MTANZIKO WA KUTUNGA KATIBA: Nini Chanzo Chake, Zipi Athari Zake Kisiasa, Na Nini Kifanyike?

1.      Utangulizi
Hivi sasa Bunge Maalum la Katiba (BMK) linaendelea kuijadili Rasimu ya Katiba, sura ya kwanza na sura ya sita. Hata hivyo, Mjadala unaoendelea umegubikwa na hisia na misimamo mikali kuhusu muundo wa serikali ya Muungano wa Tanzania. Wajumbe wengi, wengi wao wakiwa wanachama wa CCM, wanapendekeza muundo wa Muungano wa serikali mbili uliopo sasa uendelee ingawa baada ya kufanyiwa mabadiliko kadhaa.  Wajumbe wachache, wengi wao wakiwa wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani vyenye uwakilishi katika Bunge la Tanzania na Baraza la Wawakilishi, hawakubaliani na mapendekezo ya waliowengi kwa madai kwamba hayo siyo matakwa ya wananchi waliotoa maoni kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK). Hawa wanadai kwamba muundo wa Muungano wa serikali tatu uliopendekezwa na TMK ndiyo ujadiliwe na kupigiwa kura na BMK.

Hata kabla ya kukamilishwa kwa mijadala kuhusu sura ya kwanza na ya sita, baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka muundo wa Muungano wa serikali tatu, wameamua kususia vikao kwa madai mbalimbali.

Uchambuzi wangu katika makala haya unakusudia kufanya mambo matatu. Mosi, ni kudadisi kiini cha mtanziko uliopo ndani na nje ya BMK. Pili, ni kubainisha athari za mtanziko huo kisiasa. Tatu, ni kupendekeza baadhi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ili mtanziko uliopo usiwe chanzo cha migogoro hatarishi nchini.

2.      Nini Kiini cha Mtanziko wa kutunga Katiba?
Kiini cha mtanziko wa kutunga Katiba ni usanifu mbovu wa mchakato wa kutunga Katiba. Kwa ujumla mchakato wa kutunga Katiba ulisanifiwa na wanasiasa bila kuzingatia haja na umuhimu wa ushiriki bora wa wananchi katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya Katiba na katika kuunda BMK. Sote tunatambua kwamba wananchi hawakutoa maoni yao juu ya misingi mikuu ya Katiba ambayo ndiyo ingekuwa mwongozo wa kisiasa wa mchakato mzima wa kutunga Katiba.

Mwafaka wa kitaifa ni mapatano kuhusu misingi mikuu ya kikatiba yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu na shirikishi ulioratibiwa na kusimamiwa na chombo cha kitaifa chenye uwakilishi wa makundi yote ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Ujenzi wa mwafaka wa kitaifa ni zoezi la kisiasa linalofanyika wakati wa kuasisi mchakato wa kutunga Katiba. Zoezi la ujenzi wa mwafaka wa kitaifa huwa halihusishi Bunge la kawaida bali chombo mahsusi cha uwakilishi kilichoundwa na wananchi kwa utaratibu mahsusi. Kwa kawaida, mwafaka wa kitaifa hujengwa kwa njia ya mijadala ya kina na siyo kwa njia ya kupiga kura.

Dhana ya mwafaka wa kitaifa imejengwa ndani ya dhana ya Katiba. Dhana ya Katiba imefafanuliwa kwa ufasaha na Jaji Warioba, Mwenyekiti wa TMK katika hotuba yake wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum kama ifuatavyo:

Katiba ni sheria kuu au sheria mama katika nchi yeyote. Sheria nyingine zote zinatungwa kwa mujibu wa Katiba. Wakati mwingine Katiba hutafsiriwa kuwa ni mkataba wa kijamii kati ya viongozi na wananchi. Ni makubaliano ya wananchi kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao. Katiba ni mwafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya kuendesha nchi.

Kwa mujibu wa Profesa Shivji[2] (2006: uk 27-43) hatua ya mwanzo kabisa ya safari ndefu ya kutunga Katiba ni ujenzi wa mwafaka wa kitaifa. Kwa maoni yangu, hatua hii muhimu kisiasa ilivukwa kwa sababu ya shikinikizo za wanasiasa waliotaka kazi ya kutunga Katiba ifanyike chapuchapu na ikamilike kabla ya uchaguzi wa 2015. Ninabainisha aina tatu za udhaifu katika muundo wa usanifu wa mchakato wa kutunga Katiba.

Kwanza, mchakato wa kutunga sheria ya mabadiliko ya Katiba uliohusisha wabunge wote wa vyama vyenye uwakilishi Bungeni (CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-MAGEUZI, UDP na TLP) uligeuzwa kuwa uwanja wa mapambano ya kimaslahi baina ya vyama vya siasa huku kila chama kikitaka maslahi yake yazingatiwe. Ilibidi sheria hii kufanyiwa marekebisho mara kadhaa tena kwa mivutano mikali. Sheria hii ndiyo iliyowapa mamlaka Marais wa Tanzania na Zanzibar kuteua wajumbe 32 wa TMK. Wapo wajumbe wa TMK, akiwemo Profesa Baregu, ambao wamekuwa wakikosoa misingi iliyofuatwa wakati wa kufanya mabadiliko katika sheria ya mabadiliko ya Katiba.

