekee kwani ndilo hasa linadhihirisha mamlaka ya watu. Na kwa hiyo, wananchi ndiyo wanaotunga katiba kutokana na mamlaka yao.

Kwa nini Katiba Mpya
Hivi karibuni, kumekuwa na hoja mbalimbali zinazotolewa na wanasiasa, wasomi, wanahabari, n.k. juu ya kwa nini tuwe na katiba mpya. Hoja hizi zinaweza kugawanywa katika makundi mawili: kundi la kwanza linatoa hoja kwamba Katiba tuliyonayo ina mapungufu. Na kuna watu wanaonukuu ibara mbalimbali za katiba ili kuonyesha kwamba kuna mapungufu katika Katiba. Niliwahi kusoma gazeti moja ambamo mtoa hoja aliorodhesha zaidi ya mapungufu tisini katika katiba. Kwa kweli, mimi kama mtaalamu wa masuala ya katiba ningeweza kuorodhesha hata mapungufu mia mbili! Hakuna katiba, popote pale duniani, ambayo haina mapungufu. Nionanvyo mimi, hiyo sio hoja ya kuwa na katiba mpya, kwa sababu – kama serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) walivyokuwa wamesema hapo awali  kwamba –  iwapo Katiba ya sasa ina mapungufu, jibu ni kuirekebisha ili kuondoa mapungufu hayo. Na hakuna awezaye kupuuza hoja hii, kwa sababu, hoja ya mapungufu jibu lake ni kurekebisha Katiba hiyo. Ibara ya 98 ya Katiba yetu inalipatia Bunge uwezo wa kurekebisha Katiba. Na tumekuwa tukirekebisha Katiba mara kwa mara. Hivyo, katika umri wake wa zaidi ya miaka thelathini, Katiba yetu imerekebishwa mara kumi na nne.

Hoja ya pili inayotolewa ni kwamba Katiba yetu ina ‘viraka’. Na nifikirivyo mimi, hili neno ‘viraka’ limechukuliwa kwa jazba sana. Hoja hii pia haina mashiko. Je, kuna mtu anayeweza kunionesha Katiba isiyokuwa na ‘viraka’? Hii ni kwa sababu Katiba zote hurekebishwa ili ‘ziendane na wakati’. Sasa, kama marekebisho ni ‘viraka’, kuna ubaya gani ikiwa Katiba inakuwa na ‘viraka’?

Hoja nyingine katika kundi hili ni ile inayodai kwamba Katiba tuliyonayo ‘imepitwa na wakati’. Na wenye hoja hii hutoa sababu mbalimbali juu ya kwa nini Katiba ya sasa imepitwa na wakati. Mathalani, wapo wanaosema kuwa Katiba hii ina umri wa zaidi ya miaka thelathini. Kwa kusema ukweli, umri wa katiba siyo hoja. Katiba ya Marekani, kwa mfano, ina umri wa zaidi ya miaka mia mbili (karne mbili) na ile ya India ina zaidi ya miaka sitini! Na zote zimeendelea kudumu.

Katika kundi hili la pili, wapo watoa hoja wengine wanaosema kwamba Katiba imepitwa na wakati – japo hawataji moja kwa moja – kwa sababu katiba yetu bado inataja sera ya Ujamaa na Kujitegemea. Sasa watoa hoja hawapendezwi na hili, ndiyo maana wanasema kuwa Katiba imepitwa na wakati. Ukweli ni kwamba hao wanaozungumzia Ujamaa na Kujitegemea kuwa katika Katiba, hawajaisoma na kuifanyia uchambuzi wa kina Katiba yenyewe. Hii ni kwa sababu tulipoingia katika mfumo wa uliberali mambo-leo (neo-liberalism), Katiba ilirekebishwa na kwa mara ya kwanza, katika Ibara ya 151(1ya Katiba, iliwekwa tasfiri ya ‘Ujamaa na Kujitegemea’. Kwa mujibu wa ibara ya 151(1) ya Katiba ya sasa, “Ujamaa” au “Ujamaa na Kujitegemea” maana yake ni misingi ya maisha ya jamii ya kujenga Taifa linalozingatia demokrasia, kujitegemea, uhuru, haki, usawa, udugu na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano. Na ukisoma tafsiri hiyo ya ‘Ujamaa na Kujitegemea’, hakuna kiongozi yeyote duniani ambaye hawezi kuwa mjamaa. Kwa mujibu wa tafsiri hiyo, hata George Bush na Tony Blair wanaweza kuwa wajamaa! Kwa hiyo hakuna maana yoyote ya kuendelea kutumia maneno haya (Ujamaa na Kujitegemea) wakati dhana yake halisi tayari imeshachakachuliwa. Hivyo basi, mimi sioni kuwa hii inaweza kuwa sababu ya katiba kupitwa na wakati.

