WAZEE WAPENDEKEZA KUUNDWE BARAZA LAO

1. UTANGULIZI
Tarehe 19.05.2015 “Mkutano wa Siku Mbili wa Mashauriano Kuhusu Hali ya Amani na Utulivu wa Nchi Yetu” ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ulianza katika ukumbi wa Julius Nyerere Conventional Centre Dar es Salaam kwa kukutanisha pamoja viongozi wakuu wa serikali waliopo na wastaafu, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na baadhi ya wazee ili kutafakari na kujadili hali ya amani, umoja na utulivu wa nchi yetu.

Mkutano ulifunguliwa kwa hotuba IMG_8877ya ukaribisho iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi Dr. Salim A. Salim. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ndugu Joseph Butiku aliwakaribisha wajumbe katika mjadala wa pamoja kwenye makundi matatu: kundi la viongozi wakuu wa serikali waliopo na wastaafu, kundi la viongozi wa vyama vya siasa na kundi la wazee.

Kwa minajili ya Kikao hiki, taarifa ya maoni ya kundi la wazee inawasilishwa.

2. MISINGI YA AMANI
Kufuatia majadiliano ya kina, wajumbe walikubaliana kwamba kuna viashiria vya kutosha kuonyesha kwamba amani na utulivu vimeanza kutoweka katika jamii na nchi yetu. Hata hivyo, wajumbe waliainisha kwamba viashiria vya kutoweka kwa amani ni dalili ya ugonjwa na sio ugonjwa wenyewe.

Wajumbe walisisitiza kwamba amani ya Tanzania ilijengwa juu ya misingi muhimi ifuatayo ambapo jitihada za makusudi zilifanyika kuifuata katika awamu ya kwanza:

I. Umoja na Utaifa
Katika awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere hatua za makusudi zilichukuliwa kujenga utaifa kama utambulisho wa pamoja bila kujali kabila, dini, rangi, au hadhi ya mtu au mali alizonazo. Umoja na Utaifa ulijengwa juu ya msingi wa usawa na utu wa binadamu.

Wajumbe walijadili na kupembua kwa kina dhana ya Umoja na Utaifa la Tanzania. Walifafanua kwamba, mara baada ya Uhuru mradi mkubwa uliotiliwa mkazo na uongozi wa wakati huo ni kuleta umoja miongoni mwa jamii ya makabila zaidi ya 150 na ujenzi wa hisia za Utaifa.

Jambo hili kwa mujibu wa wajumbe, lazima lirejeshwe na kuzingatiwa wakati huu kuliko huko nyuma

II. Usawa na Uhuru
Katiba, sheria na mfumo wa siasa na utawala ulizingatia usawa na uhuru wa kila mwananchi na uhuru wa nchi kufanya maamuzi yake yenyewe. Ubaguzi wa aina yoyote ulipigwa marufuku na kukemewa waziwazi na viongozi wa kisiasa na kijamii. Utegemezi ulipondwa na ubeberu haukukubalika.

III. Uongozi bora
Uongozi bora uliainishwa kwa vigezo vya kisiasa na kisheria. Kiongozi bora ni mtu ambaye asiye na uchu wa madaraka au mali. Uongozi haupiganiwi bali unapewa kutokana na sifa mtu alizonazo. Nafasi za uongozi katika vyombo vya dola na chama hazikuwa ni miradi ya kujilimbikizia mali. Na miiko ya uongozi katika Azimio la Arusha iliweka wazi ili kumbana kila mtu.

IV. Uhusiano wa Wazee na Vijana
Wazee waliheshimika kwa hekima na busara zao na walitakiwa kuwa mfano wa kuigwa na vijana. Vijana walilelewa katika familia na jamii kwa misingi ya umoja, utaifa, usawa, haki na ari na moyo wa kujitolea. Taasisi mahsusi, kama Jeshi la Kujenga Taifa, ziliwekwa kulea vijana.

Misingi hiii ndiyo ilikuwa ni mwongozo wa nchi na Taifa.

3. KUACHANA NA MISINGI
Wajumbe bada ya mjadala na kutoa mifano mingi walikiri kwamba misingi hii imewekwa kando na ndiyo chimbuko la kuanza kutoweka kwa amani kama inavyodhihirishwa na viashiria mbalimbali.

