Ujenzi wa uchumi wa kitaifa

Na Issa Shivji.

Mada hii iliwasilishwa mara ya kwanza katika kongamano lililoandaliwa na Mradi wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) mwaka 2006

Utangulizi

Lengo la mada hii ni kujaribu kuelewa kwa undani mwelekeo wa uchumi wetu katika ujumla wake. Katika sehemu ya pili nimechambua kwa muhtasari kiini cha sera za kiuchumi ambazo tumezifuata katika nyakati mbali mbali tangu tupate uhuru. Nia ya sehemu hii sio kuainisha au kukosoa sera za kiuchumi kwa msimamo wa mchumi bali ni kuelewa mielekeo ya jumla kwa msimamo wa siasa-uchumi (political economy). Hoja yangu ni kwamba tukitaka kuelewa mwelekeo wa uchumi wowote ule kwa undani wake hatuna budi tuuchambue mwenendo wa uzalishaji wa ziada na ulimbikizaji wa mtaji (processes of production and accumulation of surplus). Uchambuzi wa uzalishaji na ulimbikizaji wa ziada ndio umeniwezesha kuainisha sifa kuu za uchumi wa kikompradori, dhana ambayo nimeifafanua zaidi katika mada hii. Uchambuzi wangu wa uchumi wa kikompradori kwa upande wake umenisaidia kuelewa na kuainisha masharti na mazingira ya ujenzi wa uchumi wa kitaifa ambao naujadili katika sehemu ya tatu.

I: Asili ya Uchumi wa Kikompradori

Uchumi wa Kikoloni

Historia ya Tanzania bara[1] ni mfano kamili wa uchumi wa kikoloni. Uchumi huo ulijengwa kwa matakwa ya mtaji wa kikoloni pamoja na sababu za kiutawala za dola la kibeberu la Uingereza. Sifa zote ambazo huambatanishwa na uchumi wa kikoloni zilikuwepo katika uchumi wa Tanzania. Uchumi ulitegemea zaidi sekta ya mashamba makubwa kwa upande mmoja, na wakulima na wafugaji wadogo, kwa upande mwingine. Maliasili kama madini zilimilikiwa na mtaji kutoka nje ukitegemea sana mishahara midogo ya manamba ambao waliishi maisha duni. Sekta ya viwanda ilikuwa ndogo. Kilimo kilikuwa cha kuzalisha malighafi na bidhaa kwa ajili ya masoko ya nje. Kwa hivyo, kwa ujumla, maendeleo ya njia zote za mawasiliano hususan barabara na reli zilitumika kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za asili nje ya nchi na kuingiza bidhaa za viwandani ndani ya nchi.

Uti wa mgongo wa uchumi ulikuwa biashara ya kimataifa ambayo ilipewa kipaumbele katika ugawaji wa huduma takribani zote za kiuchumi. Mabenki na taasisi zingine za fedha zilitoa huduma zaidi kwa sekta ya biashara. Biashara ilikuwa sio tu kiungo kati ya mahala pa uzalishaji na utumiaji (ambayo ni kawaida) lakini pia ilikuwa njia kuu ya unyoyaji wa thamani-ziada (surplus-value). Ingawa njia kuu ya uzalishaji ilikuwa kilimo, kwa mantiki ya uchumi wa kikoloni, sekta iliyothaminiwa zaidi kiutawala na kihuduma ilikuwa sekta ya biashara. Kwa maneno mengine, biashara ndio ilikuwa mahala pa ulimbikizaji wa mtaji. Na katika sekta ya biashara yenyewe, biashara ya nchi za nje ndio ilikuwa yenye thamani zaidi kuliko biashara ya ndani kwa sababu ziada iliyozalishwa nchini ilijikuta ikilimbikizwa nje ya nchi. Biashara ya nje ndio ikawa njia ya kuwezesha mtindo huo kuendelea (Coulson 1982).

Baada ya vita ya pili, kwa sababu mbali mbali ambazo hakuna haja ya kuzieleza hapa, sekta ya viwanda ilipanuka kiasi. Viwanda vingi vilikuwa vya kutengeneza bidhaa za anasa (bia, sigara n.k.) au bidhaa za kati kama makopo, rangi za nyumba n.k. (ang. Rweyemamu 1973). Kwa ufupi, uzalishaji viwandani haukulenga kwenye mahitaji ya walio wengi (mass consumer goods) au kukidhi matakwa ya sekta za uzalishaji (productive sectors) (Tschannerl 1974).

Kwa ufupi basi, mfumo wa uchumi wa kikoloni ukawa vertically integrated economy, yaani uchumi ambao sekta zake hazina uwiano wa ndani (Shivji 1976). Mchumi mmoja amewahi kueleza uchumi kama huo kwa usemi kwamba bidhaa au mazao yanayozalishwa hayatumiki nchini na yale yanayotumika hayazalishwi nchini (Thomas 1973). Hii ndio sifa mojawapo ya uchumi-tegemezi ingawa, kama nitavyoeleza baadaye, sio sifa pekee.

Uchumi tuliorithi wakati wa uhuru ulikuwa uchumi wa kikoloni kama nilivyoeleza hapo juu. Uchumi huo hatuwezi tukauainisha kama uchumi wa kitaifa au uchumi ambao chimbuko lake ni ndani ya nchi. Ukuaji, upanuzi au maendeleo ya uchumi kama huo hutegemea masharti na mazingira yasiyo chini ya udhibiti au uwezo wa nguvu za nchi.

Uchumi baada ya Uhuru

Uhuru ulikuwa kuhamisha nguvu za kisiasa kutoka katika dola la kikoloni na kuziweka mikononi mwa dola huru. Ingawa utawala ulikuwa chini ya wazalendo hii haikumaanisha kwamba uchumi pia ungehamia moja kwa moja kuwa chini ya nguvu za kitaifa. Ukweli ni kwamba – labda bila kukusudia – sera mbali mbali za kiuchumi zilizofuatwa baada ya uhuru ziliendelea kukuza mahusiano ya kitegemezi.[2] Kwa njia moja au nyingine nafasi ya biashara ya nchi za nje iliendelea kuchukua nafasi ya kipekee katika uchumi; kilimo pamoja na kudekezwa kisiasa jukwaani hakikupewa kipaumbele kivitendo.

Tangu tupate uhuru tunaweza kuainisha sera mbali mbali za kiuchumi zilizotawala nchini chini ya mielekeo mitatu. Mielekeo hii ni :-

 1. Mtazamo wa kisasa yaani modernisation;
 2. Mtazamo wa kidola yaani statisation; na
 3. Mtazamo wa kiliberali yaani liberalisation.

(1) Mtazamo wa Usasa (modernisation)

Sera za maendeleo kwa mtazamo wa Usasa zilienda sambasamba na dhana kwamba nchi za Afrika bado ni changa. Dhana hii ilisisitiza kwamba, ni mara ya kwanza katika historia ya nchi za Kiafrika kupata fursa ya kujenga mataifa yao ambayo hayatakuwa na muundo wa kikoloni na hata jamii zao hazitajengwa kwa misingi ya kikabila. Kwa hiyo, wasomi hasa wale wa nchi za Magharibi, waliona kwamba lengo kubwa la nchi hizo na serikali zao ni kuleta mabadiliko ya kisasa katika nyanja mbali mbali za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Kwa ujumla, wachambuzi hao walidai kwamba uduni wa maendeleo (backwardness) katika nchi hizo unasababishwa na desturi na tabia za kijadi ambazo hudidimiza ari, moyo na mwelekeo wa kuchuma. Badala yake jamii za kijadi huthamani zaidi mahusiano ya kiuchumi ya kufadhiliana (economy of affection) (Hyden 1983).

Nadharia na itikadi za usasa zilidai kwamba uchumi wa nchi za Afrika – ukiachia labda zile za Kiarabu na Afrika Kusini – uligawanyika katika sehemu mbili kubwa: sehemu ndogo ambayo iliendelea katika hali ya kisasa (modern economy) na sehemu kubwa hususan vijiji ilikuwa nyuma sana kimaendeleo (traditional economy). Na hapakuwepo uwiano kati ya sehemu hizo mbili. Kwa hiyo, ili kuleta maendeleo kulikuwa na haja ya ‘kuiburuza’ sehemu iliyo nyuma na kuiweka katika hali ya kisasa. Kwa kuwa nchi hizo hazikuwa na wenye-mitaji, serikali zingeweka mazingira ya kisiasa na kijamii ambayo yangeweza kuvuta wawekezaji kutoka nje. Kwa upande mwingine pia kulikuwa na haja ya kuwa na dola zenye nguvu na uwezo wa kulazimisha watu wake kutekeleza sera za kisasa.