Binafsi sisemi kwamba Katiba haina mapungufu, la hasha! Lakini ninachosema mimi tunahitaji katiba mpya kwa sababu – tukirudi nyuma katika historia ya nchi yetu – Katiba hii ya sasa haikuwashirikisha wananchi. Wananchi hawakushiriki kujadili na kujiwekea Katiba, huu ndio upungufu wake. Uhalali wa Katiba hautegemei uzuri au ubaya wa ibara zake, bali hutegemea jinsi Katiba hiyo ilivyotungwa pamoja na ushirikishwaji wa wananchi. Kwa hiyo, jambo la muhimu hapa ni mchakato wa kutunga katiba. Na upungufu huo (wa kutowashirikisha wananchi) haurekebishiki kwa kupitia bunge la kawaida. Hii ndio hoja yetu ya kudai Katiba mpya.

Kwa kweli, hoja ya kudai Katiba mpya haikuanza hivi majuzi au baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, la! Hoja hii ilianza takribani miaka 20 iliyopita. Mwaka 1990, Rais wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alipotangaza kwamba ataunda tume ya kupata maoni ya watu juu ya kuwa na chama kimoja au vyama vingi, baadhi yetu, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tulisema kwamba huo ndio ulikuwa wakati mwafaka wa kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya. Binafsi, niliandika makala katika gazeti la Daily News ambayo ilitoka kwa siku tatu mfululizo, nikipendekeza mchakato wa kupata Katiba mpya ambayo itakuwa na uhalali wa kisiasa pamoja na uhalali wa kisheria. Lakini wakati huo viongozi wakuu wa CCM hawakutaka katiba mpya na walilaani kwa ukali kabisa dhana ya Mkutano Mkuu wa Kitaifa (National Conference). Na hata viongozi watarajiwa wa upinzani hawakupendezwa na mapendekezo yangu.

Nakumbuka nilipopendekeza mchakato huo (ambao ungechukua miaka miwili ama mitatu) pale British Council, kiongozi mmoja wa upinzani akaniambia: ‘We Shivji vipi bwana? Haya yote ya nini? Sisi tunataka kuingia Ikulu’. Kwa hiyo, viongozi wa vyama vya upinzani walikuwa na ‘haraka ya kuingia Ikulu’! Hatimaye, Katiba ikarekebishwa vifungu vichache tu ambapo mfumo hodhi wa madaraka ukafutwa na hivyo, vyama vingi vikaanzishwa. Kwa hiyo ni muhimu sana kuangalia historia. Katika sehemu inayofuata, nitajadili, kwa ufupi, kuthibitisha kuwa Katiba yetu ya mwaka 1977 (na hata zile zilizoitangulia) haikuwashirikisha wananchi.

Historia fupi ya Utungaji wa Katiba Tanzania
Katika miaka hamsini ya uhuru wetu, tumeshakuwa na ‘Katiba mpya’ tano. Katiba ya kwanza ni ile ya mwaka 1961 inayojulikana kama Katiba ya Uhuru (Independence Constitution). Hii ilitungwa na Bunge la Waingereza. Ilikuwa ni nyongeza (schedule) katika Order in Council ya kutoa uhuru kwa Watanganyika.

Katiba ya pili ni ile ya mwaka 1962 ambayo hujulikana kama Katiba ya Jamhuri (Republican Constitution). Kulikuwa na mapendekezo ya serikali (white paper) juu ya Katiba ya mwaka 1962 na watu walitoa maoni. Lakini, waliotoa maoni, kwanza walikuwa wachache; pili, walikuwa wataalamu na hasa wataalamu kutoka nje ya Tanganyika. Katiba ya 1962 ilitungwa baada ya Bunge la wakati huo kupitisha sheria na kujigeuza kuwa Bunge Maalumu (Constituent Assembly). Bunge lile lilikuwa na wabunge 71, wote wakiwa wanachama wa TANU – Wabunge 70 waligombea kupitia tiketi ya TANU, na mmoja (marehemu Mzee Sarwatt), alikuwa mgombea binafsi (independent candidate).  Bunge hili, kwa kupitia sheria iliyoligeuza kuwa Bunge Maalum, ndilo lililopitisha Katiba ya 1962. Kwa hiyo, wananchi hawakushirikishwa.

