WAJIBU-JAMII WA MWANAZUONI WA AFRIKA

Mhadhara huu utajikita kwenye mjadala juu ya mambo ambayo yanafaa kuzungumziwa na kubishaniwa katika jukwaa la wanazuoni. Sifa muhimu ya mijadala  inayojumuisha wanazuoni ni uwezo wao wa kusikiliza maoni ya wenzao kwa utulivu; kujenga hoja; kukosoa hoja na kutokana na mgongano wa hoja kuzalisha hoja mpya, au mbadala, ambayo itasukuma mbele ufahamu na fikra. Kuna thesis, yaani hoja ya msingi, kuna anti-thesis, yaani hoja gonganishi, na kuna synthesis, ambayo inazingatia mawazo yanayojitokeza kwenye thesis na anti-thesis, na kuibua hoja mpya, au hoja mbadala. Lengo langu ni kutumia njia hii ya ubishani wa kisomi kujenga hoja zangu.

Kabla sijaanza kuwasilisha hoja za mhadhara wangu, ningependa nieleze, japo kwa ufupi, kwa nini ni muhimu kuibua suala la dhima (commitment) na wajibu-jamii (social responsibility) wa wasomi wakati huu. Kwa mtazamo wangu, nadhani kuna sababu kubwa zifuatazo. Katika miongo miwili au mitatu ya mwanzo wa Chuo hiki, na hata vyuo vingine barani Afrika, suala la nafasi na wajibu wa wasomi lilikuwa linajadiliwa sana. Kwa kiasi kikubwa tuliweza kudadisi dhima yetu, wajibu-jamii wetu na mchango wetu kwa jamii zetu.  Kadhalika, kulikuwa na juhudi kubwa, kuweka mazingira yanoyafaa kwa ajili ya kuendesha mijadala bila hofu. Pale ambapo watawala wa serikali au viongozi wa Chuo walipojaribu kubana nafasi ya mijadala, wanafunzi na walimu waliungana kupinga hatua kama hizo.

Kuanzia miaka ya 80 uhuru huo adimu na muhimu wa kitaaluma ulianza kubanwabanwa. Hali hii ilienda sambamba na nchi zetu kusalimu amri kwa taasisi za kifedha za kimataifa na wafadhili. Tukalazimishwa kubadili sera za kitaifa na kufanya mageuzi yaliyokumbatia sera ambazo kwa pamoja sasa tunaziita za uliberali mambo-leo (soko huria, ubinafsishaji, uhuru wa uwekezaji, ushindani, haki sawa kwa wananchi na wawekezaji, kwa maana haki sawa kwa wanyonyaji na wanyonywaji, n.k.). Kwa taasisi za elimu ya juu, mageuzi hayo yalimaanisha kuwa na sera za kuchangia gharama za elimu (cost-sharing).

Sera hizi hazikupitishwa na kutekelezwa bila upinzani. Katika vyuo vingi vya Afrika, pamoja na chetu, kulikuwa na upinzani. Kutokana na kuwepo kwa dalili za kubanwa kwa uhuru wa kitaaluma, vyama vya wanataaluma vya taasisi sita za elimu ya juu vilipitish The Dar es Salaam Declaration on Academic Freedom and Social Responsibility   (‘Azimio la Dar es Salaam juu ya Uhuru wa Kitaaluma na Wajibu-Jamii’) mnamo mwaka wa 1990.  Na Katika mkutano wa CODESRIA wasomi na wanazuoni wa Afrika walikutana Kampala na kupitisha ‘Azimio la Kampala juu ya Uhuru wa Taaluma na Wajibu-Jamii wa Wananzuoni’ ambalo lilitambuliwa rasmi na Umoja wa Afrika.

Hata hivyo, hali ya kudidimizwa kwa uhuru wa taaluma haikubadilika sana. Kulikuwa na mazingira ya hofu na kujidhibiti (self-censorship). Hali ambayo imeendelea kuwepo hadi leo.

Kutokana na sababu mbalimbali, mnamo mwaka wa 2008, Chuo Kikuu chini ya uongozi wa Profesa Mukandala kilizindua Kigoda cha Taaluma Cha Mwalimu Nyerere. Katika miaka mitano, Kigoda kilijaribu kutengeneza mazingira na nafasi ya kuibua na kuendeleza mijadala ya wazi na yenye lengo la kuwatoa hofu wasomi ili waweze kuzingatia ukweli kwamba hakuna jambo lolote ambalo ni nyeti ambalo haliwezi kujadiliwa hadharani. Nilifurahi nilipomsikia Profesa Penina akitupa matumaini kwamba utamaduni huu, ambao bado haujakomaa, utaendelezwa. Nakutakia kila la heri dadangu.

Kipindi hiki bado ni kigumu. Ni juu yetu wasomi, kwanza, kuilinda nafasi hii adimu, na pili, kupanua nafasi hii ili wanafunzi na walimu waweze kujadili na kuhoji bila hofu wakiwa ndani na nje ya vyumba vya mihadhara. Katika hali halisi ilivyo, hii labda ni ndoto yangu, lakini huwezi kujenga mustakabali mwema bila kuwa na ndoto.

Kutokana na sababu hizi, nimeona nirejea suala hili nikitumia nafasi hii adimu niliyopewa na wanakigoda.