Kuna mengi yameandikwa kukosoa itikadi ya kisasa. Mijadala ya miaka ya sitini na sabini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilijaribu kuonyesha kwamba itikadi ya kisasa ilikuwa na upungufu mkubwa kinadharia na katika hali halisi (Rodney 1972; Shivji 1990). Si nia yangu kurudia mijadala ya wakati ule. Tatizo moja kubwa la uchambuzi wa wananadharia wa kisasa lilikuwa kwamba hawakuangalia historia ya kutokuendelea kwa nchi hizo kwa upande mmoja, na nafasi ya uchumi wao katika jumuiya ya ubepari wa kimataifa, kwa upande mwingine. Wasomi wenye mtazamo wa kimaendeleo walionyesha kwamba tukiangalia kihistoria hali ya kutokuendelea kwa nchi hizo ilitokana na ukweli kwamba nchi hizo zilivamiwa na nchi za kibeberu kuanzia karne ya 18. Chini ya enzi zile za biashara ya watumwa bara la Afrika lilipoteza ‘rasilimali’ yake kubwa, yaani raslimali watu. Pamoja na hayo, jamii za Kiafrika zilisambaratishwa kupita kiasi. Hakuna bara lolote duniani – pamoja na nchi za Kiasia ambazo ziliwahi kutawaliwa na wakoloni – ambalo lilipata kupoteza watu wake kiasi hicho.[3]

Baada ya utumwa kilifuata kipindi cha ukoloni ambacho kiliweka miundo ya kiuchumi na kisiasa ambayo ilifanikisha mitaji ya kikoloni kunyonya raslimali za nchi hizo. Ukoloni haukuja Afrika kuendeleza jamii zetu bali kuzinyonya. Huu ndio ukweli na uwazi kuhusu ukoloni.[4] Suala lenyewe sio kulaumiana bali kuelewa kwa undani wake kwa nini tulijikuta katika hali ya kutawaliwa na kunyonywa.

Mijadala hii iliendelea kueleza zaidi kwamba hali hii ya kihistoria haikusitishwa na uhuru wa bendera. Yaani kupata uhuru wa kujitawala hakukuwa na maana ya ukombozi wa kitaifa wala wa kijamii. Uchumi wa kibepari wa kimataifa uliendelea kutawaliwa na nchi chache za kibeberu. Nchi za dunia ya tatu zimejikuta katika hali ya kutokuwa na uwezo wa kuzuia unyonyaji wa mabeberu kiasi kwamba juhudi na jasho la wananchi wao kuleta maendeleo vinaishia kwenye kuwanufaisha mabepari wa nje na kwa kiasi fulani vibepari uchwara wa ndani. Pamoja na sera mbalimbali za nchi za Afrika kuleta maendeleo, ukweli unabaki kwamba, kisiasa, watawala wapya wa Afrika baada ya uhuru ama hawakuwa na uwezo au nia – au yote mawili – kujikomboa kutokana na makucha ya ubeberu uliotawala mfumo mzima wa uchumi wa kimataifa.

Makelele yalipigwa katika vikao vya kimataifa hasa na viongozi wa dunia ya tatu ambao walisukumwa na uzalendo wao. Hata hivyo walio wengi kati ya viongozi hao hawakuwa na mwelekeo zaidi ya ule wa kujinufaisha wenyewe na matabaka ya vibwanyeye. Upeo wa mada hii hauniruhusu kuelezea zaidi hali ya kijamii katika sura yake ya kitabaka ilivyokuwa baada ya uhuru barani Afrika.[5] Labda nigusie tu kwamba nchini mwetu itikadi za kisasa zilienea kwa kiwango kikubwa katika sera mbalimbali zilizofuatwa (Coulson 1982). Nitataja mifano miwili tu ya kuonyesha jinsi itikadi hii ilifanya kazi katika ngazi ya sera.

Itikadi ya usasa ilikuwa chimbuko la sera ya vijiji vya kisasa na ufugaji wa kisasa. Madhumuni ya Sheria ya Vijiji ya 1964 yalikuwa kuwezesha wakulima wachache wateule kuhamishiwa katika vijiji vya kisasa; wakapewa huduma za kitaalamu na wakafundishwa njia za uzalishaji wa kisasa ili hatimaye waweze kuwa mfano wa kuigwa kwa walio wengi. Lengo la mpango huu lilikuwa kwamba maendeleo kwa wakulima walio wengi yangekuja kwa kutiririka kutoka juu (trickle down effect). Hata katika ufugaji, Wamaasai wakahamishiwa katika ranchi ambazo ziliongozwa na menejimenti ya kisasa.

Kwa ujumla miradi hii yote miwili ilibuniwa, kupangwa, kutekelezwa na kuendeshwa bila kujali ushirikishwaji na busara za wakulima au wafugaji wenyewe. Wataalamu walijifanya wajuaji na kujigeuza kuwa watawala, na wazalishaji wa kawaida walifanywa kama waajiriwa au walowezi ambao hawana uchungu na miradi yenyewe. Haishangazi kuambiwa kwamba miradi hii haikufanikiwa hata chembe na kwamba sera za usasa zilipoteza hadhi na zikafa hivi hivi (Cliffe na wengine 1968).

(2) Mtazamo wa Kidola (statisation)

Sera za kuingiza dola katika mambo ya uchumi na kijamii huainishwa kuwa nguzo mojawapo ya itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea. Hii ni kweli kwa kiasi fulani tu, labda kiasi kidogo kuliko kinavyotangazwa na wasemaji wasiopenda ujamaa. Ingawa udolashaji (statisation) wa uchumi ulihalalishwa na sera za Azimio la Arusha mnamo mwaka wa 1967, msukumo ulioleta sera ya kuingiza dola katika uchumi haukutokana na itikadi ya kijamaa bali ulitokana zaidi na itikadi za uzalendo wa kiuchumi (economic nationalism) kama alivyodai Mwalimu Nyerere mwenyewe katika moja ya hotuba zake (Nyerere 1968: 262-3). Hali halisi ya kutokuridhika na sera ambazo zilitoa kipaumbele kwa wawekezaji wa nje pia ilichangia. Mtaji uliotarajiwa kutoka nje chini ya sera za kuvutia na kukuza uwekezaji wa nje hazikufua dafu. Kama anavyoonyesha Rweyemamu, kati ya mwaka 1961 na 1965, mtaji zaidi ulitoroshwa nje kuliko ule ulioingizwa nchini (Rweyemamu 1973: 44).

Pili, sera za mwelekeo wa usasa zilionesha waziwazi udhaifu wake kutokana na kutokufanikiwa hasa katika sekta ya kilimo na ufugaji kama nilivyoonyesha hapo awali. Tatu, pamoja na utaifishaji wa njia kuu za uchumi uliofuata Azimio la Arusha, ukweli ni kwamba dola ilianza kujiingiza katika uchumi hata kabla ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Isitoshe hatuna budi tuelewe kwamba hakuna dola iliyokuwa inajiingizaingiza katika uchumi (interventionist state) zaidi kuliko ile ya kikoloni. Na tabia na desturi hii ya dola ya kikoloni iliendelea hata baada ya uhuru.

Ukoloni haukufuata busara za kiliberali za soko huria ingawa siku hizi nchi za kibeberu zinatufanya tuimbe nyimbo za soko huria kama kasuku. Kama nitakavyoeleza baadaye katika mada hii, chimbuko la makosa ya sera za ujamaa sio kuiingiza mno (au kutokuiingiza vya kutosha) dola katika uchumi bali ni namna ya kufanya hivyo.

Ingawa sera za Azimio la Arusha hazikutia mkazo sana uwekezaji wa nje, hii haikuwa na maana kwamba mwelekeo wa kiuchumi ulibadilika sana. Mwelekeo uliendelea kuwa ule ule wa utegemezi kwa kuchukua zaidi sura ya ‘misaada’ badala ya uwekezaji. Nitaeleza. Kinyume na itikadi ya kujitegemea, ambayo ilikuwa kama pacha wa itikadi ya ujamaa, misaada – mikopo na ruzuku – kutoka nje katika miaka sita baada ya Azimio la Arusha ilikuwa mara tatu zaidi ya ile iliyokuwa inapokelewa miaka sita kabla ya Azimio (Shivji 1976: 160). Mwishoni mwa miaka ya 70 na kuendelea, mikopo kutoka mabenki na makumpani ya kimataifa ilianza kuongezeka. Mnamo mwaka wa 1994 Tanzania ilikuwa na deni la karibu dola za Marekani bilioni 6.3, yaani kila Mtanzania – akiwemo mtu mzima na mtoto mchanga – alikuwa na deni sawa na pato lake la miaka miwili! (Daily News, 1/10/94) Hii ina maana kwamba licha ya uchumi kuwa tegemezi kupita kiasi, hata kisiasa na kimawazo, uhuru wa Watanzania wa kujiamulia sera zao na hatima yao umepungua kwa kiasi kikubwa sana. Inawezekana wako wanasiasa na viongozi ambao hawajali jambo hilo ili mradi waendelee kuvishwa kilemba cha ukoka eti kwa kufanikisha sera za soko huria. Lakini pia wako viongozi wengine ambao uzalendo wao na uchungu na nchi yao unawafanya wasishangilie hata kidogo hali hii ya nchi na uchumi. Kwa hiyo, kasoro ya itikadi ya kujitegemea haikuwa kwenye nia au dira yake bali ni kwenye tafsiri yake. Ukweli ni kwamba – kama nitakavyoonyesha baadae – haiwezekani kujitegemea kiuchumi ikiwa mahusiano mahususi ya uzalishaji ziada na ulimbikizaji wake yanatawaliwa na matakwa ya mtaji wa kimataifa.

