Siasa za ‘Wao’ na ‘Sisi’ Zikitulevya Sote, Nchi Itayumba

Makala hii kwanza ilitoka kwenye gazeti la Raia Mwema la Tarehe 5 – 11 March 2014

Na Bashiru Ali

Ni dhahiri kwamba mchakato wa kutunga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umejengwa juu ya msingi wa siasa zinazolevya, siasa za ‘wao’ na ‘sisi’. Siasa hizi huwalevya zaidi wenye vyeo, wasaka vyeo na wafuasi wao. Siasa hizi hupamba moto kila unapowadia msimu wa uchaguzi. Wakati wa uchaguzi, viashiria vya siasa za ‘wao’ na ‘sisi’ hujibainisha wazi wazi katika sura zifuatazo: ufisadi, uongo, udalali, ukuadi, uchochezi, ubaguzi, uonevu, ubinafsi, ubadhirifu wa raslimali za umma, utovu wa nidhamu na udanganyifu. Katika majukwaa ya kisiasa wenye vyeo, wasaka vyeo na wafuasi wao huumbuana hadharani. Kauli za ‘wao’ wako hivi na ‘sisi’ tuko hivi; ‘wao’ wameshindwa hili, ‘sisi’ tunaweza hili zimezoeleka sana wakati wa uchaguzi. Nionavyo mimi, hata mchakato wa kutunga Katiba nao una kiwango fulani cha viashiria vya siasa za ‘wao na ‘sisi’. Hii siyo dalili nzuri, tujisahihishe.

Siasa za ‘wao’ na ‘sisi’ zilianza kuchomoza wazi wazi tangu Tume ya Kurekebisha Katiba ilipowasilisha Rasimu ya Pili kwa Rais Kikwete mnamo Desemba mwaka jana. Tangu wakati huo hadi sasa, yameibuka makundi makubwa mawili yenye wafuasi wenye misimamo inayokinzana sana hasa kuhusu namna bora ya kukamilisha hatua zilizosalia za mchakato wa kutunga Katiba. Kundi la kwanza halitatizwi na misingi mikuu ya Rasimu ya Pili ya Katiba na kwa hiyo lingependa Rasimu hiyo ipitishwe na Bunge Maalum pasipo kufanyiwa mabadiliko makubwa. Kundi la pili linatatizwa sana na baadhi ya misingi ya Rasimu ya Pili ya Katiba na lingependa Rasimu hiyo ifanyiwe mabadiliko makubwa. Hata hivyo, wasemaji wote wa makundi haya kinzani wanadai kwamba misimamo yao haifungamani na maslahi yao binafsi bali ni kwa maslahi ya Taifa. Sidhani kama wafuasi wote wa makundi hayo wanasema ukweli.

Lengo kuu la makala haya ni kuwasihi wafuasi wa makundi haya kinzani, hususan wajumbe wa Bunge Maalum, waache kung’ang’ania misimamo yao bali wajenge hoja za kuwashawishi wenzano na hoja hizo wazianike hadharani ili zipimwe na kuchujwa. Vile vile, kila mfuasi wa kila kundi ndani ya Bunge Maalum awe tayari kusikiliza hoja zinazotofautiana na za kwake. Ndani ya Bunge Maalum, uamuzi wowote kuhusu kifungu chochote cha Rasimu ya Katiba ufikiwe kwa uwazi na uvumilivu. Madai ya kufanya maamuzi kwa kura ya siri katika mazingira ya sasa ya kushindanisha hoja hayana mantiki kisiasa na kidemokrasia. Uwazi unajenga imani ya kijamii na imani ya kijamii ndiyo kiini cha uhalali wa mchakato wowote wa kidemokrasia.

Ningependa nianze kwa kuyachambua makundi haya kinzani na misimamo yao. Kundi la kwanza linajumuisha wananchi wanaotaka Rasimu ya Pili ya Katiba ipitishwe na Bunge Maalum la Katiba bila kutenguliwa misingi yake kwa madai kwamba Rasimu hiyo imeandaliwa vizuri sana tena na wataalam wazalendo ambao wamezingatia barabara maoni ya wananchi. Kwa ufupi, hili ni kundi la wananchi wasio na mawazo mbadala kuhusu misingi mikuu ya Rasimu ya Katiba. Hawa wanataka Rasimu ya Katiba ‘ipakwe rangi’ na ‘kupambwa maua’ na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kabla ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.