Katiba ya tatu ni ya mwaka 1964 – Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Chimbuko lake ni Mapatano ya Muungano (Articles of Union). Kutokana na sheria iliyoridhia Mapatano ya Muungano, Rais (wa Jamhuri ya Muungano) alipewa mamlaka ya kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ili kuupatia nafasi (accomodate) Muungano. Na Rais akarekebisha Katiba, akatunga ‘Katiba mpya’ iliyoupatia nafasi Muungano. Na hii ikawa ndiyo Katiba ya tatu, ambayo jina lake rasmi ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Katika kupata Katiba hii pia, wananchi hawakushirikishwa.

Katiba ya nne ni ile ya mwaka 1965 – Katiba ya Muda (Interim Constitution), ambayo tunaiita Katiba ya Chama Kimoja. Katiba hii ilitungwa na Bunge kama sheria ya kawaida kwa mujibu wa ibara ambayo inatoa uwezo kwa Bunge kurekebisha Katiba. Bunge hili halikujigeuza kuwa Bunge Maalum. Badala yake likapitisha Sheria ya Katiba (kama sheria ya kawaida ambayo huwa na namba) na kupitisha Katiba ya mwaka 1965. Wakati ule suala hili halikuhojiwa na wala hakukuwa na mjadala kuhusu hilo kwa sababu falsafa ya sheria za katiba (constitutional jurisprudence) hazikuwa zimeendelea sana. Lakini kwa sasa falsafa ya sheria za katiba (constitutional jurisprudence) imeendelea sana na suala hili halikubaliki. Sababu kuu ya kutokubalika kwa suala hili ni  kwamba Bunge lililo madarakani lipo kwa mujibu wa Katiba iliyopo.

Ni muhimu kuielewa hoja hii vema kwa sababu wananchi wanapowachagua wabunge wao, huwatuma kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba. Wananchi hawawatumi wabunge wao kwenda kuua Katiba iliyopo na kutunga Katiba mpya. Bunge lina mamlaka ya kurekebisha Katiba, lakini hata kurekebisha kuna mipaka yake. Hakuna awezaye kusema kuwa katika kurekebisha Katiba unaua Katiba iliyopo na kutunga Katiba mpya! Kwani hii ni sawa na kiumbe kumuua muumba wake (the created is killing its creator). Katika falsafa ya kisasa ya sheria za katiba (modern constitutional jurisprudence) hili halikubaliki kabisa.

Katiba ya tano, ambayo ni katiba ya mwaka 1977, ni hii tuliyonayo sasa hivi. Historia yake ni ya kustaajabisha. Hata sisi wasomi tunaoizungumzia Katiba hii, sina hakika ni kwa kiasi gani tunajua jinsi ilivyotungwa. Chimbuko la Katiba hii ni Mapatano ya Muungano. Ibara ya saba ya Mapatano ya Muungano ilisema kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano na Makamu wa Rais (ambaye alikuwa Rais wa Zanzibar), ataunda Tume ya Katiba (Constitutional Commission) ikifuatiwa na kuitisha Bunge Maalum (Constituent Assembly) ili kutunga Katiba ya Muungano katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja. Kwa sababu mbalimbali, ambazo sitazijadili hapa, katika muda huo Katiba ya kudumu haikutungwa na badala yake walijiongezea muda usio na kikomo. Kwa hiyo, tukatawaliwa na Katiba ya muda ya 1965 kwa miaka ipatayo kumi na miwili.