Aidha, TMK ilijumuisha makada wengi wa vyama vya siasa. Hivi sasa, kwa mfano, aliyekuwa mjumbe wa TMK (ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais kutoka CCM) Mheshimiwa Al-Shaymaa, ameungana na wajumbe wenzake wa BMK kutunga Katiba. Kama mchakato utakamilika na kila kitu kubaki kama kilivyo, basi Mbunge huyu (ambaye pia alikuwa Mjumbe wa TMK) atakuwa mtanzania aliyepata fursa ya kuandaa Rasimu ya Katiba, kutunga Katiba na kuiidhinisha au kuikataa kwa njia ya kura. Mchakato uliosanifiwa vizuri na kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia hauwezi kuwa na kikiri za aina hii.

Kadhalika, TMK iliwajibika kwa mamlaka za uteuzi na ilikuwa tegemezi kwa mamlaka hizo kwa hali na mali. Tunafahamu pia kwamba TMK iliongozwa na sheria peke yake badala ya mwongozo wa kisiasa uliotokana na mijadala shirikishi ya wananchi. Vile vile, wanachi hawakushiriki katika kuunda Bunge Maalum la Katiba kwa njia ya kura.

Pili, sheria iliyoasisi mchakato wa kutunga Katiba haikutoa mwanya wa ushiriki wa wananchi katika hatua ya kuunda BMK kwa njia ya kura. Tangu mwanzo, mchakato wa kutunga Katiba umewaweka wananchi pembezoni. Hadi sasa ushiriki wa wananchi umezingatiwa tu katika hatua ya kutoa maoni. Pengine baadaye wanachi watashiriki kwenye kura ya maoni.

Vile vile, sheria ya mabadiliko ya Katiba iliwapa mamlaka Marais wa Tanzania na Zanzibar kuteua Wajumbe 201 wanaowakilisha makundi mbalimbali hapa nchini. Yapo pia manung’uniko mengi kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu kutokuwepo kwa uwakilishi halisi wa wavujajasho ndani ya BMK. Kuna madai kwamba uteuzi wa wajumbe 201 haujaakisi barabara uwakilishi halisi wa vikundi vya wavujajasho (yaani wakulima, mamanitilie, madereva, mafundi mchundo, wafugaji, wavuvi, wasusi, warina asali nk). Kwa nia ya kulinda maslahi yao ndani ya BMK, watunga sheria waliweka vifungu vilivyowaruhusu, wao na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kuwa Wajumbe wa chombo hicho muhimu cha kutunga sheria. Tunaweza kusema kwa usahihi kwamba, kwa kiwango kikubwa, Bunge Maalumu la Katiba siyo chombo kilichoundwa na wanachi kwa ajili ya kufanya kazi mahsusi ya kutunga katiba. Ni chombo halali kisheria lakini uhalali wake wa kisiasa una mushkeli.

Tatu, uamuzi wa kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba haukuzingatia historia ya nchi na hali halisi iliyopo hivi sasa kitaifa na kimataifa. Kutokana na ukweli kwamba Tanzania ina historia ya Muungano wa nchi mbili huru zilizozaliwa kutoka kwenye tumbo la mapambano ya ukombozi (yakiwemo mapinduzi ya Zanzibar), watanzania walipaswa kutumia fursa ya kuandika Katiba kutenga muda wa kutosha wa kuendesha mijadala shirikishi, huru na wazi ili kuweza kujenga mwafaka juu ya kuiimarisha misingi mikuu ya Muungano ambao umedumu kwa nusu karne (1964-2014).

Bila shaka kazi ya kujenga mwafaka wa kitaifa kuhusu Muungano ungezingatia historia ya mapambano ya ukombozi barani Afrika na hali halisi ya kisiasa nchini na duniani kwa ujumla. Kihistoria, ubeberu bado ndicho kikwazo kikuu cha mapambano ya ukombozi barani Afrika na uwanja wa mapambano hivi sasa umebadilika kitaifa na kimataifa. Kitaifa, yapo madai ya wavujajasho ya haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe kupitia vyombo vyao vya kikatiba; yapo pia madai ya wavujajasho ya haki yao ya kudhibiti na kusimamia raslimali za ardhi na maliasili za Taifa kupitia kwenye vyombo vyao vya kikatiba. Kimataifa, lipo wimbi kubwa la migogoro ya kidini na kisiasa inayochochewa na ubeberu na ambayo inaendelea kuzisambaratisha nchi nyingi zinazoendelea. Yanayoendelea katika nchi za Venezuela, Syria, Afghanistan, Pakistan, Iraq, Ukrain, Sudani Kusini, Libya, Afrika ya Kati, Mali, Nigeria na Somalia yangechambuliwa kwa kina ili kubaini kama kuna mafunzo na uzoefu unaofaa kuzingatiwa wakati wa mchakato wa kutunga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

