Ukimya wa wengi kuhusu muungano: Nini tafsiri yake?

Makala haya yalichapwa katika Raia Mwema, toleo la 333, Januari 8, 2014.

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Makala yangu ya juma lililopita yalihoji usambazaji wa propaganda ufanywao na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kukumbatiwa na makundi ya wajiitao wanaharakati na wanasiasa kuwa tiba pekee ya “kero” za Muungano ni kuanzisha serikali ya Tanganyika, na kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wananchi, bara na visiwani wanataka serikali ya Tanganyika, iwe ni kupitia Muungano wa mkataba au Muungano wenye serikali tatu.

Makala yale yaliibua upotoshaji wa makusudi ufanywao na Tume kwa kutumia takwimu ili kuwaaminisha wananchi wetu kuwa serikali tatu ni maoni ya wengi. Nilizichambua takwimu za Tume kuonyesha kuwa hicho kinachoitwa asilimia 60, sio asilimia 60 ya Watanzania, ambao idadi yao yapata milioni 45.Kadhalika sio asilimia 60 ya waliotoa maoni katika Tume, ambao idadi yao ni 333,537. Wala sio asilimia 60 ya waliozungumzia Muungano, ambao idadi yao ni 77,000. Bali ni asilimia 60 ya waliozungumzia kuhusu muundo wa Muungano, ambao idadi yao yapata 46,000. Na kati ya hao 46,000 jumla ya waliopendekeza serikali tatu au mkataba ni 27,870.

Kama nilivyodokeza, watu hao 27,870 ni asilimia 36 tu ya watoa maoni 77,000 waliozungumzia Muungano. Kadhalika watu hao 27,870 ni asilimia 8.4 ya watu 333,537 waliotoa maoni katika Tume ya Warioba. Kwa maana nyingine, idadi hiyo idadi yao ni ndogo, na sio sahihi kabisa kutumia idadi hiyo kuhalalisha uwingi.

Kwa hiyo swali la kujiuliza ni kuwa kama kweli muundo wa Muungano ndiyo kero kuu ya wananchi wetu, Bara na Visiwani, ilikuwaje watoa maoni wapatao 287,537 (sawa na asilimia 86.2 ya watoa maoni wote) hawakugusia kabisa suala la Muungano au muundo wake? Je, kwa nini sauti zitokanazo na ukimya wao zinapuuzwa?

Makala yangu ya leo yatajikita katika sauti zitokanazo na ukimya wa wananchi wetu wengi juu ya Muungano, sauti ambazo Tume ya Warioba imeamua kwa makusudi kabisa kuzipuuza na kukumbatia maoni ya wachache.

Kwa mtazamo wangu, ukimya wa sauti kuhusu Muungano una tafsiri kubwa mbili. Kwanza, ni kwamba watu wetu walio wengi, Bara na Visiwani, hawanatatizo na uwepo wa Muungano katika muundo wake wa sasa. Pamoja na propaganda zifanywazo na wanasiasa kujaribu kuwachonganisha wananchi wa pande mbili za Muungano bado “sumu” hiyo haijaingia katika mioyo na akili za wananchi wetu wa kawaida, na hivyo haijafanya kazi kiasi cha kutosha.

Pili, katika kutoa maoni, inavyoonekana wananchi wengi waliojitokeza kuzungumza walijikita katika “kero” zihusuzo maisha yao ya kila siku: ukosekanaji wa huduma za msingi katika maisha, kama maji safi na salama, chakula, malazi, huduma za afya, elimu bora, n.k. Licha ya uhaba wa huduma au mahitaji hayo, pale vitolewapo hupatikana kama bidhaa, tena bidhaa ambazo bei yake hupanda kila siku. Wenye pesa ndio wapatao. Ndio maana malalamiko mengi ya wananchi wetu ni yale yagusayo haki za msingi katika maisha, na hasa haki za kijamii na kiuchumi.

Lakini hata hivyo, wanasiasa na wajiitao wanaharakati, kwa ufundi wao mkubwa, wamejitahidi kuteka mijadala na hata kutoa miongozo kwa wananchi juu ya nini cha kusema mbele ya Tume. Ukiipitia miongozo mingi, utakuta imejikita katika “kero” za wanasiasa, ikiwemo hamu yao kubwa ya kugawanya nchi katika vipande viwili ili wajiongezee nafasi za ulaji.