Baadhi ya wasomi maarufu wa sheria hapa nchini wanadai kwamba msimamo wa kundi hili la kwanza ni sahihi na unakidhi matakwa ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, kifungu cha 25 (1). Hata hivyo, wapo pia wasomi wa sheria ambao wanawalaumu wasomi wenzao kwa kupotosha tafsiri ya kifungu hiki cha sheria. Makala haya hayana lengo la kudadisi ukweli kuhusu jambo hili. Mimi sina utaalam wa sheria. Hata hivyo, tafsiri tatanishi ya kifungu hiki cha sheria imeshaanza kuwagawa wananchi na wajumbe wa Bunge Maalum.

Kundi la pili linajumuisha baadhi ya wananchi wenye mawazo kosoa. Kundi hili linajumuisha baadhi ya wanachi ambao wanaamini kwamba Rasimu ya Pili ya Katiba inapaswa kujadiliwa kwa kina, uwazi na umakini mkubwa ndani na nje ya Bunge Maalum ili hatimaye Katiba itakayotungwa isiwe chimbuko la mifarakano na migogoro hatarishi kisiasa na kijamii nchini. Hili kundi linaundwa na baadhi ya wananchi wanaoamini kwamba kukamilishwa kwa Rasimu ya Pili ya Katiba ni hatua muhimu lakini siyo hatua ya mwisho ya mchakato wa kutunga Katiba ya Tanzania. Msingi mkuu wa msimamo wa kundi hili la pili ni sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayougawa mchakato wa kutunga Katiba katika hatua kuu tatu zinazotegemeana.

Hatua ya kwanza inahusu kuundwa kwa Tume ya kukusanya maoni na kuandaa Rasimu ya Katiba. Hatua hii imeshakamilika tena kwa ufanisi mkubwa. Hatua ya pili inahusu kuundwa kwa Bunge Maalum la kujadili Rasimu na kutunga Katiba. Hii ndiyo hatua inayoendelea sasa na umuhimu wake ni mkubwa zaidi kuliko hatua iliyokamilika kwa sababu matunda yake yanaweza kuwa na athari nzuri au mbaya kwa mchakato mzima wa kutunga Katiba. Matarajio ya wananchi wengi ni kwamba hatua hii nayo itakamilika vizuri na kwa amani. Hatua ya mwisho inahusu kura ya maoni ambapo wananchi wote watapata fursa ya kuridhia au kukataa Katiba itakayotungwa na Bunge Maalum. Kama Bunge Maalum litaendeshwa kidemokrasia na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa, bila shaka kura ya maoni nayo itafanyika kidemokrasia na kwa amani.

Wafuasi wa kundi hili la pili wanadai kwamba, katika hatua zote tatu, sheria inazingatia umuhimu wa kuwashirikisha wananchi kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi. Kwa hiyo, maoni ya kila mwananchi yaliyotolewa katika kila hatua ni muhimu na hayapaswi kupuuzwa. Maoni hayo ya wananchi yanaweza kuridhia au kutengua uamuzi wowote uliotangulia.

Kwa maoni yangu, hoja za kundi la pili ni nzito zaidi kuliko hoja za kundi la kwanza. Hata hivyo, makundi yote mawili hayajaweka wazi kiini cha misimamo yao kinzani. Mimi nadhani, kiini cha misimamo kinzani baina ya makundi haya ni pendekezo la muundo wa Muungano wa Serikali Tatu ambalo limo katika Rasimu ya Katiba. Jambo hili lisifanywe siri na wala lisipotoshwe kwa visingizio vyovyote vile. Ukweli ni kwamba kundi la kwanza linaundwa na wananchi ambao wanataka Bunge Maalum lipitishe muundo wa Muungano wa Serikali Tatu na kundi la pili linaundwa na wananchi ambao hawakubaliani na pendekezo la muundo wa Muungano wa Serikali Tatu. Katika kundi la pili, wapo wanaotaka muundo wa serikali mbili wenye mabadiliko makubwa zaidi kuliko huu wa sasa na wapo pia wanaotaka muundo wa Muungano wa Serikali moja. Sielewi ni kwa nini sauti za wanaotaka muundo wa Muungano wa Serikali moja hazisikiki sana. Ingawa wafuasi wa kila kundi wanadai kwamba muundo wa Muungano wanaoutaka ndiyo unaotekelezeka na ndiyo utakaodumisha umoja wa Kitaifa, sidhani kama kila mfuasi ndani ya makundi hayo ana dhamira hiyo.