3.      Zipi Athari Za Mtanziko Huu Kisiasa?

Nitabainisha baadhi ya athari chache za kisiasa. Kwa ujumla, ombwe la mwafaka wa kitaifa liliathiri vibaya utendaji wa TMK na hasa namna ilivyofikia uamuzi wa kupendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu. Kama nilivyosema awali, TMK ilifanya uamuzi huo bila kuwa na mwongozo wa kisiasa unaobainisha misingi mikuu ya kuimarisha na kudumisha Muungano ambayo ingezingatiwa na wajumbe wake wakati wa kukusanya maoni na kuandaa Rasimu ya Katiba. Katika hali hii malumbano ndani ya TMK kuhusu muundo mwafaka wa Muungano yasingeepukika. Kama alivyobainisha Jaji Warioba, TMK ililazimika kujenga misingi ya maelewano ili iweze kukabilina na misimamo mikali miongoni mwa wajumbe wake. Katika hotuba yake katika BMK Jaji Warioba alibainisha tatizo hilo na njia zilizotumika kulikabili:

Hata tulipopata matatizo ya kufikia uamuzi kwa suala lolote hatukukimbilia kupiga kura. Tulijifungia kwenye vikundi vya watu wenye mawazo kinzani na mwisho tukafikia maridhiano na muafaka. Dira yetu ilikuwa Maslahi ya Taifa. Hatukupiga kura hata mara moja kwa jambo lolote wala kuwa na mawazo mbadala. Kila Ibara iliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ninaiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba, inaungwa mkono na kila mmoja wetu.

Bila shaka, suala la Muundo wa Muungano ni miongoni mwa masuala magumu yaliyowasumbua sana wajumbe wa TMK. Hata kabla ya kusoma taarifa yake, Profesa Shivji alikuwa ameshabainisha uwezekano wa kuwepo kwa misuguano ndani ya TMK. Katika mhadhara wake wa mwezi Agosti 2013 uliochambua Rasimu ya kwanza ya Katiba[3] Profesa Shivji alidokeza:

Baada ya kuisoma Rasimu kwa kina, mimi nadhani kwamba masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume…[U]somaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii ni maelewano kwa maana ya compromise,  na siyo mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus… Katika maelewano au compromise, pande zinazokinzana hatimaye zinakubali kwa shingo upande ili kutokwamisha maamuzi. Pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili. Kwa hivyo, maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi. Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege. Mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika compromise, kila mmoja anatoka amenuna. Ni wazi kwamba huwezi ukapata mwafaka fastafasta. Lazima utachukua muda.

Misuguano iliyokabiliwa na wajumbe wa TMK sasa inawaandama wajumbe wa BMK. Kwa kiwango kikubwa, mapendekezo ya TMK kuhusu muundo wa serikali tatu ndiyo kiini cha jazba na malumbano ya kisiasa vinavyoshuhudiwa hivi sasa ndani na nje ya BMK. Jaji Warioba mwenyewe amekiri kuwa suala la muundo wa Muungano limekuwa gumu sana kiasi cha kuzua mjadala mkali:

Suala la Muundo wa Serikali Tatu limechukua nafasi kubwa sana katika mjadala tangu Tume ilipozindua Rasimu ya kwanza ya Katiba. Mjadala wa Muundo wa Muungano umekuwa mkubwa kwa kiasi cha kufunika mapendekezo mengine yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano[4].

Anachosema Jaji Warioba ni sahihi kabisa. Ni kweli kwamba mambo ya msingi ya kikatiba hayajadiliwi kwa uzito unaostahili. Na masuala mengine muhimu ya kikatiba, kama serikali za mitaa na ardhi, hayamo kabisa katika Rasimu ya Katiba inayojadiliwa sasa kutokana na pendekezo la muundo wa Muungano wa serikali tatu. Mimi naamini kwamba, kama mjadala wa kitaifa juu ya misingi ya kikatiba ungefanyika kwanza na mwafaka wa kitaifa kupatikana, mjadala kuhusu mapendekezo nyeti na magumu yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba usingegubikwa na malumbano ya kisaisa kwa kiwango kinachoshuhudiwa sasa. Hata pendekezo la muundo wa Muungano nalo lisingebishaniwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa.

Pamoja na ufafanuzi wa mara kwa mara wa TMK, mjadala mkali wenye hoja nzito dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Muungano wa serikali tatu unaendelea ndani na nje ya BMK umepamba moto na hakuna anayeweza kutabiri kitakachotokea baadaye. Hata ufafanuzi wa mwisho wa TMK uliochapishwa katika magazeti nao umepingwa vikali tena kwa hoja nzito[5].

Hotuba ya Rais Kikwete[6], aliyoitoa tarehe 21 Machi, 2014 wakati akilizindua rasmi BMK ilifafanua kwa undani zaidi changamoto na kasoro kubwa za muundo wa Muungano wa serikali tatu uliopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba. Wajumbe wa BMK wanaounga mkono mapendekezo ya TMK ya muundo wa Muungano wa serikali tatu wanaendelea kumlaumu sana Rais Kikwete kwa ‘kuchafua’ hali ya kisiasa ndani ya BMK

Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alibainisha kasoro kubwa mbili za muundo wa Muungano wa serilaki tatu. Kasoro ya kwanza, ni udhaifu wa mfumo wa kugharamia shughuli za Serikali ya Muungano. Kasoro ya pili ni kupandwa kwa mbegu zenye sumu ya utaifa finyu (parochial nationalism) wa kitanganyika na kizanzibari ambao, kwa mtazamo wake, utadhoofisha misingi ya utaifa wa kiafrika iliyodumu kwa nusu karne.