***

Mhadhara huu una sehemu nne. Katika sehemu ya kwanza nitaeleza mwanazuoni ni nani.  Katika kueleza dhana ya mwanazuoni sina budi nieleze pia dhana ya msomi na pia nibainishe tofauti iliyopo kati ya msomi na mwanazuoni. Sehemu ya pili nitazungumzia uhusiano kati ya wasomi/wanazuoni na tabaka-jamii, social class. Katika sehemu ya tatu nitadadisi dhana ya wajibu-jamii, kwa kutoa mifano hai. Na mwisho nitagusia wajibu-jamii wa mwanazuoni wa Afrika na kutoa rai yangu kwenu.

I. Mwanazuoni ni nani?
Mwanazuoni ni nani? Je, kuna tofauti kati ya mwanazuoni (intellectual) na msomi (intellect worker/intelligentsia)? Ndiyo, ipo tofauti. Wanazuoni wote, au karibu wote, ni wasomi lakini siyo wasomi wote wanakuwa wanazuoni. Mara moja moja inatokea kwamba mtu ambaye hajawahi kusoma katika taasisi yeyote ya elimu huwa mpevu kifikra na kwa hiyo huwa na sifa za mwanazuoni. Lakini hii ni nadra sana. Kwa kawaida wanazuoni wengi huwa wasomi. Kwa hivyo, hatuna budi tuanze kwa kueleza wasomi ni nani.

Msomi huishi kwa nguvu-akili wakati mvujajasho huishi kwa nguvu-mwili. Kwa maneno mengine, mfanyakazi huishi kwa jasho lake lakini msomi huishi kwa ubongo wake.  Katika mfumo wa kibepari hii ni aina mojawapo ya mgawanyo wa kazi. Na tofauti kati ya msomi na mfanyakazi ni kubwa na ya kipekee. Inakuzwa, inatuzwa.

Msomi hujivunia utaalamu na uelewa wake. Na kusema ukweli wasomi wanakubalika katika jamii kama wanataaluma ingawa utaalamu wao unaweza ukawa mkubwa juu ya jambo dogo. Elimu ya kibwanyenye huigawanya taaluma katika visehemu vidogo vidogo. Kwa hivyo, kwa mfano, msomi wa uchumi siyo mtaalamu wa uchumi kwa ujumla, bali anaweza akawa mtaalam wa fedha tu, au wa sarafu tu, na asiwe na ufahamu wowote wa uchumi kwa ujumla.  Msomi wa sheria anaweza akawa mtaalamu wa masoko ya hisa tu.  Anawashauri wacheza “kamari” katika soko hili – ni wakati gani mwafaka wa kununua hisa na wakati gani wa kuziuza ili kujiongezea faida na utajiri. Mfano mmojawapo wa mtaalamu wa masoko ya hisa na fedha ni George Sorros. Anajulikana kama msomi aliyejitajirisha kwa kuhamishahamisha fedha kutoka soko moja kwenda soko lingine. Baada ya kutengeneza faida na kutajirika kwa njia hii sasa anafadhili mashirika yasiyo ya kiserikali ya kutetea mfumo wa demokrasia ya kiliberali katika nchi nyingi, pamoja na Afrika. Huyu ni msomi; anachuma fedha na kuishi maisha ya anasa na ya heshima kwa kutumia akili zake “shupavu” za kucheza “kamari”.

Wako wasomi wa aina nyingi tu – wakuu wa mashirika ya biashara, wahandisi, wanasheria, wanasiasa, wanaharakati, wahadhiri, watumishi wa ngazi ya juu katika serikali, biashara, viwanda, na wengine wengi. Lakini wengi hawa siyo wanazuoni.

Wanazuoni hutofautishwa na wasomi kwa sifa kama sita hivi.

Moja ni kwamba mwanazuoni huchambua mambo kihistoria. Tukio au jambo limetoka wapi, liko wapi na linaelekea wapi. Mwongozo wake ni kuchambua mielekeo. Tukifananisha na mpiga picha, tunaweza kusema kwamba mwanazuoni hupiga video, sio picha. Hii haina maana kwamba kila mwanazuoni ni mwanahistoria. La hasha! Haiwezekani. Lakini kila mwanazuoni ana mwelekeo wa kihistoria katika uchambuzi wake.

Pili, na hili lina uhusiano wa karibu na hilo la kwanza, ni kwamba anaangalia mambo – hususan ya kijamii – katika uhusiano wake na mambo mengine. Kwa mwanazuoni, hakuna jambo lisiloingiliana na lingine. Kuweza kuelewa muingiliano ni muhimu, badala ya kulitenganisha tukio au jambo na muktadha wake. Kwa mfano, huwezi kuelewa chanzo au vyanzo vya umaskini katika jamii bila kuelewa historia yake na uhusiano wake na utajiri. Umaskini na utajiri ni kama mapacha na vina historia moja. Matajiri wachache wananeemeka na umaskini wa wengi. Kwa hivyo, kuna muingiliano kati ya umaskini na utajiri. Hata hivyo, baadhi ya wasomi huchambua umaskini bila kuangalia historia yake na kuchukulia, bila kudadisi, kana kwamba umaskini umekuwepo tangu enzi za kale na utaendelea kuwepo milele, isipokuwa labda unaweza kupunguzwa. Tuna mashirika mengi yanayozungumzia upunguzwaji wa umaskini (poverty  alleviation) badala ya utokomezaji wa umaskini. Na huwezi kutokomeza umaskini bila kuelewa vizuri chanzo cha umaskini, uhusiano wake na utajiri na mfumo wenyewe unaozaa matabaka ya waliyonacho na wasiyonacho.