Mnamo mwaka 1977, mchakato wa kuunganisha ASP na TANU ukaanza na hatimaye Halmashauri Kuu za vyama hivyo viwili zikakaa pamoja na kuunda Chama cha Mapinduzi, CCM. Mara baada ya kuwa na chama kimoja, mchakato wa kutunga katiba ya nchi ukaanza. Rais, Mwalimu Nyerere, akatoa matangazo mawili katika gazeti la serikali. Tangazo la kwanza Na. 38 la tarehe 25 Machi 1977 lililowekwa sahihi tarehe 16 Machi 1977, lilikuwa na majina ya watu 20 ambao Rais aliwateua kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba. Kuna mambo makuu mawili muhimu sana katika tangazo hili. Kwanza, wale wajumbe 20 walioteuliwa ni walewale ambao walikuwa katika kamati ya kutengeneza Katiba ya CCM, mwenyekiti akiwa marehemu Thabit Kombo na katibu akiwa ni Mheshimiwa Pius Msekwa. Tangazo Na. 39 la tarehe hiyo hiyo lilikuwa na majina ya watu ambao Rais aliwateua kuwa wajumbe wa Bunge Maalum. Majina yale yote yalikuwa ni yaleyale ya waliokuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Safari hii Bunge halikujigeuza kuwa Bunge Maalum. Bunge Maalum liliteuliwa lakini wajumbe wa Bunge Maalum walikuwa walewale ambao walikuwa wabunge wa wakati huo.

Jambo la pili, tangazo hili ni la siku ileile. Sasa swali linakuja: Saa ngapi Tume ya Katiba ilitoa mapendekezo (proposals) na lini Bunge Maalum lilikaa na kuyapitia mapendekezo hayo na kutunga Katiba? Kuna jambo jingine  muhimu ambalo mara nyingi sisi wa -Tanzania Bara huwa tunalisahau: Mapatano ya Muungano yalisema kwamba Rais wa Muungano akikubaliana na Rais wa Zanzibar ataunda Tume ya Katiba na Bunge Maalum. Katika matangazo yote hayo mawili haikutajwa kwamba Rais wa Zanzibar alikubali. Hivyo, Bunge Maalum lilikaa Dar es Salaam tarehe 25 Aprili 1977, likajadili Katiba kwa takribani saa tatu, wachangiaji wakiwa wajumbe wanane na likapitisha Katiba ya 1977. Ukweli ni kwamba mapendekezo ya Tume ya Katiba yalitolewa hata kabla ya Tume yenyewe kuundwa na Kamati ileile ya watu 20. Na misingi na miongozo ya Katiba mpya ilitolewa na Halmashauri Kuu ya CCM, ikapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu kuandikwa kama rasimu ya Katiba mpya. Kisha ikatangazwa katika gazeti la serikali tarehe 4 Aprili 1977 na Bunge Maalum likakaa siku 21 baadaye, yaani tarehe 25 Aprili 1977. Wananchi hawakushirikishwa, wananchi hawakutoa maoni yao. Hata wana-CCM hawakushiriki katika katiba hii kwa sababu chombo kikuu cha chama hicho, yaani Mkutano Mkuu, hakikuhusika. Iliyohusika ni Halmashauri Kuu. Na kama tunavyofahamu, mijadala ya Halmashauri Kuu haiwekwi hadharani, hubaki kuwa siri (confidential).

Katika kutunga Katiba ya 1977, wananchi hawakushirikishwa ili kutoa maoni yao. Kwa mantiki hiyo, Katiba ya 1977 haina uhalali wa kisiasa (political legitimacy). Pili, uhalali wake wa kisheria (legal legitimacy) pia una walakini, kwa sababu taratibu zilifuatwa lakini sheria zilipindwapindwa kidogo. Kwa hiyo, kwa kujumuisha tu, katika katiba zote tano wananchi hawakushirikishwa. Swali linakuja, na hapa ningependa kutoa angalizo: je, hii ina maana kwamba utawala chini ya Mwalimu Nyerere haukuwa na uhalali? Hapana, utawala chini ya Mwalimu Nyerere ulikuwa na uhalali. Lakini uhalali wake haukutokana na katiba; uhalali wake ulitokana na itikadi ya Chama pamoja na umahiri na umaarufu wa Mwalimu mwenyewe. Na tusije tukajidanganya, hasa vijana; Mwalimu alikuwa anapendwa sana na watu wake (He was very popular). Kwa hiyo, utawala wake ulikuwa na uhalali lakini uhalali wake haukutokana na Katiba. Medani ya kujenga mwafaka haikuwa Katiba. Chama ndicho kilikuwa medani ya kujenga mwafaka. Na hata wananchi hawakujali Katiba. Kwa mfano, ungewauliza kuhusu Azimio la Arusha, walilifahamu vema na walisherehekea haswa lilipotangazwa. Lakini ungewauliza kuhusu Katiba, walikuwa hawaijui!