Katika kufafanua zaidi kuhusu changamoto za kugharamia serikali ya Muungano Rais Kikwete alisema:

 …haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji…  Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama wakati wowote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo…

Rais Kikwete aliendelea kufafanua zaidi kuhusu changamoto ya gharama:

Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.

Kuhusu kupandwa kwa mbegu zenye sumu ya utaifa wa kitanganyika na kizanzibari Rais Kikwete alisema:

Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa.  Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri.  Umoja wetu utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika.

Ingawa kasoro hizo mbili zilizobainishwa katika hotuba ya Rais Kikwete ni kubwa mno, baadhi ya wajumbe wa BMK kutoka kwenye vyama vya upinzani wameendelea kumlaumu na kumtuhumu kwamba alifanya hivyo kwa maslahi ya chama chake. Kwa hakika, hotuba hiyo ya Rais Kikwete inaendelea kupanua mpasuko wa kimsimamo ndani na nje ya BMK.

Hata hivyo, Rais Kikwete hakulitolea ufafanuzi suala tata kuhusu mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Profesa Issa Shivji ndiye aliyefanya uchambuzi kuhusu suala hili mara baada ya TMK kutoa taarifa yake fupi ya mwisho kwenye vyombo vya habari ikidai kwamba mabadiliko hayo yalivunja Katiba ya Muungano kwa kuanzisha nchi mbili. Kwa mujibu wa TMK, mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ni miongoni mwa sababu kuu za kupendekezwa kwa muundo wa Muungano wa serikali tatu[7]. Baada ya kuzichambua hoja za TMK kuhusu mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, Profesa Shivji amehitimisha kwa kusema kwamba mabadiliko hayo hayajaanzisha nchi mbili.

Baadhi ya wanasiasa waandamizi wa vyama vikuu vya upinzani wamekaririwa na vyombo vya habari wakiubeza uchambuzi wa Profesa Shivji. Malumbano ya kisiasa kuhusu suala hili yanaendelea ndani na nje ya BMK. Hali hii ya malumbano na jazba za kisiasa ni ya kawaida hasa katika mazingira ambayo mijadala juu ya masuala mazito kuhusu nchi haiongozwi na mwafaka wa kitaifa. Kwenye ombwe la mwafaka wa kitaifa, hoja nzito ni rahisi kupuuzwa au kubezwa na jazba za kisiasa ni rahisi sana kutamalaki. Mchakato wa kutunga Katiba umetufikisha hapa ingawa, kihistoria, nchi yetu haijawahi kukumbwa na kikiri za kisiasa za aina hii.

Kwa kuwa kazi ya kujenga mwafaka wa kitaifa haijafanyika, misuguano mikali ya kimsimamo na kimtazamo inayoshuhudiwa sasa ni hali iliyotarajiwa. Na kwa kuwa mwafaka wa kitaifa haukujengwa mapema, mchakato wa kutunga Katiba umeendeshwa bila mwongozo wa kisiasa. Ni vema kutambua kwamba mchakato wa kutunga Katiba unaoendeshwa bila mwongozo wa kisiasa huzaa matatizo ya aina mbili: matumizi mabaya ya raslimali (misuse of resources) na kikiri za kisiasa katika mchakato wa kufanya maamuzi (confusion). Hivi sasa mchakato wa kutunga Katiba unakabiliwa na matatizo haya mawili. Ni dhahiri kwamba shabaha ya awali ya kuwa na Katiba Mpya ifikapo tarehe 26 Aprili 2014 haitafikiwa ingawa raslimali nyingi za taifa zilimetumika kwa ajili hii.

Vile vile, kikiri za kisiasa zimevuruga mwenendo wa mijadala ndani na nje ya BMK na hata kufikia kiwango cha kuwagawa baadhi ya wananchi katika makundi mawili kinzani: ‘waumini’ wa muundo wa Muungano wa serikali tatu na ‘waumini’ wa muundo wa Muungano wa serikali mbili. Kila kundi limetekwa na jazba na misimamo mikali.

Kwa ufupi, malumbano ya kisiasa yanayoendelea sasa ndani na nje ya BMK yameanza kutikisa misingi ya umoja wa kitaifa. Kwa hiyo, wajumbe wote wa BMK, wanasiasa, wasomi wa fani mbalimbali wakiwemo wanahabari na wanaharakati wanapaswa kuwa makini sana wakati huu.