Tatu, mwanazuoni huamini kwamba ukweli haugawanyiki, the truth is the whole. Maana yake ni kwamba huwezi kupata ukweli wa jambo kama hujaliangalia jambo hilo katika muktadha wake. Nikitoa ule mfano maarufu, huwezi ukasema kwamba tembo ni kama kamba nene kwa sababu umegusa mkia wake au kwamba tembo ni mpana kwa sababu umegusa sikio lake. Ili kujua ukweli wa umbo la tembo ni lazima uangalie umbo lake zima.

Nitoe mfano mwingine. Ukitaka kuchambua muundo wa kiti, huwezi ukachambua miguu yake tu. Wala huwezi kusema kwamba sehemu za kiti ni miguu na sehemu za kukalia na kuegemea. Ukijumlisha sehemu hizo hutapata kiti, utakachopata ni rundo la mbao! Ukitaka kuelewa muundo wa kiti kizima, huna budi uchambue jinsi, na katika uhusiano upi, sehemu zake zote zimeunganishwa.

Nne, mwanazuoni ni wakala wa mabadiliko ya hali iliyopo, na siyo mtumwa wake. Dhamira yake ni kuigeuza na siyo kuigandisha hali iliyopo. Dhamira yake ni kuleta hali bora katika jamii, hususan kwa walio wengi. Yeye daima ni mpambanaji. Anapambana dhidi ya dhuluma, uonevu, ukandamizaji na uovu mwingine popote pale ulipo. Ndiyo dhamira yake, ndiyo maisha yake, ndiyo uhai wake.  Anajitambulisha na wapambanaji wenzake bila kujali wanakotoka, makabila yao, au rangi yao.

Jamaa mmoja alimwandikia Che Guevara kwamba kutokana na majina yao kufanana labda wao ni ndugu wa damu. Che alimjibu kwamba yeye haoni kwamba wao ni ndugu: ‘Lakini’, namnukuu, ‘kama wewe unachukia uonevu popote pale ulipo, basi sisi ni ndugu, makamaradi’ ….  bila kujali kama sisi ni ndugu wa damu.

Tano, mwanazuoni hujali, na kupigania maendeleo ya wanadamu, maendeleo ya wote, siyo ya wachache.

Sita, ili kukidhi uelewa wa jamii na mazingira yake na ya ulimwengu, mwanazuoni hujikita kwenye uchambuzi wa kina, uchambuzi ambao unaongozwa na nadharia iliyopevuka. Ndiyo maana wanazuoni wengi, hususan wa Afrika, wanavutiwa zaidi na nadharia ya kimapinduzi ya usoshalisti. Kwa mwanazuoni huyo, ufahamu/elimu ni zana ya kukosoa hali ilivyo bila kusita na kuielekeza kwenye kubadili jamii, siyo bidhaa ya kuuzwa. Katika kusisitiza umuhimu wa nadharia ya kimapinduzi Amilcar Cabral, mkombozi na kiongozi wa Guinea Bissau, alisema: Bila nadharia ya kimapinduzi hakuna mapinduzi yatakayoshinda.

Ni wazi kwamba sio kila mwanazuoni ana sifa hizo zote kama itaeleweka vizuri zaidi katika sehemu inayofuata kuhusu wanazuoni na matabaka ya kijamii.

II. Wanazuoni wa tabaka
Wanazuoni ni sehemu ya jamii na wana uhusiano na jamii. Hawawezi kudai kwamba wao ni wachambuzi tu wa mambo na kwamba taaluma yao haiguswi kwa namna yoyote ile na matakwa, hofu, hisia, matumaini, fikra, itikadi na mitazamo ya jamii. Kwa kuwa jamii yenyewe ya kibepari imegawanyika katika matabaka na makundi basi wanazuoni pia huwa wasemaji wa tabaka fulani au kundi fulani, ama bila kujua au bila ya kujitangaza.

Tabaka linalotawala hutawala pia mawazo, fikra na itikadi, ndiyo maana katika mfumo wa kibepari itikadi ya kibwanyenye hutawala. Wanazuoni na wasomi wengi hutumikia tabaka-tawala kwa njia moja au nyingine kwa kujenga na kusambaza itikadi yao. Hata hivyo, wanazuoni wachache hutamani kujiunga na wanyonge na kuwatetea. Hao ndiyo wanazuoni wa kimapinduzi. Hakuna mwanazuoni au msomi asiyejikita ama kwenye tabaka-nyonyaji au tabaka-nyonywaji. Wote hujikita kwenye tabaka fulani hata kama hawajitambui au kujitambulisha hivyo.  Na mara nyingi, unaoonekana kama mgongano wa kimawazo au kinadharia ni mgongano wa mtazamo uliojikita kwenye tabaka au kundi fulani. 

Mwanazuoni hufanya uchambuzi wa kijamii ili ayaelewe vizuri mazingira kwa shabaha mahsusi ya kuboresha hali ya maisha ya waliowengi. Yeye huanika uovu wote hadharani bila kujipendekeza. Katika hili uchambuzi wake unakuwa kamilifu bila kujali utamfurahisha nani na utamuudhi nani, na hata kama akisakamwa na wenye mamlaka na madaraka katika jamii, – wakiwemo watawala wa kisiasa au watawala watarajiwa, au watawala wa kiuchumi, – hasiti kusema ukweli kama uchambuzi wake unamuelekeza kufanya hivyo. Kwa vyovyote vile, mwanazuoni mwanamapinduzi hawezi kukosa kuchukiwa na watawala na wenzao wa tabaka la kisiasa, political class.  Kama mwanafalsafa wa kimapinduzi Karl Marx alivyosema:

It is certainly not our task to build up the future in advance and to settle all problems for all time, but it is just as certainly our task to criticise the existing world as ruthlessly in the sense that we must not be afraid of our own conclusions and equally unafraid of coming into conflict with the prevailing powers.  