Wapo baadhi ya wananchi na wajumbe wa Bunge Maalum wanaodhani kuwa mjadala kuhusu aina bora ya muundo wa Muungano umekuzwa mno na umepewa uzito usiostahili. Siyo kweli. Kwa yakini, muundo wa Muungano ndilo suala nyeti na gumu zaidi kuliko masuala mengine yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba. Suala la muundo wa Muungano linatakiwa kuamuliwa na wajumbe wa Bunge Maalum kwa uwazi, umakini, uvumilivu na utashi wa kisiasa wa hali ya juu sana. Muungano ndiyo nchi na ndilo Taifa. Uamuzi wowote mbaya kuhusu muundo wa Muungano unaweza kuivunja nchi na kuwagawa wananchi. Kwa hiyo, kila mjumbe wa Bunge Maalum anatakiwa kutangaza hadharani uamuzi wake juu ya aina ya muundo wa Muungano anaoona ni bora zaidi.

Mimi nakubaliana na wale wote wanaofikiri kwa dhati na kwa ushahidi kwamba muundo wa Muungano wa Serikali Tatu hautekelezeki na ni njia ya mteremko ya kuvunja nchi na kuwagawa wananchi. Kazi ya Bunge Maalum ni kuidadisi miundo yote inayopendekezwa na kufanya uamuzi kulingana na uzito wa hoja na uchambuzi wa historia ya Muungano wetu. Kwa hiyo, uamuzi wa mwisho kuhusu muundo bora wa Muungano utafanywa na Bunge Maalum la Katiba.

Wapo pia baadhi ya wananchi na wajumbe wa Bunge Maalum wanaoamini kuwa muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali Mbili hautekelezeki na tayari umeshavunjwa kutokana na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (toleo la 2010). Hili nalo ni suala nyeti lakini linajadilika. Kwa wakati huu, Bunge Maalum ndiyo medani pekee ya kisiasa na kidemokrasia inayofaa kutumiwa na wawakilishi wa wananchi ili kujadili masuala nyeti na magumu kisiasa. Wajumbe wa Bunge Maalum wenye dukuduku kuhusu jambo hili wana haki ya kuhoji na kupewa majibu kamili na sahihi. Hata wananchi nao wana haki ya kujua ukweli kuhusu jambo hili kupitia Bunge Maalum. Ndani ya Bunge Maalum wapo wajumbe wote kutoka katika Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wenye uelewa mpana kuhusu asili, muktadha, shabaha na athari za mabadiliko hayo yanayobishaniwa. Wajumbe waliohusika katika mchakato wa kufanya marekebisho ya Katiba ya Zanzibar wajiandae kujibu maswali ya wajumbe wenzao kuhusu jambo hili. Jambo hili lisitumiwe kama propaganda za kuupotosha umma.

Kwa hiyo, uwepo wa makundi yenye misimamo kinzani kuhusu masuala magumu siyo ishara mbaya kisiasa na kidemokrasia. Hali hii ni ya kawaida kabisa katika muktadha wa kutunga Katiba. Ni kawaida kabisa kwa mchakato wa kutunga Katiba kuzisisimua fikra na hisia za wananchi wa tabaka na rika mbalimbali. Pamoja na mapungufu kadhaa yaliyojitokeza, na hasa muda mdogo uliotengwa, mchakato wa kutunga Katiba umewapa wananchi wa Tanzania fursa ya kuidadisi historia ya uhuru wao na historia ya uhuru wa Taifa lao. Tofauti za kimtazamo tunazozishuhudia hususan kuhusu masuala ya msingi kama Muungano siyo tishio kwa umoja na mustakabali wa Taifa.