4.      Nini Kifanyike Sasa?

Kwa kuwa kazi ya kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya Katiba haikufanyika mapema, kazi hiyo haiwezi kufanyika sasa. Ieleweke kwamba TMK haingeweza kufanya kazi hiyo kwa sababu halikuwa jukumu lake. Hata BMK na Kura ya Maoni siyo vyombo mahsusi vya kujenga mwafaka wa kitaifa kwa sababu maamuzi yake yanafanywa kwa njia ya kura. Kama nilivyosema awali, mwafaka wa kitaifa hujengwa kwa njia ya mijadala shirikishi, huru na wazi na siyo kwa njia ya kura. Hata wale wanaopendekeza kwamba suala la muundo wa Muungano liamuliwe kwa kuitishwa kwa kura ya maoni inabidi watambue kwamba pendekezo hilo siyo mbadala wa mijadala ya kujenga mwafaka wa kitaifa. Mijadala shirikishi ndiyo itakayowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa kura ya maoni na siyo vinginevyo.

Pamoja na kuwepo kwa ombwe la mwafaka wa kitaifa kuhusu misingi mikuu ya Katiba, wajumbe wa Bunge Maalum na viongozi wote wa kisiasa nchini wanapaswa kufahamu kwamba yapo masuala ya msingi yanayopaswa kuyazingatia wakati huu wa mtanziko wa kutunga Katiba nchini. Masuala hayo ni haya yafuatayo:

a)      Dira ya Ukombozi

Wajumbe wa BMK wanapaswa kutambua kuwa mchakato wa kutunga Katiba hauliumbi upya Taifa la Tanzania bali unaihuisha misingi yake ya kujitawala na kujitegemea. Watambue kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilizaliwa kutoka kwenye tumbo la mapambano ya ukombozi. Uhuru wa Tanganyika wa mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ndivyo vilivyozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964. Umoja wetu na uraia wetu mpya ni matunda ya Muungano wetu. Hizi ndizo hati zenyewe za Muungano.

Wajumbe wa BMK wanapaswa kutambua pia kwamba dira ya ukombozi ndiyo iliyowaongoza wapigania uhuru wote barani Afrika kudai haki ya kujitwala. ‘Binadamu wote ni sawa na Afrika ni Moja’ ni kauli mbiu iliyobuniwa na wapigania uhuru wa kiafrika ili kuhamasisha harakati za kujenga Umoja wa Afrika. Kwa hiyo, dira ya ukombozi ndiyo inayopaswa kuwaongoza wajumbe wa Bunge maalum na viongozi wetu wote wa kisiasa na kijamii wakati huu ambapo wanajaribu kukabiliana na mtanziko wa kutunga Katiba. Uamuzi utakaozaa mifarakano na migogoro hatarishi usifanywe na mjumbe yeyote wa BMK au kiongozi yeyote yule wa kisiasa ili kuiepusha nchi yetu isitumbukie katika mifarakano ya kisiasa iliyokuwepo kabla ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

b)     Matumizi ya Nyenzo Zote za Kazi
Tayari wajumbe wa Bunge Maalum wameanza kazi ya kujadili Rasimu ya Katiba na vitendea kazi muhimu wameshakabidhiwa. Zana muhimu amabazo Wajumbe wa Bunge Maalum wanapaswa kuendelea kuzitumia kwa makini ni: sheria ya Mabadiliko ya Katiba; Kanuni za Bunge Maalum; Rasimu ya Katiba; ripoti zote za TMK; na ripoti za kamati kumi na mbili za BMK. Nyenzo hizi zitumiwe kwa pamoja na hotuba za Jaji Warioba na Rais Kikwete zilizotolewa kwenye BMK. Hotuba hizo pia ni miongoni mwa vitendea kazi muhimu vya wajumbe wa BMK. Hata ushauri wa wataalamu na matokeo ya tafiti juu ya masuala mbalimbali ya kikatiba vitumike kama nyenzo muhimu.

c)      Historia na Uzoefu wa Maridhiano ya Zanzibar ya Mwaka 2010
Tanzania ina historia maridhawa na uzoefu mkubwa wa kutatua migogoro ya kisiasa ndani ya nchi yetu. Maridhiano ya Zanzibar ya 2010 ni kielelezo cha historia na uzoefu huo.  Hakuna mdau yeyote wa siasa za Tanzania asiyetambua kuwa maridhiano hayo yameshajenga msingi (ingawa bado haujaimarika sana) wa kukuza demokrasia ya vyama vingi na kudumisha utengamano wa kisiasa nchini. Msingi huu usidhoofishwe kwa namna yeyote ile au kwa sababu yeyote ile. Bahati nzuri vyama vikuu viwili vilivyohusika kujenga msingi wa maridhiano ya Zanzibar (CCM na CUF) bado viko hai kisiasa na bado vina nguvu na ushawishi mkubwa kitaifa. Wahusika wakuu wa maridhiano hayo (Rais Kikwete, Rais Shein, Rais Mstaafu Amani Karume, Makamu wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif) bado wako hai kimwili na kiakili na ushawishi wao kisiasa ni mkubwa sana. Hata wanasiasa wengi waandamizi walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika mpango wa kujenga msingi wa maridhiano Zanzibar hivi sasa ni Wajumbe wa Bunge Maalum (Mzee Kingunge, Profesa Lipumba, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Spika Pandu Kificho, Mwenyekiti wa Bunge Maalum Samweli Sitta, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, aliyekuwa waziri kiongozi wa Zanzibar, Mhe. Shamsi Vuai Nadodha, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Vuai, Waziri wa Afya Zanzibar, Mzee Juma Duni Haji, Waziri wa Sheria Zanzibar, Mh. Aboubakar Khamis, Mh. Hamadi Rashid, Mh. Ismail Jussa, Mh. John Chiligati, Mh. Fatuma Fereji na wengineo). Sioni kwa nini hazina na uzoefu huo visitumike sasa. Tahadhari kubwa inatakiwa kuchukuliwa na wajumbe wote wa Bunge Maalum na viongozi wote wa kisiasa nchini ili uamuzi wowote utakaofanywa wakati huu usidhoofishe au kuvunja msingi wa maridhiano ya Zanzibar ya 2010.

