Yes, In My Life Time chazinduliwa

Siku ya Jumatano, Juni 25, 2014, pale Tume ya Sayansi na Teknolojia ulifanyika uzinduzi wa selected-works-haroub-othmanKitabu cha Mkusanyo wa maandishi ya Prof. Haroub Othman aliyoyaandika nyakati mbalimbali wakati wa uhai wake. Katika hafla ya Uzinduzi, ambao ulifanywa na Dk Salim A. Salim, mhariri wa kitabu alisema maneno machache kabla uzinduzi rasmi haujafanyika. Mhariri wa Kitabu hiki, Prof. Saida Yahya-Othman alisema hivi:

Dk. Salim, Ndugu, Rafiki, Makamaradi,
Tunashukuru sana kwa kujumuika nasi. Pia naungana na Walter Bgoya kumshukuru Dk Mshinda [Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH] kwa kutukarimu, na Dk Salim kwa kuiengezea haiba shughuli yetu.

Mwezi huu wa Juni tunatimiza miaka mitano tokea Haroub afariki. Ni miaka mitano ambayo imekuwa na matukio mengi yaliyoitikisa dunia, na kutetemesha nchi yetu. Ni matukio yaliozua mijadala na tafakuri nyingi kuhusu mifumo ya uchumi na mapambano ya wanyonge. Ni miaka ambamo dhulma na unyonyaji wa wanyonge umefikia upeo wa kutisha.

Machache mno ya kuwafariji wanaharakati. Ukiondoa maridhiano ya Zanzibar, ambayo yangemfurahisha sana Haroub, angalau kwa muda, mengine mengi yangemtia khofu na kumjaza simanzi ingawa kamwe yasingemfanya asalimu amri au kukata tamaa. Kitabu hiki kinatoa ushuhuda wa kushereheka kwake, matumaini yake na khofu zake, kwa nchi na dunia.

Hiki si kitabu changu. Ni cha Haroub. Ni katika mifano ya vitabu vilivyotoka miaka ya karibuni, vya wanasiasa, waandishi na wasomi, vya makusanyo ya hotuba, makala au mihadhara waliotoa siku za nyuma. Tafauti ya hiki ni kuwa mwandishi mwenyewe hayuko nasi, na hilo pia si jambo geni. Lakini kazi inakuwa ngumu zaidi, kwa sababu mzigo wa maamuzi unamuelemea mhariri, akikosa ushauri wa mwandishi mwenyewe. Kama mhariri, nimeubeba mzigo huo kwa unyenyekevu, lakini pia kwa furaha, nikiwa na jukumu la kuingiza na kuacha, kunyofoa na kuchopeka, kupanga na kupangua. Nilifungwa na mambo mawili tu – lugha, kwa vile tulifanya uamuzi tukusanye vya Kiingereza kwanza, na mahali pa uchapishaji wa kwanza, ikiwa tumelenga zaidi makala ya kitaaluma. Lakini sikuweza kuepuka masuali yalioegelea kichwani mwangu: Je Haroub angetaka kitabu hiki kichapishwe? Je, angekichapisha mwenyewe, angechagua makala haya niliochagua mimi? Angeyapa uzito masuala ambayo mimi nimeyaona stahili? Angeukubali mpangilio huu niliouchagua? Angeridhika na makato niliyoyafanya kwenye baadhi ya makala zake? Yote masuali bila majibu, na bila tija. Nimefanya kile Haroub akinishauri nifanye siku zote – umeamua, tekeleza.