Kwa muhtasari, anachosema Marx ni kwamba kwa hakika siyo kazi ya wachambuzi/wanafalsafa kutanguliza kujenga mustakabali na kutatua matatizo yote kwa enzi zote, lakini ni kwa hakika pia kazi yao ni kukosoa hali ya ulimwengu uliyopo wakati huo bila kusita na kutokuhofia matokeo ya uchambuzi wao hata kama haya yatawaingiza kwenye misuguano na wenye madaraka.

Niongeze kusema kwamba ni wazi kabisa kwamba wanazuoni wanaotetea hali ilivyo bila shaka hawatakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wale wanaofaidika na hali hiyo. Kwa upande mwingine, wale wanaotaka kubadili hali kwa mtazamo wa wavujajasho watakuwa na hali ngumu, watasakamwa, watatungiwa uongo, watadhalilishwa na hata kujeruhiwa au kuuliwa. Kwao hii siyo hoja. Katika misitu ya Bolivia, wakati Che Guevara alipokutana uso kwa uso na wanajeshi mamluki wa Serikali, mmoja wao alimtambua na kulenga bastola yake kwake. Lakini alikuwa anasitasita kuifyatua. Che akamwambia, kwa sauti ya utulivu, ‘Unasita nini. Fyatua risasi yako, utakuwa umemuua mtu tu!’, kwa maana kwamba huwezi kuua fikra na mtazamo wa mwanamapinduzi na kweli kabisa mpaka leo fikra za Che zimedumu.

Katika historia yetu ya mapambano ya ukombozi tuna mifano mingi ya wanazuoni waliojitolea mhanga kwa sababu ya msimamo wao kuwa upande wa umma. Patrice Lumumba alitaka nchi yake iwe na uhuru kamili ili iweze kutumia utajiri wake kwa manufaa ya, siyo Wakongomani tu, bali kwa manufaa ya watu wa Afrika kwa sababu Lumumba alikuwa muumini wa Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism). Aliuliwa kikatili na wakala wa CIA. Kwame Nkrumah wa Ghana aliuchambua na kuukusoa mfumo wa ukandamizaji wa kibeberu, akitaka kuleta umoja wa Afrika kwa sababu aliamini kabisa kwamba wananchi wa vinchi vya Afrika wakiwa peke yao, hawataweza kumudu nguvu za kibeberu. Akapinduliwa na waliochukua madaraka kama mwanajeshi Afrifa aliyekuwa na mawazo finyu, wakamsakama na kumdhalilisha. Chris Hani, ambaye alikuwa na dhamira ya kujenga Afrika Kusini Mpya kwa mtazamo wa wavujajasho, aliuliwa katika kipindi nyeti cha mpito kutoka ukaburu kwenda ukombozi. John Garang, kiongozi wa muda mrefu wa Sudan ya Kusini, alikuwa na msimamo wa kutokutenga na kuvunja nchi ya Sudan; badala yake alitaka Sudan Mpya. Umma wa Sudan Kusini na Sudan Kaskazini walikuwa nyuma yake. Inasemekana alikufa katika ajali ya helikopta. Sina hakika!

Muammar Gadaffi, mwanasiasa aliyekuwa na dhamira ya kuleta mabadiliko makubwa na yenye maslahi kwa nchi na jamii yake, ingawa baadae alianza kuyumbayumba, aliuliwa na majeshi ya mamluki yakisaidiwa na NATO. Kosa lake? Alikuwa na mpango kabambe wa kuvuna maji yaliyopo chini ya ardhi ya jangwa la Sahara na kueneza maji hayo katika eneo zima la Sahel. Lakini rais wa Ufaransa, wakati ule Sarkozy, alikuwa na mpango wake mbadala. Alitaka Gadaffi akubali kutoa idhini ili mashirika ya Kifaransa wayavune maji hayo na kuyasafirisha kwenda Ufaransa kwa ajili ya kutengeneza maji ya chupa. Gadaffi alikataa katakata. Akasukiwa mpango, nchi yake ikavamiwa na hatimaye akauliwa. Leo hii nchi ya Libya imesambaratishwa na hao hao waliojiita wakombozi.  Nchi na vyombo vya habari vya Magharibi waliwakuza sana vibaraka hao na kuwatambua kama “wakombozi”, ili kuhalalisha maslahi yao ambayo yalikuwa sababu kuu ya kumpindua na kumuua Gadaffi.

Sasa nije kwenye sehemu ya tatu ya mada yangu – wajibu-jamii  wa wanazuoni.

III. Wajibu-jamii
Nitaeleza dhana hii ya wajibu-jamii wa mwanazuoni kwa kutoa mifano hai.

Mnamo mwaka 1988, kulikuwa na mjadala mkubwa juu ya riwaya iitwayo The Satanic Verses, yaani Aya za Kishetani. Riwaya hiyo ilitungwa na Salman Rushdie, ambae ni mzaliwa wa India ingawa anaishi Uingereza. Ni maarufu sana kama mtungaji wa riwaya.  Riwaya ya The Satanic Verses inakidhalilisha moja kwa moja Kitabu Kitakatifu cha Waislamu yaani Quran.  Alikejeli na hata kumtukana matusi ya nguoni Mtume Muhammad. Umma wa Waislamu ulichukizwa sana wakati wasemaji na serikali za Magharibi walishangilia na kumuunga mkono na kumtetea kwa msingi kwamba msanii ana haki na uhuru wa mawazo, freedom of expression, na lazima haki yake itetewe na kulindwa. 