Licha ya kuendelea kutegemea mitaji kutoka nje, sera na miradi mbalimbali baada ya Azimio la Arusha ilidhihirisha utegemezi wa aina nyingine ambayo ni mbaya zaidi – utegemezi wa kiteknolojia (technological dependency), kutegemea wataalamu wa nje (dependency on foreign experts) na utegemezi wa kimenejimenti (managerial dependency). Pamoja na ukweli kwamba katika nyanja nyingine hatukuwa na mbinu mbadala isipokuwa kutegemea misaada na mikopo kutoka nje, pia ni kweli kwamba katika mambo mengine mengi hatukuwa na haja wala ulazima wa kutegemea utaalamu wa nje. Kwa mfano, kulikuwa na ulazima gani wa kuajiri kampuni ya Kimarekani ya MacKinsey ili kutushauri juu ya muundo wa ‘madaraka mikoani’ (decentralisation)? Miradi mingi tu iligundulika baadae kuwa ilibuniwa na wachuuzi wa kimataifa ili kutuuzia mitambo yao ya mitumba pamoja na kuwapatia ajira wataalamu wao (mfano mzuri ni Kiwanda cha Nguo cha Mwanza – Mwatex). Lakini hayo yote tulikubali na kumezea kwa sababu ama yalikuwa katika masharti ya kupata misaada (ruzuku na mikopo) au kwa sababu wawakilishi wetu katika mapatano walipata ‘chochote’. Kwa ujumla, matokeo ya miradi kama hii ilikuwa ni kutuongezea deni la taifa kwa upande mmoja, na kutuwekea viwanda ambavyo havikuwa na uwiano – kiteknolojia, kiajira wala kisoko – kwa upande mwingine. Kama anavyosema mwandishi mmoja:

Misaada kutoka nje bila masharti yoyote ilikuwa na mchango katika muundo na tabia ya uwekezaji katika sekta ya viwanda. Kwa upande wa Tanzania mara nyingi kulikuwa na kupendelea zaidi miradi mikubwa, yenye mitaji mikubwa inayotegemea zaidi uwezeshwaji kutoka ughaibuni ili kufanikisha malengo ya miradi hiyo. Hiyo ilikuwa ni sababu nyingine ya kuhakikisha kuwa miradi hiyo inawezeshwa na wafadhili. Mfumo huu ulitokana na kuanguka kwa uchumi katika nchi zenye viwanda. Mara nyingi pia ingeweza kuwa vigumu kuzipata asasi za misaada zenye ushauri wa kitaalamu wa teknolojia ngeni kwao au wanaoweza kuleta teknolojia ngeni na inayofaa (Havnevik na wengine 1988: 80).

Kwa jumla, suala muhimu sio chaguo kati ya utegemezi au kujitegemea bali ni uwezo wa kujiamulia wapi na kwa namna gani tunaweza kujitegemea. Kwa ufupi, sifa moja wapo ya taifa tegemezi ni kwamba halina uwezo au mwelekeo wa kujiamulia mambo yake kisiasa, kisera na kijamii. Kama hiyo ni kweli basi ni wazi pia kwamba Azimio la Arusha halikuwakomboa Watanzania kutoka katika janga la utegemezi.

Katika sekta ya kilimo, sera iliyofuatwa baada ya Azimio la Arusha ilikuwa kuwahamisha wakulima wadogo vijijini kupitia operesheni mbalimbali. Hatimaye mamilioni ya wakulima walihamishiwa vijijini kati ya miaka ya 1974 na 1976. Katika operesheni hizo mambo mawili hayakuzingatiwa kabisa. Mosi, hakuna mtu au taasisi au kiongozi aliyefikiria suala la mfumo wa umilikaji ardhi. Pili, kilimo cha kulima mazao ya biashara ya nje (chakula na malighafi) hakikudadisiwa.

Kwa upande wa mfumo wa umilikaji ardhi, ilichukuliwa kwamba ardhi ni mali ya serikali kwa hivyo serikali inaweza kuamua itakavyo kuhusiana na masuala ya ardhi. Haki za ardhi za wakulima na wafugaji huko walikohama zikafutika hata bila ya kupitisha sheria rasmi. Na hakuna mfumo mpya wa haki za ardhi uliobuniwa katika vijiji vipya vilivyoundwa baada ya operesheni hizo. Matokeo yake yalikuwa kuvuruga moja kwa moja mfumo mzima wa umilikaji wa ardhi na kutoa mwanya zaidi kwa wajanja hasa kutoka mijini – wakiwemo viongozi na warasimu wa serikali, wafanyabishara na hata taasisi za serikali – kupora ardhi za wanakijiji hovyo. Uhakika wa umilikaji wa ardhi ulikosekana na wanakijiji walianza kuwa na wasiwasi kuhusu ardhi zao. Hali hiyo ilikuwa mbaya zaidi pale ambapo katika miaka ya 80 na hasa katika awamu ya pili ya uongozi maeneo makubwa ya ardhi hasa yale ya wafugaji yalimegwa na kutolewa kwa wawekezaji eti kwa ajili ya ‘manufaa ya umma’ au ‘miradi ya kitaifa’ (URT 1994 na Shivji 1994). Mwelekeo huu wa utegemezi wa kisera wa kuwapa kipaumbele wawekezaji kinyume na matakwa ya wazalishaji wa ndani unaendelea kupata msukumo wa kisiasa. Mwelekeo huu ndio kipingamizi kikubwa katika ujenzi wa uchumi wa kitaifa.

Kilimo cha mazao ya biashara kiliendelea ingawa kilianza kuonyesha kudidimia kwa sababu mbili. Katika miaka ya katikati ya 70 na kuendelea bei za mazao ya biashara zilianza kushuka sana na kusababisha pato la fedha za kigeni kushuka. Vile vile uwezo wa uchumi wa kuagiza malighafi, vipuri na bidhaa nyingine kutoka nje pia ukawa na walakini. Ndio kusema hata vile viwanda tulivyojenga kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje (import substitution industries) vikawa na matatizo ya kumudu ya uzalishaji kwa kiwango kilichotarajiwa.

Upungufu wa fedha za kigeni haukuweza kufidiwa na ongezeko katika kuzalisha mazao ya kilimo kwa sababu kilimo cha wakulima wadogo nchini hutegemea jembe, maana yake ni kwamba, uwezekano wa kuongeza uzalishaji ni mdogo sana. Pamoja na hayo, kwa sababu kilimo chenyewe huelekezwa kwenye uzalishaji wa mazao ya biashara kwa ajili ya masoko ya nje, kilimo cha chakula kwa ajili ya matumizi ya wazalishaji na soko la ndani pia kimeathirika kihistoria na kuendelea hivyo. Matokeo ni kwamba nchi ambayo inajigamba kwamba uti wa mgongo wa uchumi wake ni kilimo ndio yenyewe inakosa kujilisha. Mara kwa mara inatubidi tuagize chakula kutoka nje. Pamoja na hayo, kwa kuwa uwezo wa kuagiza na au kuzalisha bidhaa ya matumizi ya walio wengi ulididimia, wazalishaji hususani wakulima wakakosa bidhaa za motisha (incentive goods) na hivyo kusababisha ufanisi wao ushuke zaidi. Matokeo ya haya yote, kama tunavyofahamu, ni zahama ya uchumi katika kipindi kigumu sana mnamo miaka ya 80. Ni kweli kwamba sababu nyingine kama vita vya Uganda, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ongezeko kubwa la bei ya mafuta kimataifa vilichangia; na hivyo kuongeza ukali wa matatizo ya uchumi. Hata hivyo chimbuko la matatizo ya kiuchumi bila shaka ni sifa zenyewe za uchumi-tegemezi.

Kushuka kwa hali ya uchumi katika kipindi hiki pia kuliathiri sana uwezo wa serikali kumudu huduma za kijamii na kiuchumi. Huduma hizo – hasa elimu, afya, ruzuku katika pembejeo n.k. – zilikuwa nguzo moja wapo za kuhalalisha itikidi ya ujamaa kwa sababu ndio ilikuwa inadhihirisha kwa uwazi uzuri wa itikadi hiyo. Ndio maana pamoja na matatizo ya uchumi tulianza kushuhudia kuporomoka kwa uhalali wa mfumo wa kisiasa.[6] Kwa vyovyote vile serikali ililazimika, hata kabla ya Mwalimu kungatu’ka, kusalimu amri mbele ya masharti ya taasisi za fedha za kimataifa (Campbell na Stein 1992: 59.) Huu ndio ulikuwa mwanzo wa kuingia kwenye kipindi cha ulegezaji uchumi na siasa ya ukiritimba na mageuzi ya mfumo wa kisiasa.

(3) Mtazamo wa Kiliberali

Kama tujuavyo, kutokana na shinikizo la taasisi za kimataifa, Tanzania ilianza kulegeza uchumi na siasa yake kuanzia katikati ya miaka ya 80. Sina haja ya kueleza zaidi historia ya mwelekeo huo (Soma Green 1995). Lakini ni muhimu kuelewa kwa undani maana ya kulegeza uchumi katika mazingira ya uchumi-tegemezi. Kama nilivyoonyesha hapo juu, uchumi-tegemezi hutegemea sana biashara ya nje, hapo ndio hasa mahala pa nguvu zinazoendesha uchumi. Kwa hivyo, ulegezaji wa uchumi kama huo maana yake ni pamoja na:

Mosi, kufuta moja kwa moja udhibiti wowote wa biashara ya nje. Na kwa kuwa biashara ya nje huenda sambamba na shughuli zote za fedha za kigeni, hakuna shaka kwamba udhibiti wa fedha za kigeni pia nao unaondoshwa. Suala hapa sio tu kuondoa ukiritimba wa dola katika nyanja hizo nyeti kiuchumi bali pia kuinyang’anya dola nafasi ya kuratibu sekta hizo, kuwezesha mtaji wa ndani kukua. Maana halisi ya uratibu huu ni kwamba dola lisijiingize katika mambo ya biashara ya nje.