Pamoja na hayo, siasa za ‘wao’ na ‘sisi’ zilizozoeleka wakati wa uchaguzi zisiendekezwe na zisipewe upenyo wakati huu wa mchakato wa kuandika Katiba mpya. Mchakato wa kutunga Katiba siyo medani ya kuwania vyeo vya kisiasa na siyo ngao ya kung’ang’ania madarakani. Mchakato wa kutunga Katiba mpya ni fursa ya kujitathmini na kujipanga upya kama Taifa huru ili kuunganisha nguvu za kuendeleza mapambano ya kujitawala. Suala kuu linalohitaji umakini mkubwa kuliko yote ni uamuzi wa muundo wa Muungano unaotekelezeka na unaowaunganisha zaidi wananchi. Tukikubaliana hivyo, vitendo vya ufisadi, uongo, udalali, ukuadi, uchochezi, ubaguzi, uonevu, ubinafsi, ubadhirifu wa raslimali za umma, utovu wa nidhamu na udanganyifu havitapewa nafasi angalau wakati huu. Siasa hizi za ‘wao’ na ‘sisi’ zina kilevi kikali na tukilewa sote nchi itayumba.

2 thoughts on “Siasa za ‘Wao’ na ‘Sisi’ Zikitulevya Sote, Nchi Itayumba

 1. Naomba kufafanua mambo matatu yanayojitokeza katika mchango wa ndugu Massawe. Kwanza, upigaji kura ya wazi ni muhimu kutokana na umuhimu wa kazi ya kutunga katiba. Siyo hiari ya mjumbe wala busara yake bali ni haki ya wananchi kujua kwa ukamilifu na uwazi, hatua kwa hatua, shughuli zote za kila siku za Bunge la katiba. Kupiga kura kuhusu vifungu vya katiba ni moja ya kazi za wajumbe wa Bunge Maalum. Kura ya wazi ni muhimu kwa sababu inahusu mustakabali wa nchi na siyo haki ya mpiga kura au mgombea. Ni kura kuhusu masuala siyo watu. Kura ya siri inahusu masuala na watu. Maamuzi yanayofanywa leo yanawagusa watanzania waliopo hai leo na vizazi vyao vijazo. Sisi tuliopo leo na wenzetu watakaokuwepo baada yetu, tunatakiwa kujua maamuzi yatakayofanywa Bungeni yalifanywa namna gani na yalifanywa na nani na kwa nini. Idadi ya kura za siri za ndiyo au hapana imejaa ukimya na usiri. Usiri katika jambo hili zito haukubaliki kimantiki na kisiasa. Hii ni kura ya wazi ya kuhitimisha mijadala iliyoendeshwa kwa uwazi . Sio kura ya kuhitimisha kampeni za uchaguzi ambazo kwa kawaida hughubikwa na vitendo vya siri kama ubaguzi na ruswa. Ni kura ya wazi kuhusu msimamo wa mjumbe kuhusu vifungu vya Rasimu ya Katiba siyo kura kuhusu msimamo wa makundi.Kazi ya kuandika katiba ni ya watanzania wote. Na ili watanzania waweze kupiga kura ya maoni kwa uelewa mpana inabidi wajifunze kutokana na mijadala ya wazi na maamuzi ya wazi yatakayofanywa na Bunge. Mbona maoni ya wananchi wengi kwenye Tume ya Katiba yalitolewa hadharani kwa maandishi au kwa mdomo? Mbona uchambuzi wa Rasimu ya Katiba unafanywa waziwazi na misimamo ya wachambuzi hao inawekwa hadharani? Kwa bahati mbaya suala hili limechanganywa na misimamo ya kisiasa ya vyama na wanaharakati lakini suala lenyewe ni la kimantiki na liko wazi kabisa.Jambo la pili ni kuhusu misimamo ya wasomi kuhusu aina ya Muundo wa Muungano. Ingawa mijadala kuhusu suala