Wazo la kitabu hiki liliibuliwa na CODESRIA, mwaka huo huo wa 2009, pale Mkurugenzi Mtendaji wake, Dakta Ebrima Sall, alipokuja kunipa pole.  Wakati ule sikujua kama ningeweza kuifanya hii kazi. Baadae nilijiuliza kama wazo hilo Ebrima hakulitoa kama njia ya kunifariji na kuniliwaza, maana sote tunajua ugumu wa kupata maneno muafaka kwenye hali kama hiyo. Asingejua kama nitakuja kulidaka hilo wazo na kuling’ng’ania. Nawashukuru sana CODESRIA kwa kutoa mwega kwa utafiti wa kazi hii. Kaka yangu Walter Bgoya alikubali moja kwa moja pale CODESRIA walipopendekeza uchapishaji wa ubia. Nae alihimili bughudha zangu za “lini kitabu kinatoka?” kwa  utulivu mkubwa. Rafiki yangu Issa Shivji nae hakusita nilipomuomba kuandika dibaji. Mdogo wangu Chris Peter alinipa msaada mkubwa katika kupata baadhi ya makala ambayo sikuweza kuyagundua kwenye maktaba ya Haroub mwenyewe. Hawa wote nawashukuru kwa dhati, pamoja na familia yangu walonivumilia na kunidekeza wakati kazi hii ikiendelea.

Jina la kitabu linatokana na msemo wa Haroub kuhusu mapambano mengi yaliokuwa yanaendelea ambayo yeye yalimgusa na kuongoza mwenendo wa shughuli zake na harakati zake – kusambaratika kwa ubeberu, kupatikana kwa uhuru kamili wa nchi zetu (wa kisiasa na kiuchumi), kuzaliwa kwa dola la Palestina. Kwa haya alikubali kuwa hatayashuhudia wakati wa uhai wake. Lakini kitabu hiki ni mkusanyo wa yale aliyoyafanya wakati  wa uhai wake. Kwa hivyo Naam, in my life time.

Kama nilivyosema, kitabu hiki ni mkusanyo wa makala mbali mbali, zikianzia 1974 hadi 2009. Miaka 35 ya harakati na mapambano nchini na duniani. Makala haya yalichapishwa mwanzo kwenye vitabu na majarida anuai. Kwa hiyo suali ni: Chapisho kama hili lina umuhimu gani? Si makala yako tayari?

Umuhimu wake unajikita sehemu tatu. Ya kwanza, ni kuwa makala yote sasa yako kitapu kimoja, kwa hiyo kurahisisha upatikanaji wake. La pili, baadhi ya makala yaliomo humu sasa hayapatikani tena – vitabu vimeisha, wachapishaji wamefunga biashara, majarida yamekufa. La tatu na la muhimu kabisa, ni kuwa kitabu hiki ni cha kimakavani. Jamii yetu ni wadhaifu sana kutunza makavani, na kwa hiyo historia yetu inafifia chini ya vumbi na mchwa. Hii ndio njia moja ya kuifufua na kuihuisha, kuchapisha vitabu vinoweza kuwapatia vijana wetu wa sasa na wajao, mwanga wa mambo yalivokuwa na kwa hiyo, vipi yanaelekea kuwa.

Wanamapinduzi (na Haroub akijigamba kuwa miongoni mwao) siku zote wanajikita kwenye historia – wana jicho la mbali la kuona nyuma, na hivyo kujenga uwezo wa kufanya uchambuzi sahihi wa hali inayotukabili, ili kujipanga vilivyo kuendeleza mapambano. Hili ni la muhimu sana, katika jamii yetu ambamo historia inakuwa kama ukoma, ambamo wanafunzi wa chuo kikuu leo hii hawajui TANU ni nini, ambamo tunafikiri ukombozi wetu utakuja kwa kuwaiga wengine bila ya kuhoji,  ambamo tunafikiri utaifa ni chuki dhidi ya waliokuwa tafauti na sisi na uzalendo uchwara. Tungejua Wavietnam walivokomboa nchi yao tungekuwa na fikra mgando hizo? Tungejua mhanga waliojitoa Waafrika Kusini, na wanaoendelea kujitoa Wapalestina, tungeamini kuwa uhuru na maendeleo ni maghorofa marefu na posho za vikao?

Matongotongo hayo yatatolewa kwa kufahamu historia yetu na ya dunia kwa kusoma, kutafakari na kuchambua. Hakuna njia nyengine.