Baadhi ya matokeo ya awali kabisa ya ulegezaji wa usimamizi wa ndani ni kudidimiza na hatimaye kuua kabisa viwanda vichanga bila kujali vinamilikiwa na nani, serikali au watu binafsi, yaani mtaji wa kidola, wa kikompradori au wa kitaifa. Zoezi hilo katika nchi yetu linaonyesha kwamba viwanda ambavyo huathirika haraka zaidi ni vile vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi. Kwa mfano, viwanda vya mafuta ya kula (oil industry) viwanda vya kusindika vyakula, viwanda vya nguo na viwanda vya kutengeneza viatu vilikuwa vya kwanza kufa.

Kwa upande mwingine viwanda vinavyopata msukumo kwa kiasi fulani ni vile ambavyo huzalisha bidhaa za anasa (k.m. vinywaji na sigara). Mara nyingi sekta na shughuli ambazo hupanuka ni biashara za kichuuzi na sekta za huduma kama vile mahoteli, migahawa, maduka makubwa, na nyingine za aina hiyo. Kwa jumla, shughuli zile ambazo kimsingi sio za uzalishaji (non-primary productive activities) kwa upande mmoja, na ambazo huegemea kwenye soko finyu la vikundi vya kijamii vya hali ya tabaka la juu na wageni kutoka nje[7], kwa upande mwingine, ndizo huonyesha maendeleo. Ni kweli kwamba takwimu za kiuchumi kama zile za pato la taifa huonyesha kukua kwa asimilia fulani. Lakini swali la kujiuliza ni, je, maendeleo ya aina hii yanaweza yakaelekeza uchumi na jamii kwenye maendeleo endelevu na hatimaye kuinufaisha jamii kwa jumla?

Pili, masharti ya kufuta ruzuku zote za kiuchumi, huduma za kijamii na kuleta uwiano katika bajeti ya serikali, huwa na athari zake kwa wazalishaji wadogowadogo na wa hali ya kati kwa jumla, na hasa wakazi wa vijijini. Sina haja ya kuorodhesha athari hizo zote. Kutokana na upeo wa mada hii nisisitize tu kwamba athari mojawapo ya umuhimu wa pekee ni kwamba wakulima wenye uwezo wa kati na wa juu wa kulimbikiza mtaji nchini na kuugeuza kuwa kitega-uchumi katika sekta ya kilimo huuawa (Hadjivayanis 1987). Badala yake shughuli za aina za kichuuzi ndio hupata msukumo hata vijijini – usambazaji wa vikororo, majumba ya kufikia wageni, wachuuzi wa kununua nafaka ambao wengine ni matapeli tu, n.k.

Wachumi na wasemaji wa taasisi za kimataifa hudai kwamba uondoshwaji wa ukiritimba wa dola katika biashara ya bidhaa za kilimo na soko huria husaidia kupandisha bei za bidhaa za wakulima na kwa hiyo kuongeza pato lao. Kwa kiasi fulani hii ni kweli kwa sababu ukiritimba wa dola ulichangia sana kuhakikisha unyonyaji wa ziada kutoka kwa wakulima na hii ilidhihirishwa na tofauti ya bei kati ya ile anayolipwa mkulima na bei katika soko la kimataifa. Hata hivyo, hayo hayana maana kwamba hata kama pato la wakulima linaongezeka nyongeza hii inageuzwa kuwa vitega-uchumi katika kilimo. Ukweli ni kwamba, mosi, thamani halisi ya nyongeza ya pato lenyewe ina mushkili kutokana na mfumuko wa bei. Kwa hiyo labda anayefaidika zaidi ni mtu wa kati ambaye ana uwezo wa kuwa na fedha za kigeni lakini sio mkulima wa hali ya kati au hata hali ya juu ambaye pato lake lote ni fedha za ndani. Kwa kuwa hakuna ruzuku katika pembejeo na huduma za kijamii (k.m. afya) nyogeza ya pato la wakulima hurudi tena kwa wafanyabiashara kama malipo ya huduma hizo. Hatimaye nyongeza yoyote ya pato la wakulima kama ipo kutokana na soko huria hutoweka kwa sababu mbalimbali ambazo baadhi nimezigusia. Kwa ufupi katika sekta ya kilimo (kama ilivyo katika sekta ya viwanda) faida zinazodaiwa kutokanana na sera za soko huria kama zipo basi hazibaki kijijini kuendeleza ukuaji wa mtaji wa ndani.

Tatu, katika enzi hizi za utandawazi, muhimu zaidi kuliko biashara ya kimataifa ya bidhaa ni biashara inayohusu fedha – hususani, mabenki, bima na mifuko ya akiba ya wafanyakazi, na soko la mitaji. Ulimwenguni leo hii makampuni makubwa ya kimataifa ni yale machache ambayo humiliki na kudhibiti sekta ya fedha ya kimataifa. Chini ya makubaliano ya Uruguay (Raghavan 1990), kutoa mfano moja tu, serikali za kibeberu na ujumbe wao wa wafanyabiashara walisisitiza sana (na hatimaye kulazimisha) ulegezaji wa soko la fedha katika nchi za dunia ya tatu. Nchini mwetu pia ishara ya maana ya awali ya ulegezaji ilikuwa mabenki na hivi sasa bima iko hatarini kumezwa. Sitashangaa nikisikia kwamba watetezi wa soko huria “wanashuari” serikali kwamba hata mifuko ya akiba ya wafanyakazi (PPF na NSSF) ibinafsishwe ili, eti, kuleta ufanisi.

Kwa jumla, taasisi za fedha, ni vyanzo vikuu vya kulimbikiza mtaji vyenye umuhimu wa kipekee. Hata katika nchi zetu ambamo tunaambiwa kuna uhaba wa mtaji wa ndani, sekta hii inaweza ikawa na nafasi ya pekee ya kuchochea ulimbikizaji. Ndio maana taasisi binafsi za kimataifa huwa na uchu mkubwa wa kujiingiza katika sekta hii na wataalamu wao hushauri serikali zetu kulegeza masharti. Lakini, kwa upande wa uchumi wetu, athari za ulegezaji masharti katika sekta ya fedha ziko wazi. Akiba inayozalishwa na jasho la waajiriwa hairudi katika uchumi wa kitaifa bali ‘hutoroshwa’ na kulimbikizwa huko nje. Hali hii haitegemewi kubadilika hata chembe ikiwa wawekezaji wa nje wataendelea kumiliki njia hizo moja kwa moja au katika ubia na wazalendo. Kwa vyovyote vile ni wawekezaji wa nje ndio wadhibiti wa sekta ya fedha kwa sababu wana uwezo mkubwa wa menejimenti na ujuzi wa mfumo wa kimataifa wa fedha na ndio wenye kauli ya mwisho. Hatimaye,wawekezaji wa nje hunufaika kwa kiasi kikubwa kuliko wawekezaji-uchwara wa kizalendo.

Hoja ambayo ningependa kuisisitiza zaidi ni kwamba, ingawa inahitaji utafiti na uchambuzi zaidi, ulegezaji wa uchumi kwa upande mmoja unaendeleza mwelekeo wa utegemezi kwa mtaji wa kimataifa ukishikamana na ule wa kikompradori na kwa upande mwingine, kuweka mazingira magumu ambayo hukandamiza vichocheo vyovyote vya mtaji wa kitaifa. Hii ndio sifa maalumu ya uchumi wa kikompradori ambayo naichambua zaidi katika sehemu inayofuata.

Sifa Kuu za Uchumi wa Kikompradori (compradorial economy)

Kabla sijaanza kueleza sifa zenyewe niseme maneno machache juu ya kwa nini nimetumia maneno ‘uchumi wa kikompradori’ kuainisha uchumi kama wetu. Kwanza, ni kwa sababu sikuweza kupata neno la Kiswahili ambalo linafanana. Pili, nimetumia maneno hayo badala ya yale ambayo hukubalika zaidi, yaani ‘uchumi-tegemezi’ au ‘uchumi wa kikoloni mambo-leo’ kwa sababu neno ‘uchumi-tegemezi’ halileti maana kamilifu ya uchumi tulionao. Maneno ‘uchumi wa kikoloni mambo-leo’, pamoja na kuwaudhi sana wanasiasa, yanasisitiza zaidi hali ya siasa badala ya uchumi au siasa-uchumi (political economy). Tatu, ninatumia maneno hayo kutofautisha – na hasa kuelewa sifa kuu, kwa undani wake za – uchumi wa kitaifa na ule usio wa kitaifa, ambalo ndilo kusudio la mada hii.

Awali kabisa nieleze kwamba sera hizo zote za kiuchumi nilizoainisha – yaani zile zenye mwelekeo wa kisasa, kidola au kiliberali – kwa uchambuzi wangu zinaweza zikaainishwa chini ya uchumi wa kikompradori. Hii haina maana kwamba hakuna tofauti za maana baina ya sera hizo. Tofauti zipo na ni muhimu kuzielewa. Lakini, hoja yangu ni kwamba sera hizo hazitofautiani katika mwelekeo wake wa ulimbikizaji. Jambo hilo litaeleweka kwa ufasaha zaidi tukianza kuainisha sifa kuu za uchumi wa kikompradori.