Umma wa Waislamu walifikiri tofauti. Chuki na hasira za Waislamu zilisambaa kwa kasi kiasi kwamba kulikuwa na maandamano, ghasia na maafa katika nchi nyingi. Hatimaye, Kiongozi wa Kiroho wa Iran, Ayatollah Khomeini, alimlaani Rushdie kwa fatwa na kulikuwa na hisia kwamba angeweza kuuwawa. Rushdie alilazimika kwenda mafichoni  huku akilindwa na askari wa Uingereza.

Mabishano na malumbano kati ya wasomi wa Magahribi na wasomi Waislamu yalijikita kwenye mgongano kati ya dhana ya uhuru wa mawazo, haki mojawapo ya haki za binadamu, na wajibu-jamii wa mwanazuoni.

Shirika moja la uchapishaji wa vitabu, Penguin, walitaka kutoa toleo la India. Wakaomba ushauri wa wanazuoni wa Kihindi. Karibu wote (Waislamu na wasio Waislamu) walipinga kuchapishwa kwa kitabu hiki wakitoa hoja kwamba kitauchochea umma na kusababisha umwagaji wa damu na hata kuhatarisha umoja wa nchi yao.  Hatimaye serikali ya India ilipiga marufuku kitabu cha The Satanic Verses.  Hatua hiyo ya serikali iliungwa mkono na wanazuoni mashuhuri wa Kihindi wakiwemo Waislamu na wasio Waislamu. Barua iliyoandikwa katika gazeti la The Indian Post na jopo la wasomi iliuliza: je, kupigwa marufuku kitabu hiki ni mfano wa kujenga jamii kandamizi? Gazeti la The Times of India likajibu:

No, dear Rushdie, we do not wish to build a repressive India. On the contrary, we are trying our best to build a liberal India where we can all breathe freely. But in order to build such an India, we have to preserve the India that exists. That may not be a pretty India. But this is the only India we possess.

Tafsiri ya haraka haraka ni:

Hapana, mpendwa Rushdie, sisi hatutaki kujenga India kandamizi. Kinyume chake, tunajaribu kwa dhati kujenga India ya kiliberali ili kila mmoja wetu aweze kupumua hewa kwa uhuru. Lakini ili kujenga India kama hiyo, hatuna budi tuilinde hii India iliyopo. Inawezekana India iliyopo haipendezi, lakini ndiyo India tuliyonayo.

Mzee wetu, mwanazuoni mashuhuri, Profesa Ali Mazrui amefanya uchambuzi mahiri sana wa kitabu cha The Satanic Verses akionesha kwamba Rushdie alikusudia kabisa kuwadhalilisha Waislamu na kubeza Mtume wao ili ashangiliwe na watu wa Magharibi.  Hata baada ya kumkosoa Rushdie kwa hoja nzito, Profesa Mazrui anahitimisha kwa kusema kwamba Waislamu wamuombe Ayatollah Khomeini ili aondoe fatwa ya kifo, na kama ikibidi, basi amlaani tu.

Huyu ni Profesa Mazrui, mwanazuoni mahiri wa Afrika. Mfano huu unadhihirisha kwamba wakati mwanazuoni ana uhuru na haki ya kujieleza, lakini pia ana wajibu-jamii ili haki yake hiyo isilete madhara makubwa kwa jamii. Na wajibu-jamii huo siyo wa kushurutishwa kwa sheria bali unahitaji kutumiwa kwa busara, uelewa na hiari ya mwanazuoni mwenyewe ili asiweze kufanya jambo ambalo litaleta madhara na maumivu kwa wengine.

Nitatoa mfano mwingine mmoja kuhusu Profesa Mazrui kuonesha kwamba mara nyingine inambidi mwanazuoni aseme ukweli  ambao wengine hawataki kuusema au kuusikia hata kama kwa kufanya hivyo atakuwa anahatarisha usalama wake .  

Kati ya miaka ya 1971-72, nduli Idi Amin Dada aliwafukuza Waasia kutoka Uganda. Profesa Mazrui, wakati huo akiwa Chuo Kikuu cha Makerere, aliandika kipeperushi kiitwacho When Spain expelled the Jews and the Moors … A Lesson in History. Huu ulikuwa ni mfano wa kihistoria wa karne ya 15-17 wakati Wahispania Wakristo walio wengi walipowafukuza Waislamu wa Afrika ya Kaskazini na Wayahudi kwa sababu hawakuonekana kama ni wenzao ingawa wengi wao walibadili dini. Idadi yao ilikuwa ndogo lakini wengi wao walikuwa wafanyabiashara, madaktari, wenye mabenki, wasomi na kwa ujumla wataalamu mbalimbali. Inasemekana, baada ya kufanya kitendo hicho cha ubaguzi, uchumi wa Spain ulididimia. Profesa Mazrui anahitimisha kipeperushi chake kwa kusema:

Yes, let me once again repeat myself – we study history in order to understand ourselves. But we should also study it to be wiser, more humane, less rash, certainly less brutal, and often with an eye on the future.

Tafsiri:

Naam, hebu nirejee yale niliyowahi kusema – tunasoma historia ili tujielewe. Lakini pia inatubidi tuisome ili tuwe na busara zaidi, ubinadamu zaidi, ili tuupunguze ujinga, na hakika tuupunguze ukatili, na mara nyingi kwa kuangalia mustakabali wetu.