5.      Hitimisho
Mazingira ya utulivu, uvumilivu na utashi wa kisiasa yanahitajika zaidi sasa kuliko wakati wowote wa historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wavujajasho ndiyo wenye jukumu kubwa sana la kufanya tathmini ya hali halisi na kuchukua hatua mwafaka. Ili waweze kutimiza wajibu wao, wavujajasho wanatakiwa kuzikataa siasa za kuwagawa na kuwadanganya.

Hoja kwamba Rasimu ya Katiba ndiyo imebeba maoni ya wananchi wote haipaswi kuwa chimbuko la mifarakano ya kisiasa hapa nchini kwa sababu hiyo Rasimu iliandaliwa na TMK katika ombwe la mwafaka wa kitaifa. Aidha, Rasimu ya Katiba inayojadiliwa ndani ya BMK inazo kasoro nyingi sana zinazotakiwa kurekebishwa. Sehemu inayohusu muundo wa Muungano ndiyo iliyokosewa mno. Kama shughuli za BMK zitaendelea, basi maoni ya baadhi ya wananchi kuhusu kasoro za muundo wa Muungano wa serikali tatu yapewe uzito unaostahili na wala yasibezwe au kupuuzwa. Katika hatua ya sasa ya mchakato wa kutunga Katiba, chombo pekee kinachoweza kurekebisha kasoro hizo ni BMK.

Kadhalika, wananchi wanaokubaliana na Rasimu ya TMK na wale wenye fikra kinzani wote wana haki sawa siyo kwa sababu ya wingi wao au itikadi zao za kisiasa bali kwa sababu ya haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni. Kazi ya wajumbe wa BMK ni kuzisikiliza hoja za wananchi wote bila jazba wala ubaguzi ili waweze kufanya uamuzi kwa hekima, haki na bila woga wala upendeleo. Na tusisahau kwamba, hatimaye, uamuzi wa BMK utafanywa kwa njia ya kura. Na hapa ndipo wajumbe wa BMK wanapotakiwa kufanya siasa safi ili hoja nzito pekee ndizo zipitishwe kwa kura nyingi. Kazi ya kutoa maoni itakoma mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura ya maoni.

Kwa yakini, suala la muundo wa Muungano linahitaji kuamuliwa kwa umakini sana. Wajumbe wa BMK wanapaswa kutambua kwamba hakuna upande wowote (wa serikali mbili au serikali tatu) ambao uko sahihi kwa asilimia mia moja. Ni muhimu kusisitiza pia kwamba bado upo umuhimu wa kulinda hadhi na utambulisho wa Zanzibar ndani ya Katiba ya Muungano wa Tanzania. Yapo pia mapendekezo kwamba katiba ya Jamhuri ya Muungano inapaswa kuwa na sura mbili mpya. Sura hizo zinahusu misingi ya kuendesha mfumo wa serikali za mitaa na misingi ya kudhibiti na kusimami raslimali za ardhi na maliasili za Taifa. Wapo baadhi ya wananchi wanaopendekeza kwamba suala la ardhi liwe mojawapo ya mambo ya muungano ili watanzania wote wawe na haki ya kutumia raslimali za ardhi katika shughuli za uzalishaji wa chakula, makazi na ukuzaji wa uchumi wa Taifa. Haya nayo ni mambo muhimu sana ya kujadiliwa na BMK.

Kama serikali tatu zitakubalika, itabidi dola ya shirikisho iwe ndiyo yenye nguvu zaidi kuliko dola za Tanganyika na Zanzibar. Ili kufanya hivyo, orodha ya mambo ya Muungano itabidi iongezeke na kujumuisha mambo ya sera za fedha, fedha za kigeni, usimamizi wa mabenki na taasisi zote za fedha; aina zote za kodi ya mapato; mikopo kutoka nje, maendeleo ya elimu ya juu, maendeleo ya sayansi na teknolojia na sera za uchumi na uwekezaji. Wajumbe wa BMK watambue kwamba hakuna popote pale duniani ambapo serikali ya shirikisho imedumu na kushamiri bila serikali hiyo kuwa na nguvu kubwa juu ya mambo niliyoyataja hapo juu. Serikali za Shirikisho kama Marekani, India, Australia na Ujerumani ni madhubuti kwa sababu zinadhibiti taasisi zote nyeti za kisiasa, kiulinzi, kisayansi na kiuchumi.