(1) Ni wazi na imeelezwa mara nyingi tu kwamba sifa mojawapo ya uchumi wa nchi zinazoendelea ni kwamba sekta ya viwanda ni ndogo na uchumi hutegemea sekta ya kilimo (humo ninaweka ufugaji pia). Yaani, kwa maneno mengine, uzalishaji wa bidhaa za viwandani (manufactured products) ni mdogo ukilinganishwa na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Sifa hii bado ina ukweli katika nchi nyingi barani Afrika lakini imebadilika au imeanza kubadilika kwa kiasi kikubwa katika bara la Asia na Amerika Kusini. Zipo hoja kwamba wawekezaji hupendelea kuhamishia viwanda vyao katika nchi zinazoendelea kwa sababu mbalimbali zikiwemo zile za kutokumudu sheria na kanuni za kudhibiti hali ya mazingira za nchi zilizoendelea (export of ‘dirty industries’).

(2) Kunakuwa na uwiano mdogo sana kati ya sekta za uzalishaji na utumiaji na, miongoni mwa sekta ya uzalishaji wenyewe, kati ya vijisekta mbalimbali. Kwa maana nyingine, kwa usemi wa mchumi maarufu Clive Thomas, yale yanayozalishwa nchini hayatumiki na yale yanayotumika hayazalishwi humo. Na hii ni kweli, sio kwa bidhaa za kuzitumia (consumer goods) tu, bali pia kwa bidhaa za uzalishaji (producer goods). Katika mijadala ya miaka ya 60 na 70, jambo hilo lilisisitizwa sana na watetezi wa nadharia za utegemezi. Lakini ukuaji wa uchumi kama ule wa nchi za Kiasia (kama Korea ya Kusini, Taiwan, na sasa Malaysia n.k.)[8] umepunguza ukweli wake kama sifa pekee.

(3) Biashara ya nje huwa na nafasi ya kipekee katika uchumi huo. Biashara kwa jumla na bishara ya nje hasa ni mahala pa uchumaji wa haraka haraka na wenye faida kubwa. Ingawa ziada huzalishwa katika kilimo, hulimbikizwa katika sekta ya biashara. Kwa hiyo shughuli zinazoonekana kuwa na faida ni zile zinazohusu biashara na uchuuzi. Labda tuseme yule anayezalisha ziada (mkulima) hailimbikizi, na yule anayelimbikiza (mfanyabiashara ambaye ni kiungo tu) hazalishi. Vivyo hivyo sekta ya uzalishaji hukosa vitega-uchumi wakati sekta za huduma na utumiaji ndizo hupata wawekezaji kwa sababu hizi ndio sekta zenye uchumaji wa haraka haraka. Na kwa jinsi hali halisi ilivyo, mitaji midogo (wawekezaji-uchwara) hufuata faida ya haraka haraka. Kwa jumla basi sekta za uzalishaji, hasa ile ya kilimo na ufugaji, hukosa vitega-uchumi ambavyo vingeweza kuziendeleza kwa ufanisi.

Kwa sababu uchumi wenyewe hutegemea biashara za nje, wakulima huegemea zaidi kwenye kulima mazao ya biashara ya nje kuliko yale ya ndani hasa vyakula na nafaka. Kwa hiyo uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya soko la ndani hudidimia. Ni ukweli ambao haupingiki kwamba hakuna nchi yoyote – ikiwemo nchi iliyoendelea au yenye dalili za kuendelea – iliyoweza kurekebisha jambo hilo bila kuwa na sera ya makusudi kabisa ya kufanya mageuzi katika mazigira na mahusiano ya kijamii ‘vijijini’ pamoja na mageuzi katika mfumo wa umilikaji ardhi (land reform). Na ‘mageuzi’ hayo kama hayakutokana na mapinduzi ya kitabaka basi yameletwa na mageuzi kutoka ‘juu’ yaani dola yenyewe huyabuni na huyasimamia (kwa nguvu). Kwa ufupi, ninachotaka kusema ni kwamba hakuna mfano wowote wa mageuzi ya kilimo yaliyotokana na mfumo wa soko huria bila dola kuingilia kati.

(4) Wasomi wengine wamedai kwamba sifa mojawapo katika uchumi wa kikompradori ni kwamba ziada huzalishwa kwa wingi na wazalishaji wadogowadogo vijijini. Isitoshe, katika hali hiyo, mtaji hunyonya ziada kupitia njia za kibiashara, yaani, unyonyaji hujidhihirisha katika sura ya biashara badala ya uzalishaji. Ukweli huo humaanisha kwamba nafasi ya dola katika mfumo huo ni ya kipekee. Dola hutumia nguvu zake ama moja kwa moja au kupitia njia zingine zisizo za kiuchumi kuweka mazigira ambayo huwezesha unyonyaji wa aina hiyo. Kwa maneno mengine, uzalishaji na unyonyaji hauwezi kutegemea njia za kiuchumi tu kwa uhai wake bali huegemea kwenye matumizi ya nguvu za dola (Mamdani 1987).

(5) Sifa ya kiini, kwa maoni yangu, ni ile tunayopata tukichambua hali ya ulimbikizaji. Ulimbikizaji katika uchumi wa kikompradori una sifa zifuatazo:

(a) Mahali pa uzalishaji ziada na mahali pa ulimbikizaji hutengana kwa upande mmoja, na mchakato mzima wa ulimbikizaji hutegemea kanuni na masharti yasiyo na chimbuko ndani ya nchi (Amin 1990). Ndio kusema sekta inayozalisha ziada kwa wingi ndio inayokosa vitega-uchumi na ziada inayozalishwa nchini kwa wingi hulimbikizwa nje katika uchumi mwingine. Na ukweli huo haujali mtaji upi unahusika. Mtaji hufuata faida na uhakika wa mazingira ya uchumi bila kujali utaifa wake.

(b) Kwa jumla, mitaji mikubwa ya kimataifa ndio hutawala medani ya ulimbikizaji. Wenye mitaji ndio huweka (ama moja kwa moja au kupitia dola za kibeberu au taasisi za kimataifa za fedha au zote hizo) masharti, mazingira na kanuni za ulimbikizaji kufuatana na matakwa yao. Mitaji ya ndani, kwa vyovyote vile, husalimu amri mbele ya mitaji mikubwa. Wakati mwingine mtaji wa ndani hujipachika kama nyongeza ya mtaji wa nje, ndio maana halisi ya mtaji wa kikompradori.

(c) Ingawa ni kweli kwamba katika mazingira ya uchumi wa kibepari mitaji midogo midogo ya kitaifa huongezeka, mitaji kama hii hukosa mazingira ya kukua. Hatima ya mitaji hii ni ama kumezwa na mtaji mkubwa wa kimataifa na kitaifa au kujiunga na mtaji mkubwa kama “mbia mdogo”

(d) Katika kuhitimisha uchambuzi wa sifa kuu za uchumi wa kikompradori, tunaweza kusema kwamba kuna aina ya ukiritimba wa kimtaji ambao hutokana na mantiki yenyewe ya ushindani wa kibepari. Hii haizuiliki hata katika mfumo wa soko huria. Matokeo ya mantiki hiyo katika mazingira ya ubepari wa kimataifa na uchumi mchanga chini ya himaya ya ubeberu ni kwamba soko huria ndio huwa mazingira safi na ya muafaka kabisa katika kulea mwelekeo wa ukiritimbishaji wa mtaji mkubwa wa nje na wa kikompradori wa ndani. Na hii ina maana kwamba mitaji midogo ya ndani, hasa ile inayoelekea kwenye sifa ya mtaji wa kitaifa,[9] huathirika.

Katika enzi hizi za mahubiri mazuri ya soko huria, na wahisani na wasemaji-uchwara wao hufananisha ukiritimba na dola. Yaani wanafanya kana kwamba ukiritimba wa kidola ndio ukiritimba wenyewe bila kudadisi zaidi ukiritimba katika jamii na uchumi. Kwa kurahisisha maelezo magumu kidogo, niseme hivyo.

Ushindani wa kiuchumi ndio huzaa ukiritimba. Katika ushindani wa kimtaji, mitaji mikubwa humeza mitaji midogo na kuelekea kwenye ukuaji wa mtaji wa kuhodhi. Leo hii soko na uzalishaji ulimwenguni vinatawaliwa na makampuni machache ya kimataifa ambayo yanaendelea katika hali hiyo ya ukiritimba ingawa wasemaji wake huhubiri soko huria na ulazima wa kuweka medani sawa ili kuchochea ushindani. Sharti moja wapo la kuweka medani sawa, tunaambiwa, ni dola kujitoa na kuweka mazingira ya ushindani. Ukweli ni kwamba hakuna jamii yenye medani sawa na hakuna uchumi ambao hauingiliwi na dola.[10]

Maswali muhimu ya kujiuliza ni: Je, medani sawa kati ya nani na kwa ajili gani? Je, dola linajiingiza katika uchumi kwa upande gani, kumnufaisha nani na kuchochea maendeleo ya aina gani? Maswali kama haya ndio yanaweza yakatusaidia kuelewa vizuri maana halisi ya sera na mahubiri ya kiliberali; nafasi ya mtaji wa kuhodhi katika kukuuza mfumo wa kikompradori na nafasi ya mtaji wa kitaifa katika kujenga uchumi wa kitaifa, na, kwa jumla, nafasi ya dola katika maendeleo ya jamii. Sidai kwamba majibu ya maswali haya ndio ufunguo wa matatizo yote ya kiuchumi. La hasha! Ninachosema ni kwamba kuuliza maswali sahihi pamoja na kua na dira na malengo ya muda mrefu ni muhimu sana, angalau kama hatua ya kwanza, kujua tunakotoka na kama kuna uwezekano wa – na njia za – kuelekea kule tunakotaka kwenda kama jamii na kama taifa. Ni wazi kwamba uwezekano wa maendeleo ya aina tunayowazia na njia za kuyafanikisha zitategemea sana hali ya kihistoria, kisiasa na uwiano wa nguvu/matakwa ya kijamii kimataifa na kitaifa (international and national balance of forces). Baada ya kujiuliza maswali kama haya na kutafakari hali halisi yetu ningependa kutoa hoja kuhusu ujenzi wa uchumi wa kitaifa kama ifuatavyo.