Nakala 1000 za kipeperushi hicho zilisambazwa katika jiji la Kampala na watu kwa utashi wao wenyewe walianza kutoa nakala zaidi.  Ingawa Mazrui kwa ubunifu mkubwa hakusema waziwazi kuhusu kufukuzwa kwa Waasia, ujumbe wake ulikuwa wazi. Hakuna mtu ambaye angeshindwa kufananisha yaliyokuwa yanatokea nchini Uganda na yale yaliyonukuliwa na Mazrui kutoka katika historia ya kale. Ilibidi Mazrui afunge virago na kuondoka akihofia kushughulikiwa na Iddi Amin Dada. Lilikuwa ni jambo la ujasiri kwa upande wa Mazrui lakini alikuwa anatekeleza wajibu-jamii wake wakati baadhi ya wasomi wenzake walikuwa wameamua kukaa kimya na wengine walikuwa wakishangilia siasa za uzawa za Iddi Amin. Lakini Iddi Amin baada ya kuwafukuza Waasia aliwageukia Waganda ili kuendesha utawala wake wa kikatili kwa zaidi ya miaka minane.

Sasa nimalizie na sehemu yangu ya mwisho, wajibu-jamii wa mwanazuoni wa Afrika.

IV. Wajibu-Jamii wa Mwanazuoni wa Afrika
Kwa muhtasari ningependa kusisitiza mambo matatu juu ya dhima (commitment) yetu kama wanazuoni na wajibu-jamii wetu.

Moja, tunahitaji uelewa na ufahamu wa kutosha wa historia ya bara letu kwa mtazamo wetu. Ninasisitiza mtazamo wetu, siyo historia tuliyolishwa na kumezeshwa na wasomi na wanazuoni wa kibeberu wa Magharibi. Katika hili nidokeze, kwa maoni yangu, mahali pa kuanzia.

Kipindi cha nusu karne ya uhuru wetu tunaweza kukigawa katika awamu mbili.  Kipindi cha miaka 25 ya mwanzo nakiita kipindi cha utaifa (yaani nationalism) na kipindi cha miaka 25 iliyofuata  tunaweza kukibatiza jina la uliberali-mambo leo (yaani neo-liberalism). Itikadi iliyotuongoza katika awamu ya kwanza ilikuwa ya utaifa. Kuna sifa mahsusi ya itikadi ya Utaifa katika Afrika. Utaifa wa nchi (territorial nationalism) ulizaliwa na itikadi ya Umajumui wa Afrika (yaani Pan-Africanism). Kizazi cha kwanza ambacho kilipigania uhuru kilijikita kwenye umajumui wa Afrika. Kwa hivyo, umajumui wa Afrika ulitangulia utaifa wa nchi na siyo kinyume chake. Historia hii inatutofautisha kabisa na Umoja wa Ulaya, ambao huwa mara kwa mara tunaurejea kama mfano wa kuigwa. Tofauti ya pili ya kimsingi kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika tunaotamani ni kwamba nchi za Ulaya zina historia ya ubeberu na ukoloni, historia ya kututawala, wakati sisi hatuna historia inayofanana. Ukweli ni kwamba sisi tulitawaliwa.

Kwa hivyo, siyo jambo la kushangaza kwamba kizazi cha waasisi wetu tangu mwanzo kilianza kujadili suala la kuunganisha nchi zao.  Waliposhindwa ndipo walipoanza kujenga utaifa wa nchi zao. Wakala mkuu wa kujenga utaifa akawa dola tuliyorithi kutoka kwa wakoloni. Huu moja kwa moja ni mgongano kwa sababu dola yenye sifa za kikoloni itakuwaje chombo cha kujenga utaifa?

Kulikuwa na mielekeo miwili katika itikadi ya utaifa. Mwelekeo wa utaifa wa mrengo wa kushoto (yaani radical nationalism) na mwelekeo wa utaifa wa mrengo wa kulia (yaani narrow nationalism).  Utaifa wa mrengo wa kushoto hujikita kwenye ukombozi na mabadiliko makubwa. Kielelezo cha utaifa wa mrengo wa kushoto ni Mwalimu Nyerere; kielelezo cha utaifa wa mrengo wa kulia ni wengine wengi ambao utaifa wao ulizizamisha nchi na jamii zao kwenye tope la uzawa, ukabila, udini na ubaguzi wa rangi.

Kwa maoni yangu, utaifa wa kinchi ulishindwa (yaani the national project failed). Uliberali mambo-leo umedhihirisha wazi kwamba utaifa uliojikita kwenye kinchi ulikuwa dhaifu kiasi kwamba uliposhambuliwa na itikadi ya uliberali mambo-leo, ambao wanauita utandawazi, ulisalimu amri. Utaifa wa kinchi haukuweza kuhimili mashambulizi ya hali, mali na itikadi ya nchi za kibeberu. Ukweli huo ndiyo umewafanya wanazuoni wa Afrika, ingawa siyo wengi, kufikiria upya dhana na itikadi ya umajumui wa Afrika. Mwalimu katika hotuba yake ya mwaka 1997, wakati wa kuadhimisha miaka 40 ya uhuru wa Ghana, alikiri kwamba kizazi chake kilishindwa kujenga umoja wa Afrika.  Aliwasihi Waafrika wa kizazi kipya, – viongozi, wanazuoni na vijana, – kuelekeza nguvu zao kwenye kujenga umoja wa Afrika, badala ya kuzama kwenye utaifa finyu wa vinchi na makabila yao. Bila umoja, Mwalimu alisisitiza, Afrika haina mustakabali mwema. Aliwaonya Waafrika wasijitumbukize kwenye ukabila au uzawa au utaifa wa vinchi. Wasione fahari kushangilia vinchi vilivyogawanywa kwa mipaka ya wakoloni. Hii ilikuwa ni alama ya utawala wa kikoloni, siyo utambulisho wao, aliwakumbusha.

