SALAMU ZA MWAKA JANA

SALAMU ZA MWAKA JANA

nikadamkia jijini leo
nikizurura mitaani darisalama
kuelekea kijiweni kwangu
zanaki na libya
penye kahawa na kashata
matukano na mahuba.

duh! majengo yale mawili
yanatazamana, yanadokoana
uzuri wa mwenzake
kana kwamba ni ushindani wa warembo.
moja linajigamba: one-stop ports authority,
mwenzake anamjibu: psps, apartments, duplexes, offices …

Kichwa kikazunguka,
Akili zikazirai,
FFB (fast forward backwards)
Ikajibofya yenyewe.

nikajikuta niko Parakuyo,
kijijini Kilosa.
vitoto vinagombana
vinagombea mifuko …
mifuko ya plastiki,
mifuko yenye pilau!

nchi yangu, darisalama yangu,
imejaa vituko
ushindani wa majengo darisalama
ugomvi wa mifuko-pilau kilo-sama

lahaula! Mola wangu,
kama upo, unijibu,
ni muujiza wako? au madudu ya wanao?

Issa bin Mariam

27/12/2015

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box