Ujenzi wa Uchumi wa Kitaifa na Masharti yake

Kabla sijaanza kutoa hoja zangu kuhusu ujenzi wa uchumi wa kitaifa, sina budi niweke wazi mambo ambayo nayachukulia kama yanajieleza yenyewe bila ya kudadisiwa zaidi. Jambo la kwanza, na la msingi, ni kwamba, kama jamii na taifa, tunataka kuikomboa jamii yetu kutokana na hali duni na kuelekea kwenye hali nzuri ambayo binadamu kama binadamu anaistahili. Haya yanaweza kuwa kama malengo ya muda wa kati. Malengo ya hatima ni ukombozi wa kijamii jambo ambalo nalichukulia kama ni jema bila kuhitaji uthibitisho.

Jambo la pili ambalo naamini silazimiki kutoa uthibitisho zaidi ya ule niliotoa katika kuangalia historia ya uchumi wetu ni kwamba mfumo wa uchumi wa kikompradori (au uchumi-tegemezi) hauna matumaini ya kuleta maendeleo ya walio wengi yatakayodumu bila kuathiri ubinadamu wao na wa vizazi vijavyo. Maendeleo, kama yakipatikana kwa njia hiyo ya kikompradori, yatakuwa:

(1) kwa wachache wa matabaka finyu ya kijamii;

(2) yataweka pembezoni sehemu kubwa ya jamii;

(3) yanaweza kuharibu mazingira ya kijamii na ya kirasilimali kiasi cha kuhatarisha uhai wa vizazi vijavyo;

(4) yatatuzamisha zaidi chini ya himaya ya kibeberu na kwa hiyo kutuweka katika hali ya utumwa mambo-leo kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni; na

(5) hatimaye kutupotezea malengo yetu ya ukombozi wa kitaifa na wa kijamii.

Ninakiri kabisa kwamba mambo haya yote yanaweza kupingwa kwa nia nzuri tu lakini, kwa mujibu wa lengo la mada hii, sitaki kuingia kwenye mjadala huo.

Suala la kwanza kabisa ni kuitambua sekta na wakala wa maendeleo au uchumi wa kitaifa. Ni wazi kwamba katika uchumi wa nchi yetu kilimo na ufugaji bado ni sekta ambayo ni chanzo kikuu cha kuzalisha ziada. Suala la pili ni kuyaelewa mahitaji ya awali kabisa ya jamii. Hii pia ni wazi na haipingiki: ni chakula. Ukweli ni kwamba ingawa sisi ni nchi yenye sekta kubwa ya kilimo na ufugaji hatujitoshelezi kwa chakula kwa maana mbili. Moja ni kwa maana kwamba wako watu nchini ambao bado hukosa kadirio la chini la mahitaji ya chakula. Maana ya pili ni kwamba ingawa walio wengi hawafi na njaa, wengi wao hukosa lishe bora. Suala la tatu ni kwamba mazao ya chakula yana soko la ndani na kama kuna ziada, yanaweza kuuzwa nje. Hii ina maana kwamba kukua kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kunaweza kupunguza utegemezi kwa soko la kimataifa.[11]

Suala la nne ni kwamba ingawa kilimo ni chimbuko la ziada, ziada hiyo huhama na kulimbikizwa katika sekta zingine na nchi za ng’ambo. Kwa hiyo, kilimo hukosa vitega-uchumi au ulimbikizaji na matokeo yake ni kutokuwa na maendeleo katika njia na ufanisi wa uzalishaji. Kwa sababu hizo zote kilimo na ufugaji vinaweza vikawa sekta au mahala sio tu pa uzalishaji ziada bali ulimbikizaji wa mtaji. Je, kuna dalili zinazoashiria uwezekano huo? Je, kuna vikundi au matabaka katika sekta ya kilimo ambayo yanaweza yakawa chimbuko la ulimbikizaji? Kwa maneno mengine, je, sekta hiyo ina wawekezaji? Hoja yangu ni kwamba wapo. Na hao ni wale ninaowaita wakulima (na wafugaji) matajiri na wa hali ya kati vijijini miongoni mwa jamii ya wakulima wenyewe. Isipokuwa tatizo chini ya mfumo wa kikompradori ni kwamba wawekezaji hao hukosa mazingira na hali itakayowezesha mtaji huo kuchipuka na kukua. Jambo la pili ni kwamba mtaji huo chipukizi pia una sifa ya kuwa mtaji wa kitaifa. Hii ni kwa sababu uzalishaji na soko lake ni vya ndani, yaani mahitaji muhimu katika mwenendo wa uzalishaji yanapatikana ndani. Huu tunauita ‘ulimbikizaji kutoka chini’. Basi, kama kweli ndivyo ilivyo, na nia yetu ni kuchochea ulimbikizaji kutoka chini hatuna budi kusaidia uwekezaji wa aina hii kwa kuweka mazingira bora ambayo yatakidhi na kukuza mtaji wa wakulima tajiri na wa hali ya kati. (Matabaka haya yalikuwa yanapigwa vita kwa kuitwa makaibala ya kikabaila, nyakati za itikadi ya Ujamaa. Hii, ninavyoona mimi, ilikuwa ni kosa na ilitokana na imani potofu ya kujenga ujamaa kutoka juu kupitia taasisi za dola badala ya kuwashirikisha kikamilifu matabaka ya wanyonge). Kuna hatua fulani na masharti mbalimbali ambayo ni lazima katika kujenga mazingira ya uwekezaji wa aina hiyo. Nitayataja machache.

Moja, ni mageuzi katika mfumo wa umilikaji ardhi. Lengo la mageuzi hayo sio tu kugawa ardhi kwa wale wasio nayo bali kuweka mfumo ambao utalinda uhakika wa umilikaji ardhi ambao kwa sasa unakosekana. Kama ilivyothibitishwa na ushahidi uliowasilishwa kwa Tume ya Ardhi na uchambuzi wake unaonyesha, wakulima vijijini hukosa uhakika wa umilikaji ardhi; ardhi zao huporwa na kumegwa na watu binafsi kutoka nje na taasisi za kiserikali eti kwa manufaa ya umma ikiwemo kuchochea uwekezaji kutoka nje. Ushahidi tulionao unaonyesha wazi kwamba hakuna uwekezaji wa maana kutoka nje ya nchi wala nje ya sekta ya kilimo na ufugaji. Wawekezaji wanaomegewa ardhi za vijiji ni wale ambao wametawaliwa na uchu wa kutengeneza faida haraka haraka au wa kupora maliasili wakiwemo wanyama pori na ndege (Chachage 1996). Huu ndio mtaji wa kubabaisha wa kikompradori. Jambo hilo limechambuliwa kwa undani na taarifa ya Tume ya Ardhi na sina haja ya kurudia (URT 1994).

Pili, upangaji wa sekta ya uzalishaji wa bidhaa za viwanda hauna budi kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya wananchi waishio vijijini. Kwa jumla, hii ina maana kwamba bidhaa za matumizi ya walio wengi kama nguo, mafuta ya kupikia, viatu, madawa n.k. na viwanda vya kuzalisha zana za kilimo na pembejeo vipewe umuhimu wa kipekee. Ni kweli kwamba katika awamu ya kwanza, kinadharia, jambo hili lilitambuliwa. Lakini tatizo lilikuwa kwamba halikufuatiliwa kwa umakini hasa katika maana yake ya kuchochea ulimbikizaji wa mtaji wa ndani. Kwa mfano, kulikuwa na mkanganyiko wa hali ya juu katika kuchagua aina ya mitambo (k.m. Kiwanda cha Mbolea, Tanga; na Mwatex) na katika suala zima la umilikaji wa njia za kiuchumi. Hapo ndio lingekuwa jambo la busara kuweka vivutio kwa mtaji wa ndani kuwekeza katika sekta ya nguo badala ya dola kujiingiza moja kwa moja na kuwaachia warasimu wa serikali kuendesha viwanda. Pamoja na kukosa uzoefu, wakuu wa mashirika mengi ya serikali wakaingia kwenye mambo ya rushwa. Hatima yake tukauziwa mitambo mikuukuu au teknolojia ambayo tusingeweza kuimudu kuiendesha na kuikuza. Kwa hivyo tukajikuta kwamba, kwa upande mmoja tukalimbikiza madeni na kwa upande mwingine viwanda venyewe vikashindwa kutosheleza mahitaji ya soko. Mifano michache ya viwanda na teknolojia ambayo tungeweza kuiendeleza – Urafiki – tuliiua kutokana na kukubali ushindani usiokuwa na maana kitaifa. Kwa kifupi, ninachotaka kusisitiza ni kwamba jambo la kujenga uchumi wa kitaifa haliwezi kuwa la kiholela, mradi kwa mradi, kufuatana na upatikanaji wa msaada au mikopo na shinikizo la wachuuzi wa kimataifa wa mitambo, bali, lazima uwe kwa mujibu wa mpango thabiti ambao umebuniwa kutokana na dira na malengo yaliyowekwa na dola lenye mizizi yake katika umma wa walio wengi.

