MTAZAMO NA MAPENDEKEZO YETU JUU YA KUIFANYA ARDHI NA MALIASILI ZOTE KUWA MASUALA YA KIKATIBA

TAASISI YA UTAFITI NA UTETEZI WA HAKI ZA ARDHI

(HAKIARDHI)

MTAZAMO NA MAPENDEKEZO YETU JUU YA KUIFANYA ARDHI NA MALIASILI ZOTE KUWA MASUALA YA KIKATIBA

1.0         KUTAMBUA ARDHI NA MALIASILI NYINGINE KUWA NI MALI YA TAIFA NA SEHEMU YA MAMBO YA MUUNGANO

1.1     ARDHI  na maliasili zingine ni moja ya masuala ambayo wananchi wengi wameyatolea maoni mengi wakati Tume ya Marekebisho ya Katiba ilipokuwa ikikusanya maoni yake kutoka kwa wananchi. Katika hotuba yake mbele ya Bunge Maalumu la Katiba mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba alisema hivi kuhusu ardhi:

Moja ya mambo ambayo wananchi waliyatolea maoni kwa msisitizo mkubwa ni ardhi. Wananchi wengi walilalamika kwamba wanayo matatizo kutokana na ugumu wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine lakini wawekezaji wakubwa wanapewa upendeleo wa kupata ardhi kwa urahisi. Pia, kuna migongano isiyokwisha ya makundi mbalimbali, wakulima na wafugaji, wananchi na mamlaka za hifadhi za taifa na kadhalika. Kuna malalamiko mengi kuhusu huduma za kilimo kama vile zana za kilimo, pembejeo na mizania ya bei.

 1.2     Ubaini huu wa Tume ya Katiba ni mwangwi tu wa sauti na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi walio wengi juu ya kutoridhishwa kwao na namna rasilimali za Taifa zinavyotumiwa na kuvunwa bila kuzingatia matakwa na maslahi yao.

1.3    Itakumbukwa kwamba katika miaka ya mwanzoni mwa 1990 Tume ya Rais ya Kuchunguza Juu ya Masuala ya Ardhi, ilionesha kuwa wananchi walilalamika kuwa hawakuwa na uhakika wa milki juu ya ardhi walizokuwa wakizikalia na kutumia; na kwamba hawakuridhishwa na namna ambavyo maamuzi juu ya rasilimali yao muhimu kwa ajili ya uzalishaji yalivyokuwa yakifanywa bila wao kushiriki katika uamuzi, hali ambayo iliwaondolea haki na uhakika wa kuishi na kuendelea kujizalishia chakula chao na ziada kwa ajili ya mahitaji mengine ya msingi.

1.4      Pamoja na kuwepo kwa malalamiko hayo kwa muda mrefu, sera na mipango ya serikali haielekei kupunguza bali kuongeza tatizo hili na malalamiko ya wananchi. Katika miongo zaidi ya miwili iliyopita wananchi, hasa wafugaji, wakulima wadogo wadogo, wachimbaji wadogo wadogo, watu wanaoishi maeneo ya pwani za bahari, na watu wanaoishi maeneo jirani ya Hifadhi za Taifa, wavuvi, na wawindaji na wakusanyaji wamekuwa wakiondoshwa kwa nguvu na mabavu ya Dola ili kupisha watu wenye nguvu ya pesa au mamlaka (wa ndani na wa nje) kutumia rasilimali hizo; hatua ambazo zimekuwa na matokeo yenye kudhalilisha, kunyanyasa, kufukarisha, na kuvunja utu na staha za wavuja jasho.

1.5  Aidha katika kipindi hicho wananchi wameonyesha kutoridhishwa na namna ambavyo utajiri na maliasili mbalimbali za nchi kama vile ardhi, madini, misitu, wanyamapori, mafuta na gesi zinavyosimamiwa, kugawiwa, na kuvunwa. Wananchi katika kueleza kutoridhishwa kwao na hali hii, na katika kuzuia baadhi ya hatua za kuwapora rasilimali hizi, wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kama vile maandamano, mapambano baina yao na wawekezaji, na mapambano baina yao na vyombo vya dola vilivyotumwa na kuamriwa kuzima jitihada zao mbalimbali za kupinga uonevu, unyanyasaji, na dhuluma dhidi ya haki yao ya kumiliki na kutumia rasilimali hizo.