hili imejikita zaidi, tena kimakosa, katika kulumbana juu ya idadi ya serikali za Muungano ambazo ni mwafaka, ipo pia mijadala ambayo inaenda mbali zaidi ya kujadili idadi ya serikali. Wapo watanzania ambao wanataka serikali tatu lakini wanawasiwasi kuhusu utekelezaji wake ikiwa mambo fulani fulani hayatachambuliwa kwa undani sana. Mmoja wao ni Profesa Lipumba, msomi mahiri wa uchumi na kiongozi wa chama cha CUF ambacho kina nguvu sana hapa nchini. Waomi wenzakewanatofautiana naye kuhusu masuala fulani lakini wanakubaliana naye kuhusu utata uliopo ndani ya Rasimu hasa masuala ya mapato, matumizi, uchumi, ulinzi na usalama, fedha n.k. Yeye angalau hatuhumiwi na Ndugu Massawe kwa kutumia usomi wake kulinda maslahi ya vyama vya siasa kwa sababu ameamua kuwa msomi na mwanasiasa. Lakini pia wapo wasomi ambao wana hoja nzito na za kibunifu ambazo zinaweza kutumika kuusuka upya muungano kwa kuwa na muundo wa serikali moja au serikali mbili kulingana na mahitaji ya sasa na historia ya muungano wenyewe. Wasomi hawa hoja zao hazijadiliwi kwa kina badala yake wanahusishwa na misimamo ya makundi ya kivyama au vinginevyo. Wasomi wanaopendekeza serikali mbili zilizoundwa kwa ubunifu ndiyo wanaoshukiwa zaidi kuliko wale wanaopendekeza serikali moja. Kisa? msimamo wa CCM ni serikali mbili na msomi wa kweli lazima akubaliane na mapendekezo ya serikali tatu kama yalivyo kwenye Rasimu. Tena wengine wanaitwa waongo na wanaowatuhumu ni watu amabao hawana uthubutu wa kuthibitisha tuhuma zao kwa ushahidi. Hali hii ilitarajiwa na ni kati ya matunda mabovu ya mchakato wa Katiba ambao haukubuniwa kwa ustadi na uangalifu.Makosa yaliyoko ndani ya mchakato ndiyo yanatutafuna. Ni muhimu kwa wasomi kuendelea kupaza sauti za kuwaunganisha wananchi badala ya kulaumiana bila ushahidi tena kwa misukumo ya kishabiki tu au hisia. Tujenge hoja bila kushutumiana na pia tujadili hoja badala ya kuhangaika na hesabu za serikali. Muundo wa muungano ambao utawapa nafasi wananchi kuamua namna ya kujitawala bila kuingiliwa na mabeberu wala vibaraka wao ndiyo unaotakiwa na wananchi. Muundo wa Muungano ambao utaendelea kuwaunganisha wavujajasho wa pande mbili za muungano ndiyo unaowafaa wananchi. Muundo wa Muungano amabao hautazua migogoro hatarishi ya kuvunja muungano ndiyo mwafaka. Mijadala yetu ielekezwe huko hata kama hatimaye uamuzi utakuwa ni muungano wa serikali moja, mbili, au tatu. Kung\\’ang\\’ania muundo wa Muungano ni utovu wa uwajibikaji kwa umma.Jambo la tatu ni kwamba makosa yaliyoko kwenye mchakato hayawezi kusahihishwa sana. Makosa hayo ndiyo chimbuko la hoja zinazotolewa na wananchi na wasomi kupewa majibu mepesi mepesi na wakati mwingine kwa kejeli na kebehi. Mchango wa wasomi katika hili ni kuziepuka siasa hizi. Hoja za kisomi zihojiwe, zikosolewe na zikataliwe kwa hoja na kwa nidhamu ya kimapinduzi.