Wajumbe walitoa mifano michache ya viashiria kama ifuatavyo:

a) Kupuuza na kutoheshimu Katiba na miongozo mbalimbali iliyopo. Wajumbe walieleza kwamba licha ya nchi yetu kuwa na Katiba na miongozo mbalimbali baadhi ya viongozi na wananchi wamekuwa vinara wa kuvipuuza na hivyo kusababisha manung’uniko miongoni mwa wanajamii.

• Aidha, kwamba mara baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi jamii ilihama kutoka katika msingi wa maadili uliowekwa na Azimio la Arusha na kukumbatia mfumo wa soko huria unaojali zaidi mali. Watu wametawaliwa na mali na kupuuza Utu. Mjumbe mmoja aliweka vizuri kwa kusema: “Watu wanatawaliwa na uchu wa mali na viongozi wanatawaliwa na uchu wa madaraka ili wajilimbikizie mali.”

b) Nchi na Jamii kutokuwa na mfumo wa Malezi kwa vizazi. Kwamba kwa sehemu kubwa jamii ya Watanzania imekosa mfumo muafaka unaolea jamii kutokana na kuiga mfumo wa siasa wa Nchi za Magahribi ambazo zinamtazama kiongozi kama mtu binafsi aliyeshinda katika ushindani wa soko huria ya kisiasa badala ya kuwa taswira ya jamii nzima.

• Hakuna mfumo wa malezi unaoandaa jamii kama lilivyokuwa Azimio la Arusha hivyo jamii yote kuwa na mtazamo wa pamoja juu ya mema na maovu. Mfano, Azimio liliweka msingi uliokataza watu kuwa na uchu wa mali na madaraka.

• Mfumo uliopo unaandaa vijana kuwa wahalifu zaidi kuliko kuwa raia wema.

c) Unafiki na Kuikwepa Kweli. Viongozi wa kada zote katika jamii wanashiriki katika kujenga utamaduni wa kuikwepa kweli na kuijengea hofu jamii. Baadhi ya viongozi wa dini, kwa mfano, hawawakemei waumini wao ambao ni mafisadi na badala yake ndio hupewa nafasi za juu katika nyumba za ibada kutokana na mitaji yao.

d) Uongozi. Kwamba uongozi wa nchi yetu hivi sasa umepoteza dira kutokana na kukosekana kwa mtu anayeweza kusimamia na kukemea maovu yanayojitokeza kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu Nyerere.

• Viongozi wamekuwa wakitoa matamko na maelekezo kwa wafuasi wao yanayochochea na kuhamasisha uadui na shari miongoni mwa wanajamii..

• Viongozi wa kisiasa na vyama wamekuwa wakihamasisha na kulazimisha masuala kwa matakwa binafsi. Baadhi wamekuwa wakitumia kila mbinu ili kujitwalia madaraka ikiwemo matumizi makubwa ya fedha. Uongozi umekuwa bidhaa sokoni ambayo kila mwenye mtaji (wa ndani na wa nje) anainunua na kuliangamiza Taifa.

e) Wazee kutoheshimika. Kwa muda sasa kundi la wazee ambao ni wastaafu limekuwa haliheshimiwi wala kupewa fursa ya kuchangia uzoefu wao katika uendeshaji wa masuala ya nchi.

f) Mfumo wa Kibeberu usiozingatia Utu na kuthamini zaidi Mali. Kwamba migongano mingi na kutoelewana katika jamii ya kitanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla inachochewa na mradi wa nchi za kibeberu kutaka kuitawala dunia kupitia rasilimali kama madini, mafuta na gesi.

• Angalizo lilitolewa kuwa Tanzania kimkakati ni lango kuu kuelekea nchi zilizo katikati ya Afrika ambazo nyingi zake zina hazina kubwa ya rasilimali kwa hivyo mataifa makubwa yanatumia kila mbinu kuharibu hali ya utulivu na amani katika nchi yetu. Kukosekana kwa amani katika nchi za Kongo-DRC, Somalia, Afrighanistan, Syria, Palestine ni muendelezo wa mradi wa nchi za Kibeberu kuitawala dunia.