1.6     Kwa kuwa suala la maliasili ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa na watu wake, na kwamba zinaposimamiwa vibaya huwa chanzo cha migogoro na machafuko katika Taifa; na kwa kuwa sehemu kubwa ya watu wetu bado wanategemea maliasili hizi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na mahitaji mengine mbalimbali; na kwamba hali hii ya kutegemea rasilimali na utajiri huu wa maliasili za nchi hauna kikomo; na kwa vile nchi yetu inatambua haja na umuhimu wa kujenga misingi ya kujitegemea kijamii na kiuchumi; na kwamba usimamizi na uvunaji wa maliasili kwa kuzingatia maslahi mapana na endelevu ya walio wengi ni jambo muhimu na lenye manufaa kwa Taifa zima; na ni wazi kwamba usimamizi na uvunaji wa maliasili hizi hauwezi kuachiwa sera na sheria peke yake, ambazo ni rahisi kubadilishwa pengine hata bila wananchi kufahamu; hivyo basi misingi ya kusimamia, kuendeleza, na kugawa manufaa na faida zitokanazo na maliasili hizi lazima uwe wa kikatiba.

1.7      Kwa misingi hiyo na kwa nia ya kujibu hofu, malalamiko, na matamanio ya wananchi walio wengi, na katika shabaha ya kudumisha misingi ya haki, uhuru, umoja, na amani, kwa nchi na watu wake KATIBA: 

1.      Itamke wazi kwamba, Maliasili zote, ikiwemo ardhi na utajiri unaopatikana chini ya ardhi (madini, mafuta, gesi na maji, n.k) na utajiri unaopatikana juu ya ardhi (mapori, maji, uoto wa asili, wanyama pori na baioanuwai) ni mali ya Taifa na vizazi vijavyo, na ndiyo msingi wa uhuru na mamlaka kamili ya Watanzania (sovereign right);

2.      Ardhi na maliasili zote hizi ni Mambo ya Muungano;

3.      Katiba itamke na iweke masharti yanayoilazimisha Dola (Serikali) kutumia faida zitokanazo na uendelezaji na uvunaji wa maliasili za Taifa kwa ajili ya kukuza na kuendeleza sekta muhimu za uzalishaji endelevu zenye kuleta tija katika uzalishaji na hivyo kuleta mapinduzi ya haraka na endelevu katika maisha na ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa wananchi walio wengi na kwa vizazi vilivyopo na vijavyo. 

4.      Katiba itamke na kuweka masharti kuwa usimamizi wa maliasili za taifa utakuwa chini ya vyombo huru vya kikatiba, vinavyowajibika kwa wananchi, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maliasili isiyo ndani ya maeneo ya Vijiji/Shehia; na Mikutano Mikuu ya Vijiji kwa Tanzania Bara, na Mikutano Mikuu ya Shehia kwa Tanzania Zanzibar kwa maliasili yote iliyomo katika maeneo ya Vijiji/Shehia;

 

2.0   KUWEKWA KWA SURA MAHSUSI YA ARDHI KWENYE KATIBA

2.1    Pamoja na kutambua umuhimu wa maliasili zote zilizopo, zilizokwisha gunduliwa na ambazo hazijagunduliwa, ardhi inabaki kuwa na umuhimu wake wa kipekee katika uhai, maendeleo na ustawi wa Taifa na watu wake.

2.2    Wakati maliasili nyingine huwepo, kwisha, na kutoweka, ardhi ndio rasilimali ya msingi yenye uhakika wa kudumu kwa miaka, miongo, karne na milenia; na kwamba uendelevu wa Maisha ya Taifa na watu wowote duniani hutegemea uwepo wa ardhi.

2.3      Aidha ni ukweli ulio wazi kuwa amani na utulivu uliopo hapa nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa ardhi inayowaruhusu wananchi wengi hasa wakazi wa vijiji kujizalishia chakula chao wenyewe na ziada kwa ajili ya watu wasioshiriki moja kwa moja katika kilimo, uvuvi, ufugaji, ukusanyaji na uwindaji; kwamba kwa kuwa na uhakika wa kupata ardhi katika maeneo ya vijiji ni wazi kwamba watu wengi washindwapo kuendelea na maisha ya mijini hurejea vijijini na kufanya shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, n.k.

