TANZANIA! TANZANIA

TANZANIA! TANZANIA[1]

Na Mwalimu Julius. K. Nyerere

 

Niliuliza mwanzoni:

Sera hii ni ya nani?

Serikali kuwa tatu

Hapa Tanzania kwetu?

…..

Ye yote mwenye akili

Asiyekuwa jahili,

Sera hii anajua

Itavunja Tanzania.

 

Wanajua wanavunja,

Na kusema kwa ujanja

Tanganyika kujitenga

Si kuvunja, ni kujenga.

 

Ati “ndani ya Muungano”,

Tudhanie ni maneno

Ya uwezo wa hirizi

Kukinga maangamizi.

 

Misingi mkishavunja,

Msidhani kwa ujanja

Nyumba mtashikilia,

Ikose kuwafukia.

 

Kwanza fikiri gharama

Zitobebwa na kauma:

Hizi serikali mbili

Sasa twaona thakili,

Sembuse zikiwa tatu?

Wataweza watu wetu?

 

 

Nakiri Wazanzibari

Katiba waliathiri,

Nilidhani kazi yetu

Ni kuwabana wenzetu,

Viongozi wa Zanzibar,

Waiheshimu Katiba.

 

Lakini ni Serikali

Ambayo haikujali,

Na kitendo kama hicho

Ikakifumbia jicho,

Na kuanza kufokea

Wale waloikemea.

 

 

Wala kuvunja Katiba

Kuvunja Nchi si tiba.

 

Hivi wakifanikiwa

Na nchi wakaigawa,

Kumbe hawataandika

Katiba ya Tanganyika?

 

Wataacha utawala

Uwe shaghalabaghala?

Na kama ikiandikwa,

Katu haitakiukwa?

 

Endapo itatukia

Nayo ikavunjwa pia,

Tanganyika itengane,

Wapate nchi nyingine?

 

Wanaovunja sharia

Na Katiba Tanzania

Dawa ni kuwashitaki

Waadhibiwe kwa haki:

Nchi yetu kuigawa

Ni uhaini, si dawa.

 

 

Tanzania yetu ina

Watu aina aina:

Inao hao Wapemba

Watachomewa majumba,

Sera hii ikipita

Bila ya kupigwa vita.

 

Lakini ina Wahaya,

Na Wasumbwa na Wakwaya,

Ina Waha na Wamwera,

Na Wakwavi, na Wakara.

 

Ina Anna ina Juma,

Ina Asha ina Toma,

Kadhaka ina Pateli,

Na wengine mbali mbali.

 

Uhasama ukipamba

Mkafukuza Wapemba,

Anojua ni Manani

Mbele kuna mwisho gani.

 

 Hivi mnavyofikiri,

Wenzetu Wazanzibari

Walitokea mwezini

Kuja hapo visiwani?

 

 

Visiwani humo humo

Wamakonde, Wazaramo,

Wanyamwezi na Wamwera;

Na mbari nyingi za Bara.

 

Walotoka Arabuni

Waliondoka zamani,

Walobaki ni wenzetu,

Raia wa Nchi yetu.

 

Mzaramo wa Unguja

Akizuiliwa kuja

Kuishi Darisalama,

Nambieni Msukuma

Mgogo au Mngoni

Aruhusiwe kwa nini.

 

Na Mchagga watamwacha?

Na Muha na kina Chacha?

 

Mwajuma wa Zanzibari

Mkimwona ni hatari,

Hivi Juma wa Pangani

Ana uhalali gani?

 

Na Shabani wa Kigoma?

Na Fatuma wa Musoma?

 

Na vita vya uhasama

Vitapamba nchi nzima:

Hawa fukuza hawa

Kwa udini na uzawa,

Yalo Yugoslavia

Yatufike Tanzania.

 

Chuki hizi msidhani

Hazina udini ndani,

Maana behewa hili

Lina watu wa kila hali.

 

Wamo na maaskofu,

Na mashehe watukufu:

Na wasomi wa sharia,

na wachumi wetu pia,

Kila mtu ana lwake,

Anazo sababu zake.

 

 

Hizi pilika pilika

Za kutenga Tanganyika

Ni kutafuta nafasi

Za kupata Uraisi

 

..

Tanganyika mnadhani

Ina mvutano gani

Wenye nguvu kuzidia

Umoja wa Tanzania?

 

Wa Pwani na wa Unguja

Mkiona si wamoja,

Mtawaona wa Mtwara

Ni wamoja na wa Mara?

 

Wa Pemba mkiwatenga

Na ndugu zao wa Tanga,

Mtaacha wa Tabora

Wadumu na wa Kagera?

 

Wafipa wa Sumbawanga,

Na Wasegeju wa Tanga,

Wawetenge Waunguja,

Wao wabaki wamoja?

 

Hivi Waha wa Kigoma

Na Wakurya wa Musoma

Na Wazaramo wa Pwani

Watabaki majirani?

 

Msidhani Tanzania

Si sawa na Somalia,

Ati mtaitabanga,

Msihiliki kwa janga.