Kwa kutoijua Katiba na namna Walivyompenda na kumwamini Mwalimu wananchi hawakustuka hata pale Mwalimu aliponukuliwa akisema kwamba Katiba ilimpatia uwezo mkubwa sana hata wa kuwa dikteta. Lakini mimi huwa najiuliza: endapo wananchi wangeulizwa kuhusu uwezo mkubwa aliokuwa nao Rais wangesemaje? Binafsi nahisi wananchi wasingesema: ‘Duh! Tuna Katiba mbaya kiasi hicho?’ La hasha! Wananchi wangesema: ‘Alhamdu Li lah! Tuna kiongozi mzuri mno’. Hii ni kwa sababu wananchi hawakujali kuhusu Katiba. Lakini hii ilikuwa ni enzi za chama kimoja. Unapokuwa na vyama vingi, medani ya kujenga mwafaka haina budi iwe Katiba na si sera za Chama.

Pendekezo la Mchakato wa Kutunga Katiba Mpya
Kwa hiyo, tunapozungumzia Katiba mpya hatuna budi tusisitize kwamba Katiba hiyo lazima iwe na uhalali wa kisiasa na uhalali wa kisheria, kwa maana ya kwamba wananchi wanashiriki na kushirikishwa kikamilifu katika upatikanaji wa Katiba hiyo. Njia mbalimbali za kutunga Katiba lazima ziweke mbele suala la ushirikishwaji wa wananchi ili wananchi hatimaye wapate Katiba yao, ambayo wanaielewa na hivyo watailinda kwa sababu wameshiriki katika upatikanaji wake. Hivyo, mchakato sharti uhakikishe kwamba wananchi wanapewa nafasi za kutosha na muda wa kutosha wa kujadili masuala muhimu ya taifa lao – dira yake, mwelekeo wake, mustakabali wake, mifumo yake ya kiuchumi na ile ya kisiasa, matakwa na maslahi ya walio wengi (wanyonge), n.k. Wananchi wanapaswa kujadili mambo haya yote kwa uhuru bila kutishwa ama kuzuiliwa.

Naamini zipo njia na michakato mbalimbali ya kufikia malengo haya. Mchakato ninaoupendekeza una hatua mbili: hatua ya kisiasa ya kujenga mwafaka wa kitaifa na hatua ya kisheria ya kuipitisha Katiba yenyewe ili iwe na nguvu za kisheria.

Hatua ya kwanza inaanzia kwenye mijadala midogo midogo kote nchini. Hii ni mijadala inayoandaliwa na wananchi wenyewe, taasisi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, vyama vya ushirika, vyama vya siasa n.k., vijijini na mijini. Mijadala yote midogo midogo hatimaye itafikia kikomo chake katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa (National Convention). Hii ni mithili ya mito na vijito vimiminikavyo katika bahari, ambayo ndiyo kikomo chake.