Kwa hiyo, orodha ya mambo ya muungano itabidi iwe na mambo zaidi ya saba yaliyopendekezwa ndani ya Rasimu ili dola ya shirikisho iwe na uwezo wa kujiendesha kwa uhakika na pia kuratibu maendeleo ya kisiasa na kiuchumi katika nchi nzima. Je, wale wapendao muundo madhubuti wa Muungano wa serikali tatu wako tayari kukubaliana na ongezeko kubwa la mambo ya Muungano? Sina hakika kama wako tayari. Ikiwa ongezeko hilo kubwa la mambo ya Muungano halikubaliki, basi muundo wa Muungano wa serikali tatu utazaa dola ya Muungano iliyo dhaifu na kwa vyovyote vile Muungano wenyewe hatimaye utavunjika. Na ikiwa nia ya wajumbe wa Bunge Maalum ni kuendelea kulinda hadhi na utambulisho wa Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano na kuimarisha misingi ya utaifa, ni dhahiri kwamba muundo wa serikali mbili ndiyo mwafaka zaidi kuliko muundo wa serikali tatu.

Wavujajasho wa Tanzania bara na Zanzibar wanatakiwa kutambua pia kwamba misuguano mikali iliyopo sasa ni hatarishi kisiasa na hata kiusalama. Wasikubali kudanganywa au kutumiwa na wanasiasa kwa kisingizio kwamba Katiba itakayotungwa fastafasta ndiyo mwarobaini au ‘Kikombe cha Babu’ cha kutibu ndwele zote za kisiasa na kiuchumi zinazolisibu taifa lao na jamii zao. Wavujajasho wa Tanzania wakumbuke kwamba Katiba iliyotungwa kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia ni moja ya nyenzo muhimu sana za kisiasa za kuendeleza mapambano yao dhidi ya ubeberu yaliyoasisiwa miaka hamsini iliyopita na wapigania uhuru wa Tanzania walioongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Wavujajsho wakumbuke pia kwamba mchakato wa kutunga Katiba ni sehemu mojawapo ya mapambano yao ya kudumu dhidi ya ubeberu na vibaraka wake.

Ni dhahiri kwamba wavujajasho ndiyo watakaopata hasara iwapo watatekwa na siasa za jazba na ubaguzi. Na ikiwa itabidi mchakato wa kutunga Katiba kuvunjika au Bunge Maalum kuahirishwa kwa muda au hata muda wa uhai wa Bunge Maalum kuongezwa kwa sababu zozote zile basi hali hiyo itabidi ikabiliwe na wavujajasho wote kwa uangalifu mkubwa na kwa mshikamano ili misingi ya amani na umoja wa taifa lao visidhoofishwe au kuvunjwa. Badala ya kulaumiana na kulumbana, kila mvujajasho nchini anapaswa akiri kwamba usanifu mbovu wa mchakato wa kutunga Katiba ndiyo umelizamisha Bunge Maalum, na Taifa kwa ujumla, kwenye mtanziko wa kutunga Katiba. Kwa kukiri hivyo, wavujajasho wa Tanzania watakuwa wamewasuta mabeberu na vibaraka wao ambao kiu yao kubwa ni kuwagawa ili waweze kuendeleza vitendo vyao vya unyonyaji na ukandamizaji. Ubeberu ndiyo unaopaswa kuwekwa kizimbani na kuhukumiwa siyo umoja na utu wa waafrika.[1] Hoja kuu na uchambuzi katika makala haya vimetokana na mijadala inayoendelea katika tovuti iitwayo CHECHE ZA AFRIKA MPYA au www.checheafrika.org.

[2] Issa.G. Shivji (2006); Let the PeopleSpeak: Tanzania Down the Road to Neoliberalism; Dakar, CODESRIA

[3]Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]” Mwaka 2013, (Ukurasa wa 7-8)

[4] Hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mh. Jaji Joseph Sinde Warioba, Akiwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katika Bunge Maalum la Katiba, Machi 2014

[5] Soma gazeti la Mwananchi la 26, Machi 2014 ukurasa wa 37: ‘Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa Umma kuhusu Ufafanuzi wa Baadhi ya Maeneo Muhimu ya Taarifa ya Tume’.

[6] Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa Kulihutubia Bunge Maalum la Katiba Tarehe 21 Machi,2014,Dodoma

[7] Mada ya Profesa Shivji: ‘Uchambuzi wa Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984: Je, ‘Sasa Tunazo Nchi Mbili’? Usome uchambuzi huu kupitia www.checheafrika.org

3 thoughts on “MTANZIKO WA KUTUNGA KATIBA: Nini Chanzo Chake, Zipi Athari Zake Kisiasa, Na Nini Kifanyike?