Tatu, katika sekta nyingine kama mawasiliano na nishati pia inaelekea hatujakiri makosa tuliyofanya katika awamu ya kwanza ambayo yametugharimu sana. Kwa mfano, katika uzalishaji wa umeme mitambo yetu mingi ilitegemea ama miradi mikubwa inayotumia nguvu za maji au mitambo ya mafuta. Yote mawili, pamoja na ukweli kwamba ni ghali, pia hatuwezi kumudu mahitaji ya kitaalamu na kiteknologia. Je, isingewezekana kufikiria mitambo midogo midogo ya umeme iliyosambazwa nchini kote inayoendeshwa na nguvu za maji?

Kwenye mawasiliano tumetafuta mikopo mikubwa na ya gharama kubwa ili kujenga barabara. Magari kama njia ya mawasialiano ni ghali sana. Wanaoweza kumudu ni nchi tajiri tu ambao pia wanazalisha mafuta kama Marekani. Sisi tungetilia mkazo njia za reli, barabara za vijiji na usafiri wa maji. Hata ile reli ya TAZARA ambayo ilikuwa na matumaini makubwa ya kuweka njia rahisi ya mawasialiano na kuchochea maendeleo kandokando ya reli hatukuisimamia vizuri kiasi kwamba hali ya kifedha ya TAZARA sio nzuri tena.

Nne, katika sekta za huduma za kijamii – elimu na afya – hatuna budi kuelewa kwamba sekta hizi pia ni kichocheo kikubwa katika kuleta maendeleo. Awamu ya kwanza, pamoja na makosa yake mengi, ilijitahidi lakini haikufanikiwa. Mosi, kwa sababu, haikuchukulia kama ni sehemu ya maendeleo ya kiuchumi; ilichukulia kama ni sehemu ya huduma inayostahili kutolewa na dola, na, kwa hivyo, ni mzigo unaobebwa na bajeti ya serikali. Pili, kama huduma, isingeweza kufanikiwa bila sera sahihi katika medani ya uzalishaji na ulimbikizaji. Hata hivyo, sera za kiliberali kuhusu sekta hiyo ni ya kutukandamiza moja kwa moja sio tu kwa sababu inainyima jamii huduma muhimu lakini pia kwa sababu inahatarisha ukuaji wa uchumi. Nchi za Kiasia ambazo hunukuliwa mara kwa mara siku hizi kama mifano ya kuigwa (Korea ya Kusini, Taiwan n.k.), zote, zilitilia mkazo mkubwa sana katika sekta za elimu, afya, maji na nyumba. Wao hawakuchukulia kama ni mzigo kwa bajeti ya serikali bali ni kama gharama ya uzalishaji kwa upande mmoja, na sehemu ya malipo ya wafanyakazi kwa upande mwingine. Katika hali hii, hakuna budi kuhakikisha kwamba wawekezaji lazima wabebe mzigo huo ama moja kwa moja au kupitia mfumo wa kodi; tuhakikishe wanalazimishwa kufanya hivyo sawa sawa na jinsi wanavyolazimishwa kulipia leseni ya biashara.

Haya ni masharti machache ya kujenga uchumi wa kitaifa. Ni wazi kwamba kama tukikubali masharti haya hatuna budi tukubali vilevile kwamba utekelezaji wa masharti haya unahitaji mipango; pili uongozi, udhibiti na usimamizi wa kidola; tatu ushirikishwaji wa wazalishaji. Maana yake ni kwamba hatuwezi tukachukulia mahubiri ya ulegezaji kama msahafu ambao lazima utekelezwe katika hali yoyote ile. Sisemi kwamba hatuna haja ya ulegezaji wa uchumi. Ninachosema ni kwamba sera za ulegezaji lazima zitekelezwa kwa uangalifu mkubwa.

Kwanza kabisa kuna haja ya kutofautisha kati ya ulegezaji na utandawazi (Brecher & Costello 1994). Mengi ya yale tunayoshurutishwa kufanya na taasisi za kifedha za kimataifa ni aina ya ulegezaji ambao katika hali yetu halisi ni utandawazi. Na matokeo ya utandawazi kama nilivyoeleza, ni kuendeleza uchumi wa kikompradori kwa kuua vichocheo vyovyote vya mitaji ya kitaifa. Tunachohitaji sisi ni kulegeza masharti ndani ya uchumi wetu kwa uchaguzi wa sekta ili kuchochea ukuaji wa mtaji wa kitaifa. Kwa mfano, ninashindwa kabisa kuelewa mantiki ya kulegeza biashara ya bima au ubinafsishaji wa akiba za uzeeni au kuruhusu ushindani katika nyanja hizi. Biashara ya bima inaweza ikawa chimbuko la ulimbikizaji wa mtaji ambao unaweza kuelekezwa, kwa uchaguzi, kwenye sekta mbalimbali, kwa mfano, kilimo, ili kupiga jeki juhudi za mitaji midogo ya kitaifa. Inawezekena kabisa kuhalalisha ukiritimba wa kidola katika sekta hii bila kuuonea haya. Papo hapo, pamoja na kuwa na ukiritimba wa umilikaji na udhibiti wa biashara hiyo ya bima, taasisi zenyewe na mashirika yanayosimamia biashara hiyo yanaweza yakawa huru na kuendeshwa kibiashara. Yaani hakuna mgogoro wala pingamizi kati ya ukiritimba wa kidola katika umilikaji na misingi ya kibiashara katika uendeshaji. Ni ndoto za mchana kuamini kwamba mashirika ya bima ya kitaifa yanaweza kumudu ushindani kutoka kwa makampuni makubwa ya bima ya kimataifa. Ni upuuzi mtupu, na haina maana, kukubali kuweka medani sawa ya ushindani kati ya kampuni ya kimataifa ya bima, Prudential na shirika la Bima la Taifa, NIC, kwani ni sawa na kusema kijana wa miaka 18 ashindane katika mbio na kizee wa miaka 90 katika medani sawa!

Hata hivyo hakuna maana kwamba hatuhitaji ubinafishaji. Jambo la kusisitiza ni kutokurudia makosa yale yale ya awamu ya kwanza. Katika awamu ya kwanza kulikuwa na utaifishaji bila uchaguzi, kiholela, yaani tulitaifisha hata maduka ya nyama na vituo vya mafuta ya magari! Chini ya sera ya kiliberali tumeanza kubinafsisha bila uchaguzi – hata bima na viwanda vya bia, ambavyo vikiendeshwa vizuri vinaweza kuingiza faida bila gharama kubwa.

Jambo la mwisho ambalo ningependa kusistiza ni kwamba hatuwezi tukamudu masharti ya kujenga uchumi wa kitaifa bila ya kuwa na dola na mfumo halisi wa kidemokrasia. Yaani, ili dola iweze kubeba mzigo mzito wa kujenga uchumi wa kitaifa haina budi kuwa na mizizi na uhalali katika jamii yenyewe. Na uhalali hauwezi kupatikana kama hakuna ushirikishwaji wa hali ya juu wa umma katika shughuli na mambo ya kiutawala na ya kisiasa. Upeo wa mada hii hauniruhusu nifafanue zaidi suala hilo isipokuwa labda nihitimishe kwa kusema kwamba uchumi wa kitaifa unahitaji dola ya kitaifa na sio ya kikompradori ambayo inaweza kutumwa-tumwa na wawekezaji wa nje na wawekezaji-uchwara wa ndani pamoja na wataalam, washauri, wasomi na wasemaji wao.

Hitimisho

Katika mada hii nimejaribu kueleza kwa muhtasari viini vya sera mbalimbali za kiuchumi ambazo zimefuatwa nchini tangu tupate uhuru. Sera hizi nimeziainisha chini ya vichwa vitatu vya maelezo ambavyo nimeviita mageuzi ya mrengo wa kisasa (modernisation), mageuzi ya mrengo wa kidola (statisation) na mageuzi ya mrengo wa kiliberali (liberalisation). Hoja yangu ni kwamba sera hizo zote, bila labda kukusudia hivyo, zilisaidia kuendeleza mfumo wa uchumi wa kikompradori kwa maana kwamba masharti na kanuni za ulimbikizaji wa mtaji zilikuwa zile ambazo zinakidhi matakwa ya mitaji ya kimataifa kwa kiasi kikubwa na yale ya mtaji wa ndani wa kikompradori kwa kiasi kidogo. Ukweli ni kwamba uhai wa mtaji huo wa ndani unategemea kuwepo kwa mtaji wa kimataifa.

Nimeonyesha pia kwamba ingawa sera hizi zina tofauti zake hata katika mwelekeo wa kiutawala na kisiasa, mfumo wa uchumi unabaki vile vile, yaani, mfumo wa kikompradori. Sifa kuu ya mfumo huo ni mwelekeo wa ukiritimba wa mtaji wa kimataifa (kutoka nje) kwa upande mmoja, na ukandamizwaji wa mtaji wa kitaifa (wa ndani), kwa upande mwingine. Kwa maneno mengine, kuna utengano kati ya mahala pa uzalishaji wa ziada na mahala pa ulimbikizaji wa mtaji. Hitimisho langu ni kwamba hakuna matumaini kwamba maendeleo halisi yatakayotuelekeza kwenye ukombozi wa kitaifa na wa kijamii yanawezekana chini ya uchumi wa kikompradori. Zaidi zaidi labda wachache wa matabaka finyu wanaweza kunufaika na maendeleo kama hayo lakini wanyonge, ambao ndio wengi, wanaweza wakawekwa pembezoni na kujikuta wanazama siku hadi siku kwenye umaskini wa kupindukia wa hali, mali na utamaduni kama tunvyoshuhudia katika nchi nyingi za Amerika ya Kusini.