Hatua ya pili inaanzia kwenye Bunge na itaishia kwenye kura ya maoni. Vyombo vikuu vitakavyohusika ni pamoja na chombo cha kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na kuwawezesha wananchi kushiriki katika mijadala. Chombo hiki, tukipenda, tunaweza kukiita Tume. Na mheshimiwa Rais tayari amekwishatangaza kwamba ataunda Tume. Mimi sina tatizo na hili, lakini nina maswali matatu: Kwanza, Hadidu za rejea, yaani Tume hii itakuwa na majukumu gani? Pili, muundo wake utakuwaje? Tatu, taarifa au mapendekezo yake yatapelekwa wapi? Sasa, mheshimiwa Rais, ingawa hakufafanua, alisema kwamba jukumu la Tume litakuwa ni kukusanya maoni na wajumbe wake watakuwa wawakilishi wa makundi mbaalimbali katika jamii, na mapendekezo yake yatapelekwa kwa vyombo husika. Hii inanipa shida kidogo: kama jukumu la Tume ni kukusanya maoni na kuwezesha mijadala; basi hii ni tume ambayo haina uwezo wa kufanya maamuzi. Kwa maana hiyo, hakuna haja ya wajumbe wake kuwa wawakilishi wa makundi mbalimbali. Kwa sababu, ukiunda tume ambayo ni shirikishi, unakuwa umeiua tume hiyo tangu mwanzo – hawataweza kukubaliana chochote. Kama kazi ya Tume ni kukusanya maoni, kuwezesha mijadala, kuchambua mijadala na kuainisha maeneo makuu ya msingi, na kutoa mapendekezo yake; basi tume hii haina haja ya kuwakilisha makundi mbalimbali. Tume hii inapaswa kuwa Tume ya wataalamu, ambao siyo wakereketwa wa vyama vya siasa. Tume hiyo ipewe hadidu za rejea na iwe huru, isiingiliwe katika utendaji wake. Kazi ya Tume hiyo ni kuwezesha mijadala na hatimaye taarifa yake na mapendekezo yake yanapelekwa katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa. Tume hiyo ipewe jukumu na uwezo wa kuandaa huo Mkutano Mkuu wa Kitaifa. Mheshimiwa Rais, kwa heshima na taadhima, amesema kwamba Tume itapeleka mapendekezo yake kwa vyombo vinavyohusika. Sasa, ni vyombo gani hivyo? Hatuna vyombo vinavyohusika! Chombo kinachohusika ni wananchi wenyewe. Hapa tunazungumzia Katiba mpya, na sio marekebisho ya katiba. Katiba mpya hiyo ni lazima idhihirishe mwafaka wa kitaifa; ndiyo maana taarifa ya Tume inapaswa kupelekwa katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa.

Mkutano huo utakuwa na wajumbe ambao watawakilisha maslahi (interests) mbalimbali katika jamii – asasi za kiraia, taasisi za kidini, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafanyabiashara, vyama vya siasa, n.k. Makundi yote katika jamii yanapaswa kuwakilishwa katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa, na Mkutano huo ndiyo utakaojadili taarifa ya Tume. Baada ya kukubaliana, Mkutano Mkuu wa Kitaifa utatoka na misingi mikuu ya Katiba. Misingi hiyo ndiyo itakuwa ni mwongozo kwa wataalamu kuandaa rasimu ya Katiba mpya. Na rasimu hiyo itaandikwa na jopo la wataalamu lililokubaliwa na Mkutano Mkuu wa Kitaifa, sio mwanasheria mkuu! Kwa upande mmoja Tume hiyo ya wataalamu itaandika rasimu ya Katiba kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa na Mkutano Mkuu wa Kitaifa, na kwa upande mwingine Bunge lililopo, kwa mujibu wa ibara ya 98, litapitisha sheria ya kuunda Bunge Maalumu (Constituent Assembly). Wajumbe wa Bunge Maalumu watachaguliwa na wananchi. Mtu yeyote, bila kujali chama chake, alimradi awe na sifa za kupiga kura (awe na umri usiopungua miaka 18, awe Mtanzania, awe na akili timamu, n.k.) anaweza kugombea kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu. Bunge hilo litakaa na kujadili kwa kina ibara zote za rasimu ya katiba iliyoandaliwa na jopo la wataalamu. Na baada ya kukubaliana, Bunge Maalumu litaikubali (adopt) rasimu ya Katiba. Hii haitaipa rasimu hiyo nguvu za kisheria, la hasha! Baada ya hapo rasimu hiyo itawekwa hadharani na wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano watapiga kura ya maoni. Rasimu hiyo ikipitishwa kwa kura ya maoni, ndipo itakuwa Katiba mpya ya nchi. Tendo la wananchi kupiga kura ya maoni na kusema ‘ndiyo’ ndilo litakaloipatia Katiba nguvu za kisheria.

Kwa hiyo, wananchi wenyewe ndio watakaoipitisha Katiba yao, na hivyo kuipa uhalali wa kisheria Katiba yenyewe. Hivyo ndivyo walivyofanya Ireland mwaka 1937 pale wananchi walipopitisha katiba kwa kura ya maoni. Hivyo basi, Katiba yetu mpya haitasema ‘Sisi Bunge Maalum tumetunga Katiba hii kwa niaba ya wananchi…’; hapana! Itasema ‘Sisi wananchi wa Tanzania tumejitungia Katiba yetu wenyewe…’ yawezekana zipo hofu na hoja kuwa mchakato huo hauwezekani. Mimi naamini mchakato wa aina hii unawezekana kabisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box