 1. Namshukuru na kumpongeza sana ndugu Bashiru kwa hii mada nzito aliyoitoa wakati muafaka inapohitajika sana na yenye manufaa makubwa iwapo itazingatiwa na wote wanaohusika kwenye maboresho ya Rasimu ya katiba mpya yanayoendelea ndani ya Bunge maalum la katiba.
  Niionayo kuwa na umuhimu wa pekee miongoni mwa hoja za Ngugu Bashiru zilizomo kwenye mada yake ni hii ifuatayo:
  ‘’Kama serikali tatu zitakubalika, itabidi dola ya shirikisho iwe ndiyo yenye nguvu zaidi kuliko dola za Tanganyika na Zanzibar. Ili kufanya hivyo, orodha ya mambo ya Muungano itabidi iongezeke na kujumuisha mambo ya sera za fedha, fedha za kigeni, usimamizi wa mabenki na taasisi zote za fedha; aina zote za kodi ya mapato; mikopo kutoka nje, maendeleo ya elimu ya juu, maendeleo ya sayansi na teknolojia na sera za uchumi na uwekezaji. Wajumbe wa BMK watambue kwamba hakuna popote pale duniani ambapo serikali ya shirikisho imedumu na kushamiri bila serikali hiyo kuwa na nguvu kubwa juu ya mambo niliyoyataja hapo juu. Serikali za Shirikisho kama Marekani, India,Australia na Ujerumani ni madhubuti kwa sababu zinadhibiti taasisi zote nyeti za kisiasa, kiulinzi, kisayansi na kiuchumi’’
  Kama hoja hii itazingatiwa na kukubalika na wengi ndani ya Bunge la Katiba na hatimaye pande mbili za muungano, uwezekano wa kupatikana katiba mpya na bora zaidi kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu ujao ni kubwa. Kukubalika shirikisho la serikali 3 ni kuondokana na kero zilizosabishwa na serikali 2 kushindwa kutoa fursa sawa kwa watanzania ndani ya pande mbili za muungano, mdogo kujisikia amemezwa na mkubwa na mkubwa kujikuta akiingiliwa na mdogo kwenye yale yasiyokuwa ya muungano.
  Ongezeko la maswala ya Shirikisho lenye lengo la kuipa Serikali ya Shirikisho uwezo mkubwa unaohitajika kuiwezesha kuimarsha na kudumisha Shirikisho ni zuri na toshelezi lengo kwa sababu halitaathiri utoaji fursa sawa kwa watanzania ndani ya pande mbili za Shirikisho na ni wezeshi wa maendeleo ya Shirikisho kuelekea Muungano wa Serikali mbili uliolengwa na Waasisi na unaofikika kwa nji moja pekee ya ongezeko la maswala ya shirikisho hatua kwa hatua hadi hapo yote yote yasiyokuwa ya Shirikisho yatakapokuwa yamekwisha. Ushauri uliotolewa kwenye Bunge la Katiba na Mh. Z. Kabwe wa kutaka Shirikisho la Serikali tatu likubalike na liwe na Raisi wakati kila nchi mshirika ikiwa na Makamu Raisi au Governor (nionavyo mimi) naona utafaa pia ukikubalika.

 2. Ninakubaliana na hoja ya haja ya ndugu Bashiru kwamba watunga katiba (BMK) hatuna budi kuongozwa na Dira ya ukombozi katika kutunga katiba mpya. Hata hivyo, pamoja na kutawala kwa hisia za kisiasa jambo ambalo limekuwa ngumu kuliepuka, nionavyo mimi ni kwamba zipo chembechembe za ubeberu ambazo kwa namna fulani zinachochea mkwamo kwenye mchakato huu wa kutunga katiba. Ni dhahiri kwamba tunapita kwenye kipindi ambacho hatujawahi kuki experience. Lakini kuna utashi wa kisiasa uliogubikwa na uchwara ndani yake unaopelekea kupungukiwa uzalendo. Pengine jambo hili linaweza kupelekea kushindwa kutambua ukweli kwamba hatuwezi kukwepa historia ya mapambano dhidi ya ubeberu katika kutunga katiba yetu. Katika hili ukweli lazima utafutwe na ubainishwe wazi juu ya wale walioathirika na chembechembe za ubeberu. Vilevile tunapaswa kuendelea kukumbushwa historia ya nchi yetu hususan juu ya namna wananchi walivyopambana kuikomboa nchi yetu.

  Kadhalika, msimamo wangu tu ni kwamba, Wabunge wa Bunge la Jamhuri pamoja na Wajumbe wa Baraza la wawakilishi ndiyo wawakilishi halali wa wananchi kwenye BMK kwa kuzingatia ukweli kwamba wao walichaguliwa na wananchi wao kwa njia ya kura.

 3. Nakubaliana na Mh. Zainabu kuunga mkono Dira ya ukombozi iwe mwongozo kwenye utunzi wa Katiba mpya ya Tanzania pamoja na kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi Barani Afrika ambazo zote ziko huru baada ya kuondokana na utawala wa kikoloni. Pamoja na kujipatia uhuru wa kujitawala zenyewe, nyingi Barani Afrika zinazidi kudidimia kwenye dimbwi la umaskini kunakosababishwa na kuendelea kutawaliwa kibeberu chini ya ukoloni mamboleo kama alivyosimulia Prof. George N. Ayittey hapa chini: WE LET AFRICA DOWN BADLY by Prof George N. Ayittey …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box