Nimetoa hoja kwamba ujenzi wa uchumi wa kitaifa labda unaweza kuchochewa na ‘ulimbikizaji wa kutoka chini’ katika sekta za kilimo na ufugaji. Nimetaja masharti machache na sifa za mazingira yanayoweza kukuza na kukidhi matakwa ya mtaji wa kitaifa hususun matabaka ya wakulima-tajiri na wakulima wa hali ya kati.

Mwishowe, nimedadisi kwa ukali kidogo uwezekano wa sera za ulegezaji na ubinafsishaji kutuelekeza kwenye maendeleo halisi ya walio wengi. Nimetahadharisha kwamba sera hizi za ulegezaji ambazo zinahubiriwa siku nenda siku rudi zinaweza zikatuzamisha zaidi katika mfumo ambao unaweza kuhatarisha hata uhuru wetu kama taifa na nchi. Nimeshauri kwamba tunahitaji ulegezaji wa ndani kwa uchaguzi bila kukumbatia kiholela ulegezaji wa nje au matakwa ya utandawazi.

[1] Mada hii haitahusu Zanzibar.

[2] Kusema ukweli, sera zilizofuatwa zilibuniwa na Benki ya Dunia (World Bank). Angalia taarifa ya IBRD 1961.

[3] Wazawa wa Amerika ya Kusini yaani “Wahindi wekundu” waliuawa na bara lao likakaliwa na Wazungu. Ndio kusema watu wa Bara la Afrika wakaibwa kutoka bara lao na watu wa Amerika ya Kusini wakauawa na bara lao likaibiwa.

[4] Ingawa inanishangaza kwamba siku hizi umetokea mtindo miongoni mwa baadhi ya wasomi na wanasiasa wetu ambao hujaribu kuhalalisha ukoloni bila aibu.

[5] Angalia kitabu cha Frantz Fanon (1967) ambacho kinaeleza kwa ufasaha na uchungu ufinyu wa kimawazo na wa kiutamaduni wa vibwenyeye wa Afrika waliotawala baada ya uhuru.

[6] Kampeni dhidi ya wahujumu uchumi ya mwaka wa 1983 chini ya uongozi wa marehemu Sokoine ambaye alikuwa Waziri Mkuu ilikuwa ni jaribio la mwisho la kuongeza kiwango cha uhalali wa kisiasa na kuiokoa serikali chini ya itikadi ya ujamaa.

[7] Bila shaka idadi ya wageni ambao huingia nchini kwa shughuli na visingizio mbali mbali – k.m. wataalam, wawekezaji, wazururaji na wachuuzi wa kimataifa, wamafia, watafiti na ma-“consultants”, watendaji wa masharika yasiyo ya serikali – huongezeka kwa kasi ya kupindukia.

[8] Kisiwa cha Mauritius barani Afrika hutajwa tajwa kama mfano mwingine wa maendeleo ya aina hii. Suala hilo linahitaji uchambuzi zaidi ya hali halisi ya kihistoria kuliko nafasi yangu inayoniruhusu na siwezi kulijadili hapa.

[9] Nikitumia dhana ya ‘mtaji wa kitaifa’ sina maana ya watetezi wa uzawa. Katika uchambuzi wangu ubaya au uzuri wa mtaji hautegemei alikozaliwa mwenye mtaji (yaani bepari mwenyewe); bali inategemea mahala pa uzalishaji na ulimbikizaji wa mtaji. Mtaji wa kitaifa ni ule ambao kwa kiasi kikubwa unazalishwa na kulimbikizwa katika sehemu ya uzalishaji na hutegemea malighafi ya ndani kwa upande moja, na soko la ndani kwa ajili ya bidhaa zake, kwa upande mwingine.

[10] Siku hizi ni mtindo wa kunukuu nchi za Kiasia (Korea ya Kusini, Taiwan, Malaysia n.k.) kama mfano wa kuigwa kwa maendeleo ya kiuchumi. Tukiangalia maendeleo ya nchi hizo tunakuta kwamba, wao hawakufuata kabisa mahubiri ya taasisi za kimataifa za fedha kama vile –

 • dola kutokuingilia uchumi;
 • soko huria;
 • ulegezaji wa masharti ya biashara ya nje; n.k.

Ukweli ni kwamba maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo yalitegemea sana, kwanza, usimamizi na udhibiti wa dola (bila dola kumiliki njia kuu za uchumi moja kwa moja), pili, mfumo wa udikteta wa kisiasa na, tatu, ufadhili wa kulindwa na majeshi ya kibeberu. Sisemi kama ni jambo jema kuiga udikteta wa aina hiyo katika bara la Afrika.

[11] Juzi juzi tumeshauriwa na msemaji mmoja wa Benki ya Dunia kuendeleza kilimo cha maua kwa sababu yana soko zuri kimataifa. Ushauri kama huo haudadisi kabisa mwelekeo wa utegemezi ambao umetufikisha katika hali tuliyonayo.

10 thoughts on “Ujenzi wa uchumi wa kitaifa

 1. Наше производство

  Компания «Пожтехспас» выполняет полный производственный цикл, а значит полностью отвечает за высокое качество и надежность продукции в эксплуатации. Все сотрудники компании — квалифицированные специалисты и профессионалы своего дела. Для производства противопожарной техники они используют только высококачественные материалы, самое современное оборудование и новейшие технологии.
  Лафетные стволы “Пожтехспас”

  Предназначены для бесперебойной подачи сплошной или распыленной струи воды (в некоторых случаях пены низкой кратности) в зону возгорания. Учитывая мощность напора, который подается на ствол, лафет также обеспечивает устойчивость конструкции и позволяет ствольщику свободно управлять.

  Входит в комплект обязательного оборудования любой пожарной команды. Также он может устанавливаться на территориях больших промышленных объектов с целью обеспечения общей пожарной безопасности и незамедлительного реагирования в случае возникновения непредвиденной ситуации. Кроме тушения пожаров, универсальный лафетный ствол может использоваться для осаждения токсичных и ядовитых облаков газа, пара или пыли, а также для охлаждения любых строительных или технологических конструкций.
  Разновидность лафетных стволов

  Модели бывают разными и отличаются в зависимости от их основного предназначения и целей, которые в будущем будут выполняться.

  На нашем сайте представлены:

  – стационарные (обычно устанавливаются непосредственно на объекте для быстрого реагирования на огонь),

  – переносные (более легкие и мобильные устройства, которые транспортируются к месту возгорания),

  – с дистанционным управлением (максимально безопасные для человека, так как позволяют тушить пожар в непосредственной близости к огню),

  – ручные (имеют небольшой вес, поэтому легко переносятся одним человеком и дают больше возможностей для маневра),

  – с осциллятором (специальным устройством, которое позволяет осуществлять автоматические повороты ствола по горизонтали и вертикали),

  – взрывозащищенные (специальная категория оборудования для применения в условиях потенциально взрывоопасной среды).

  Выбирая пожарный лафетный ствол (сокращенно ЛС), стоит учитывать пожароопасность объекта и площадь территории либо помещения. При покупке также рекомендуем обращать внимание на дополнительные опции (например, защитный экран) и насадки, которые могут идти в комплекте. Если таковые отсутствуют, советуем обратиться к специалистам, чтобы решить нужны ли в вашей ситуации усовершенствования. Модели с разнообразными насадками более функциональны и эффективны.

  Современные лафетные стволы, которые мы выпускаем очень экономичны в использовании противопожарных ресурсов. Это особенно важно на промышленных предприятиях, где не всегда есть свободный доступ к открытым водным источникам. Покупая лафетный ствол от производителя «Пожтехспас», вы всегда можете быть уверены в надежности, качестве и долговечности устройства. Вся продукция изготавливается с помощью современного оборудования в соответствии со всеми требованиями ГОСТов.

  Мы предлагаем довольно выгодные цены на лафетные стволы, так как реализуем их напрямую от производителя. Если вы хотите приобрести нашу продукцию, отправьте предварительную заявку на нашем сайте либо же позвоните по указанным выше номерам. Наши менеджеры свяжутся с вами в ближайшее время и финально оформят ваш заказ.

  В свою очередь, мы гарантируем самую низкую цену на свою продукцию. При наличии предложений лучше – мы готовы опустить цену вплоть до себестоимости.

 2. W wielu miejscowościach działają firmy, które zajmują się wynajmem kontenerów. Kontenery na gruz Poznań są dosyć atrakcyjne, bowiem są niezbyt kosztowne oraz są one wręcz konkurencyjne gdy je porównamy do kontenerów z odmiennych miejscowości. Wynajem kontenerów Poznań jest bardzo bezproblemowy, ponieważ musimy jedynie zadzwonić do przedsiębiorstwa jak również złożyć dyspozycję. Przedsiębiorstwa wychodzą naprzeciw swoim klientom i wykonują zgłoszenia zgłoszone online a poza tym za pomocą telefonu. Takie firmy oferują wywożenie gruzu z różnorodnych miejsc. Do zlecenia jest równie dobrze wywóz odpadów poremontowych Poznań, czyli takich, które powstały danemu klientowi po pracach remontowych.

 3. Ребята, нужна ваша помощь!! Где купить
  ламинат квик степ интернет – магазин

  Может кто подкажет?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box