Si kawaida kwa mwandishi au mhariri kufanya mapitio ya kitabu chake mwenyewe. Kwa hiyo sitafanya hilo. Nitawaachia wengine. Lakini nitaje tu kuwa makala yaliomo yanatembea kutoka mapambano dhidi ya ubeberu, kupitia mshikamano wa wapigania haki za wanyonge kote duniani, kuegemea kwenye umajumui wa Afrika, na bila shaka, kutua muda mrefu kwenye  muungano wa Tanzania. Nasikia mitaani kuna njia mpya ya kusabahi siku hizi – Vipi, mbili au tatu? Mimi nafahamu Haroub alikuwa wa mbili, yumkin kuelekea moja. Na ingawa wanasiasa wameingia mtindo wa kuwasemea wale wasiokuwa nasi tena (Fulani angekuwa hai angeunga mkono serikali tatu!) mimi siwezi kusema hivyo kwa niaba ya Haroub. Nalitaja hili kwa sababu ya muktadha tulio nao, na pia kwa sababu sehemu kubwa ya kitabu inawanda kwenye eneo hilo.

Kazi ya kukinadi na kukiuza kitabu ni ya mchapishaji. Ninamwachia Walter na wenzake. Mimi ninachojua ni kuwa kwangu kusoma ni uhai. Na uhai huo unapaliliwa na wale wanaoandika na wanaotoa mrejesho kwa njia ya mijadala. Natumai nanyi mna mawazo fananishi.

Namalizia kwa moja ya beti nilizoandika baada ya Haroub kufariki:

Fikra hazipotei
Yako wapi maneno
Yaliokuwa yakitiririka
Kama mto uliofurika.
Ziwapi fikra
Zilokuwa zikijikwaa
Na nyengine,
Kwa wingi na kasi.
Uwapi uchambuzi
Ulotufikirisha, kutuchangamsha, kutugonganisha.
Yote haya yamejificha,
kuripuka siku nyengine?
Yanauguza majaraha
kutokana na mapigo?
Yatarudi na nguvu mpya
Kwa vita vya kudumu?
Lazima, lazima yarudi,
Sababu hamna kilichobadilika,
Historia haifutiki,
Mapambano hayazizimi
Shauku haififii
Hadithi ya wanyonge haina tamati.

Asanteni sana.

 

4 thoughts on “Yes, In My Life Time chazinduliwa

 1. Fikra za Profesa Haroub bado zinatufikirisha na kutufundisha kuhusu mwelekeo na hatma ya mapambano dhidi ya ubeberu na uvunjifu wa haki za binadamu. Shukran Profesa Saida kwa kazi nzito ya uhariri wa maandiko ya Profesa Haroub. Nami niwakumbushe wasomaji wa cheche Shairi nililotunga kusherehekea maisha ya rafiki yetu na mwalimu wetu. Profesa Othmani, atakumbukwa daima.Enyi wana Mlimani,tulieni msilie,Ingawa mna huzuni, nawasihi mtulie,Maisha ya Othmani, ni mema yashangilie,Profesa othmani, Atakumbukwa daima.Atakumbukwa daima, na kila mwanazuoni,Kwa hoja alozisema, na zile za vitabuni,Ukweli aliusema, kwa upana na undani,Profesa Othmani, atakumbukwa daima.Atakumbukwa daima, Bara hata visiwani,Kwa kuchukia dhuluma, ukabila na udini,Kidete alisimama, kuupinga ukoloni,Profesa Othmani, atakumbukwa daima.Atakumbukwa daima, kwa kazi za utetezi,Kutetetea wakulima, wafugaji na wakwezi,Alizitoa huduma, kwa usawa na uwazi,Profesa Othmani , utakumbukwa daima.Atakumbukwa daima, kama mpenda amani,Kwa kudai usalama, Iraq na Lebanoni,Dunia ilo salama, hakika alitamani,Profesa Othmani, atakumbukwa daima.Atakumbukwa daima, na ndugu na marafiki,Kwa upendo na huruma, na kupigania haki,Maisha yake mazima, yana mafunzo lukuki, Profesa Othmani, atakumbukwa daima.Atakumbukwa daima, na wana “UDASA “wote,Wakiwemo Lwaitama, Saida Issa na Kente,Wanaomba kwa Karima, ili pepo aipate,Profesa Othmani, atakumbukwa daima.