2.4    Ni wazi pia kwamba kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na hali ya mizozo, migogoro, na pengine mapigano baina ya wananchi, mathalani wakulima na wafugaji; wananchi na vyombo vya dola; wananchi na wawekezaji toka ndani na nje ya nchi wanaopora ardhi zao za kilimo, uvuvi, ufugaji, uwindaji na ukusanyaji, na maeneo mengine yenye umuhimu kwao kama urithi na tunu za kihistoria, kitamaduni na kijamii;

2.5       Ni wazi pia kuwa katika miongo ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la makampuni makubwa ya kimataifa kutamani, kunyemelea, na kupora ardhi za nchi za kiafrika kwa sababu mbalimbali zikiwemo kuzalisha chakula na nishati uoto kwa ajili ya kukidhi mahitaji na uhakika wa chakula na nishati kwa masoko ya nje hasa Ulaya, Amerika ya Kaskazini, na Bara Asia; kuwekeza katika sekta za madini na pwani za bahari kwa ajili ya kuvuna faida kubwa na za haraka zisizo na maslahi ya moja kwa moja na ya kudumu kwa Taifa na watu wake;

2.6       Kwamba wimbi hili limezua ugombaniaji wa awamu ya pili wa maliasili za Afrika (Second Scramble), ikiwemo hazina kubwa ya maji baridi iliyoko chini ya ardhi ya nchi za kiafrika, na hivyo kuhatarisha usalama na utulivu wa nchi zetu katika nyakati zilizopo na zijazo.

2.7       Kwa kutambua umuhimu huu wa ardhi na kwa kutambua na kutaka kujiepusha na hatari mbalimbali zisizo na maslahi ya kudumu na endelevu kwa Taifa letu, na ili kujihakikishia uhakika wa kuwepo kwa Taifa na Watu huru ndani ya Tanzania na dunia, ardhi (kama ilivyotamkwa awali kwa rasilimali nyingine) lazima iwe suala la Kikatiba na iwe na Sura yake Mahsusi itakayoweka ufafanuzi fasaha juu ya mamlaka zitakazoongoza usimamizi na matumizi yake, na makundi ambayo maslahi yake yatawekwa mstari wa mbele katika kufaidika na rasilimali hiyo.

2.8       Bila kuathiri mapendekezo ya jumla kuhusu usimamizi, utumiaji na uendelezaji wa maliasili nyingine zote, masuala na masharti yafuatayo yatamkwe katika Sura Mahsusi ya Katiba juu ya Ardhi:

                                i.            Shabaha na misingi mikuu ya umiliki, usimamizi na matumizi ya ardhi ni kutoa na kuwahakikishia wazalishaji wadogo wadogo uhakika wa milki ya ardhi;

                              ii.            Kutamka kwamba ubadilishaji wowote wa misingi mikuu ya kikatiba katika milki ya Ardhi sharti ifanywe na watu wenyewe kwa njia ya kura ya maoni.

                            iii.            Kwamba kutakuwa na aina mbili kuu za ardhi, Ardhi ya Taifa na Ardhi ya Kijiji/Shehia;

a.       Kwa mujibu wa Katiba Ardhi ya kijiji/shehia itambulike kuwa ni ardhi yote iliyo ndani ya mipaka ya Vijiji/Shehia;

b.      Ardhi ya Taifa ni ardhi yote ambayo siyo ya kijiji/shehia  na ambayo matumizi yake yatapangwa kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na maslahi ya taifa;

                            iv.            Kwamba kutakuwa na Milki kuu Mbili za Hatima, moja kwa ajili ya Ardhi ya Taifa na nyingine kwa ajili ya Ardhi ya Kijiji/Shehia;

a.       Milki ya Hatima kwa Ardhi ya Taifa itakuwa chini ya chombo huru cha kikatiba ambacho kinawajibika kwa wananchi kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

b.      Milki ya Hatima kwa Ardhi yote ya Kijiji/Shehia itakuwa chini ya milki ya wanakijiji/wanashehia na mkutano mkuu wa Kijiji/Shehia utakuwa ndicho chombo chenye mamlaka ya mwisho kuhusu umiliki, usimamizi na matumizi ya ardhi;

                              v.            Milki na matumizi ya ardhi yatatofautiana kutegemeana na Ardhi inayohusika iko katika kundi gani kati ya Ardhi ya Taifa na Ardhi ya Kijiji/Shehia:

a.       Ardhi ya Taifa itamilikiwa kwa njia kuu mbili ambazo ni kwa njia ya hati na kimila;

b.      Ardhi ya kijiji/shehia itamilikiwa kimila au kwa njia ya hati ya ardhi ya kimila;

c.       Aina zote za milki zitakuwa na hadhi sawa kwa mujibu wa Katiba.