Na kwa hila za hali ya juu, wamejitahidi kuwaaminisha baadhi ya wananchi kuwa “kero” zao za maisha ya kila siku zitatauliwa kwa kuwa na Tanganyika huru au Zanzibar huru. Jambo hili halijitokezi kwa bahati mbaya. Huko Visiwani, kabla ya serikali ya Umoja wa Kitaifa, wafuasi wa CUF waliaminishwa kuwa mwisho wa matatizo na dhiki zao ni pale ambao CUF itaingia madarakani. Na sasa hata baada ya CUF kuingia katika serikali hali za wananchi wa kawaida zinazidi kuwa ngumu zaidi. Hili la ugumu wa maisha linashuhudiwa na Ahmed Rajab, katika makala yake katika Raia Mwema, toleo na. 281, la Februari 13, 2013:

Kadhalika, wengi wakitumai kwamba hatimaye Zanzibar inaelekea ndiko — kwenye maendeleo. Wengine wakihisi kwamba angalau kutawekwa msingi madhubuti wa kuzitengeneza huduma zilizo muhimu sana na miundombinu imara pamoja na kuufanya uchumi ustawi. Alhasili wakiamini kwamba mambo yataanza kutengemaa.

Walikosea. Tunaelekea mwaka wa tatu tangu iundwe hiyo Serikali ya ubia na wengi wa Wazanzibari wanaona kuwa hali zao za maisha zimezidi kuwa ngumu. Siku hizi, kwa mfano, wakitaka kununua chakula inawabidi wanunue kwa bei za kuruka juu sana kushinda zile walizokuwa wakilipa katika 2010. Ukizilinganisha bei za vyakula zilivyokuwa miaka miwili iliyopita na zilivyo sasa hutoshangaa ukiwaona wanalia.

Isitoshe zile idara au wizara zilizo chini ya udhibiti wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama vile za afya na elimu hazikufanya mengi ya kutia moyo.

Tujifunzacho hapa ni kwamba ubadilishaji wa sura ama vyama katika madaraka ya kisiasa sio ufumbuzi wa matatizo ya wananchi, ikiwa vyama mbadala havitofautiani kisera na chama kinachotawala. Vyama vyetu vyote vinahubiri ama kutekeleza sera za uliberali mamboleo ambazo ndio chanzo kikuu cha ufukara wa walio wengi, hivyo tusitegemee miujiza vikiingia madarakani.

Hicho ndicho kilichotokea Zanzibar. Na ili kuficha ukweli kwamba sera za kiuchumi za CUF hazina utofauti na za CCM, kikazuka kisingizio kuwa ufukara wa wananchi unasababishwa na Muungano, na kwamba suluhisho pekee ni kuvunja Muungano ili Zanzibar ijitegemee kisiasa na kiuchumi.

Kwa bahati njema, kama takwimu za Tume zinavyotueleza, Wazanzibari walio wengi hawana tatizo na Muungano. Hii inatokana na ukweli kwamba kati ya Wazanzibari 38,000 waliozungumzia kuhusu Muungano, nusu yao (19,000) hawakuwa na tatizo na Muundo wake, na hivyo hawakuugusia. Ukichukua idadi yao ukajumlisha na Wazanzibari 6,460 waliotaka serikali mbili na wale 25 waliotaka moja, utapata jumla ya watu 25,485. Hawa ni asilimia 67.1 ya Wazanzibari 38,000 waliozungumzia Muungano. Waliotaka mkataba ni Wazanzibari 11,400 ambao ni asilimia 30 ya Wazanzibari 38,000 waliozungumzia Muungano.

Kwa hiyo, bado kuna idadi kubwa ya wanyonge wa Kizanzibari walioukataa huo uitwao Muungano wa Mkataba, ambao unashadadia kuanzishwa kwa Tanganyika huru. Maoni yao, iwe ni kwa kutogusia muundo wa Muungano, au kwa kutaka serikali mbili au moja, yasipuuzwe!

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th[at]yahoo.com.

One thought on “Ukimya wa wengi kuhusu muungano: Nini tafsiri yake?

  1. Idadi ya wanaotaka muundo wa serikali tatu kati ya wale wwakliogusia Muungano ndiyo ya kuzingatia.
    Idadi kubwa ya waliochangia maoni kutokuzungumzia Muungano haimaanishi hata kidogo kwamba walio wengi Zanzibar na Tanganyika wametosheka nao chini ya muundo uliopo wa serikali mbili.
    Tunaweza tu kusema kwamba wengi waliotoa maoni hawakuzumgumzia ya Muungano kabisa kwa sababu ya kutokutaka au ya Muungano kuwa magumu mno kwao kuyazungumzia.
    Ukweli ni kwamba la muundo wa serikali ya Muungano ndiyo zito kuliko yote kwenye katiba mpya inayotengenezwa na kuheshimu uliochaguliwa na wengi Zanzibar na Tanganyika ndiyo njia pekee ya kuhakikisha katiba mpya itakuwa imesimama kwenye msingi imara kama chaguo la wananchi wenyewe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box