 2. Kwenye makala fulani ( Barua Ndefu Kwa Prof. Shivji) niliandika maneno haya ambayo yanafaa kurudiwa hapa kumuenzi Prof Haroub. \’\’ Wakati ule wa sekondari nilivutiwa sana niliposimuliwa habari ya Profesa Haroub Othman na Wewe. Kwa kweli nilipata mshawasha mkubwa wa kukutana nanyi na kupata darasa maridhawa kutoka kwenu. Kwa bahati mbaya, mauti yalitupokonya kipenzi chetu Profesa Haroub Othman hata kabla sijamuona. Mauti hayakutaka nipate walau nafasi ya kumtunukia kwa kupigania bila kuchoka mustakabali wa haki za binadamu, hasa upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wanyonge wasio na uwezo huko Zanzibar. Hebu haya tumuachie Rabana kwa sababu imeshanenwa kwamba kazi yake haina makosa. Hata wewe nilikuta umekwishastaafu shughuli ya uhadhiri. Sikubahatika kukaa darasani ambamo mbele yake kuna mhadhiri aitwaye Prof. Issa Gulamhusein Shivji!\’\’. Nafikiri nilikuwa nimekosea kudhani kwamba siwezi kukutana tena na Prof Haroub. Kadiri ninavyoendelea kusoma kazi zake ndipo ninapomuona yu karibu yangu tukikubaliana, kubishana na wakati mwingine kutokubaliana kabisa. Bila shaka \’\’YES IN MY LIFE TIME\’\’ kitaniweka karibu zaidi na Komredi Haroub Othman. Ni njiani kukisoma!

 3. Fikra, busara, hekima na mawazo ya Prof.Haroub vinapaswa kutunzwa kwa weledi mkubwa sana kwani kadiri muda unavyokwenda tunazidi kugundua ni kwa jinsi gani aliipenda nchi yake, taaluma, utawala wa haki, umajumui na haki za binadamu. Nampongeza sana Prof.Saida kwa kazi hii makini na yenye weledi wa hali ya Juu.
  Lakini katika upande wa pili ningependa kutoa changamoto au wazo ambalo linaweza kuleta mantiki kubwa katika hili.
  “CD YENYE HOTUBA, MIJADALA NA UCHAMBUZI WA KAZI ZA Prof.HAROUB”.
  Nachelea kutoa wazo hili kwani watanzania wengi hawapendi kusoma, lakin kazi hizi zitakapokuwa katika mfumo wa CD ni rahisi kwa watanzania na familia zao kuangalia na kujifunza mengi.
  Mungu ailaze pema roho ya Prof.Haroub!

 4. Kwenye kijitabu hiki mawazo ya Professa Haroub Othman ambayo ya kujenga moja kwa moja na yenye kufikirisha mwenendo wa suala zima la maendeleo katika bara letu la Afrika. kuna sehemu kwenye kijitabu Professa anatuambia kuwa azimio la Arusha lilitoa ahadi ya matumaini na kuleta maendleo. Na hata bara lote la Afrika lilikuwa na maendeleo kabla ya ubinashishwaji. Lakini hali ikaja kuwa mbaya zaidi pale tulipo chukua marekebisho ya uchumi SAP, umaskini uliongezeka maradufu na leo umezidi kuongezeka baada ya kuingia kwenye shimo la uliberali Mambo leo.
  Hii ni limu tosha juu ya kizazi kinacho kuja na kuiona kazi hii na kujua juu ya maendelo ya Afrika katika mapambano yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Please type the characters of this captcha image in the input box

Please type the characters of this captcha image in the input box