4. NAFASI YA TAASISI KATIKA MUKTADHA HUU
Katika kuhitimisha majadiliano, wajumbe wanaipongeza Taasisi ya Mwalimu Nyerere kutokana na juhudi zake za kuhakikisha umoja, amani na utulivu katika Taifa letu unadumishwa. Kwamba ili Watanzania waendelea na imani hii kwa Taasisi ni muhimu ikabakia na jukumu hili pasipo kujifungamanisha na maslahi ya kundi fulani isipokuwa ustawi wa Taifa Tanzania na Bara la Afrika.

5. NAFASI YA WAZEE KATIKA MUKTADHA HUU
Wajumbe walikubali juu ya wajibu wa msingi wa kundi la wazee kuwa ni kushauri, kukemea na kuonya jamii dhidi ya masuala mbalimbali yanayoharibu amani na taswira ya nchi..

6. MAPENDEKEZO MAKUU
6.1 Wazee walikiri kwamba kuna haja ya kuhuisha MISINGI MIKUU ya Taifa letu ambayo ilijenga amani na utulivu. Kuna haja ya kuibua mijadala katika maeneo mbalimbali kuhusu misingi hii na Taasisi ya Mwalimu Nyerere iendelea kuiandaa mijadala kama hii.

6.2 Wazee pia walikiri kwamba wana wajibu wa kijamii kuedeleza mijadala kwa nafasi yao wenyewe bila kusubiri kuitwa na Taasisi au vyombo vingine. Pia wazee wana wajibu wa kukemea uovu katika jamii na pia kuwakemea viongozi waovu wanaohubiri shari kwa maslahi yao binafsi.

6.3 Wazee walipendekeza kwamba hatimaye kuna haja ya kuwa na chombo rasmi na huru cha wazee kinachotambulika na Katiba au sheria ya nchi. Hata hivyo wazee wasisubiri mpaka chombo kilichopendekezwa kiundwe; bali waanze kutekeleza wajibu wao maramoja kwa kuwashawishi wazee wenzao popote walipo.

7. MAPENDEKEZO MENGINE

7.1 Wazee wawe wawazi na kuongoza jamii katika kukemea maovu kila yanapojitokeza katika jamii.
7.2 Tanzania kama Taifa lazima isimamie vyema na kugawa sawia rasilimali zake kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
7.3 Kwa kuwa Tanzania ni eneo Mkakati katika Bahari ya Hindi, ni muhimu kuwa makini na mataifa yanayohusiana nayo ili isigeuke wakala wa Ubeberu Mamboleo katika eneo hili.
7.4 Tabia ya viongozi kuhamasisha wafuasi wao ikemewe kwa uwazi bila ya kuoneana haya.
7.5 Uongozi ni kitu nadra hivyo haupaswi kununuliwa na kugombewa kama bidhaa sokoni. Wazee wakemee watu wanaojipitisha mitaani kununua Uongozi.
Prof. Issa G. Shivji
Mwenyekiti wa Kamati

Wajumbe wa Kamati:
1. Prof. Issa G. Shivji Mwenyekiti
2. Edgar Atubonekisye Katibu
3. Kept. Mstaafu Mohamed Ligora
4. Rev. Canon Thomas Godda +255 766 149 325
5. Bi. Cecilia M. Kamba +255 0758/713 413 360
6. Ignasi Agustino +255 754 433 116
7. Abas Idi Kirobo
8. Limboa B. Limboa (Yombo kwa Limboa) +255 712 674 567
9. Rajabu Mbwana Mkufunzi
10. Balozi Adam Marwa (mst)
11. Seleshi J. Msangi
12. Eng. Muhidin Mchoropa +255 788 068 228
13. Maja Habib Hassan (mst)
14. Ali Rashid Ali (Chake Chake—Pemba) +255 777/715 431 181
15. Angelus Machege
16. Haji Machano Haji +255 773 135 425
17. Waziri Mbwana Ali +255 777 463 401
18. John Kalage
19. Bi. Salama Mzee Majaliwa +255 777 858 162
20. Ahmada Khamis Hilika (Zanzibar) +255 713 492 739
21. Shaban Bakari Mirocho (Rufiji)
22. Eng. William Bocco +255 784/655 307 316

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box