  • Namshukuru ndugu Bashiru kwa kujitolea tena kutetea kwa kirefu kura ya wazi itumike badala ya siri kwenye maamuzi yote husika kwenye utunzi wa Katiba mpya ndani ya Bunge la Katiba.
   Hata hivyo, utetezi wake huo bado hauridhirishi hata kidogo kwani haukutofautisha kura ya wazi inafaa au haifai itumike kwenye mazingara yapi na ya siri inafaa itumike au isitumike kwenye yapi, na faida dhidi ya hasara zitakazotokana na matumizi ya kura ya wazi badala ya kura ya siri kwenye maamuzi yote yahusuyo utunzi wa Katiba mpya ndani ya Bunge la Katiba.
   Mimi ninatetea kura ya siri itumike badala ya kura wazi ndani ya Bunge la Katiba kwa sababu karibu kila mjumbe ndani ya Bunge hilo ni sehemu ya makundi tofauti ndani ya nchi Muungano Tanzania kitaasisi, kidini, kisiasa, kinchi, n.k; na baadhi ya wajumbe wakiwa wameingia Bungeni na mashinikizo ya baadhi ya makundi yao ya kuzingatia maslahi ya makundi hayo dhidi ya yale ya nchi Muungano kwenye kura zao.
   Kwenye mazingara kama hayo kura ya wazi itafanikisha agenda za baadhi ya makundi dhidi ya ile agenda inayotakiwa kuwa ya wote na makundi yote ndani ya nchi Muungano Tanzania pale baadhi ya wajumbe watakaposhindwa kupiga kura kwa kuzingatia maslahi ya nchi Muungano kutokana na uwazi kuweza kusabisha waadhibiwe na/au kutengwa na makundi yao hapo baadaye kutokana na kuyaasi kwenye kura zao.
   Mara nyingi kura ya wazi ni hatari na isiyofaa pia kwa sababu huwezesha makundi yatumie rushwa ili kuhakikisha maslahi yao yanazingatiwa dhidi ya yale ya nchi Muungano kwenye upigaji kura ndani ya Bunge la katiba kwani huwezesha kuhakiki kila aliyepokea rushwa anatekeleza matakwa ya makundi dhidi ya nchi Muungano kwa sababu kura zote ziko wazi.
   Kura ya siri inazima matumizi ya rushwa kwa sababu ni vigumu kuhakiki aliyepokea rushwa atatekeleza matakwa ya makundi dhidi ya yale ya nchi Muungano na hivyo mjumbe kuweza kupokea rushwa lakini kutokana na ukomavu wa kizalendo alionao na usiri wezeshi kwenye kupiga kura akaamua kuzingatia maslahi ya nchi Muungano anayoposhwa kuzingatia dhidi ya yale makundi yanayotumia rushwa ndani ya Bunge la Katiba.
   Hata hivyo nakubaliana na ndugu Bashiru mia kwa mia kwamba ni muhimu majadiliano yote yanayopelekea kufanyika maamuzi mbali mbali husika kwenye utunzi wa katiba mpya Bungeni yakawekwa wazi na kwa umakini wa hali ya juu kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwa wananchi kwani ufahamu wa yote kwenye majadiliano na maamuzi kwenye utunzi wa Katiba mpya ndio wezeshi kwa watanzania kupiga kura ya kuikubali au kuikataa katiba mpya kutokana na ufahamu wa kutosha kuhusu ubora wa yaliyomo.
   Wanachotakiwa wananchi wafahamu ni kwa kiwango gani michango inayokinzana ya wajumbe kutoka makundi mbalimbali ilivyozingatiwa kwenye kufanikisha Katiba mpya kwa njia ya demokrasia ya majadiliano na makubaliano yanayohusisha makundi yote ndani ya Bunge la Katiba.
   Kuwezesha ushiriki wa makundi yote kwenye majadiliano yahusuyo vipengele mbali mbali ndani ya Katiba mpya na mazingara mazuri ya upigaji kura yasiyokuwa wezeshi kwa rushwa kutumika au maslahi ya makundi kuzingatiwa dhidi ya yale ya nchi Muungano kutokana na uoga wakati wa upigaji wa kura ndiyo muhimu sana kwenye kuhakikisha hoja zote zitakazochangiwa na makundi mbali mbali zimezingatiwa ili kuhakikisha Katiba mpya ni ya wote na makundi yote ndani ya Bunge la Katiba.
   Wajumbe huwa wanaingia Bungeni wakiwa na hoja kinzani kutoka makundi mbali mbali wanayowakilisha kuhusiana na Rasimu ya Katiba mpya iliyoandaliwa na Tume ya Warioba na kinachotarajiwa kwenye majadiliano ya pamoja Bungeni ni kuzingatia hoja zote kinzani kwenye majadiliano na maamuzi ya pamoja kuhusu ni hoja zipi zenye maslahi kimuungano na ni vipi zote zinaweza kuzingatiwa kwenye kuboresha Rasimu ya Katiba mpya ili kuwezesha upatikanaji wa Katiba mpya inayokidhi matakwa ya makundi mengi zaidi na kwa haki ndani ya Bunge la Katiba na Muungano Tanzania kwa ujumla.
   Wasomi wanaweza sana kuwezesha upatikanaji wa Katiba nzuri na ya wote pale watakapodhubuti kuzingatia umuhimu wa kutumia kikamilifu uhuru wao wa kutafakari kwenye kubaini kasoro kwenye Rasimu ya Katiba mpya, athari zake na njia bora za kukabiliana nazo ili kuwezesha Katiba nzuri na ya wote ipatikane bila kujaji baadhi ya makundi hayatafurahishwa. Nmejaribu kuchangia kwa njia hiyo kwenye mada yangu inayopatikana kwenye hapa: https://db.tt/g5OxwAXs

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box