Mwalimu alitoa ushawishi wa kiitikadi na kisiasa kwa kutumia kipaji chake. Sisi wanazuoni tunatakiwa kwenda mbali zaidi. Tueleze awamu hii ya mashambulizi mapya ya kibeberu dhidi ya nchi za Afrika kwa mtazamo wa kihistoria. Kwa muhtasari, nataka nijenge hoja ya kuwafikirisha.

Sifa kuu inayoutambulisha mfumo wa kibepari ni ulimbikizaji wa mtaji bila kupumua (endless accumulation). Katika kipindi hiki cha ubepari wa kimataifa, ambao unajidhihirisha kwetu kwa jina la uliberali mambo-leo, ulimbikizaji wa mtaji ni ulimbikazji wa kiporaji (primitive accumulation). Ndiyo mwelekeo wa ulimbikizaji unaotawala – uporaji wa rasilimali na maliasili; udidimizaji wa hali ya maisha ya wavujajasho; upanukaji wa sekta isiyo rasmi – (eti sekta isiyo rasmi!) – ambayo unaongeza maradufu unyonyaji wa wavujajasho; ukuaji wa sekta ya fedha – mabenki, mashirika ya bima, soko la hisa, n.k. –  ambayo ni mirija ya kunyonya mtaji wetu; ukopeshaji wa fedha na mabenki ya kibiashara na kutufanya tulipe madeni pamoja na riba na gharama zingine ambazo zinatufanya tuwe watumwa milele; na njia nyengine.

Hizi ni njia za kisasa za kulimbikiza mtaji kwa kupora jasho la wavujajasho na rasilimali na maliasili za nchi zao. Lakini kimsingi, ulimbikizaji huu hauna tofauti na ulimbikazaji wa kiporaji wa enzi ya biashara ya utumwa. Uhusiano wetu na Ulaya ulianza zaidi ya karne tano zilizopita, zikiwemo karne mbili za biashara ya utumwa. Ni bara la Afrika tu lililokumbwa na janga hili. Mwanasiasa-uchumi mmoja (Bagchi, 2005) anajenga hoja kwamba biashara ya utumwa ilikuwa na mchango wa kipekee katika ulimbikizaji wa mitaji na maendeleo ya nchi za Ulaya. Isitoshe, anadai kwamba biashara hii ndiyo iliyowezesha nchi za Ulaya kushindana katika soko la bidhaa na nchi za Kiasia na hatimaye kuwatawala. Nieleze kidogo. Hoja yake ni kwamba, mazao – miwa, viazi, mahindi, na malighafi nyingine kama pamba n.k. – yaliyolimwa na watumwa wa Kiafrika huko Marekani na katika visiwa vya Carribean kwa gharama ndogo sana yaliziwezesha nchi za Ulaya kumudu lishe bora kwa wafanyakazi wao ambayo iliwasaidia kuongeza ufanisi wao kiuchumi, kwa upande mmoja, na kuyatuliza mapambano ya tabaka la wafanyakazi kisiasa, kwa upande mwingine. 

Kwetu sisi, biashara ya utumwa ina nafasi ya kipekee kwa sababu siyo tu jambo la kihistoria bali inatusaidia kuelewa na kuchambua hali halisi ya leo, au utumwa mambo-leo.  Kama nilivyoainisha, njia ya kulimbikiza mtaji kwa kupora ilitawala wakati wa utumwa; na njia hii imerudi kwa sura mpya katika kipindi hiki cha uliberali mambo-leo.

Mwanazuoni wa Afrika anayejali hana budi aielewe historia hii. Suala la historia siyo suala la kulaumiana, bali ni nyenzo ya kutuongezea uelewa na kuongoza uchambuzi wetu wa hali halisi.

Jambo la pili ni kuhusu nadharia ya kufanyia uchambuzi. Nadharia (theory) ni ufahamu wa hali ya juu – higher form of knowledge. Katika fani hii ya kujenga nadharia sisi wenyewe kutokana na hali yetu halisi, wanazuoni wa Afrika, tumekuwa nyuma sana. Na hii siyo kwa sababu hatuna uwezo, bali ni kwa sababu tumekuwa wepesi kukubali unyonge wetu. Hatuna kiburi cha uanazuoni. Kama ilivyo mifumo ya uchumi wetu, sisi huzalisha malighafi, husafirisha nje na kununua kutoka nje bidhaa zilizotengenezwa. Vilevile wasomi wetu hukusanya data ghafi (raw data) na kuwapelekea wasomi wa Magharibi. Wao huchambua na kujenga nadharia ambayo sisi humeza bila kuhoji.