                            vi.            Kuhusu Matumizi ya Ardhi Katiba itamke:

a.      kwamba msingi Mkuu wa umilikaji wa ardhi ni Matumizi ya ardhi kwa mujibu wa masharti na taratibu zitakazowekwa kuhusu Ardhi husika kwa mujibu ya sheria itakayotungwa na Bunge;

b.      Kwamba kila mmiliki wa Ardhi ataitumia Ardhi aliyonayo au kupewa kwa misingi ya matumizi bora na endelevu ya ardhi;

c.       Kwamba itakuwa ni marufuku kwa mtu, taasisi, au kikundi cha watu kuhodhi na kujilimbikizia ardhi; na kwamba ardhi yoyote itakayoonekana haitumiki kwa masharti na taratibu zilizowekwa itatwaliwa na kugawiwa kwa watumiaji wengine na Mamlaka zinazohusika;

d.      Iweke ukomo wa muda na ukubwa wa eneo la ardhi inayoweza kumilikishwa na vyombo vya kikatiba kwa mujibu wa sheria itakayotungwa na Bunge;

e.       Katiba izuie ardhi ya kijiji/shehia kutolewa kwa watu ambao sio wanakijiji

                          vii.            Kuhusu utawala na usimamizi wa ardhi:

a.       Katiba itamke kwamba usimamizi wa Ardhi ya Taifa utakuwa chini ya chombo huru cha kikatiba kitakachowajibika kwa wananchi kupitia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

b.      Katiba itamke kwambausimamizi wa Ardhi ya kijiji utakuwa chini ya mkutano mkuu wa Kijiji/Shehia;

 c.       Mamlaka Zote Mbili, yaani Kile chombo cha Kitaifa na Mkutano wa Kijiji/Shehia mipaka na mamlaka yake vitamkwe ndani ya Katiba;

d.      Katiba itamke kwamba watendaji wa serikali na mamlaka nyingine yoyote yenye dhamana  ya usimamizi wa ardhi kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa watawajibika kwa vyombo vya kikatiba;

3.0  KUTAMBUA NA KUSAIDIA SEKTA YA WAZALISHAJI WADOGOWADOGO

3.1       Pamoja na kwamba mchango wa wazalishaji wadogo wadogo katika uchumi na ustawi wa Taifa ni mkubwa, kwamba huzalisha sehemu kubwa ya chakula na mahitaji mengine ya msingi ya watu wa mijini na vijijini; na kwa mujibu wa sensa ya Taifa ya watu ya 2012, ardhi na maliasili ndivyo vyanzo vikuu vya mahitaji ya msingi na ustawi wa wazalishaji wadogo wadogo ambao ni zaidi  ya asilimia 70.4 ya watanzania  wote; hali za maisha ya makundi haya ya wazalishaji  zimebaki kuwa duni, na uzalishaji umebaki kuwa wenye kiwango kidogo cha tija, kutokana na utumiaji wa maarifa, sayansi na teknolojia ya hali ya chini; hali inayotokana na kukosekana kwa msukumo na uwekezaji wa fedha na utafiti wa ki-Dola katika sekta hii; kwamba hali hii imezidi kuwa mbaya zaidi tokea nchi yetu kukumbatia mfumo wa uchumi wa soko.

3.2       Kwa ujumla wake hali hii si tu inawafanya vijana wengi kuhama vijijini na kukimbilia mijini kwa matumaini ya kupata kazi na maisha bora, ambako pia ajira si nyingi sana, bali pia huongeza uwezekano wa kumomonyoka kwa misingi ya utengamano na umoja wa Kitaifa; hali hii pia inachelewesha mapinduzi katika mfumo wa uzalishaji mali na ulimbikizaji mtaji katika Taifa letu. Ili kubadilisha hali hii kuna haja ya kuweka misingi ya kikatiba inayotambua umuhimu wa sekta hii na kundi la wazalishaji lililomo, na kuweka mwongozo wa kikatiba wenye kutoa msukumo wa kuijali na kuibadili sekta na watu waitegemeao. Ili kufikia shabaha hiyo:

i)         Katiba itamke kwamba kijiji ni kitovu cha uzalishaji, demokrasia na maendeleo ya kisasa katika Taifa letu;

ii)      Katiba itoe wajibu kwa  Serikali kuendeleza sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na uchimbaji wa madini kwa kuzingatia mahitaji ya wazalishaji wadogo wadogo;

iii)    Ili kuharakisha mapinduzi katika mfumo wa uzalishaji mali nchini na kuchochea maendeleo vijijini, katiba itamke kiwango cha uwekezaji katika sekta za kilimo, uvuvi, mifugo na uchimbaji wa madini kwa kuzingatia mahitaji ya wazalishaji wadogo wadogo;

iv)    Katiba itambue mifumo ya maisha ya uzalishaji mali ya makundi maalum na ilinde mifumo hiyo kulingana na taratibu na mahitaji ya jamii husika;

v)      Endapo umiliki wa mtu, kikundi ama jamii utaingiliwa kwa maslahi ya taifa na kwa mujibu wa sheria itakayo tungwa na bunge, Katiba iweke masharti ya haki ya malipo ya fidia ya haki na kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box