 

 

Kikao mchanganyiko

Cha Dodoma huko huko,

Kimesema wazi wazi

Kuwambia Viongozi:

 

“Serikali kuwa mbili

Si sera ya Serikali,[1] Chanzo: Julius.K.Nyerere (1993.Tanzania! Tanzania, Dar es Salaam, Tanzania Publishing House

2 thoughts on “TANZANIA! TANZANIA

 1. Sanaa ya ushairi nayo ina nafasi kubwa katika uwasilishaji wa fikra na hoja hasa wakati wa mjadala unaohusu mustakabali wa nchi na maslahi ya tabaka la wavujajasho. Mwalimu Nyerere alikuwa mshairi mahiri na maarufu. Inhagawa utenzi huu wa Mwalimu Nyeyere ulichapishwa mwaka 1993 bado una ujumbe mzito sana hivi sasa (2014) hasa katika kipindi hiki ambapo misuguano mikali ya kiimani, kiitikadi na kimitazamo ndiyo inatawala mjadala kuhusu aina bora ya mfumo na muundo wa Muungano ndani na nje ya Bunge Maalum. Mwalimu alitumia mtazamo wa umajumui wa Afrika kutetea uwepo wa Muungano wa Tanzania. Udini, ukabila wa kitanganyika na kizanzibari, uchoyo wa vyeo na mali pamoja na ubaguzi wa rangi ni dalili za ugonjwa mbaya ambao kiini chake ni mfumo kandamizi na wa kinyonyaji ulioasisiwa na wakoloni na sasa unaendelezwa na mabeberu wa utandawazi wakisaidiwa na vibaraka wao. Wanaoeneza gonjwa hili hawakuzaliwa hivyo bali waliambukizwa kupitia katika taasisi za dola, elimu, dini, siasa, uchumi na jumuiya za kijamii. Tiba ya gonjwa hili ni mfumo mbadala ambao dira yake ni ukombozi. Umoja ndiyo nyenzo ya kuendesha mapambano dhidi ya mfumo huu kandamizi. Naomba na mimi nitumie sanaa ya ushairi kumuunga mkono Mwalimu kutetea muundo wa Muungano wa serikali mbili. Shairi hili limechapishwa katika kijitabu cha Mhadhara wa Profesa Issa Shivji aliyoutoa 2013 katika Chuo Kikuu Cha DSM. Kwa maoni yangu, mhadhara huo ‘Utatanishi na Ukimya katika Rasimu ya Katiba’ una hoja muhimu za kuchochea tafakuri kuhusu muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba. Nashauri moderator auweke mhadhara huo ndani ya baraza hili ili ujadiliwe

  UMOJA HAUWI TUNU, KABLA YA UKOMBOZI

  1. Naialika kaumu, tutafakari pamoja,
  Kuhusu Tunu muhimu, Rasimu ilizotaja,
  Kati ya Tunu adhimu, mojawapo ni Umoja,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu

  2. Umoja hauwi Tunu, Kwa taifa tegemezi,
  Bali umoja ni Tunu, baada ya Ukombozi,
  Umoja hasa ni mbinu, ya kuunda Mapinduzi,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu.

  3. Uchumi wa nchi yetu, ni uchumi tegemezi,
  Na hasa kilimo chetu, siyo cha kimapinduzi,
  Na pia elimu yetu, ni chombo cha Ubaguzi,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu.

  4. Tanzania nchi yetu, sasa haina amani,
  Uhuru na utu wetu, kwa sasa viko rehani,
  Fikra na mila zetu, havina tena thamani,
  Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu,

  5. Tutafakari maoni, ya waliotangulia,
  Ya Nyerere na Fanoni, Karume na Bi Titi pia,
  Umoja walithamini, hoja waliujengea,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu.

  6. Umoja tunoutaka, siyo uliopo sasa,
  Huu umoja wa sasa, ni Umoja wa mikasa
  Mikasa ya kisiasa, na hila za wenye pesa,
  Kabla ya ukombozi, Umoja hauwi Tunu.

  7. Umoja si mapatano, baina ya wala tonge,
  Umoja si mikutano, ya Jangwani na Kisonge,
  Umoja ni Muungano, wa tabaka la wanyonge,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu,

  8. Umoja sio ubia, wa mitaji ya ‘mabwana’,
  Umoja ni Ujamaa, wa watu wasonyonyana,
  Umoja kwa wenye njaa, ni nyenzo muhimu sana,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu.

  9. Mhimili wa Umoja, ni dira ya Ukombozi,
  Na adui wa Umoja, ni mifumo kandamizi,
  Na kitanzi cha Umoja, ni sera za kibaguzi,
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu.

  10. Tunataka Ukombozi, wa fikra za wanyonge,
  Tunataka Mapinduzi, ya uchumi wa wanyonge,
  Tunataka mageuzi, ya Umoja wa wanyonge
  Kabla ya Ukombozi, Umoja hauwi Tunu

 2. I have checked your page and i’ve found some duplicate content, that’s why you don’t rank high in google,
  but there is a tool that can help you to create
  100% unique articles, search for: Boorfe’s tips unlimited
  content

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box