Kwa ujumla, rai yangu kwenu ni kwamba kuna haja ya kufanya utafiti wa msingi na wa maana katika hali yetu halisi (basic research). Kutokana na tafiti hizo tutaweza kujenga nadharia zitakazotuelekeza na kutuongoza juu ya namna ya kuleta mabadiliko ya maana. Katika Chuo hiki tulianza vizuri lakini tukakumbwa na hizi sera tulizoletewa na ubeberu; sera kama za ushindani, biashara na utafiti wa kisera wa kutoa majibu fastafasta. Kwa mfano, ziko wapi tafiti zinazotuonesha jinsi jamii zetu zilivyobadilika chini ya uchumi na utawala wa uliberali mambo-leo? Ziko wapi tafiti zinazobainisha muundo wa matabaka katika jamii yetu, mijini na vijijini? Ziko wapi tafiti zinazobainisha sifa za dola na siasa tulizonazo? Ziko wapi tafiti zinazobainisha wakala wa kusukuma gurudumu la maendeleo yetu? Ziko wapi tafiti zinazobainisha muundo na mtindo wa mshikamano baina ya tabaka/matabaka ya ndani na ubeberu, na kuainisha sifa na athari za ubeberu mambo-leo? Tafiti kama hizo ndizo zinaweza kutusaidia kubadili hali halisi na kuchagua tufanye nini, kwa ajili gani na kwa manufaa ya nani. Tafiti kama hizo ndizo zinazoweza kutusaidia kujenga nadharia zetu sisi wenyewe ambazo zitatusaidia kuamua nini tukubali na nini tukatae kutoka nje; zitatuwezesha kutofautisha mahindi na makana.

Tafiti za msingi kwa ajili ya kujenga nadharia zetu, zinahitaji mazingira mwafaka. Tunahitaji mazingira yanayofaa katika taasisi zetu za elimu ya juu ya kujadili, kudadisi, kuhoji na kutokubali chochote ambacho hakina ushahidi na hoja.  Tusijenge mazingira kandamizi ya hofu kiasi kwamba vijana wakose kupumua. Na miongoni mwetu tusiwanyamazishe wale ambao tunatofautiana nao. Njia mojawapo ya kuua hoja na mawazo mbadala ni kujenga mazingira ya kuogopesha, yaani intimidation. Kila anayehoji siyo mchochezi. Kila anayekuwa na mawazo mbadala siyo mamluki. Yeyote anayekataa kujipendekeza siyo mpinzani.  Tutafakari.

Jambo la tatu ni kujihoji sisi wenyewe, wasomi na wanazuoni. Tunawajibika kwa nani na kwa nini. Je, tunatekeleza wajibu wetu ipasavyo? Nimesema kwamba katika mfumo huo wa kibwanyenye kuna matabaka yanayozaa itikadi na mitazamo yake. Sisi wasomi na wanazuoni hatuwezi kujidanganya kwamba hatuna upande. Upande tunao. Tujitambue. Tujiulize, sisi ni wanazuoni wa nani, tabaka gani, tuko upande gani?

Sisi, nyie na mimi, ni tabaka la vibwanyenye, petty-bourgeoisie.  Tuna chaguo; ama kukumbatia mtazamo, itikadi, maslahi na fikra za mabwanyenye na masahiba wao, mabeberu, au kuwa na mtazamo wa wavujajasho na kutetea maslahi yao. Nimetumia neno chaguo maksudi. Mfanyakazi hana chaguo, mama nitilie hana chaguo, machinga hana chaguo. Kwao haya ni maisha yao. Mfanyakazi ni mfanyakazi; mama nitilie ni mama nitilie; machinga ni machinga. Lakini sisi, kwa lugha nyepesi niseme, walalahai, tuna chaguo. Tunaweza kuchagua kuwa upande wa walalaheri au upande wa walalahoi.

Chaguo ni letu. Tutafakari. Tuamue. Tutende. Tusijipendekeze kote kote; tutaanguka, na pamoja nasi tutayaangusha matumaini ya waliowengi kwetu.

Ahsanteni.

Marejeo          

Bagchi, Amiya Kumar, 2005, Perilous Passage: Mankind and the Global Ascendancy of Capital. New York: Rowman & Littlefield.

 Baran, P. A., 1969, ‘The Commitment of the Intellectual’, in The Longer View. New York & London: Monthly Review Press.

 Chachage, C. S. L., 2008, ‘The University as a Site of Knowledge: The Role of Basic Research’, in Chachage Seithy L. Chachage, Academic Freedom and the Social Responsibilities of Academics in Tanzania. Dakar: CODESRIA.

 Cabral, Amilcar, 1969, ‘The Weapon of Theory’, in Amilcar Cabral, Revolution in Guinea: An African People’s Struggle, London: Stage 1.

 Harvey, D., 2005, A Brief History of Neo-liberalism, Oxford: OUP.

 Luxembourg, R., 1913, The Accumulation of Capital, London: Routledge.

 Marx, Karl, 1867, Capital, vol. I, Part VIII, ‘The so-called Primitive Accumulation’. Moscow: Progress Publishers.

 Mazrui, Ali, 1973, ‘When Spain expelled the Jews and the Moors’, Africa Today, Vol. 20, No. 1, United States Policy toward Africa (Winter, 1973), pp.73-75. Published by: Indiana University Press Stable URL: http://www.jstor.org/stable/4185282. Accessed:  06/04/2014 10:25

 Mazrui, Ali, 1989,  ‘The Satanic Verses or a Satanic Novel?’ Moral Dilemmas of the Rushdie Affair’, based on a lecture originally given at Cornell University, Ithaca, New York on 1 March 1989.

 Mwalimu Nyerere Chair in Pan-African Studies, 2010, Chachage’s Intellectual Versatility, Dar es Salaam: University of Dar es Salaam.

 Nyerere, J. K., 1997, ‘Without unity, there is no future for Africa’, speech at the 40th Indedpendence Anniversary of Ghana, in New African, February 2006.

 Shivji, Issa G., 2009, Accumulation in an African Periphery: A Theoretical Framework. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota.

 Toussaint, E., 1999, Your money or your Life! The tyranny of global finance. London: Pluto Press.

 Williams, Eric, 1964, Capitalism and Slavery. London: Andre Deutch.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box